Tuesday, 29 July 2014

SIKU NAJA DUNIANI


NIKIKUMBUKA NAZIDI KUMPENDA
Na Moringe Mhagama
Zilikuwa zimepita wiki mbili tangu mwanamke mmoja arudishwe kutoka hospitalini ambako licha ya vipimo na dawa mbalimbali za kunywa,sindano na hata za kuchua hakupata afuheni ya ugonjwa alikuwa nao.Wanawe pamoja na mumewe waliamua kumpeleka katika kitongoji cha KILIMUSI eneo ambalo yeye na mumewe waliamua kupafanya nyumbani kwao licha ya nyumba walizokuwa nazo katika vijiji vingine
Wakati mwanamke huyo ambaye tabia ya kumwita kila aliyemwona MWANANGU bila ya kujali umri wake ilimfanya hata wajukuu zake na hata wakubwa wenzake kumwita mama akigalagala kwenye godoro kuukuu pale sebuleni, nje yake kulikuwepo na mwanamke mwingine ambaye naye alihangaika juu ya kipande cha mkeka akiota jua la asubuhi.Sauti yake ya upole uliochanganyika na uoga iliuliza swali moja kwa kila aliyemhisi kuwa alitokea pale sebuleni."kaka mama anaendeleaje?"aliuliza yule mwanamke wa pale nje ambaye haikuhitajika elimu ya uuguzi kujua kama alikuwa mjamzito labda kwa sisi wa enzi hizooo ambao bado tunaamini watoto hununuliwa."Hivi hivi tuombe tuu Mungu"Alijibu yule baba akionekana kukata kabisa tamaa. "Mhhh,,"aliguna yule mwanamke akimtazama usoni kaka yake mwingine ambaye alikuwa ametoka tu kufika kumwangalia mama yake lakini hali aliyokutana nayo ndani kama si kujilazimisha kujikaza kiume angeweza kulia kwa sauti.
Kiukweli hali ya mgonjwa aliyekuwa akijaribu kupambana na mauti ilimkatisha tamaa kila aliyemwona.Hakuna hata mmoja kati ya wengi waliokuwa pale kuwaza kitu kimoja tuu MSIBA wa mama ,mama ambaye watoto wake wengi na wajukuu walikuwa wakimkimbiamara tu muda wa kusali rozali ukifika kutokana na tabia yake ya kumlaazimishakuu walikuwa wakimkimbiamara tu muda wa kusali rozali ukifika kutokana na tabia yake ya kumlazimisha kila aliyekuwa jirani yake kujumuika naye kusali.Sala ndicho kitu alichokipenda huenda kupita vitu vingine japo uvivu na utoto wa wanae ndivyo vilivyowafanya wamkimbie na kumwona kama msumbufu.
''Jamani mama ameongea! Anamwita dada Kalista"ilikuwa ni sauti ambayo kwa kila aliyeisikia hakuhitaji utambulisho wa mhusika wake,Mtoto wa mwisho wa yule mama ambaye wakati wote alikuwa pembeni ya mama yake akimtaka apone huku kilio chake kikiwafanya wengi waliomwona akihangaika kumlazimisha mama yake aongee washindwe kuvumilia na waishie kutoka nje huku macho yao yakishindwa kuficha kilichokuwa moyoni mwao.
"Wanini na we Thelesia, dada yako si anaumwa halafu unampigia kelele?"Aliongea Lusida mtoto wa kwanza wa yule mama ambaye alisutwa na sauti ya mama yake ikimwita Kalista na kuwafanya wote walioisikia wakimbilie pale sebuleni wakimwangalia yule mama ambaye yeyote ambaye angefika muda ule asingeamini kama mgonjwa yule ndiye aluyesikia habari zake kuwa alisubiri tu Israel mtoa roho ampitie.
"Si nimemwita kalista nyie mnafuata nini?"aliongea yule mama akimalizis na kicheko na kumfanya mumewe awaamuru wengine kutoka kwa ishara.
"Na wewe mbona unaelekeza tuu wenzako?, basi we mume wangu ubaki" sauti yenye tumaini ilisikika kutoka kinywani mwa yule mama na kuwafanya wengine kucheka huku wakitoka pale nje.
"Niambie na mimi nitoke pengine mna siri zenu"aliongea mumewe skitishia kutoka lakini aliishia mlangoni ambapo alifunga mlango na kuketi kwenye kigoda kilichokuwa pembeni.
"Sawa mwanangu haa mume wangu"yule mama aliongea na kuziba mdomo kwa kiganja chake na kuwafanya waliokuwepo kucheka.
"Sawa mama nimekuelewa"alijibu yule baba na kupafanya pahala pale palipokuwa na huzuni muda mchache uliopita pawe pa furaha.
"Enhee mwezi wa ngapi mama?"aliuliza akimgeukia Kalista ambaye mwonekano wake ulionesha wazi alikuwa akiumia.
"Wa mwisho''alijibu kwa unyonge akikaa vyema.
"Huyo sasa ni wa kiume na utampa ng'ombe wangu mmoja, najua huamini hadi umuone maana nasikia mumeo amechachamaa anataka vidume kwani kama mahari za wale wawili zinatosha"baada kuongea maneno yale alianza kubadika na kupoteza nguvu zake alizokuwa nazo muda mchache uliopita.
"Mwanangu usiogope mtu akaribiaye kufa hupona kuaga, naona malaika wale wanakuja ,zingatia sal sa, ,sala mwanao wa kiume"Aliongea na kutulia kimya wakati huo Kalista naye alikuwa akilalamika maumivu makali hadi walipimtoa pale sebuleni kwa kumbeba na kumuingiza kwenye chumba kilichokuwa karibu.
Wakati mauti yakimshinda yule mama pale sebuleni mkunga wa jadi ambaye naye alikuwa mfiwa alikuwa akisaidia kuokoa maisha ya kiumbe ambacho leo hii kinatimiza miaka ishirini na mbili.******★******
MWISHO**--

Asanteni
Mungu,mama na baba,marafiki na maadui zangu wote bila kuisahau Tanzania,,,,,
NIMEMALIZA THELUTHI MOJA BADO MBILI ZA KUISHI WEWE JE?******★★★★
"

0 comments:

Post a Comment