Tuesday, 19 January 2016

RIWAYA ; NITAKUUA KWA MKONO WANGU

MTUNZI; Moringe Mhagama
MWANZO
Ukimya ulitawala ndani ya ukumbi wa Msarikie uliopo ndani ya Chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph huku karatasi zikifunuliwa na kufunikwa wa utaratibu ili kuzuia bugdha kwa yeyote aliyekuwemo ndani ya ukumbi ule.Hali ilikuwa hivyo karibu kwa kila darasa chuoni pale na hakuna aliyeshangaa kwani zilikuwa zimebaki siku tatu tuu kabla ya kufanyika kwa mitihani ya kumaliza mhula wa kwanza (First semester University Examination). Hivyo ukimya huo uliashiria kuwa kila mtu alidhamiria kufanya vizuri kwenye mitihani hiyo iliyokuwa mbele yake.


Lakini kama kawaida palipo na wengi pana mengi, licha ya watu wengi kutingwa na maandalizi ya mwisho ya mitihani iliyokuwa mbele yao, kuna wanafunzi waliokuwa kama hawana habari kabisa na mitihani hiyo. Kwani walionekana wamekaa kwenye makundi ya watu wawili wawili wa jinsi tofauti na bila ya kuelezwa lazima ujue kuwa yalikuwa ni makundi ya wapenzi.
Wengine walikuwa hosteli wakipiga soga huku wakiangalia filamu na kuonekana kero kwa wenzao waliamua kusomea vyumbani badala ya darasani.Wengine hawakuwepo kabisa ndani ya chuo huku wakihangaika na kutafuta usafiri wa kuwapeleka mjini kulikokuwa na onesho la wasanii fulani waliokuwa na ziara ya kimuziki Mkoani Kilimanjaro.
Wale waliokuwa wamepanga mitaani walionekana kuwa harakati tofauti kwani wapo waliokuwa wanajisomea vyumbani na wengine kama ilivyokuwa ndani ya hosteli za ndani ya chuo walionekana kufurahia mapumziko ya mwisho wa wiki ambao ulikuwa na sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo wasanii wengi waliamua kufanya ziara mikoani.Wengine walikuwa wakiangalia filamu kwa makundi huku wengine wakiwa wamekaa mmmoja mmoja chumbani akijisomea na kuna wale waliokuwa na ama wake na waume zao au wapenzi wao wakifurahia mwisho wa wiki ile.
Wakati hayo yakiendelea usiku huo wanachuo wawili Alice na Raheem ambao bila kuelezwa ungejua kuwa walikuwa ni wapenzi walionekana wakiwa na furaha wakielekea chuoni walikopanga kwenda kujisomea kama walivyofanya wanachuo wengine nao waliamua kwenda kusomea kwenye ukumbi wa Msarikie .Waliamua kukaa kwenye viti vya nyuma kabisa ya ukumbi ule.
Dakika mbili tangu waingie simu ya Alice iliita kwa sauti iliyoonekana kuwakera wanafunzi wengine na kuwafanya wageukie upande aliokuwa amekaa.Wa kusonya walisonya, wakutukana kimya kimya ama kwa sauti ya kunong’ona walifanya hivyo huku wengine wakikunja sura zao kwa hasira.
Kitu kilichomshangaza Raheem ni kutoipokea na kuikata kisha kusonya kwa sauti iliyosikika mbali kidogo.Dakika moja baadaye ile simu iliita na kama awali aliikata na kuizima simu yake jambo ambalo lilionekana kumtia mashaka mpenzi wake.
‘’Si uipokee uongee naye ‘’Alishauri Raheem.
‘’Wa nini msumbufu tuu huyu’’Aliongea Alice akionekana kweli alikuwa amechukizwa na ile simu iliyokuwa imepigwa.
‘’Ongea naye au kwa sababu upo na mimi ?”Aliongea Raheem akioneosha wivu wake wazi wazi.
‘’Hapana love halafu ni namba ngeni inanisumbua sana’’Alijibu Alice akideka kwa mpenzi wake.
‘’Namba ngeni , si inaishia na kumi na saba?’’Alihoji Raheem.
‘’Hata siikumbuki love’’Aliendelea kudeka Alice.
‘’Kwa taarifa yako hiyo namba naifahamu na inaonekana mnapigiana sana’’Raheem aliongea kwa ghadhabu na kuwafanya wanafunzi wengine waliokuwa wamekaa karibu yao kuanza kuusikiliza mzozo ule.
‘’Hapana mpenzi labda umeichanganya hii ni mpya na huyu mtu ananisumbua sana’’Alice aliongea kwa masikitiko.
‘’Usinifanye mtoto hembu lete hiyo simu tumpigie huyo mwanaume wako unayejitia humfahamu’’Raheem aliongea kwa ghadhabu bila kujali uwa sauti yake ilisikika kwa wengi mle ukumbini.
Alice alimpa simu huku akiwa na uhakika kabisa na alichokuwa akikiongea akijiuliza sababu ya mpenzi wake kumfikiria vile.Alimpenda sana Raheem, na hakutaka kumpoteza hata kwa dakika moja.Alimwona kama mwanaume wa pekee ambaye alikuwa chaguo lake akijilaumu kuchelewa kumjua akijiona kuwa alikopita kabla ya kuwa naye alikuwa ameteleza haswa.
‘’We hii si ile namba yangu ya Zantel?’’Raheem aliuliza akiwa amehamaki.
‘’Namba yako ya Zantel?’’Alice aliuliza.
‘’Ndiyo hii namba simu ninaitumia kwenye Moderm tuu na sijawahi kupigia’’Raheem alieleza.
‘’Labda kama umechanganya , lakini hii namba huwa inanisumbua kweli’’aliongea Alice.
‘’Hii namba,,,hiii namba niliitumia,,, ngoja nitakuambia siku nyingine mpenzi’’Raheem aliamua kubadili mada.
‘’Niambie bwana au una kitu unakificha Raheem?’’ Alice alijikuta akimwita mpezi wake kwa jina lake kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu sana cha kuitana love,baby, sweety, honey mpenzi na majina mengine mengi jambo ambalo kwa Raheem alijua kabisa kuna kitu kilichokuiwa kikiendelea.
‘’Umesema?’’Raheem alijifanya kuuliza .
‘’Kuna kitu unanificha Raheem, ndo maana nilikuambia nakuchukia sana kwa tabia yako ya kunificha ficha , kama hutaki kuniambia NIACHE NIMESEMA NIACHE RAHEEM endelea na usiri wako najua yupo mtu umpendaye zaidi yangu na huwa unamwambia mambo yako si mimi Raheem , Raheem nimekukosea nini lakini mwenyewe unajua kuwa ulimyang’anya mtu penzi lake na aliumia na anaumia kwa sababu alidhurumiwa haki yake , bora ningempenda yeye hakunikosea nikamwacha bila sababu, NAJUTA RAHEEM ‘’Alice aliongea huku machozi yakitoka , wambea hawakuwa mbali kusikiliza makasa ule licha ya kujifanya kuwa walikuwa bize na kujisomea.
‘’Unasema?’’Aliuliza Raheem kwa hamaki.
‘’Niache, nimekukosea nini hadi unaamua kunificha mambo yako?’’Alice alizidi kulalama.
‘’Sema kama ulipanga uniache nimekuficha nini kikubwa hadi ufikie hatua hii jamani? Kweli nimeamini kuwa wanawake si watu’’Raheem alilalamika.
‘’Ndiyo niache wanawake sio watu ,watu hao wapenzi wako’’Sauti ya Alice sasa ilifika mbali huku wanafunzi wengi wakionekana kukerwa na kelele zao na wengine walitoka ukumbini waliokuwa wamevutiwa na mzozo walisogea na kutega masikio yao vyema na wale waliokuwa mbali walijisogeza kujua kulikoni lakini waliokuwa wamekaaa mbele kabisa ya ukumbi hawakuwa na hili wala lile.
‘’Nakuhakikishia Alice NAKUUA KWA MKONO WANGU na huyo MALAYA WAKO NITAMPATA’’Raheem aliongea na wakati huo huo Alice aliinuka na kuelekea chooni akimwacha Raheem akianza kuona aibu baada ya kugundua kuwa watu wengi walikuwa wakiufuatilia mzozo wao ikizingatiwa kuwa alikuwa ametambulisha mapenzi yake kwa watu wengi sana chuoni kupitia kipaji chake cha kuchora alichokuwa nacho.Ilikuwa kawaida kwa wapenzi hao kuvaa nguo zilizokuwa na picha yao wakiwa wameshikana mikono.
Japokuwa wengi walijua ni namna ya kukitangaza kipaji chake na biashara yake ya fulana lakini kwao ilikuwa ni kuwakomesha wapenzi wao wa zamani ambao kiukweli bado walikuwa na mapenzi nao hadi kipindi hicho lakini bila sababu mapenzi yao yalikuwa yakilazimishwa kufa.
Dakika tano baada ya Alice kuelekea chooni mita thelathini kutoka ukumbi huo simu ya Alice iliita na namba iliyopigwa ni ile ilee ambayo Raheem alikuwa na uhakika kuwa ilikuwa ni namba yake ya Zantel.
‘’Hallow, nani,,,,upo na mke wangu chooni? Mnafanya nini? Nini,,,,. Nawaua wote Malaya wakubwa nini msokuwa na haya kunisaliti mita chache mbele yangu’’sauti ya Raheem ilipaa karibu ukumbi mzima.
Kwa kasi ya ajabu Raheem alitoka kuelekea chooni na bila hata kufikiria dakika moja ilitimia akiwa ndani ya vyoo vya kike lakini alichokutana nacho kilimfanya apigwe na butwaa.
Aliukuta mwili wa Alice ukiwa sakafuni huku damu ikichafua sakafu ya choo kile ikitokea shingoni.
‘’Alice , mke wangu nani kakufanya hivi?’’ Raheem alilalamika kwa sauti kubwa bila kujali kuwa alikuwa kwenye vyoo vya wanawake.
‘’Alice! Alice! Amka mke wangu mpenzi’’Aliongea Raheem kwa uchungu mkubwa na kuwafanya wasichana waliokuwa wakielekea kwe ye vile vyoo wabadili njia na kwenda kutumia vyoo vilivyokuwa kwenye majengo mengine kwa kuhisi mwanaume aliyekuwa humo ndani alikosea choo na kuingia huo na alikuwa akiongea simuni.
Hadi dakika kumi zinapita Raheem alikuwa bado akiwa ameukumbatia mwili wa Alice uliokuwa umeshaanza kupata ubaridi kama ishara ya uhai wake kupotea.Akili yake ni kama iligoma kufikiria zaidi ya kumfanya alie na kulalamika pale chini badala ya kufikiria juu ya aliyefanya yale mauaji.
Ingawa kweli alikuwa ametoka kukorofishana na Alice na kumtishia kumuua lakini hakuwa tayari kwa tukio lile la kuondokewa na msichana huyo mrembo ambaye alikuwa ameuteka moyo wake na hata kukorofishana naye kulitokana na wivu wake kwake.
Baada ya kilio cha kwikwi na maumivu yaliyoigandisha akili yake Raheem alitoka pale chini na kuanza kuchunguza eneo lile na kukiona kisu kilichokuwa na damu zilizokuwa zimeanza kuganda.Bila kutafakari alikishika kile kisu na kuifuta ile damu na hapo akili yake ni kama ilifikiri zaidi kidogo na kuanza kutoka nje ya kile choo huku akiwa amefura kwa hasira kisu mkononi akiwa na wazo moja tuu la kwenda kumtafuta aliyekuwa amefanya yale mauaji ya msichana aliyekuwa akimpenda kwa dhati.
Alipofika nje ya kile choo kajiuliza kwa nini watu walikuwa hawaingii kwenye kile choo akakutana na karatasi iliyokuwa imebandikwa kwenye mlango mkubwa wa kuingilia pale chooni ikiwa imeandikwa kwa maandishi meusi yaliyochapwa USIINGIE VYOO VINATENGENEZWA.Hapo Raheem aligundua sababu ya watukuingia kule chooni lakini akajiuliza matengenezo gani ya usiku ule lakini alijua ile ilikuwa ni hila za muuaji kutaka kufanikisha mauaji yake bila bughudha lakini pia akajiuliza kwa nini kama karatasi ile ilikuwepo pale kwa nini Alice aliingia mle ndani au ndiyo ilikuwa njia waliyoipanga Alice na huyo mtu ili wafanye mapenzi chooni bila bugudha kutoka kwa watumiaji wa choo usiku ule.Wakati huo Raheem alikuwa akifikiria hayo na karatasi aliyokuwa ameibandua pale mlangoni mkono mmoja na mkono mwingine akiwa ameshika kile kisu chenye damu iliyokuwa imegandiana akirandaranda kwenye yale maeneo ya chuoni bila uelekeo maalum.
Wazo la kuwa Alice alikuwa ameenda kumsaliti kisha akauawa lilikuja kichwani mwake huku akishindwa kuunganisha matukio yale vizuri kwani alishindwa kuelewa kama aliyekuwa amemuua alikuwa amefanya naye mapenzi kabla ya kufanya mauaji hayo ama kulikuwa na mtu mwingine alimuua baada ya kumkuta akifanya mapenzi mle chooni na huyo mtu ndiye aliyekuwa akimpigia simu.
Alifikiri huenda Alice alikuwa na wanaume wengi zaidi yake na mmoja kati ya hao wanaume ndiye aliyefanya yale mauaji baada ya kumkuta akifanya mapenzi mle ndani lakini mapenzi kwa dakika zile chache hakuwa na hakika kama kweli mpenzi wake alikuwa amefanya mapenzi na kujikuta akichukua uamuzi wa kwenda kuuchunguza mwili wa Alice kama kweli alikuwa ametoka kufanya mapenzi.
Kwa mwendo wa haraka na wa shari alirudi kule chooni kuthibitisha alichokuwa akikiwaza , lakini kabla ya kufika chooni aliwapita wasichana waliokuwa wakielekea kwenye vile vyoo na ule mwonekano wake uliwaogofya wale wasichana na kuwafanya wapige kelele na kukimbia huku hako wengine wakianguka na wengine wakirudi darasani.Kelele zile ziliwashtua watu wengi hadi walinzi waliokuwa getini na maktaba ambao waliamua kwenda kuangalia kilichosababisha kelele zile.Njiani walikutana na Raheem aliyekuwa akijaribu kutoka kwani alishajiona akiingia matatizoni , jambo la kwanza walilolifanya ni kumkamata na kumweka chini ya ulinzi na kuanza kumuuliza sababu za kuwa katika hali ile.
Wakati wale walinzi wakiendelea kumuuliza maswali walikatishwa na kelele za vilio vya wanafunzi hasa wa kike zilizosikika kutokea chooni na kuwafanya walinzi wajigawe wengine wakiendelea kumshikilia Raheem wengine wakaelekea huko zilikosikika kelele.Hakika ilikuwa taharuki kwani baada ya kuuona mwili wa Alice ukiwa na damu kule chooni wanachuo wa kwanza kuuona waliwaita wenzao walikuwa darasani na kusababisha kundi kuwa la wanachuo kukusanyika nje ya vyoo vile huku kila mmoja akiogopa kuukaribia ule mwili na kubaki wakiongea hili na lile hasa wale waliokuwa wakisomea kwenye darsa alimokuwa Alice na mpenziwe Raheem.
‘’Wamegombana sana na Raheem darasani’’Aliongea msichana mmoja akiwa haamini alichokuwa amekiona.
‘’Nani Raheem! Atakuwa kamuua maana kakamatwa akiwa na kisu chenye damu akitokea huko chooni’’Alidakia mwingine.
‘’We! Kweli maana kule darasani aliapa kuwa angemuua kwa mkono wake’’Alichangia mwanafunzi mwingine ambaye alipomaliza kauli yake tuu alishikwa mkono na mmoja wa walinzi waliokuwa pale kujua kilichosababisha vilio na mkusanyiko ule kisha kuondoka naye kuelekea zilipokuwa ofisi za walinzi.
Alikuwa Mlinzi Jonathan , mlinzi aliyesifika kwa kuwa na ukaribu sana na wanachuo hali iliyowafanya wenzake wamchukie wakihisi kuna kitu haramu kilichokuwa kikiendelea kati yake na wanafunzi kwani walinzi wengi waliamini kutozoena na wtu ilikuwa ni ishara ya ufanyakazi bora na umakini.Jonathan hakuingia mle chooni kuangalia maiti zaidi ya kukaa pale nje akisikilizia taarifa za watu wakiwa kwenye hali ya mshtuko aliamini angepata pa kuanzia upelelezi wake juu ya tukio hilo na alifanikiwa kupata maneno aliyokuwa akiyataka na akaondoka na aliyeyatoa ili akaelezwe vizuri.
Habari za Raheem kuhusika kwenye kile kifo zilisambaa kama moto wa kiangazi kwenye savanna na kuwafanya wengi kumchukia na kumwogopa Raheem aliyekuwa chini ya ulinzi wa polisi waliokuwa wamemshikilia wakati ule baada ya kupigiwa simu na wale walinzi.Wakati huo mlinzi Jonathan naye alikuwa kwenye kundi la walinzi waliokuwa chini ya ulinzi wa askari polisi kwani alikuwa miongoni mwa walinzi waliokuwa langoni hivyo walionekana kuwa wazembe na kuruhusu watu kuingia na kisu chuoni kitu ambacho hakikuruhusiwa na ndio maana kila aliyekuwa na begi alikaguliwa langoni wakati wakikagua vitambulisho.
Kila ambaye angekuwa hana kitambulisho alitakiwa kuwa na maelezo ama ruhusa ya maandishi ya kuingia pale na si vinginevyo pia ambaye angekuwa na vitu visivyoruhusiwa kama kisu hata kama ni mwanachuo asingeruhusiwa kuingia nacho hivyo kukamatwa kwa Raheem akiwa na kisu kuliwafanya walinzi wawe katika wakati mgumu zaidi.Raheem alihamishiwa kituoni akiwa pamoja na wale walinzi huku kampuni ya ulinzi iliyowaajiri akina Jonathan ikiwaleta walinzi wengine wengi ambao walitapakaa kila mahali pale chuoni na kupoteza kabisa ule uhuru waliokuwa nao wanachuo hasa waliokuwa wakikaa hostel za ndani ya chuo.
Kwa upande wa wanachuo waliokuwa , chuoni ama wale waliokuwa mtaani na kupata taarifa za kifo cha Alice amabaye ilishajulikana kuwa aliuawa na mpenzi wake hali haikuwa sawa kabisa , hakuna aliyepata hamu ya kujiandaa na mtihani tena kila mtu alionekana kuwaza na kusema lake aliloliona linafaa.Wengi walimlaumu Raheem kwa kukosa uvumilivu na kuendeshwa na hasira zaidi ya busara baada ya kuhisi kuwa alisalitiwa pia kulikuwepo na wale waliokuwa wakimlaumu Alice kwa usaliti licha ya kupendwa sana na Raheem ambaye alikuwa maarufu si tuu chuoni bali hata nje ya chuo kile na vyuo vingine Mkoani Kilimanjaro la Arushwa kwani kipaji chake cha uchoraji kilimtambulisha yeye na mpenzi wake.
Ndani ya kituo cha polisi ambako Raheem kama akili za kawaida zilimrudia akajikuta akilia tuu na kushindwa kujibu maswali aliyokuwa akiulizwa na askari na kujikuta akiambulia kipigo ambacho hakimuumiza kama kilivyomuumiza kifo cha mpenzi wake.Hakujua cha kufanya ili abadilishe kila kilichokuwa mbele yake kwani alijua hakuwa muuaji kama wengi walivyoamini. Lakini angesema nini wamuelewe?
Kisu anacho na kina damu ya marehemu, ndiye aliyesema mbele za watu kuwa angemuua pia hata namba aliyodai ilikuwa ikimpigia mpenzi wake ilikuwa ni namba yake ya simu na ilipofuatwa nyumbani kwake ilikutwa huko mbaya zaidi hata kile kisu ambacho alikuwa amekikuta chuoni alikuwa amekinunua mchana wa siku ile akiwa na lengo la kununua vitu vyake ili akakae peke yake ili afaidi mahusiano yake na Alice kwani kabla alikuwa akiishi na rafiki yake ambaye alikuwa kwenye msiba wa dada yake huko Newala.
Alijikuta hana cha kujibu zaidi ya kulia , kilio kilichomfanya aongezewe kipigo kutoka kwa askari na kumfanya apoteze fahamu.
Asubuhi ya siku iliyofuata ilimkuta Raheem akiwa amesharejewa na fahamu huku maswali mengi aliyokuwa akiulizwa jana yake yakijirudia akilini mwake na kumkumbusha uchungu mkubwa wa kumpoteza Alice msichana aliyempenda kwa dhati.Hakuwa na namna nyingine ya kujipooza na uchungu na maumivu makali ya kufiwa zaidi ya kulia, kilio cha kimya kimya ambacho nacho hakikuzuia sauti za kamasi kupandishwa na kuwashtua askari wa zamu amabao hawakujishughulisha naye tangu alipopoteza fahamu na kumfuata mahali alipowekwa.
‘’We muuaji kumbe umeshaamka, kikulizacho nini haswa na kuua umeua mwenyewe?’’Sauti ya askari ilimshtua Raheem.
‘’Naongea na wewe kikulizacho kipi?’’Aliendelea kumuuliza huku akimpiga piga na kichwani na kirungu kidogo cha mpigo mabegani na kumsababishia usumbufu na maumivu.
‘’Huyo mwanachuo aliyeuwa yuko hapa?’’Ilisikika sauti ya kishabiki kutoka nje na kumfanya Raheem apatwe na maumivu makali ya kuambiwa kuwa ameua wakati alijijua kuwa hakuwa muuaji na wala hakuwahi kuwaza kumuua mpenzi wake.
‘’Yupo huko ndani lakini hataki kujibu chochote’’ Alijibiwa yule muulizaji kisha sauti za viatu zilisikika zikielekea upande wa chumba kilichomhifadhi Raheem.
Sauti zile za viatu zilifika hadi ndani ya chumba alimokuwa amehifadhiwa Raheem kwa ajili ya mahojiano.Raheem aliinua uso wake na kumwangalia mtu aliyekuwa ameongezeka kwenye kile chumba cha mahojiano na baada ya kumwona alifarijika kwani licha ya kusikika akiongea kishabiki huko nje alionekna ni mtu mwenye sura ya upole na huruma sana.Moyoni aliamini huenda ule ulikuwa mwisho wa mateso yale aliyokuwa akipewa pale.
Yule askari aliyekuwa akimuuliza maswali alipiga saluti kisha akatoka na kuwaacha wawili yaani Raheem na Yule askari aliyekuwa ameingia pale lakini hakuwa na sare ila kwa ile saluti alijua kabisa Yule alikuwa ni Askari tena mwenye cheo kikubwa zaidi ya Yule aliyekuwa akimuuliza maswali kadhaa ambayo hakuyajibu.
‘’Pole sana kijana’’aliongea Yule askari akimsogezea kitiRaheem na kumwinua kisha kumkalisha kitini.
‘’Asante sana mkuu’’Raheem alijibu kinyonge.
Kwa hiyo ulilala humu?’’ Aliuliza Yule askari kwa sauti ya upole.
‘’Ndiyo nililazwa humu ndani wakinihoji maswali niyoyajua majibu yake’’ Raheem alitoa jibu lilokuwa na tuhuma ndani juu ya wale askari waliokuwa wakimpa adhabu kucha ili atoe maelezo ya kifo kile kwa kigezo cha kutafuta ushahidi.
‘’Dah! Pole sana lakini ni kweli ulimuua Alice?’’Yule askari aliuliza kwa sauti ya upole.
‘’Afande , sijaua na wala simjui muuaji na naomba mnisaidie kumkamata muuaji’’Raheem aliongea kwa hisia huku akionekana kuguswa sana kifo cha mpenzi wake.
‘’Kama hujaua unadhani nani atakuwa ameua Raheem?’’
‘’Sijui Afande’’
‘’Hujui vipi wakati umekutwa eneo la tukio ukiwa na kisu kilichotumika kwenye mauaji?’’
Afande kile kisu nilikishika kimakosa baada ya kuona mpenzi wangu ameuawa’’
‘’Ila mbona inasemekana hata kile kisu ulikuwa umetoka kukinunua mchana?’’ Yule askari alizidi kumuuliza Raheem maswali ambayo aliona kama yanazidi kumtumbukiza shimoni kwani kujulikana kwa habari za kile kisu kulimfanya aamini kuwa polisi walikuwa wamejua mengi sana kwa muda mfupi tena waliyoyajua yalikuwa hayamtoi hatiani hata kidogo.
’’Hapana visu hufanana’’Raheem aliamua kujitoa hatiani kwa ushahidi wa kisu kile.
‘’Lakini ulikuwa umenunua kisu mchana wa jana?’’
‘’Ndiyo’’
‘’Kiko wapi kisu ulichokinunua?’’
‘’Kipo nyumbani’’
‘’ Una uhakika?’’
‘’Ndiyo’’
‘’Sawa lakini marehemu alionekana alikuwa amefanya mapenzi kabla ya kuuawa je unadhani ni nani alikuwa amefanya naye mapenzi’’Yule askari aliongea akimtazama bila kujua lile neno la kuwa alikuwa amefanya mapenzi kabla ya kuuawa lilimuumiza sana na kumchoma sana moyoni mwake kwani kujua kuwa mpenzi wake alikuwa amemsaliti kabla ya kuuawa lilikuwa ni pigo linguine katika moyo wake.
‘’Haiwezekani afande nimlifika pale chooni dakika moja baada ya Alice kuingia pale na nilimkuta kauawa hayo mapenzi walifanya muda gani?’’Raheem aliongea kwa ghadhabu huku akiw ana uchungu mkubwa.
‘’Kama ulifika dakika moja baada ya Marehemu kufika chooni we unadhani ni nani atakuwa amefanya naye mapenzi kisha kumuua?’’Aliuliza swali lililommaliza kabisa nguvu za kujitetea na akajikuta akibaki kimya akiwa hana cha kusema tena kwani alijua hakukuwa na njia nyingine ya kumtoa kwenye ile kesi zaidi ya mapenzi ya Mungu.
‘’Nani atakuwa amemuua zadi yako?’’Yule askari aliongea akiwa amemsogelea Raheem akiweka mikono yake juu ya meza ndogo iliyokuwa imewatenganisha, lakini hakupata jibu zaidi ya kutazamwa na macho yalionekana kama yalikosa uhai , yakitazama lakini hayaoni.
‘’Wewe sema nani amemuua Alice?’’Askari aliendelea kumsonga Raheem kwa maswali safari hii akimkwida shati lake na kulikusanyia shingoni lakini Raheem aliendelea kumkazia macho yake yaliyoonekana kama hayana uhai tena mbona imetulia tuli mithili ya macho ya kwenye picha ya kuchorwa.
‘’Nani kamuua Alice ? sema!’’ Yule askari alizidi kumbughudhi Raheem aliyeonekana kama sanamu kwani licha ya kupokea makofi kadhaa alibaki amemtumbulia macho askari aliyekuwa akimhoji.
Kilichofuata ni maumivu makali ya mwili yaliyotokana na kupigwa shoti ya umeme , kutishiwa kuchomolewa kucha kwa kuzivuta kwa milimita kadhaa , kubanwa kwa korodani na koleo na mateso mengine mengi ambayo yalimfanya Raheem apoteze fahamu kupata majeraha mengi sana mwilini yalimfanya apoteze damu nyingi na afya yake kuwa ovyo.Lakini licha ya yote Rahem alibaki akiwatumbulia macho waliokuwa wakimpa mateso hayo bila kusema chochote hadi pale alipooteza fahamu.
Fahamu ziliporejea alijikuta kwenye chumba kingine kilichokuwa na giza sana alijitahidi kufumbua macho yake lakini kama yaligoma kumwonesha kitu kilichokuwa mbele yake. Kwa mara ya kwanza alihisi kupata maumivu katika kila sehemu ya mwili wake , kwa shida alisikia sauti za wtu wakiongea lakini hakusikia kilichoongelewa. Alijitahidi kutumia nguvu nyingi ili asikie kilichokuwa kikiongelewa lakini badala ya kusikia sauti alijikuta akisiaka maumivu makali mwilini mwake.Hakuacha kufikirisha ubongo wake na kutumia nguvu nyingi asikie kilichokuwa kikisemwa hakusikia chochote hadi pale aliposikia jina lake likiitwa kwa mbali.
Sauti ya kuitwa jina lake alizidi kuisikia safari hii ikiwa kama na mwangwi na kumfanya azidi kupata taabu ya kugundua ilikuwa ni sauti ya nani.Kama alikumbuka sauti ile,kumbukumbu zilikuja na kupotea, aliisikia wapi, lini sauti ya nani ? baadaye alijikuta akianza upya kukumbuka kwani alioneka kusahau tena ile ilikuwa sauti ya nani hadi pale alipojikuta akibebwa juu juu na kutupwa upande wa pili.
Raheem alijitahidi kufumbua macho lakini hakuona vizuri kwani alikuwa akiona vitu vikiwa kwenye maumbo yaliyomtisha.Kama ni mtu basi alimwona akiwa mrefu ana na umbo la ajabu na kila kilichokuwa kikiongelewa alikisikia kama mwangwi , aliona mkono wake ukishikwa na kufungwa kwenye chuma kisha sauti ya kuondolewa gari aliiskia safari hii tofauti na ilivyo kawaida sauti ya gari ilikuwa inakera sana na ya kutisha.Baadaye alijiona akifunguliwa na kuwekwa juu ya kitu kingine kisha akiwaona watu wannne wakisukuma na kuvuta kile kitu alichokuwa amekilalia.
Hapo akajua alipokuwa.
‘’Hospitalini’’alijikuta akiongea kwa mara ya kwanza.
‘’Ndiyo we ulijua upo wapi?’’ Aliisikia vizuri sautiiliyomjibu kwa karaha.
‘’Kwani naumwa?’’ Aliuliza akiwa kama amechanganyikiwa kwani hakujijua kabisa kama alikuwa mgonjwa.
‘’Huumwi, we unafikiri ni wakati wa kukutibu we muuaji, unatakiwa ufe kwa mateso kuliko uliyemuua’’Sauti ya Daktari ilisikika na kumkumbusha Raheem maumivu ya kufiwa na Alice mpenzi wake aliyempenda kwa dhati kwani alikuwa kama amechanganyikiwa na kusahau kama kilichomfanya awe kwenye hali ile ni kifo cha mpenzi wake.Kifo kilichosababishwa na mtu aliyeamua kumuua na kutengeneza mazingira yalioyomwonesha yeye kama muuaji.
‘’Kama siumwi kwa nini mmenileta hapa?’’ Raheem aliuliza kwa sauti ya upole iliyobeba hasira kubwa.
‘’Umeletwa hapa kwa uchunguzi wa mwisho kwa ajili ya kusomewa shtaka la mauaji’’
‘’Mauaji?’’
‘’Ndiyo umesahahau kuwa umemuua Alice au huko mahabusu ulikoenda kumekusahaulisha kila kitu?’’ Aliuliza daktari kwa mtindo wa kumwachia swali Raheem ambaye kwa mara ya kwanza aitambua kuwa alikuwa amehamishwa kutoka kituo cha polisi hadi mahabusu.
‘’Kwa hiyo nimeletwa hapa ili iweje?’’
‘’Tunakuja kupima vinasaba vyako (DNA) kama vinalingana na manii yaliyokutwa kwenye mwili wa marehemu kwa alionekana kuwa alikuwa amefanya mapenzi dakika chache kabla ya kifo chake’’
‘’Manii, kwa hiyo muuaji alimbaka Alice wangu?’’Raheem alipaza sauti na kumfanya Yule daktari kutoongea naye tena zaidi ya kumchoma sindano na kuchukua damu kiasi kisha kumchoma sindano nyingine kwa ajili ya kutibu marejaha yaliyokuwa mwilini mwake.
‘’Damu hii itasema ukweli kama kuna muuaji mwingine zaidi ya Raheem’’Aliongea Yule daktari akimwonesha chupa iliyokuwa imejaa damu ya Raheem na kuondoka.
Mara aliingia askari aliyemfunga pingu na kusimama pembeni mwa kitanda na bunduki yake begani akimwangalia kwa macho ya hasira.Raheem alimtazama Yule asskari huku akifikiri mambo mengi sana yaliyomchanganya ikiwemo taarifa ya kuwa muuaji alifanya mapenzi na marehemu kabla ya kumuua.
Taarifa hiyo ilikuwa na pande mbili , upande wa kwanza ni tumaini la kuokolewa na majibu kwani alikuwa na uhakika kuwa alikuwa hajafanya mapenzi na Alice siku zote walizokuwa wakijiandaa na mitihani lakini kwa upande wa pili taarifa ile ilimuumiza kwani kitendo cha mtu aliyempenda kufanya mapenzi na mtu mwingine kwa hiari ama lazima kilimchoma na kumuumiza sana.Alijua kabisa kabla ya kuwa naye Alice alikuwa mpenzi wa mtu mwingine lakini baada ya kuwa naye hakutaka kabisa mtu mwingine ale tunda ambalo alijihakikishia kuwa lilikuwa ni mali yake peke yake.
Kwa mbali alianza kusikia jina lake likiitwa lakini hakuweza kujua ni nani aliyekuwa akimwita kwani hakusikia sauti ile iliyokuwa ikimwita.Sauti za kuitwa jina lake zilizidi kuongezeka kadiri muda ulivyosonga na kusikika vizuri kwenye masikio yake.Aligundua sauti zile zilisikika kutoka nje ya ile hospitali akaamua kumuuliza yule askari aliyekuwa akimlinda.
‘’Ni akina nani hao?’’
‘’Wanachuo wenzako wanaandamana kupinga kitendo cha kinyama ulichomfanyia mwenzao’’
‘’Ila sijaua jamani’’Alijibu lakini askari kwa tahadhari kubwa alimfungua pingu kutoka kweye nguzo moja ya kitanda na kumfunga mikononi mwake kisha kumwonesha kwa ishara aelekee dirishani awaangalie wanafunzi wenzake waliokuwa nje ya geti la hospitali, naye akafanya kama alivyoelekezwa.
Hakuamini macho yake baada ya kuona umati mkubwa wa wanatu ambao aligundua kuwa hawakutoka chuo kimoja bali vyuo karibu vyote vya Arusha na Kilimanjaro pia aliwaona wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari kutokana na sare zao lakini pia aliwaona wananchi wengine hasa wanawake waliokuwa wakilia huku wakiliimba jina la Alice kisha wakimuuta Raheem muuaji.
Alishindwa kujizuia kutoa machozi baada ya kugundua kuwa aliwatua wanafunzi wa vyuo vile kutokana na fulana walizokuwa wamezivaa kwani kila chuo walikuwa na rangi yake na mbaya zaidi yale mashati yalipambwa na picha yake nay a marehemu Alice fulana hizo ndizo zilizompa umaarufu awali kwali licha ya kutangaza kipaji chake pia vilitangaza mahusiano yake.Hakutaka kuamini kama umaarufu wake ulikuwa na upande wa pili wa maumivu kwani kwa haraka haraka alitambua uwepo wa wanafunzi kutoka Vyuo vya Ualimu Marangu,Pantandi, chuo kikuu cha Arusha, Makumira,Chuo cha Ushirika na Chuo alichokuwa akisoma cha Mtakatifu Joseph.
Aliwatazama watu wale kwa uchungu mkubwa ghafla alishangaa kila mtu akiangalia upande aliokuwa amesima huku waandishi wa habari waliokuwa kwenye jingo la ghorofa lililokuwa likitazamana na dirisha alilokuwa amesimama wakipicha picha nyingi hapo alijikuta kwenye hali mbaya zaidi ya uchungu.
Koo lake alihisi likikabwa na kitu kizito kwa ndani huku mapigo yake ya moyo yakienda kasi mikono ilitetemeka kwa uoga miguu yake nayo ilikosa nguvu ya kuendelea kusimama macho yalimtaka asitazame kilichokuwa kikitendeka nje ya geti la hospitali ile kwani kilimuumiza zaidi.Aliziona fulana zilizokuwa zimevaliwa na kundi kubwa lilikokuwa pale nje zimerundikwa katika makundi yasiyopungua kumi na tano na kuwangiwa mafuta kisha kuchomwa huku sauti zikitaja jina lake kuwa ni muuaji afe.
‘’Raheem afe ni muuaji asitibiwe’’Masikio yake yalifanya kazi na kumfanya azidi kukabwa na kile kitu shingoni akajikuta akipiga magoti pale dirishani huku akitazama kule nje kupitia dirisha la kile chumba kilichokuwa ghorofani upande wa getini na kumfanya aendelee kuona mambo yale ya kuumiza ambayo alijikuta akiendelea kuyatazama kwa uchungu mkubwa akisahau kabisa uwepo wa askari mwenye silaha nyuma yake.
Moshi uliotokana na kuchomwa zile fulana ulimzuia kuendelea kutazama fulana zilizokuwa na picha ya Alice iliyokuwa na maandishi makubwa RIP.
‘’Kwa hiyo wapo hapa tangu lini?’’ Alijiuliza kwa sauti bila kugundua.
‘’Walikuwa na wewe tangu kituoni wakachoma mashati yako, kule mahabusu pia na leo hii wamefanya hivi wakati wakisubiri ndugu wa marehemu waje kuuchukua huu mwili wakauzike’’Alijibiwa na yule askari ambaye hakuonekana kuficha chuki yake dhidi ya Raheem aliyemwona ni muuaji.
‘’Kwa hiyo mwili wa Alice upo hapa?’’Aliuliza Raheem safari hii swali alililenga kwa yule askari baada ya kuona uwezekano wa kupunguziwa maswali mengi yaliyokuwa kichwani mwake.
‘’Ndiyo na gari la kuuchukua mwili wake ndo lile linaingia’’Alijibu Yule askari aliangalia nje kupitia dirishani.
Raheem alisikia vilio vikiongezeka mara baada ya rafiki aliyekuwa akikaa naye akishuka garini, alikuwa ni Mathayo ambaye kabla ya kuwa naye alikuwa ni mpenzi wa Alice lakini kosa moja dogo lilimfanya ampoteze mrembo huyo na kuangukiamikononi mwake.
Alimhurumia Mathayo ambaye alikuwa akitoka kufiwa na dada yake wiki moja iliyopita na siku ile alikuja kweye msiba ambao ulimhusu sana hata kama hakuwa kwenye mahusiano naye lakini kutoka kijiji kimoja kulimfanya ahusike tena kwenye msiba ule.Mara alishtushwa na kelele za vilio vilivyoongezeka na kumfanya achungulie nje ambapo alishuhudia jeneza likiingizwa kwenye gari huku wengi wakilia wakimtaja Mathayo jambo lilimshtua na kujikuta akitazama kwa makini na alichokiona kilimshtua.
Alishtuka kuona mtu akiwa katika machela akiingizwa hospitalini, hapo ndipo akajua sababu ya watu kutaja jina la Mathayo wakilia wakiamini kuwa alikuwa amepatwa na jambo baya.Moja kwa moja akili yake ilimtuma kuamini kuwa alikuwa amepoteza fahamu baada ya kulishuhudia jeneza lililokuwa na mwili wa aliyekuwa mpenzi wake na rafiki yake ambaye walitoka kijiji kimoja huko Newala.Licha ya kuwa walikuwa wameachana kimapenzi lakini ukaribu na undugu wao kutokana na kutoka kijiji kimoja haukufa na daima Mathayo alikuwa akimtania Raheem kuwa ni shemeji yake.
Raheem alijikuta akiumia zaidi baada ya kuona lile gari lilibeba mwili wa marehemu Alice likitoka kwenye eneo la hospitali ile na kumwachia maumivu makubwa sana kwani alijua kabisa asingepata muda wa kumzika mpenzi wake ambaye alimwahidi mara nyingi kuwa angekuwa naye hadi siku ya kufa na asingeweza kuishi bila uwepo wake.Alikumbuka mengi sana na kububujikwa na machozi kiasi kwamba hata askari aliyekuwa pembeni yake akamhurumia na licha ya mwanzo kuonesha chuki kwake akimwona ni muuaji.
Akiwa bado amepiga magoti gari lile lilipotea mbali ya upeo wa macho yake huku kundi kubwa la watu wakilisindikiza kwa vilio huku wakimlaani yeye (Raheem) kwa unyama alioufanya ingawa hakukuwa na aliyeujua ukweli kuwa hakumuua Alice zaidi ya muuaji, yeye pamoja na marehemu Alice ambaye aliujua ukweli wa tukio zima lakini hakuwa na uwezo wa kuuambia ulimwengu ule uliobadili mapenzi yake kwake na kuwa chuki kali ambayo aliona kabisa ilikuwa ni vigumu kufutika.
Mtegemeo yake makubwa yalibaki kwenye jambo moja ambalo aliamini kuwa lilikuwa ni kosa la muuaji japokuwa lilimuumiza sana lakini alijua huenda lingekuja na majibu sahihi kwake kosa la kufanya naye mapenzi na kuacha ushahidi wa manii.Lakini kwa upande mwingine alijikuta akipata shaka juu ya uwezekano wa muuaji kufanya mapenzi na Alice kabla ya kumuua kwani ni muda mfupi sana ulikuwa kati ya Alice kutoka darasani hadi muda alioenda chooni na kumkuta pale chini akiwa ameshapoteza uhai.Hapo wazo la kuwa huenda Alice alikuwa amefanya mapenzi na mwanaume mwingine kabla ya kumpitia pale nyumbani kisha wakaenda chuoni lilikuja kichwani mwake na kupata nguvu na akajikuta kwa mara nyingine akimtupia shutuma za usaliti Alice ambaye jioni ile kabla ya kwenda chuoni alidai alikuwa na marafiki zake.
‘’Alinisaliti Alice’’ alijikuta akiongea badala ya kuwaza kama alivyofikiri na kumfanya askari amwangalie kwa hasira.
‘’Kwa hiyo ukaamua kumuua?’’ Aliuliza Yule askari kwa hasira.
‘’Hapana, sikumuua kaka yangu’’Aliongea Raheem baada ya kugundua kuwa alichokuwa amekiwaza amekitamka.
‘’Usiiite kaka yako sina undugu na muuaji kama wewe’’Aliongea yule askari kwa hasira akimwinua pale chini na kumkalisha kitandani kwa nguvu kisha akamfunga pingu mkono mmoja kama awali.
Raheem hakuwa na cha kufanya zaidi ya kutii amri ile huku akisubiri majibu ya vipimo vya vinasaba kwa wahka mkubwa huku tukio la usiku ule alipoukutwa mwili wa mpenzi wake kule chooni.Maumivu makali yaliupata moyo na akajikuta hatamani kukumbuka tukio lile ambalo lilikuwa limebadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa sana , kwani ndoto zake zote zilikuwa zikizimika baada ya kujiona akiwa karibu kabisa na kifungo cha miaka mingi gerezani huku dunia ikimhukumu na kumwona kama muuaji wakati alijijua kwa hakuwa muuaji bali palikuwa na mtu mwingine alikuwa amemuua mpenzi wake aliyekuwa akimpenda kwa moyo mmoja.
Baadaye aliingia mama Raheem akiwa ameongozana na askari na kuanza kutoa kilio baada ya kumwona Raheem akiwa amefungwa pingu, huku hali yake kiafya ikiwa mbaya sana kwani sehemu yngi za mwili wake zilikuwa na majeraha sana huku sehemu nyingine zikionesha dalili ya damu kuvia kutokan na kipigo.
‘’Mwanangu’’Alisikika mama yake Raheem huku akitokwa na machozi.
‘’Naaam mama’’Raheem aliitika akitokwa na machozi na kujaribu kumkumbatia mama yake kwa mkono wake mmoja uliokuwa huru.
‘’Pole Raheem…. Pole mwanangu pole sana pole sana….’’Alionge mama yake Raheem kwa uchungu, kubwa huku mauivu ya uchungu wa kumleta Raheem duniani yakijirudia tena.
‘’Asante mama asante sana, sijaua Mungu anajua na hata Alice huku aliko anajua kuwa sijamuua’’Aliongea Raheem akibubujikwa na machozi.
‘’Mungu yupo anajua mwanangu kwani……’’Kabla hajamaliza kauli yake mlango wa kile chumba kile ulifunguliwa na watu watatu wakaingia, alikuwa ni Neema, Mathayo na askari mmoja.
Wote waligeuka kuwatazama ambao nyuso zao ni kama zile za wale waliokuwa mle ndani wote walionekana kuwa katika uchungu mkubwa kila mtu alikuwa na jambo lilimsikitisha wakati mama yake Raheem akiumizwa na mateso aliyokuwa akiyapata mwanaye kwa upande wa Neema alisikitishwa na kitendo cha mpenzi wake huyo wa zamani kumuua msichana asiyekuwa na hatia na hata angekuwa na hatia kuua haikuwa ni adhabu aliyostahili na kwa upande wa Mathayo alikuwa nammengi ya kumuumiza ikiwa ni pamoja na maumivu ya kufiwa na aliyekuwa mpenzi na ndugu yake.
‘’Kwa nini umemuua Alice si bora ungemwachia Mathayo kama ulikuwa humpendi jamani’’Alilalamika Neema akilia.
‘’Sijaua niamini Neema sijaua Mungu anajua na hata huko aliko Alice anajua kuwa sijamuua’’Alijitetea Raheem akilia.
‘’Naona mnaleta fujo hapa mliomba mje kumwona mgonjwa sahizi mnakuja kutupia kelele tokeni humu’’Askari aliyekuja na na akina Mathayo akiwatoa nje.
‘’Kwa hiyo ulimchukua kwangu ili umuue?’’Aliongea Mathayo wakati akitoka wakimwacha mama yake Raheem akitokwa na machozi akiumia kwa uchungu sana.
Mama Raheem alijua ule ulikuwa ni mwisho wa Raheem ambaye aliamini angekuwa mkombozi wa familia yao iliyokosa baba kwa miaka mingi iliyopita naada ya kupoteza maisha miaka michache iliyopita.Giza lililotokana kifo cha baba wa familia hiyo lilianza kutoweka baada ya Raheem kuanza kjujifatia ridhiki kwa kuuza fulana zilizokuqa na picha mbali mbali alizokuwa akizichora pamoja na picha mbalimbali azlizokuwa kiziuza na waliamini baada ya kuhitimu basi nuru halisi ingeonekana kwenye familia hiyo.
Lakini dakika kama zilikimbia sana na kubadilisha mambo kwani yote ambayo yalikuwa yakitegemewa kufanywa na Raheem yalikuwa ni kama hadithi moja ya kubuni iliyokuwa ikifikia ukingoni na kuwafanya wafuatiliaji wabaki vinywa wazi.Wakati mama yake akiwaza hayo Raheem alikuwa mbali sana akiwaza baada ya kufikiria mengi san baada ya ujio wa Mathayo na Neema watu amabo aliamini walikuwa ni watu aliokuwa amewatenda vibaya sana maishani.
Alikumbuka mengi sana mabaya lakini yote hayo yalianzia siku moja, siku ambayo aliamini hakuna kati yao ambaye angeisahau, siku iliyobadilisha kila kitu katika historia.Siku iliyopelekea hata mambo yale yakawa vile wakati ule.
_____________________________________
Tarehe tano oktoba miaka miwili ilyopita ilikuwa ni siku muhimu san kwa wafunzi wa vyuo vikuu vilivyokuwa mkoani Kilimanjaro na Arusha ambako kulikuwa na shindano kubwa la kumsaka Miss na Mister University kanda ya kaskazini.Kila chuo kilikuwa kimejipanga kuibuka na ushindi kutokana na washindani wao waliokuwa wamewaandaa wakiamini walikuwa ni zaidi wa washindani vyuo vingine.Shindano hilo lililotamguliwa na mashindano ya michezo mbalimbali iliyofaynyika mchana ikiwa ni pamoja na soka, mpira wa wavu, kikabu na riadha ambayo kwa upande wa Chuo ya Mtakatifu walikuwa wametoka patupu na karata zao za mwisho zilibaki kwa Mr$Mrs University shindano ambalo lilikuwa likifanyika usiku.
Dakika kumi kabla ya shindano hiilo kufanyika katika ukumbi mmoja maarufu uliokuwa katikati ya jiji la Arusha minong’ono ikaanza kuzagaa miongoni mwa wanafunzi kuwa mshiriki mmoja aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kushinda kwa upande wa wanaume alikuwa amejiondoa kwenye mashindano kutoka kwenye chuo cha Mtakatifu Joseph kwani kila mtu alikuwa akiamini alikuwa anatetea taji lake alilolichukua mwka uliopita.
‘’Haiwezekani itakuwa ni janja tuu ya kuwanyong’onyesha wapinzani wake’’Alisikika mwanafunzi kutoka Chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph.
‘’Kweli kajitoa nimesikia waandaaji wakijadiliana na ‘Dean of Students’ kule ndani’’ Alithibitisha mwingine ambaye alikuwa ameitoa ile taarifa kwa wanafunzi na kusambaa kama upepo wa jangwani.
Wakati wanafunzi wa Chuo kikuuu cha mtakatifu Joseph wakiulizana wa masikitiko makubwa juu ya taaria hiyo upande wa pili kwa waanafunzi wa vyuo vingine walikuwa wakifurahia taarifa ya kujitoa kwa mshindani waliyemwona kama mshindi hivyo kufufua matumaini yao ya kutwaa ushindi kwenye kipengele hicho.
‘’Dah! Usiniambie hapo tumeshachukua ubingwa’’Aliongea mshindani wa kipengele hicho kutoka Chuo Kikuu Cha Tumaini Makumira.
Je,nini kilifuata?
Mkono upi umemuua Alice?

0 comments:

Post a Comment