Monday, 19 May 2014

KIKOSA UTATAMANI

KIKOSA UTATAMANI
Malenga na wahakiki,habari zenu jamani,
Pia kwenu marafiki,'meamkaje jamani,
Najua wakuafiki,na wasioniamini,
Kiwa nayo hutamani,kikosa utatamani.

Mtu ampenda mama,basi baba ana tabu,
Hata akosee mama,baba tamwona sababu,
Na mama akimtuma,hatoibua sababu,
Kiwa nayo hutamani,kikosa utatamani.

Hata kama hohehae,baba ana umuhimu,
Kiwa chini umwinue,pendo kwake likadumu,
Siyo kwetu mkimbie,eti baba wa binamu,
Kiwa nayo hutamani,kikosa utatamani.

Mtu amkana baba,kisakutwa amelewa,
Atasema hana baba,hata kama hajafiwa,
Kasoro za wake baba,wengine wataambiwa,
Kiwa nayo hutamani,kikosa utatamani.

Ni kama ule mafano,babu aloniambia,
Kushoto wako mkono,waona wakusumbua,
Kikosa huo mkono,kazi yake utajua,
Kiwa nayo hutamani,kikosa utatamani.

Pendo la baba si njia, sema utazichagua,
Kifa utamlilia,kazi yake utajua,
Ulivyo amekulea,mama yako kumuoa,
Kiwa nayo hutamani,kikosa utatamani


KWA RIWAYA, MASHAIRI, NA TUNGO MBALIMBALI, WAWEZA TEMBELEA PAGE YETU YA FACEBOOK NA KULIKE

0 comments:

Post a Comment