Monday, 25 May 2015

SHAIRI;MWANANGU LISHIKE NENO


Nimekuona ulivyo,usidhani sijajua,
Ubakie hivyo hivyo,hadi unajifungua,
Siyo dhambi kuwa hivyo,ila dhambi kuitoa,
Mwanangu lishike hili,usifikiri kuua.

Najua unaumia,kuzaa bila ya ndoa,
Ila nachokwambia,dhambi kubwa kuitoa,
Kipi kinakuzuia,ukafikia kuua,
Mwanangu lishike hili,usifikiri kuua.

Si mkosi binti yangu,mola amekuteua,
Nawe upate uchungu,wa kuishi si kuua,
Pia mipango ya mungu,yeye yote atambimbua,
Mwanangu lishike hili,usifikiri kuua.

Baba yake akipenda,asipopenda tulia,
Kama kweli hajapenda, acha kumsumbukia,
Sasa wapi unaenda,usijaribu kuua,
Mwanangu lishike hili,usijaribu kuua.

Alee asimlee,wewe jali apumua,
Acha yeye angojee,mwana wako atakua,
Mola usimkosee,kaja waza kumuua,
Mwanangu lishike hili,usifikiri kuua.

Kwa nini sasa utoe,mwanangu sasa waua,
Penzi lisikuzuzue,mwanao ukamuua,
Umri namba ujue,ogopa sana kuua,
Wanangu lishike hili,usifikiri kuua.

Kuna watu wanalia,wanalilia watoto,
Mola hakuwapatia,ndoa zinawaka moto,
Sasa nini kuitoa,mwana wausaka moto,
Mwanangu lishike hili,usifikiri kuua.

Mwisho mwana utambue,na mimba usiitoe,
Huyo mwana usimwue,pesa zisikusumbue,
Hivi mie nikutoe,ungekuwa wapi wewe,
Mwanangu kuuua dhambi,usitoe hiyo mimba.

0 comments:

Post a Comment