Wednesday, 30 July 2014

WIVU NA MAPENZI

KASORO
Kila mtu ana yake,wengine hawazijui,
Mie sina neno kwake,na wala simsumbui,

Nikimwacha peke yake,kalala hajitambui,
Kasoro yangu ni wivu,kwa huyu mpenzi wangu
.

Nikipiga hapokei,nalalama siku nzima,
Namba yake sikosei,nimemeza nzimanzima,
Nikiona haongei,naweza mwambia mama,
Kasoro yangu ni wivu,kwa huyu mpenzi wangu.


Kisema niko na kaka,lazima nitalalama,
Hapo kweli nitawaka,ntashindwa hata kusoma,
Kila siku nalalama,hivyo ndivyo anasema,
Kasoro yangu ni wivu,kwa huyu mpenzi wangu.

Unaongea na nani,simu yangu kuiacha,
Utaniua jamani,ama umeshaniacha,
Huyo joshua ni nani,siku nitakukamata,
Kasoro yangu ni wivu,kwa huyu mpenzi wangu.

Huyo ulomwita wangu,ni nani uniambie,
Waumiza moyo wangu,kwa nini unisumbue,
Sawa nitapata vyangu,mali zisikusumbue,
Kasoro kubwa ni wivu,kwa huyu mpenzi wangu.

Malenga na marafiki,nambieni kipi dawa,
Chonde msinidhihaki,kusema nimepagawa,
Kuachwa miye sitaki,hata pia kuibiwa,
Kasoro yangu ni wivu,kwa huyu mpenzi wangu....

0 comments:

Post a Comment