Tuesday, 20 May 2014

USHAIRI: HADHI YAKE IMESHUKA

Ninavyojua zamani,ilikuwa na thamani,
Kirudi wale wa shimoni,wataudhika jamani,
Ilokuwa na thamani,sahizi huitamani,
Imeshuka hadhi yake,sijui hata kwa nini.

Maneno yeye baraka,na maua ya rangirangi,
Utakuwa wanacheka,kiwa na ua la bangi,
Na maneno ya dhihaka,pia kata ya mtungi,
Imeshuka hadhi yake,hivi kwa nini jamani.

Nitakapopata ajira,mama nitampatia,
Japo kulipa fadhira,hivi nilifikiria,
Nitakuwa taahira,hadhi imeshapotea,
Imeshuka hadhi yake,sina hamu nayo tena.

Misemo yenye vijembe,iliingia kwa kasi,
Na za nyundo na jembe,zikapata wafuasi,
Wakazivaa wapambe,warembo kujinafasi,
Imeshuka hadhi yake,mama nitakupa suti.

Michezo ikaibuka,kanga moja wakaivaa,
Majini wakaloweka,kucheza kwenye jukwaa,
Matangazo wameweka,dola ninaishangaa,
Imeshuka hadhi yake,sasa nguo ya chumbani.

Ishara ya machombezo,si heshima kama kale,
Si kwa wenye uwezo,busara kutupa kule,
Hawana hata vigezo,hata waloenda shule,
Kanga vazi la heshima,ilikuwa hapo kale.

0 comments:

Post a Comment