Monday, 2 June 2014

SHAIRI: USISEME YATAKWISHA

MTUNZI: Moringe Jonasy Mhagama
ANWANI: KALAMU YANGU

Wewe bado mwanafunzi,walia wapigwa sana,
Walaumu uongozi,nao sio wa maana,
Wawaheshimu wazazi,eti hutaki laana.
Usiseme yatakwisha,bila kufanya lolote.

Eti unakosa kula,wajisifu yatakwisha,
Kila siku wewe hola,hadi kesho panakucha,
Kila siku tatu bila,leo katubeba mcha,
Usiseme yatakwisha,huku umelala ndani.

Kijiji hakina maji,wewe wimbo yatakwisha,
Kijana huna mtaji,malezi umejitwisha,
Shambani hakuna mboji,na mbolea imeisha,
Usiseme yatakwisha,huku unapiga soga.

Mama mwana ana mimba,baba yake humuoni,
Kaka kaoa mgumba,sasa akesha pombeni,
Baba ana ndogo nyumba,hujui ufanye nini,
Usiseme yatakwisha,hakuna ukifanyacho.

Maadui wengi sana,yakupasa kupambana,
Kama ana nguvu saa,kimbia ukakazana,
Silalamike sana,jikaze wewe kijana,
Usilalamike sana,pambana upate kitu.

0 comments:

Post a Comment