Tuesday, 19 May 2015

SHAIRI;KAPIKA KAHAWA MBICHI

Habarini ndugu zangu,poleni na kazi zenu,
Natoa shairi langu,kichwa nasubiri kwenu,
Kipaji kanipa mungu,namshukuru mwenzenu,
Tabia na sura mwanzo,mapishi nayo muhimu.

Ndoa safi mwapendana,chakula hakipiki mama,
Japo mwasaidiana,eti haki za wamama,
Mlo apike Diana,alokuja mwaka jana,
Tabia na sura mwanzo,mapishi nayo muhimu.

Kufua afua dada, mnamwita beki tatu,
Imekuwa kawaida,yeye atandike kwetu,
Badaye tupate shida,tukibaki peke yetu,
Tabia na sura mwanzo,mapishi nayo muhimu.

Chai huwezi kupika, tuagize hotelini,
Mdalasini kuweka,wakufundishe shuleni,
Jamani watatucheke,tukija pata wageni,
Tabia na sura mwanzo,mapishi nayo muhimu.

Mlenda nautamani, mama waniangalia,
Nitaingia jikoni,ndani umejilalia,
Hata tukiwa sokoni,vyote waniulizia,
Tabia na sura mwanzo,mapishi nayo muhimu.

Sikusomea shuleni, chai haitoki mbichi,
Sikubanduka jikoni,nikikaanga kabichi,
Leo hii sina soni,siwezi pika vibichi,
Tabia zako ni nzuri,mapishi sikugundua

0 comments:

Post a Comment