Saturday, 26 July 2014

USHAIRI: MACHWEO


MACHWEO
Sijui yangu kasoro,au ninacho kilema,
Hata kipata kihoro,huku nashindwa kuhema,
Kifika moja kasoro,ama na nusu Kigoma,
Machweo yana faraja,jua linapojichotama.

Ile rangi ya manjano,huku kuna hudhurungi,
Hunifanya kama pono,kushangaa hizo rangi,
Si leo tangu magono,haziishi hizi langi,
Machweo yana faraja,naweza tupa mtungi.
Hiyo naiona kwangu,kilimani na ziwani, Huwa wanisha uchungu,na kuzama fikirani,
Nitazamapo mawingu,nachora mengi
kichwani,
Machweo yana faraja,naweza achwa njiani.

Sijui ina nguvu gani, hadi yateka akili,
Baridi na siioni,kisa kijua cha mbali,
Naweza kuona soni,mawio kutoyajali,
Mawio yana faraja,naweza kuwaza mbali.

Kelele za ndege wema,waimba kwa nyingi
tambo,
Hunifanya kusimama,wakaniacha kitambo,
Nawaza na mengi mema,na kuyatupa ya
shombo,
Machweo yana faraja,naweza kuzotamba
tambo.

Mawio sitoyatenga,kwani huleta machweo,
Ndio mwanzo wa kujenga,huwezi weka uzio,
Huwezi kamwe yafunga,na kusubiri machweo,
Machweo yana faraja, nayaheshimu mawio.
★★★★

0 comments:

Post a Comment