Tuesday, 29 July 2014

SHAIRI;MAMA YANGU VUMILIA

MAMA YANGU VUMILIA
Nilijua simulizi,haziwezi kutokea,
Wakuota hao wezi,leo ninashuhudia,
Kuvumilia siwezi,mama namsaidia,
Mama yangu vumilia,mola yupo hakutupi.

Baba alipofariki,najaribu kukumbuka,
Hakupigwa na mkuki,mafua yalimshika,
Namengine sikumbuki,najua wayakumbuka,
Mama yangu vumilia,mola yupo hakutupi.


Maneno waliongea,kuwa wewe wahusika,
Kila mara nasikia,eti mali wazitaka,
Ila ninavyokujua,mamangu hukuhusika,
Mama yangu vumilia,mola yupo hakutupi.

Shangazi kakuvamia,wale ng'ombe eti wake,
Shemejio nasikia,eti wewe wake mke,
Leo umetimuliwa,nyumba baba sio yake,
Mama yangu vumilia,mola yupo hakutupi.

Leo eti tumepanga ,ziko wapi zile hati,
Wanakutishia panga,eti mali huzipati,
Wifi zako wanachonga,eti upige magoti,
Mama yangu vumilia,mola yupo hakutupi.

Mie darasa la tano,mama naona wateswa,
Siji kwenye mikutano,juzi nilikoswa koswa,
Wanitishia sindano,nile vilivyotokoswa,
Mama yangu vumilia,mola yupo hakutupi.

MOLA AWAPIGANIA,MSICHOKE KUMWABIA

0 comments:

Post a Comment