Tuesday, 29 July 2014

HUYU NDIYE MWANAMKE

HUYU NDIYE MWANAMKE
Huwa aniita bebi,hata angekuwa wapi,
Nguo hazifui dobi,hata tungekuwa wapi,
Chakula chake sishibi,hata zingekuwa hopi,
Huyu ndiye mwanamke,popote najisifia.

Kiumwa naye aumwa,huruma namuonea,
Sichoki kutumwatumwa,mama namhurumia,
Jina lake litasomwa,milele nakuambia,
Huyu ndiye mwanamke,popote najisifia.

Napenda akifurahi,lazima atanambia,
Mapema anisabahi,hali yangu kuijua,
Kila siku asubuhi,simu ninampigia,
Huyu ndiye mwanamke,popote najisifia.

Nampenda siku zote,siulize kwa nini,
Akiniomba chochote,kumpa soni sioni,
Napenda tungekufa wote,tukazikwa kaburini,
Huyu ndiye mwanamke,popote najisifia.

Mola mjalie mema,baraka zake zidumu,
Umtunze wangu mama,dhambi usimhukumu,
Daima nitasimama,mtu asimdhulumu,
Huyu ndiye mwanamke,popote najisifia.

Waweza uliza jina,wengine 'tasema sara,
Kalista lake jina,wala siyo masihara,
Sara hatujaachana,nisije pata hasara,
Huyu mwanamke mama,mola ampe uzima

0 comments:

Post a Comment