Tuesday, 17 January 2017

MEDA CLASSIC ACHANA NA DIAMOND FANYA YAKO


Na;Mwanakalamu
Huenda nilichelewa kumsikia huyu mkali aliyeweka makazi yake kwa muda mrefu mjini Iringa, kwani nilianza kumsikia baada ya kuandika na kuimba kibao matata kilichoenda kwa jinala ''Barua kwa Diamond''.Kwa haraka haraka nikadhani ilikuwa njia ya kutaka kutoboa kwa kupitia jina la mwanamuziki ambaye alikuwa akitambulika ndani na nje ya Afrika ya mashariki.


Lakini inawezekana nilikuwa nimekosea kwani licha ya ukali wake wa maandishi na uimbaji na kuandika nyimbo kadhaa kali ambazo zingeweza kumtambulisha kama Meda Classic mwanamuziki mwenye kipaji kikubwa cha kuimba, kwani niliendelea kumsikia na kumwona akiimba na kuonekana kama 'kivuli cha Diamond' kuanzia mwonekano wake hadi kuimba nyimbo nyingine ambazo zilikuwa ni kama za kuonesha tuu namna gani anapenda uimbaji wa bwana Diamond.
Baada ya ngoma kadhaa ambazoo ni kama zilipuuzwa tuu na vyombo vya habari vya nje ya kanda ya kusini hususani Iringa Mbeya na Njombelicha ya ubora wake , nyimbo kama Kongoi,I love you,Somebody,Alele, na wimbo wa mrembo wa uswazi alioshirikiana na Nasi alijikuta akiendelea kuimba nyimbo za kumpaisha zaidi Diamond badala ya kumweka zaidi yeye juu.


Alikuja kuimba wimbo mwingine wa ''Princes Tiffa'' na sasa Kokoro remix ambazo licha ya kuzitendea haki kwa kuzifanya kwa ubora wa hali ya juu bado haziweza kumweka pale alipokuwa akitegemea.
Meda nakiona kipaji chake lakini naona kinapuuzwa na kuonekana na mwanamuziki mdogo na wakawaida kwa kuwa bado wengi wanakuchukulia kama shabiki tuu wa Diamond anayeamua kuimba nyimbo kujifurahisha na kuwafurahisha mashabiki wengine na si mtu mwenye mikakati ya kuwa Diamond mwingine ama Meda Classic mwanamuziki mkubwa.
Mwanakalamu nakushauri achana na Diamond fanya yako , wewe ni mkubwa na utakuwa mkubwa zaidi ya huyo unayefuata njia zake kama tuu utajua nini unakitaka.

Tuesday, 3 January 2017

Shairi:Wewe maana ya pendo

WEWE NI MAANA YA PENDO
Siihitaji kamusi,kuipata tafsiri,
Ninaiota harusi,na haitokuwa siri,
Siyo mbio za mjusi,ukingoni kusubiri,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.

Kila ninaposikia,sauti yako kipenzi,
Sipendi kwona walia,sababu yangu mpenzi,
Na kwangu umetulia,tena enzi na enzi,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.

Nitakijaza kitabu, kuzitoa zako sifa,
Lakini isiwe taabu,nilishakupa wadhifa,
Mola atupe thawabu,atujaze maarifa,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.

Uzuri uvutiao,mola amekujalia,
Haufanani na wao,hilo nalishuhudia,
Pesa huifanyi ngao,mengi wayavulimia,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.

Wafanya nijiamini,nikatuna kila kona,
Na wakora wa mjini,hawaishi kunong'ona,
Eti unanipa nini,wanahamu ya kuona,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.

Na unapokuwa mbali,zile njozi hazinishi,
Nazikumbuka asali,picha hazikinaishi,
Ninaishia kusali,rohoni kwangu uishi,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.

Pia nakumbuka mbali,kipindi tunayaanza,
Nyimbo nilizikubali,hivyo ndivyo tulianza,
Zilivuka majabali,ulizipanga stanza,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.

Sitoisahau siku,ile siku twaonana,
Si mchana si usiku,sura yako niliona,
Yeyote hatokupiku,wala sitopiga kona,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.

Unapopata tatizo,waniita Morry wako,
Ninapokupa liwazo,watamani nije kwako,
Mpenzi wanipa tunzo,na daima niwe kwako,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.

Mpenzi wanithamini,kwa maneno na vitendo,
Huna roho ya kwa nini,unachojali upendo,
Laziz nakuamini,wala huhitaji lindo,
Wewe maana ya pendo,ninakupenda muhibu.

Napita kifua mbele,sina hofu abadani,
Wala sihofu kelele,nitazihofu kwa nini,
Wangoje vigelegele,kuvipiga kanisani,
Wewe maana ya pendo, ninakupenda muhibu.

Nitayasema mengi, siku ile ikifika,
Japo neno halijengi, kwetu linahitajika,
Wambea hatuwatengi,nao tunawaalika,
Wewe maana ya pendo, ninakupenda muhibu.

Monday, 2 January 2017

SHAIRI;KAMA HUKUJA KUWINDA


Tumeshafika nyikani,rungu huku sime kule,
Na mikuki mabegani,mbwa huku na kule,
Hatutorudi nyumbani,bado tunasonga mbele,
Kama hukuja kuwinda, usingekuja nyikani.

Ungebakia nyumbani,cheza na wadogo zako,
Mkaenda kisimani,uwatwishe ndugu zako,
Mkaziosha sahani,huku kweli sio kwako,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja nyikani.

Eti waogopa mwitu,eti waogopa miba,
Mara unahofu chatu,na mkuki umebeba,
Eti wataka viatu,katambuga umebeba,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja mwituni.

Eti huku kuna simba,mara waogopa mvua,
Unaulizia nyumba,wahisi tumepotea,
Utaja kosa mchumba,ukishindwa vumilia,
Kama hukuja kuwinda, usingekuja nyikani.

Wahangaikia uyoga, hiyo kazi ya dadako,
Mara waenda kuoga,huyataki masumbuko,
Umejawa na uoga,kama vipi rudi huko,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja nyikani.

Bado washangaa kenge,swala anakukimbia,
Nawaza nikucharange,bakora kukushitua,
Mara vijiti uchonge,muda watupotezea,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja mwituni.

Mwanaume huna haya,waogopa hata nyani,
Nyoka naye wamgwaya,mbonde rungu kichwani,
Eti wenzetu Ulaya,nyoka anawekwa ndani,
Kama hukuja kuwinda,usinge kuja nyikani.

Kitoweo wakipenda,kikiwekwa bakulini,
Nyikani wataka kwenda,na mikono mfukoni,
Utapikiwa mlenda,wende kula kwa jirani,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja nyikani.

Hulka kubwa ulonayo,tutapofika nyumbani,
Maneno yakutokayo,eti wewe namba wani,
Hutaki kupiga mbiyo,ngoja tukwache mbugani,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja nyikani.

Sungura tumempata,haraka kutia kisu,
Nafsi haijakusuta,asante wairuhusu,
Na mvi zitakuota,tabaki kuomba busu,
Kama hukuja kuwinda,usingekuja nyikani.....

"Kauli za Makabwela 2017"

SHAIRI; KWAKO MWANANGU MPENZI


Naandika kwa furaha,furaha ya kuwa nawe,
Nataka upate raha,usilie juu ya mawe,
Upendo na uwe silaha,pendo lako uligawe,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Usiyashike maneno,kukashfu ulimwengu,
Ukaja yaficha meno,kuhofu ya walimwengu,
Ulishike langu neno,siogope ulimwengu,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Mama na babako tupo,twakuombea kwa Mungu,
Hata ikiwa hatupo,usiuote uchungu,
Na wema wa Mungu upo,wastahili lako fungu,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Brigita na Anita, majina tuu mwanangu,
Vyovyote tungekuita,hata jina la mamangu,
Majina ni ya kupita,hayo ni chaguo langu,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Usihofu ufukara,hicho ni kitu kidogo,
Ni akili pia busara,hutochukia mihogo,
Mwanangu kugangamara,si kutwa kupiga zogo,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Usiisake sababu,ya kuukosa ukapa,
Sijui tangu mababu,ufukara upo hapa,
Kujituma ni jawabu,kweli hutotoka kapa,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Pia usijidanganye,utaupata kwa mume,
Ukwasi akunyang'anye,moyo uje ukuume,
Mwanangu kutwa uhanye,matunda uje uchume,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Alice kipenzi changu,wewe ni faraja yangu,
Nimekupa damu yangu,umebeba sura yangu,
Faraja ya mke wangu,twasema asante Mungu,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Utapata marafiki,pia hata maadui,
Pia kuna wanafiki,ambao huwatambui,
Uwe rafiki wa dhiki,upendo haubagui,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Kuna nyakati za dhiki,zisikutoe akili,
Kufuru usidiriki,muhimu kustahimili,
Hiyo mikiki mikiki,isije haribu mwili,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Wana maneno matamu,kutaka kukupoteza,
Wakikidhi zao hamu,ubaki kuomboleza,
Rahisi kuwafahamu,mama atakueleza,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Wengi wanaharibiwa,kila iitwayo leo,
Wengi wanajaribiwa,kwa maneno na vileo,
Akili za kuambiwa,zisije kupa vimeo,
Kwako mwanangu kipenzi,dunia mahali pema.


Mama msikize sana,atakushauri mengi,
Usiwaze kugombana,hekima iwe msingi,
Hakutokuwa na mana,ukimwekea vigingi,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Mungu muweza wa yote,mshukuru muamini,
Simwache siku yoyote,sipaparikie dini,
Siwaze kuwa Dangote,bila Mungu kuamini,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Malezi ni kazi ngumu,ya akili siyo mwili,
Usiongeze ugumu,ukiutumikia mwili,
Ukaja tamani sumu,ukaharibu akili,
Kwako mwanangu kipenzi,dunia mahali pema.


Mheshimu kila mtu,tajiri na hoe hae,
Ila uthamini utu,utu pipa ujae,
Ila usije thubutu,madume yakuhadae,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Dunia mahali pema,kila mtu na riziki,
Waza kuyatenda mema,na usiwe mzandiki,
Nikifa ‘talala vyema,Mungu ukimsadiki,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Wednesday, 21 December 2016

Shairi;Iwe chungu iwe tamu

IWE CHUNGU AMA TAMU
Kwetu ulimi maneno,mengine ni ya ziada,
Siye twatoa misemo,na nyimbo kwenye ibada,
Ladha kwetu siyo somo,ladha kwetu siyo shida,
Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba.

Vya maana twaviona,twanusa na kusikia,
Hizo suti za kushona,na vingi vya kuvutia,
Tulivitamani sana,tumeshindwa kufikia,
Iwe chungu iwe tamu, cha msingi ni kushiba.

Iwe biringanya mbichi,ama pilipili manga,
Karoti ama kabichi,ama dagaa mchanga,
Sie milo haichoshi,tunatamani kusonga,
Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba.

Sie hatuna ratiba,tupatacho tunakula,
Tunachopenda kushiba,hatuchagui vyakula,
Bila soda tunashiba,tunakula kisha sala,
Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba.

Kwetu hatuna jokofu,hatuchachishi viporo,
'Tabaki na yako hofu,utumbo hauna kasoro,
Kunenepa hatuhofu,leo twala kesho doro,
Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba.

Si kwamba hatutamani,tamaa twaweka ndani,
Twapiga kazi jamani,siku tuwe na vyetu ndani,
Maisha hatulingani,tajiri na masikini,
Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba.

Shughuli na matukio,twajua chungu na tamu,
Jaani ndo kimbilio,kama vile si timamu,
Njaa huleta kilio,hatujui neno hamu,
Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba.

''Kauli za makabwela 2017''

Shairi;Mie kuku wa fukara
MIE KUKU WA FUKARA
Sisemei banda bovu,linavyotesa masika,
Ama wa kwangu uchovu,wa kutwa kahangaika,
Kula kuisaka nguvu,na uhai kuuweka,
Siha njema siha mbaya,kwangu vyote ni mashaka.

Masika kuna wadudu,minyoo na kadharika,
Mahindi nayahusudu,kucha zangu zapondeka,
Mama sura ya bandidu,atishia kunipika,
Siha njema siha mbaya,kwangu vyote ni mashaka.

Kiangazi ni nafuu,vigunzi na kadharika,
Sema mawe ya miguu,mwenyewe akikwazika,
Nafaka zawekwa juu,ili nisije kufika,
Siha njema siha mbaya,kwangu vyote ni mashaka.

Vicheche na paka pori,waniletea mashaka,
Nyoka nao ni hatari,na mie ananisaka,
Mwenyewe hana habari,banda langu linanuka,
Siha njema siha mbaya,kwangu vyote ni mashaka.

Kama mayai tayari,kweli ninasononeka,
Najua naleta shari,watashindana kupika,
Kwangu hali siyo nzuri,hapo kweli nateseka,
Siha njema siha mbaya ,vyote wangu ni mashaka.

Nikijifanya ngangari,kutaga wakatosheka,
Ama nitagie pori,nikakwepana na nyoka,
Bado kwangu siyo heri,vifaranga kuleleka,
Siha njema siha mbaya,vyote kwangu ni mashaka.

Wageni na sikukuu,hunifanya nawehuka,
Sina hata mjukuu,wa kuja kunikumbuka,
Nawaza kupaa juu,kama mwewe nikaruka,
Siha njema mabaya,kwangu vyote ni mashaka.

Likipita gonjwa kuu,atanuna na kucheka,
'Taliwa hata miguu,utumbo na kadharika,
Kweli wakati ni huu,wa vitambi kuchomoka,
Siha njema siha mbaya,kwangu vyote ni mashaka.

Nikiwa na siha njema,na hapo pia siponi,
Mgeni mwenye heshima,akibisha mlangoni,
Nitawafanya kuhema,watie kisu shingoni,
Siha njema siha mbaya,kwangu vyote ni mashaka.

'Kauli za makabwela 2017''

Shairi;Wakati Rafiki Mwema

WAKATI
Huyu ni rafiki mwema,hana unafiki katu,
Wala hahofu kusema,kwa miti hata watu,
Liwe baya liwe jema,kuficha hatothubutu,
Wakati rafiki mwema,hajawahi kuongopa.

Hajawahi kuogopa,ama kuona aibu,
Hohe hae kwa vibopa,wakati kwao jawabu,
Ya ukweli atakupa,hata kwa kukuadhibu,
Wakati rafiki mwema,husema kweli daima.

Husema kweli daima,tena bila kuamuru,
Uwe chali uwe wima,wakumbuka ya Kaburu,
Hasemi ufanye hima,ama jifanye kunguru,
Wakati rafiki mwema,daima namthamini.

Daima namthamini,namfanya mali yangu,
Afanya nijiamini,sihofii mwisho wangu,
Kaskazi na kusini,kwa weusi na wazungu,
Wakati rafiki mwema,haujui unafiki.

Haujui unafiki,aje akulishe sumu,
Anapenda urafiki,hata ukimdhulumu,
Na usipomuafiki,wala hatokulaumu,
Wakati rafiki mwema,atakupa uatakacho.

Atakupa utakacho,wala usimuabudu,
Iwe wazi na kificho,mpole ama bandidu,
Hawezi kupa kisicho,mwema akupe kibudu,
Wakati rafiki mwema,wakati ni kiongozi.

Wakati ni kiongozi,huumbua ufichacho,
Wakati ni kama ngozi,ama mboni ya jicho,
Wakati ni mkombozi,asiyevujisha jasho,
Wakati rafiki mwema,huumbua hufumbua.

''Kauli za Makabwela, 2017''

NGOJA KAZI IWE KWANGU


Kazi ngumu ya kupewa,kijipa rahisi sana,
Katu huji kuchelewa,daima utakazana,
Huhitaji kuombewa,kazi yako itafana,
Ngoja kazi iwe kwangu,kuamua hili jambo.

Imeshapita miaka,nalia nabembeleza,
Sikuzihofu dhihaka,sikuchoka kuchombeza,
Leo ni wa tatu mwaka,pendo ninalikoleza,
Ngoja kazi iwe kwangu,kuamua hili jambo.

Maghani na mapambio,nilitoa kwa hisia,
Daima nakuja mbio,ninapohisi walia,
Hufurahii ujio,japo hujaniambia,
Ngoja kazi iwe kwangu,kuamua hili jambo.

Maneno yaniishia,nitasema jipya gani,
Moyo nauhurumia,umeshakupa thamani,
Kwako ulishahamia,ulihamia zamani,
Ngoja kazi iwe kwangu,kuamua hili jambo.

Jambo gumu kuamua,hilo ninalitambua,
Umeshindwa kuchagua, kati ya mvua na jua,
Moyo ulishaugua,nabaki napiga dua,
Ngoja kazi iwe kwangu,kuamua hili jambo.

''Kauli za Makabwela 2017''

''Kings Music''Alikiba fanya yafuatayo


Na.Mwanakalamu
Miezi michache iliyopita,mwanamuziki Alikiba alitangaza rasmi kuwa ana ''Music Lebel'' ambayo itakuwa inasimamia wanamuziki kadhaa;Abdukiba, Jokate, AbbySkills ,Brown Mauzo na wengine wengi.Kwa mujibu wa maelezo yake alidai kuwa lebel hiyo ilikuwepo tangu muda kidogo hakuamua tuu kuitangaza,mwanzoni nilidhani ni ile tuliyokuwa tukiisikia kwenye nyimbo zake nyingi za albam yake ya pili ''After the middle finger Entertainment'' kumbe ni mpya yenye jina la 'Kings Music'.
Muziki na usimamizi wake ni biashara inayolipa sana kwa kipindi hiki lakini pia huhitaji gharama kubwa kuanzia fedha,muda,, ujuzi na mengine mengi.
Najua Alikiba ni mwanamuziki makini sana ambaye ameudhihirishia ulimwengu kwa kufanya mambo mengi sana kwa mwaka huu likiwa ni hilo la kuazisha lebel ya Muziki.Lakini pamoja na umakini wake kuna ushauri pia atahitaji kutoka kwa wadau wa muziki ili kufanikisha hili alilo lianzisha.Yafuatayo ni mambo makubwa matano ambayo Alikiba anaweza kuyafanya katika kuifanya Kings Music kufanikiwa zaidi.

1.FUNGUA STUDIO YA MUZIKI
Hili linaonekana kutokuwepo kwenye mipango yakO kwa mujibu ya maneno uliyoyatoa kwenye #Papokwapapo na Papi wakati ukijibu swali la mmoja wa watumiaji wa twiter.Japokuwa ulisema jambo hilo ni muhimu pia kwa wanamuziki hasa katika kuhifadhi nza kuendelea mawazo ya nyimbo yanapomjia kichwani.Lakini kwa 'lebel' kuwa na studio yake itasaidia mengi sana kufanyika kwa uhuru zaidi kwani kundi litakuwa na nafasi ya kufanya mambo yake kwa uhuru zaidi badala ya kusubiri zamu kwenye studio nyingine.

2.UWE NA BENDI YAKO
Alikiba ni mtu wa Live Band na hata wanamuziki wako wanaonekana kuwa ni wafuasi wa muziki wa aina hiyo hivyo litakuwa jambo la busara sana kuwa na kitu hiki.Pia itasaidia sana kupunguza gharama za kuzilipa bendi nyingine wakati mwingine kuepusha kutofautiana ratiba na bendi hizo za kukodi.Studio iwe imekamilisha na bendi ili pia kuweka uhuru wa wanamuziki wake kufanya mazoezi kwa uhuru na kujenga kile kiitwacho ''Chemistry'' inayoeleweka ya muziki.
Hili si tuu litawapa uhuru bali litaingizia lebel pesa za kutosha pale bendi yake itapotumiwa na wanamuziki wengine.

3.WASAJIRI ABBY DADY,MAN WATER NA GODLUCK GOZBET 
Hawa wana studio zao ila unaweza kuwaleta studio kwako kwa makubaliano na pesa za kutosha.Wanaweza kuwa pia kama wamiliki wenza wa lebel yako.Unaweza kujiuliza kwa nini ufanye hivyo jibu rahisi tuu sana ukilinganisha biashara ya muziki na biashara nyingine katika zama hizi za kibepari kukusaya raw materials ni moja ya mbinu ya kibiashara.
Abby Dady ni mtu ambaye najua mmezoeana sana na anajua nini unakihitaji kwa wakati gani lakini pia ni mtengenezaji mzuri wa midundo hivyo ataweza kukupa nini wanamuziki wako wanataka.
Man Water huyo ni habari nyingine kwenye kuzalisha muziki unaokubali kupigwa na live band.Si unakumbuka Dushelele na Mwana?Huyo anaweza kuendelea kuwa studio kwake lakini akifanya kazi kwako kama part time lakini akiwa mwanaKings Music itakuwa poa sana.
Huyo Godluck kama jina lake ,kabarikiwa vipaji vingi anaweza kutunga,kuimba na kuproduce hivyo unaweza kumsajiri ukizingatia vipengele hivyo 
 yaani hapo ni kama unasajiri watu watatu na usiogope kutumia pesa maana itarudi zaidi.Huyo atasaidia katika kubalance muziki wa lebel yako badala ya kuegamia kwenye muziki wa kuchezeka zaidi.
Ukiwa na hao watatu muziki wenu hautochosha watu wala kufanana sana na utakuwa ni chakula bora kwenye bongo za wasikilizaji.

4.ABBY SKILS
Huyo ni mwanamuziki mkongwe uliyemkuta kwenye muziki, na anamchango mkubwa kwako.Unatamani awe juu kimuziki ukijaribu kurejesha fadhila.Ni mkali pia wa kutunga nyimbo hivyo ni vyema akatumika zaidi upande wa kutunga zaidi kuliko kuimba.Si kwamba hajui kuimba bali anajua zaidi kutunga na nyimbo zake nyingi anaonekana kuhitaji kushirikiana na wengine hivyo mwache atunge huku akija kuimba kwa mara moja moja sana pale anapojisikia.
Si kitu kibaya kwa muziki huu unavyoenda.

5.MR BLUE ,RAMA DEE,MAD ICE NA KALAJEREMIA
Najua ni wanamuziki ghali ila ukifanikiwa kuwasajiri na kuwaweka kwenye lebel hiyo mtakuwa mmeongeza madini ghali kwenye muziki wenu.
Hao ni kati ya wanamuziki wakali na wakubwa sana hivyo kwa lebel yenu kuwa nao ni faida kwao na kwa lebel.

Mwisho nikupongeze kwa mafanikio uliyoyapata kwa mwaka huu huku nikikuombea mafanikio makubwa sana mwakani na miaka minginge ijayo.Natumai chati yako itazidi kupanda kadri siku zinavyoenda. Pia kuwa na studio yako, maproducer na bendi yako siyo kufuli la kukufunga wewe na wanamuziki wa lebel yako kurekodi kwako pia muwe na vifungu vya kuwaruhusu kurekodi kwingine pia wao kurekodi nyimbo za wanamuziki wengine.Pia uwe na Dj na Cameraman pia wafanye ziara ya kwenye vyombo vya habari vya ndani na nje ya Afrika ili kuutangaza muziki wenu kimataifa zaidi.
Naomba kuwasilisha.

SHAIRI;NAJUA NIPO SALAMAMama asante sana,pole kwa magumu yote,
Ninajua twafanana,kuliko viumbe vyote,
Siwazi tutagombana,ukinifanya vyovyote,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Najua umeteseka,kuumwa na kutapika,
Pia ulisonononeka,pia ulisikitika,
Moyoni ukaniweka,mama hukutikisika,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Marafiki ulikosa,wengi walipukutika,
Waliona kama kosa,wala hukusikitika,
Na hukufikiri posa,huruma ulijivika,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Bibi alinung'unika,kuona mama walia,
Uoga hukujivika,kweli ulivumilia,
Hujafa hujaumbika,moyo uliuambia,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Mwili ulipukutika,afya ikanyong'onyea,
Uoga ukafunika,huku ukiniombea,
Chakula hakikulika,mama ukanitetea,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Niliihisi faraja,ulipokuwa na baba,
Lilibomoka daraja,hukupunguza mahaba,
Nikawaza mama naja,wapi yupo wangu baba,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Ile sauti ya baba,ilinifanya niruke,
Nami nampenda baba,nilitamani nishuke,
Anayo hekima baba,daima umkumbuke,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Siku ile ninashuka,uliteseka mamangu,
Chakula hukukumbuka,hata ugali nachangu,
Neno lile nakumbuka,karibu sana mwanangu,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Usichoke usumbufu,na huku kulialia,
Kilio ni maarufu,pakiuma nitalia,
Utacheka maradufu,kiona nimetulia,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Yapo mengi ya kusema,ila nakomea hapa,
Nimesharibu mama,mama usijenichapa,
Nibadili nguo mama,nzi wanifuata hapa,
Asante mama mpenzi,nipo mikono salama.

Nakupa ahadi mama,nitakuwa mama bora,
Sitokudharau mama,hata nipigwe bakora,
Daima nitasimama,nije kuwa mke bora,
Asante mama mpenzi,nitakupenda milele.