Sunday, 17 May 2015

SOTE TUSEME BASIKemeeni kwa kusudi,hili janga halifai,
Kuomba hamna budi,sio kila siku bai,
Nyingine za maksudi,kuuwa hawashangai,
Sote tuseme hapana,ajali si haki yetu.


Musoma watu walia,ndugu wametangulia,
Myoyo haijatulia,Kihonda tukasikia,
Tanga nako yatokea,lakini pia Songea,
Wote tuseme hapana,ajali si haki yetu.

Magari na bodaboda,zinaongoza kuua,
Ya ndani ama ya boda,kama wanayatungua,
Hatuhitaji misada ila ni kujitambua,
Sote tuseme hapana,ajali si haki yetu.

Mbio kama mashindano,eti tuwahi kufika,
Twafa kama mapigano,basi linapopinduka,
Sasa sote tuseme no,kuzikana tumechoka,
Sote tuseme hapana,ajali si haki yetu.

Gari limejaa watu,laendeshwa na mlevi,
Dereva kalewa topu,konda ameweka movi,
Trafiki hela ya supu,na pombe ka mlevi,
Sote tuseme hapana,ajali si haki yetu.

Hivi ninyi madereva,kweli hamna uchungu,
Trafiki hasemi ova,na hana hofu ya mungu,
Atafanya nini kova,ama awapige pingu.
Sote tuseme hapana, ajali si haki yetu.

Sasa wapo mambulula,kipata picha ni kero,
Yani kwao halahala,zipo kwenye mitandao,
Tarusha kila pahala,kama vumbi la ugoro,
Sote tuseme hapana,ajali si haki yetu.

Naandika nikilia,Tanzania panatisha,
Msingi kujitambua,haya mambo yataisha,
Sasa ona wamemwua,yule nilompa posa,
Sote tuseme hapana,ajali si haki yetu

Eti nini makafara,uzembe mwautetea,
Mnazidi kunikera,lawama mwazikimbia,
Leo naiweka sera,ajali kuikataa,
Sote tuseme hapana,ajali si haki yetu.

Ajali si haki yetu,wala siyo laana,
Bali ni uzembe wetu,twajikuta twauana,
Kipinga kwa guvu zetu,na kumwomba labana,
Sote tuseme hapana,ajali si haki yetu.

Leo ninatamatisha,ujumbe ushike sana,
Kapoteza na maisha,tulopanga kuoana,
Tukicheza tutaisha,utumwa urudi tena,
Mola zipokee roho,zilotoka ajalini.

0 comments:

Post a Comment