Wednesday, 9 March 2016

RIWAYA;NI YEYE KWELI? SEHEMU YA KWANZA
MTUNZI: MORINGE JONAS

Nilikuwa nikitembea tembea stendi kuu ya Magari mjini Iringa baada ya kuchelewa gari ya kwenda Dabaga, ambapo niliambiwa hakukuwa na gari lingine la kunipeleka huko. Nilijikuta nimeanguka chini na kama kawaida mijini watu walinizunguka wakinizomea wengine wakionekana kunihurumia.Nilikuwa nimeanguka mara baada ya kugongana na mtu ambaye sikumwona awali, nadhani kutokana na mawazo juu ya kukosa gari.

Watu waliniangalia nikijiinua kuna walionionea huruma kuna walionicheka na wengine walidiriki kunisukuma.Niliondoka na kwenda kukaa mahali ambapo abiria wengine hukaa wakisubiri magari wengine huja kuwapokea wageni wao, nikijaribu kuwaza juu ya safari ya kwenda huko Kilolo huku nikiwa sina pesa ya kutosha hata kulala sikujua ningelala wapi. Nikiwa nawaza yote hayo alikuja binti mmoja kukaa karibu yangu na kunipa pole kwa kuanguka, nilijibu kwa aibu mara baada ya kujua kuwa mrembo yule aliniona bale chini wakati nazomewa.
Muda uleule alipita mama mmoja akizunguka zunguka pale tulipokaa, baadaye aliondoka na watu wengi waligeukia na kuniangalia,jambo lililonifanya niinamishe kichwa chini.
Yule dada aliyejitambulisha kwa jina la Eliza aliniambia kuwa yule mama ndiye aliyenifanya nikaanguka,niliinuka kumwangalia. Nilimwangalia yule mama akipotelea kwenye magari akiwa bado anatembea kama hajielewi vile.
Ni mama wa makamo ambaye alikuwa akizurula katika stendi kuu ya mabasi mkoani Iringa, kila aliyemuona alijua kuwa alikuwa na upungufu wa akili yaani kichaa.Hakuna mtu aliyejua alipokuwa anapokaa licha ya watu mbalimbali kujaribu kujua ukweli juu ya maisha yake wengi hawakupata jibu sahihi.
Wapo waliodai kuwa alikuwa analala popote pale wengine walidai alilala maeneo ya Kitanzini njia ya mkato ielekeayo Ipogolo pale darajani, wengine walidai ni jini, ilimradi watoe jibu waliloliona linawafaa.
Hakuna aliyemjali zaidi ya wageni waliobahatika kumwona pale stendi, wengi walimpuuza na kumwona si lolote chochote.Nilikuwa miongoni mwa wageni wachache waliovutiwa na kutaka kujua undani wa maisha ya yule mwanamke ambapo nakumbuka nilikuwa safarini kuelekea Kilolo nikitoka Njombe.
Nilitamani kumfuatilia lakini nilipotaka kuondoka yule dada alinizuia na kudai nimpotezee tuu,nilikubali shingo upande na kumlaumu yula dada kimoyomoyo kwa kujifanya wa kuniendesha japo hakunifahamu.Sikujua ni nini kilichonisukuma nimfuatilie yule mama,niliamua kukaa chini na kumuuliza yule dada maswali mengi juu ya yule mama kitu ambacho hakukipenda kwani alijibu kwa mkato na kutaka ''nimpotezee tuu'' Yule mama.
Aliamua kubadilisha mada na kuniuliza jina langu na niendako nilimweleza yaliyonisibu na kumweleza kuwa sikuwa na pesa zaidi ya nauli.Yule dada alinitoa hofu na kuniomba twende kwake kwani alipopanga palikuwa na vijana ambao angewaomba nilale kwao, nilikubaliana naye huku nikiwa na shauku kubwa ya kujua maisha ya yule mama ambaye alikuwa akizurula pale stendi kuu.
Tuliondoka na kuelekea upande wa chuo cha Mkwawa na alinieleza kuwa alikuwa mwanachuo wa mwaka wa pili chuoni pale.Tulipokuwa njiani tulipishana na yule mama, safari hii alikuwa akitembea kwa kasi sana nusura agongane na yule dada.Tulipofika mbele kidogo yule dada alinitania kuwa nimfuate nami niwe chizi, nilicheka lakini kichwani nikiamini yule mama ana akili zake timamu ila sikujua ni kipi kilichonipa imani hiyo.
Tulipofika kwake nilikaribishwa na alidai wenzake wengi walikuwa chuoni kwani hakuwa na vipindi vingi siku ile.Niliingia ndani na kuketi kitandani kwani hapakuwa na kiti chochote kile, kilikuwa ni chumba nadhifu kilichoonesha ni kweli kilikaliwa na mwanachuo wa kike kwani palikuwa na kioo kikubwa na meza yake, kompyuta mpakato, kitanda na godoro la sita kwa sita, vipodozi vingi sana na palikuwa na TV ndogo. Nililetewa chakula ambacho kilionekana kununuliwa kwanikilibebwa kwenye mfuko mdogo wa plastiki, zilikuwa ni chipsi mayai soda mbili na tulianza kula huku tukiongea hili na lile.
Ulipofika usiku sikuona dalili zozote za watu,kuja pale nyumbani na nilipomuuliza mwenyeji wangu juu ya suala hilo, alinijibu kuwa kulikuwa na mashindano ya kumtafuta Mrembo wa chuo hivyo wangekuwa huko ingekuwa vyema tukiwasubiri tukiangalia filamu ya kinaijeria, hadi watakaporudi au aniache nilale pale naye angeenda kulala kwa rafiki zake kwenye nyumba nyingine ambayo aliamini lazima angemkuta rafiki yake kwani aliamini huwa si mpenzi wa mambo yale.Tulikubaliana tuwasubiri kwa kuangalia ile filamu kwanza.
Kabla ile filamu haijafika nusu kuna mmoja wa wanachuo wale alifika lakini alikuja na msichana ambaye tuligundua kuwa alikuwa ni mpenzi wake kwani baada ya kuondoka kwake nilielezwa na mwenyeji wangu alikuwa ana tabia ya kuja na wasichana tofauti tofauti kila ifikapo ijumaa , na alizoeleka kwa hiyo tabia japo aliponea chupuchupu kufumaniwa na mwanafunzi wa shule moa ya sekondari ya wasichana mjini Iringa lakini tabia yake haikukoma.Tuliamua kuendelea kusubiri tukiangalia ile filamu walikuja wanafunzi wengine watatu lakini wengi walikuja na wapenzi wao nilijikuta nachukuwa kuwa mwanachuo suala ambalo mwanzoni nililiona kama ni ufahari kuitwa mwanachuo lakini kwa tabia ile nilijikuta naapa sitokuwa mwanachuo tena kama ndiyo tabia za chuoni zilivyo.
Baadaye usingizi ulinipata pale kitandani na Eliza aliniacha nilale yeye akiendelea kuangalia ile filamu hadi ilipoisha ambapo aliniambia angeenda kulala kwa rafiki yake baada ya kumpigia simu.Nilikumbuka kuwa siku ile sikuoga kabisa nilimuuliza kama nigeweza kupata maji maana nilijihisi mwili wangu unanata japo palikuwa na baridi ila niseme ukweli tuu nilikuwa sijaoga siku tatu kabla kutokana na shughuri na baridi siku ile safari ya kutoka Njombe hadi Iringa kidogo ilinifanya nione mwili wangu mzito kwa jasho.
Nilielezwa bafu la ndani ya chumba na niliondoka kwenda kuoga naye alienda kulala huko kwa rafiki yake. Baada ya kuoga nilianza kufikiria juu ya safari yangu ambayo nilionekana kuisahau kidogo kutokana na uwepo wa yule dada ambaye alionekana kunisahaulisha kidogo juu ya safari ya kwenda wilayani Kilolo kijijini Uluti ila niliambiwa gari zinaishia Dabaga.Niliwaza juu ya umbali kutoka hapo Dabaga hadi kufika huko Uluti,wazo la yule mama lilinijia tena akilini niliwaza kwa nini nilikuwa sitaki kuamini kuwa ni kichaa kama wengine wadhanivyo nilijikuta sina jibu juu ya maswali yale niliona bora nilale tuu.
Usingizi uliponichukua niliamshwa na sauti ya mtu akigonga mlango, mwanzoni nilifikiri labda mlango wa chumba kingine lakini baada ya kusikiliza kwa muda niligundua ni chumba nilichokuwa nimelala.Niliamua kutoka na kwenda kufungua mlango, nilikaribishwa nje na la kofi shavuni, sikuelewa ni nani aliyenipiga niliangalia tena vizuri niliwaona vijana wawili ambao walionekana wamekuja kwa shari .
Walinivamia na kuanza kunipiga, baada ya kuona hivyo nailijitetea kwa kuwapiga ngumi na mateke mawili matatu kabla ya kufanikiwa kukimbia.Nilikumbuka kuwa kuna begi mle ndani ila nilona kitu cha kwanza ni usalama wangu na habari za nguo nitajua siku nyingine na hata nisingezipata ningenunua nyingine lakini uhai ukipotea haurudishwi kwa gharama yoyote ile.
Nilikimbia nikielekea upande wa sekondari ya Mawelewele huku nikiwa sijui kama nilikuwa nafuatwa na wale vijana au walikuwa wameniacha.Nilipunguza mwendo nilivyojiona nipo peke yangu nilikumbuka juu ya yule mama waliyesema ni kichaa na huwa hulala popote niliona bora nami ningelala tuu popote na si kutafuta kulala pazuri na yakanikuta yale yaliyokuwa yamenikuta.
Nilifikiria pia juu ya ujinga wangu wa kumwamini Eliza na kukubali kulala kwake nikianza kuhisi kuwa huenda ni mpango wake ili mimi nipigwe na wale vijana ambao kama si silaha yangu namba moja katika maisha yangu(mbio) kuniokoa pengine kama siyo kifo basi ningeambulia ulemavu.
Mbio, ndiyo silaha yangu popote na huwa naitumia hii kuepukana na matatizo kama yale naamini siwezi kupambana kwa kupigana lakini mbio zisizo rasmi kwangu ni silaha yangu.Sasa nilichofikiri baada ya kukaa kwenye jengo ambalo lilionekana kutokamilika na kama vile limetelekezwa vile na mmiliki kwani lilikuwa na nyasi nyingi ndani mwake na paa lake haikumalizwa ni juu ya safari yangu ya kwenda wilayani Kilolo ambako niliambiwa na baba angu mdogo kuwa naweza kupata vibarua vya kupanda miti ya mbao ili nijipatie pesa kwa ajili ya ada ya shule kwani nilikuwa natakiwa kulipa ada ya kuingia kidato cha sita baada ya likizo ile.
Sikuwa na mtu wa kunisaidia kwani wazazi wangu walishapoteza maisha kipindi nipo darasa la tano vifo vilivyotokana na mlipuko wa kipindupindu kijijini kwetu miongoni mwa watu kumi na moja waliokufa katika janga lile walikuwa ni wazazi wangu na mdogo wangu wa pekee ambaye alikuwa na miaka miwili tuu kipindi hicho.
Maisha yangu yalitegemea huruma ya ndugu na marafiki wa wazazi wangu licha ya kusimuliwa na baba kuwa alianza kuwasomesha wadogo zake na kaka zake hakutokea ndugu hata mmoja aliyekuwa tayari kunisomesha zaidi ya kutangatanga huku na huko nikihitaji misaada nakumbuka pio tukio la kufungwa wiki tatu baada ya kuchoma mashamba ya miwa wakati nafanya kibarua cha kuandaa maeneo ya kulima.
Nilijikuta ile picha ikijirudia kichwani.
__________________________
Ilikuwa ni siku ya jumamosi ambayo kama kawaida niliamka mapema kufanya usafi wa nyumba ambayo nilikuwa nikilala ,nyumba ya udongo iliyoezekwa nyasi ambayo ni miongoni mwa urithi nilioachiwa na wazazi wangu.Niliipenda ile nyumba kama nilivyowapenda wazazi wangu ambao sikuamini kama kweli walikuwa wamekufa ,nilijua lazima kuna siku watatoka kule waliko lala na kuja kukaa mle ndani.
Nilisafisha chumbani kwao ambako licha kuwa na kitanda kizuri na godoro zuri sikudiriki kulala kule zaidi ya kulala kwenye kitanda changu cha ngozi na godoro kuu kuu ambalo baba aliniambia lilikuwa likitumiwa na wazazi wake ambao waliachiwa na mzungu ambaye babu alikuwa anafanya kazi kwake kama msaidizi wake akimpikia na kufanya kazi mbalimbali(oboi).
Niliamini mdogo wangu atakuja akiwa mkubwa na nitacheza naye na kila siku ya kifo cha wazazi na ndugu yangu ifikapo nilishinda chumbani kule nikiwalilia na kuwaomba warudi tuishi wote.Hakukuwa na ndugu aliyekuwa tayari kuishi namimi wakidai ni mkosi na ningeleta balaa kwenye familia zao hivyo licha ya kuwa na umri mdogo nilishi peke yangu tangu wazazi wangu walipozikwa.Alikuja binamu yangu mmoja ambaye naye baada ya wiki tatu aliondoka na kwenda kufia mtera alikoenda kuvua hali iliyowafanya waamini mkosi ulitoka kwangu.
Niling’oa mihogo shambani kwetu na kuichemsha wakati huo nikimsubiri bwana shamba anipitie akanionesha shamba la kusafisha kama kibarua ili nipate pesa kwa ajili ya kulipa kwa ajili ya kipaimara ambako nilibaki peke yangu kulipia na siku kumi zilibaki kabla ya kupata kipaimara.
Niliamua kupata sakramenti hiyo ambayo wazazi wangu waliniambia ni lazima niipate kama taratibu za kanisa letu zilivyotaka.Nikiwa naipua mihogo motoni na kutenga maji nikoroge uji nilisikia mtu akibisha hodi kwa sauti yake tuu nilimjua na kumtaka aingie ,alinipa mfuko wa sukari na kudai nipate nguvu ndipo twende shambani nilimpokea wakati huo alikuwa amesha chukua mhogo na kuanza kula alinizoea kama mdogo wake kwani ndiye niliyempokea siku anaripoti pale kijijini kuanza kazi.
Nilibadilisha wazo la kukoroga uji ambao nilipanga niweke chumvi kwa kuwa sukari ilikuwepo niliamua kupika chai nikitumia majani ya michaichai yaliyokuwepo pale uwanjani.Baada ya kula nilibeba mihogo mingine ya shambani tuliondoka na kuelekea kwenye shamba jipya ambalo lilikuwa kwenye bonde la mashamba ya miwa na alidai alikuwa na safari siku hiyo na angekaa huko wiki tatu hivyo angeniacha huko na kurudi aanze safari yake ya kwenda kwenye semina Iringa mjini.
Baada ya kuoneshwa shamba nilianza kazi ile ambapo alinishauri kukwaa barabara za pembeni na kuchoma moto akisisitiza upana wake uwe zaidi ya mita mbili kwa uoga wangu niliweka urefu wa mipini minne ambayo ilikuwa ni kama mita nne na nusu.
Saa tisa kamili nilikuwa nimebaki peke yangu kule shambani na wakulima wengine walikuwa kwenye mashamba ya jirani walikuwa wameshaondoka na kufikia saa kumi namoja na dakika kama ishirini hivi nilikuwa nimieshamaliza kutengeneza barabara kuzunguka shamba, nilijipumzisha nikisubiri upepo upungue ili nichome shamba lile.Baada ya kujiridhisha na utulivu wa hali ya hewa nilifuata mfuko wangu uliokuwa na kiberiti na mihogo ambayo kutokana na shughuli nzito hata sikuwa na hamu hata ya kuila ikizingatiwa maji niliyoenda nayo shambani nilikuwa nimeshayamaliza na kuwapa wapiti njia wawili watatu waliopita pale na kuniomba.Nilichukua kiberiti na kuawasha nikiangalia mwelekeo wa kiupepo kidogo kilichokuwepo.
Niliwasha ulikotokea ili iwe rahisi kuenea shamba zima kasha nikaenda kukaa kwenye jiwe pembeni kidogo nikiangalia zile nyasi zilivyoteketea, nikiwa naamini kazi ilikuwa inakaribia kuisha nilisikia sauti ya kitu ikitokea upande wa mashariki ambayo iliyonifanya nisimame na kuangilia ni nini hicho kilichokuwa na sauti ile.Nilishtuka na kukimbilia upanga nilipouweka. Niliuchukua na kukata matawi ya miti ambayo niliamini yangenisaidia kuuzima moto ambao ulikuwa unaelekea mwishoni kabisa na shamba kwani kulikuwa na kimbunga kilichokuwa kinakuja kwa sauti kubwa kingesababisha moto ule kuvuka barabara niliyotengeneza na kuunguza mashamba mengine.
Lakini nilikuwa nimechelewa na moto ule ulivuka na kuanza kuchoma mashamba yaliyokuwa jirani.Nilihangaika kwa karibu masaa mawili kujaribu kukwaa njia kuzuia ule moto kuunguza eneo kubwa zaidi la bonde lile lakini sikufanikiwa zaidi ya kupata majeraha mawili matatu ya kuungua.Nilikaa chini nikilia kimya kimya na kujiuliza kikubwa nilichomkosea Muumba ikizingatiwa nilienda pale kutafuta pesa kwa ajili ya kulipia kipaimara kitu ambacho ni miongoni mwa sakramenti ambazo tulifunzwa kuwa Mungu hupendezwa nazo.
Giza lilipoingia niliona eneo kubwa ambalo liliungua kwani miale ya moto ilionekana huku na kule huku sauti za wadudu na wanyama wadogo walioshindwa kuukwepa moto huo kupasuka zikisikika hapa na pale.
Niliamua kuanza safari ya kurudi nyumbani huku nikiwa na hofu kuu kitu kulichonishangaza ni kuwa licha ya watu kuniona nahangaika kuuzima ule moto hakukuwa na hata mtu aliyekuja kunisaidia jambo ambalo lilinifanya niwe mnyonge zaidi.Sikupita njia ya stendi ambako nilijua ningewakuta watu wengi niliamua kupita njia ya kuzunguka ili nisionane na mtu yeyote kwani nilijua taarifa zilikuwa zimeshafika pale kijijini.
Saa tatu na nusu usiku nilikuwa nimelala kitandani nikiwa najaribu kufikiria mambo yale yaliyoniandama vile, njaa iliniuma na niliinuka na kufuata mihogo niliyokuwa nimeibakisha asubuhi lakini nilipojaribu kuila sikuona kabisa radha yake huku uoga ukinisogelea kwa kasi nilijua kabisa nitatakiwa kulipa kwa mashamba yaliyoungua na kwa jinsi walivyonichukia bila sababu pale kijijini nilijua hata ambao mashamba yao hayakuwa na chochoze zaidi ya migomba miwili iliyokuwa ni kama alama ya mashamba yao katikati ya chaka kubwa wangedai kulipwa.
Nilijaribu kufikiria watu wa kuwaomba msaada sikumuona hata mmoja zaidi ya yule bwana shamba ambaye naye alikuwa amesafiri na hata angekuwepo mashamba yote yale yaliyoungua lazima naye angeshidwa kulipa.Niliwaza mambo mengi hadi nilipopitiwa na usingizi, niliamshwa asubuhi na sauti ya mlango wa bati ukilalamika kwa mateso ya kugongwa kwa fujo muda mrefu.Niliamka na kumuangalia mgongaji alikuwa ni mgambo wa kijijini pale ambaye hata bila ya kupokea salamu yangu alinitaka nifunge mlango twende zilipokuwepo ofisi za kijiji , nilikumbuka kuwa ilikuwa ni jumapili na ilikuwa ni jumapili ya kwanza kukosa ibada jambo ambalo liliniumiza sana.
‘’Kwani kuna nini?’’ nilijaribu kumuuliza yule mgambo ambaye badala ya kunijibu alinipiga kofi na kuanza kunifunga kamba mikono yangu kwa nyuma.
‘’We si unajifanya unavuta hadi uchome mashamba ya watu, sijui kwa nini hukufa na babako’’aliongea yule mlinzi jamabo ambalo lilianya nihisi michirizi ya mashozi ikishuka mashavuni mwangu
‘’Jamani nilikuwa nasafisha shamba ni bahati mbaya ‘’nilijaribu kujitetea
‘’Bahati mbaya ehhe babako alikuachia shamba kule enhhe! bangi gani zivutwazo na watoto shule ya msingi sasa ona unashindwa hata kujitetea eti shamba mna shamba kule, subiri shughuri utakayoipata kwa mwenyekiti mtu anategemea ekari zake kumi za mihogo kwa ajili ya wake zake na watoto wake wewe unamlazimisha ang’oe kwa siku moja’’ aliongea yule mlinzi jambo ambalo lilinitia hofu zaidi hasa nikikumbuka juu ya kauli za yule mwenyekiti wa kijiji juu yangu.
Tulipofika ofisini nilimkuta mwenyekiti wa kijiji na watu wengine ambao nilijua lazima mashamba yao yatakuwa yameungua wakiwa wamefura kwa hasira.Niliwasalimia lakini hakuna aliyenijibu zaidi ya kuniangalia kwa macho makali.Yule mgambo alinikabidhi na kusogea pembeni kidogo nikiwa najaribu kuwaangalia wale watu na kuwatambua nilishtukia napigwa kofi lililonipeleka chini kwani kamba nilizofungwa mikononi zilikuwa zimenifanya nikose uimara ikizingatiwa jana yake sikula.
Niliinuliwa na kupigwa kofi la pili lililonifanya niende tena chini safari hii alininyanyua na kunielekeza kwenye chumba kidogo ambako nilifunguliwa kamba na kufungiwa humo. Nilisikia wakijadiliana pale ofisini juu ya mashamba sijui habari za kuuzwa jambo ambalo nilihisi lazima watataka kuuza mashamba niliyoachiwa na wazazi wangu kitu ambacho wazazi wangu katika uhai wao walinisisitizia kununua mashamba na si kuuza.Niliumia sana lakini sikuwa na jinsi zaidi ya ya kukaa mle ndani.
Nilianza kusali na kumwomba Mungu aniepushe na janga ambalo nililiona mbele yangu mtoto wa darasa la sita nakutana na mambo kama ya yale bora wangekuwepo wazazi wangebeba mzigo ule lakini nilikuwa nimebaki peke yangu mimi ndiye baba mama kaka dada shangazi mjomba na ndugu wengine unaowafahamu msomaji.Nilianza kuhisi njaa kali ilianza kusokota tumbo langu iliuma zaidi baada ya kujua kuwa sikuwa na uhakika wa kuletewa chakula nilibaki nimetumbua macho nikijifanya kusubiri chakula kutoka kwa mtu ambaye nilijua Mungu atamtuma pale kuniokoa.
Niliona taswira za wazazi wangu wakiwa na machungu makubwa nilimwona mdogo wangu akija kunikumbatia lakini nilijikuta najikumbatia mwenyewe na hakukuwa na yeyote kati ya niliowaona.Baadaye sikujua kilichoendelea zaidi ya kuona giza nene mbele yangu.
____________
‘’Moringe ana nini mbona hajaja kanisani na hata kwenye mafundisho hayupo’’ aliuza mama mchungaji akiwauliza watoto ambapo siku chache zijazo walitaraji kupata sakramenti ya kipaimara.
‘’Alisema haji tena hana hela ya kulipa’’aliongea mmoja kati ya wale watoto.
‘’Mmhh wakati amefungwa ‘’aliongea mwingine akiwafanya wenzake wacheke.
‘’Unajua sitaki utani mwenzenu yupo wapi mbona mnachekacheka na kuleta utani wake’’aliongea yule mama akibadilisha sura yake kuwa ya ukali akiwafanya wale watoto wakae kimya.
‘’Kweli mwalimu amechoma mashamba ya watu leo nilimwona akipigwa kule ofisini’’ aliongea mtoto mmoja akimwambia mama mchungaji ambaye walizoea kumwita mwalimu.
‘’Mhh ‘’ aliguna yule mama na kutoka kuelekea nje ya kanisa
‘’Mwalimu,,, mwalimu mwali…. si tuondoke?’’ aliongea mtoto mmoja wakati huo yule mama alikuwa ameshafika mlangoni.
''Hivi unataarifa ya Moringe kuwekwa ndani?'' Alikutana na swali kutoka kwa baba mchungaji baada tuu ya kufika nyumbani
''Ndicho kilichonitoa kanisani baba''Alijibu akiingia ndani na kuangalia kama kulikuwa na chakula.
''Ngoja nikawaambie hawa wamafundisho waondoke halafu wewe umpelekee chakula lazima atakuwa hajala'' Aliongea mchungaji na kuondoka kuelekea kanisani ambako hapakuwa mbali na alipokuwa akiishi.
''Kumbuka kuhusu mpango wa kumtoa yule mtoto kwani ndugu zake wanaweza wakawa ndio kwanza wakakesha vilabuni wakisherekea janga hili badala ya kumsaidia''Aliongea mama mchungaji wakati huo akiweka sahani zenye chakula kwenye kikapu chake na kuanza kutoka.
''Lakini hizo pesa sijui tutapata wapi ,maana huu mwezi wa tatu hata ile posho baba hajapewa tungeweza hata tungemlipia yule mtoto majanga mengine asingekutana nayo''.
Aliwaza mama mchungaji ambaye kila mtu aliyepishana naye alionekana kumshangaa kwani bado alikuwa amevaa nguo za wanakwaya ambazo hakukumbuka kuzivua alipofika nyumbani.
''Ana nini huyu mama mbona kama anaongeaongea peke yake?''Aliuliza kijana mmoja aliyepishana naye.
''We huwajui hao utashangaa ana wanga huyo ''Alijibiwa na mwenzake akiwafanya waliosikia kauli ile wacheke hali iliyowafanya watu wengi kuwageukia kuwatazama.
''We mama mchungaji na kuwanga wapi na wapi?'' aliuliza mwenzake kinafiki huku akicheka
''Huwajui ile ni kama sehemu tuu ya kujificha wanga wana akili sana hadi kanisani wapo hao ndio mbwa mwitu waliovaa ngozi za kondoo''Aliitetea hoja yake na kuwafanya wenzake wajishike mbavuni kwa vicheko.
Baada ya kufika ofisini hakumkuta mtu yeyote hali iliyomfanya aweke kikapu kwenye bechi lililokuwa pale nje na kwenda kwenye nyumba ya jirani na ile ofisi kuulizia alikoenda mtendaji ambapo alielezwa kuwa lazima angekuwa kilabuni hali iliyomfanya aelekee huko.Alipokaribia kilabuni alimwagiza mama mmoja akamwitie ndani walikokuwa wanakunywa pombe na yeye wakati huo akiongea na nesi mmoja juu ya suala lile ambalo lilionekana kuwafurahisha watu wengi bila sababu yoyote ya msingi.
Wengine wakiamini wangetajirika kwani ni lazima ningelazimika kuuza mashamba yake iwe kwa hiari ama lazima ili awalipe wengine walijua watapata mashamba ambayo kila walipotaka kununua nilikuwa kikwazo kikubwa.Diwani na wafanya biashara wakubwa walilitaka lile shamba pia palikuwa na tetesi juu ya uwepo wa sanduku lenye mali kwenye mashamba yale hicho ndicho kilichowavuta watu wengi kutaka kuyamiliki mashamba yale pia tetesi za kuhamishwa kwa stendi ya kijijini pale kuwa eneo kubwa la mpango wa ujenzi wa halmashauri kuwa kwenye mashamba yale niliyoachiwa na wazazi wangu utajiri ndicho walikisaka nami sikutaka kupingana na kauli ya baba juu ya mashamba yale.
Alisubiri kwa karibu dakika kumi bila mtendaji kuja hali iliyomfanya amfuate mle ndani na kufanya watu wengi wacheke kinafiki kila alipopita.Alipanga kunisaidia Moringe kijana ambaye wengi walinichukia kwa sababu zao ambazo hata hazikuwa na mashiko yoyote.
''Samahani mtendaji nakuomba hapa nje''Aliongea alipofika alipokaa mtendaji na wenzake wakinywa pombe.
''Unataka kuninunulia pombe au kunisumbua sumbua, kama habari za ofisini sitaki leo jumapili bwana siku ya wewe na mumeo''Aliongea kilevi na kuchukua pombe na kuinywa, huku akiwafanya wenzake kucheka.
Aliinuka akionesha kabisa kuwa amelewa na kutoka pale nje na mama mchungaji.


''Enhee sema mama Mchungaji umekuja kuniombea nifike mbinguni, maana nasikia ninyi nni wana uamsho sijui mnatukataza watu kunywa pombe, Yesu mwenyewe aligeuza maji yawe pombe sasa nyie mnamfuata nani?''.Aliongea maneno mengi ambayo kwa wakati huo mama Mchungaji hakutaka kuyasikia zaidi yakunisaidia.

Alimhurumia mtendaji yule ambaye mara ya mwisho kuongea naye ni kipindi anapata mafundisho juu ya ndoa na siku ya mwisho kuonekana kanisani ni siku ya ndoa yake, ulevi na uzinzi na mitara ndicho kilichotwala maisha yake kumfanya baba asiyewafanya watoto na mke wake kujivunia kuwa naye, licha ya kuwa na mke ambaye alikuwa ni mcha Mungu na mwenye hekima lakini familia yake ilipoteza kabisa sifa ya kitwa familia bora kutokana na tabia mbaya za yule baba.

Maombi tuu yatamsaidia baba yenu, ndiyo ilikuwa kauli ya mke wake mkubwa akiwaambia wanae kila walipoonekana kumweleza jinsi tabia za baba yao zilivyowafanya wakose raha na hata marafiki shuleni.

''Nilikuwa naomba nikampelekee chakula Moringe kwani,’’Hata kabla hajamalizia alichotaka kukisema mtendaji aligeka na kuanza kuondoka kuelekea kilabuni
''Samahani baba naomba nisaidie'' alibembeleza mama Mchungaji
''We ni nani kwake hadi umpelekee chakula ,we ndugu yake au hana ndugu mbona mnapenda kujifanya watakatifu kwa watu kujifanya mnasaidia watu mbona mtoto wa mzee Maliyatabu anajiuguza pale nyumbani kwake bila msaada wowote hamjawahi kwenda kumsaidia huyu tuu,wangapi wamelala njaa hamjawapa chakula kwa nini leo kwa huyu mnajifanya wemaa,,, hembu niondokeehapa''Aliongea mtendaji akirudi kilabuni.
Ni kweli aliyemtaja hakuwa amemsaidia lakini alikuwa na hata ndugu waliomkumbuka pia ni wangapi wenye matatizo utawasaidia matatizo mengine huna uwezo nayo alikumbuka jinsi walivyoendesha harambee ya kuchangia matibabu ya mtoto wa Maliyatabu harambee iliyowafanya wakachukiwa na waumini waliodai kuwa ni kuwaongezea mzigo wa rundo la michango kwani walikuwa na michango mingi lakini walifanikiwa kupata kiasi kidogo cha fedha na chakula kumsaidia mgonjwa yule leo alishangaa kauli ya mtendaji yule ambayo aliamini aliwakilisha wenzake ambao walikuwa wengi pale kijijini waliokuwa wakiamini kama alivyoamini .Alichokifanya ni kuondoka na kwenda pale ofisini kwani aliamini hakukuwa na sehemu nyingine ambako angepata msaada wa kunifungulia nipate chakula,kwani mwenyekiti wa kijiji alikuwa amesafiri siku ile asubuhi.
''Mungu wangu!''Aliongea baada ya kufika pale ofisini kwani alichokiona kilimuumiza moyo na hakujua aliyefanya vile.Alistaajabu alichokiona pale ofisini kwani sahani zilizokuwa na chakula zilikuwa zimejazwa mchanga na kile kikapu hakikuwepo.
Alikusanya vile vyombo vyake huku akiwa na mawazo mengi juu ya waliofanya kile kitendo, aliondoka na kurudi nyumbani ili aandae chakula kingine kwani safari yake ilikuwa na kama kazi bure.Aliondoka pale ofisini huku watu wengi wakimwangalia kama punguani , hakumjali yeyote aliyemdhihaki kwa vicheko vilivyokuwa vikisikika kila alipokuwa akipita.
‘’Huyu mtoto kakosea nini ambacho kinamfanya kila mtu kumchukia mbona anateseka hivi?’’ Aliongea alipofika nyumbani kwake ambako aligundua pia hakuwa na mboga hivyo ilimbidi aende sokoni kufuata chakula.
‘’Mama Mchungaji’’Alisikia sauti kutoka nyuma yake
‘’Abee’’Aliitika akigeuka kumtazama aliyemwita.
‘’Shikamoo mama ‘’Alisalimiwa na yule mtu ambaye alikuwa ni mmoja wa watoto wa mtendaji ambaye babake alikuwa ametoka kumkwaza muda mfupi uliopita.
‘’Marhaba mwanangu ulikuwa na shida gani?’’Aliuliza yule mama kwa upole kwani licha ya tabia mbaya ya baba yake alikuwa na mwenendo mzuri sana shuleni kanisani na hata nyumbani.
‘’Mhh…nilikuwa’’Aliongea akisugua viganja vya mikono yake huku akiangalia kama palikuwa na mtu mwingine karibu.
‘’Sema ni nini, au wewe ndiye uliyemwaga chakula changu’’Aliongea yule mama kwa sauti ya ukali kidogo na kuanza kuondoka.
‘’Samahani mama ni mimi ndiye niliyempelekea chakula Moringe na kuzichafua sahani zile pale chini’’Aliongea yule mtoto kwa sauti ya upole Mama Mchungaji akiwa haamini alichokisikia kutoka kwa yule mtoto.
______________ 
Ilikuwa asubuhi wakati anatoka kuchota maji kisimani ili aende kanisani alimwona Moringe akipigwa vibao na babake hali iliyomfanya amuhurumie sana.Hakuwa na njia yoyote ya kumsaidia hasa kutokana na tabia ya ukali aliyokuwa nayo baba yake.Alipita kama vile haoni huku moyoni akiumia sana na kwenda nyumbani ambako alijiandaa na kwenda kanisani huku akijiuliza kilichomsibu Moringe hadi kufikia hatua ya kupigwa vile na baba yake.
Kanisani hakuna kilichoingia zaidi ya kumwazia kijana yule huku akimlaumu baba yake alimaini ulevi ndiyo sababu kuu ya kuwa katili kiasi kile.Alivyotoka kanisani baada ya mwalimu wao wa mafundisho kutoka kitu cha kwanza alichokifanya ni kuondoka na kuelekea nyumbani kwao huku akili yake ikiwa moja tuu kuchukua chakula na kumpelekea Moringe kule ndani kwani baada ya kumweka ndani baba yake alikuja nyumbani huku akijigamba kumkomesha Moringe na kuwa angefia mle ndani kwa njaa.
Alipofika pale ofisini ambako kulikuwa ni njia ya kuelekea kwao alisimama kidogo baada ya kuona kikapu ambapo baada ya kukisogelea na kuangalia ndani mwake aliona kuwa kuna chakula alipoangalia upande wa pili alimwona mwalimu wao wa mafundisho ambaye alikuwa ni mama Mchungaji.Alijua alikuwa anamfuata baba yake kilabuni lakini alijua kabisa kwa tabia ya baba yake lazima angekataa kuja kumfungulia ili apate chakula.Wazo lilimjia kichwani kuwa akachukue funguo na kumpa yule mama lakini wazo hilo lilipigwa na wazo lingine pale alipowaza kuwa angemsababishia matatizo yule mama kwa kudaiwa kuingia ofisini mle bila ruhusa tena peke yake.
Alichoamua ni kwenda hadi mezani kwa baba yake nyumbani nakufungua droo iliyokuwa na funguo za ofisini kwa baba yake.Alitoka na kwenda moja kwa moja zilipokuwa ofisi za kijiji kilae na kuchukua kikapu kulichokuwa na chakula na kuzunguka nyuma ya ofisi ile ambako kulikuwa na mlango wa kuingilia.Alipohakikisha haonwi na mtu yeyote alifungua
mlango ule taratibu na kuufunga kwa ndani huku akielekea kulikokuwa na chumba kidogo ambacho alikuwa na uhakika kuwa ndani mwake kulikuwa na Moringe .Aliizoea ile ofisi kwani mara kwa mara baba yake alimtuma mle ofisini kuchukua ama kupeleka vitu hivyo haikuwa kazi ngumu kwake kujua ufunguo upi ulifungua wapi.Alipofungua mlango hakuamini alichikiona mle ndani kwani Moringe alikuwa amekaka ameegemea ukuta akionesha amechoka sana hali iliyomfanya atokwe na machozi akimhurumia.
‘’Ehhe Mungu msamehe baba yangu najua hana kosa lolote kijana wako’’Aliongea kwa sauti ndogo ambayo ilitosha kabisa kumshtua Moringe na kumfanya amwangalie aliyekuwa mbele yake.
‘’Alijikuta akipatwa na uchungu baada ya kumwona mtoto wa mtendaji mbele yake ambaye baba yake masaa machache yaliyopita alimpa kipigo ambacho angeweza kukiita kitakatifu kwani kilimsababishia maumivu yaliyokusudiwa na mtenda.Alijikuta akitokwa na machozi hali iliyomfanya hata yule kijana kuacha kulia na kuanza kumpa maji ya kunywa ambayo aliyafakamia kwa fujo na kumaliza kopo zima la lita moja.Badaye alimpa chakula ambacho alikila kimya kimya hadi alipomaliza alimshukuru na kumtaka atoke kwani angemsababishia matatizo makubwa.
Wakati anakusanya vyombo na kutaka kutoka alisikia sauti za watu zikielekea mlangoni mwa ile ofisi, hali iliyowafanya waingiwe na uoga.Mlango ulifunguliwa na sauti za viatu vikisugua sakafu ya ofisi ile zikisikika,walijaribu kukisia sauti za wale watu lakini hawakuzigundua hali iliyowafanya wazidi kuwa na uoga.
Zile sauti zilidumu kwa dakika kama tatu tuu na wale watu kuondoka ,kutokana na mazungumzo yao wailigundua kuwa ni mtendaji kata mpya ambaye aliripoti siku chache zilizopita baada ya aliyekuwepo kutimuliwa kutokana na ubadhirifu wa fedha na pia ilisemekana alikuwa akitumia cheti cha kaka yake ambaye alikufa mwaka mmoja tuu mara baada ya kuhitimu elimu yake ya sekondari.Sakata hilo lilisemwa kuwa lilitokana na ugomvi kati yake na diwani wa kata ile ambaye aliamua kumchongea kwa wahusika na mwisho alitimuliwa ingawa wengine walidai kuwa walikuwa wanachangia mwanamke mmoja ambaye alikuwa maarufu sana pale kijinini kwa kutembea na waume wa watu.
Baada ya kuhakikisha kuwa walikuwa wameondoka alitoka taratibu na kwenda kuvitia mchanga vyombo na kukaa sehemu ambayo angeona nyendo za mwenye vyombo vile na baada ya kumwona aliamua kumfuatilia hadi alipomwelezea kisa hicho.
_____________
‘‘Sawa mwanangu asante sana’’Aliongea Mama mchungaji na kuanza safari ya kurudi nyumbani baada ya kusimulia jinsi ilivyokuwa na sababu ya kuvichafua vile vyombo.
‘’Haya mama mafundisho tena lini?’’Aliuliza mtoto yule akiwa ameshaanza kuondoka.
‘’Mje kesho jioni’’ Alimjibu na kuondoka kuelekea nyumbani kwake ambako alimkuta mumewe akiwa anajisomea biblia akijiandaa kwenda kwenye vipindi vya jioni vya dini ambavyo vilishirikisha waumini waliojiita ‘’wanauamsho’’.
‘’Vipi mbona vyombo vichafu hivyo?’’Aliuliza mchungaji baada ya yule mama kukaa.
‘’We acha tuu baba huyu mtoto anawidwa na shetani kama nini’’Alijibu yule mama jibu ambalo alijua fika lingezaa swali lingine ambalo ndilo alijiandaa kulijibu kwa wakati ule.
‘’Kwa nini mama?’’Aliuza mchungaji akiangalia saa ya ukutani kwani muda wa kwenda ulikuwa umekaribia kufika.
‘’Mtendaji amenikatalia katakata kuniruhusu kumpelekea chakula yule mtoto, amekazania pombe yaani huwezi kuamini kama ni yule mwanafunzi wetu wa mafundisho ya ndoa’’Alitoa maelezo mengi ambayo nayo hayakuonekana kumridhisha mumewe akijaribu kuunganisha sababu ya vyombo vile kuchafuka vile na ulevi wa mtendaji.
‘’Kwa hiyo aliamua kuvichafua vyombo vyangu?’’Aliuliza Mchungaji akicheka, ambapo mkewe alianza kueleza kisa kile tangu mwanzo hadi mwisho.
‘’Mhh hapa Mungu asaidie tuu maana hata kusema tutamtoa sijui kama tutaweza kwani hata hizo pesa za kuwalipa hao watu tutapata wapi sisi wenyewe tunaishi kwa kudra za mwenyezi Mungu huu sijui hata mwezi wa ngapi hata posho hakuna nauli za kwenda kwenye semina nachukua mfukoni mwangu’’Alilalamika Mchungaji yule ambaye licha ya kazi yake kubwa ya kuchunga kondoo wa bwana hakuambulia chochote hata kujikimu maisha yake huku tumaini lake likiwa kwenye vimiradi vidogo vya mkewe ili waishi.
‘’Baba Mungu ataonesha njia tuu wala tusikate tamaa’’Alishauri Mama Mchungaji akimtaka mumewe amtumaini Mungu kama ilivyokuwa kawaida yake hasa wapatwapo na jambo walionalo gumu kwao.
‘’Hapa watamlazimisha auze mashamba yake ili watimize lengo lao la kujinufaisha hawana huruma wale watu’’Aliendelea kulalamika mchungaji wakati huo muda wa kwenda kanisani ulikuwa umeshafika hata bila ya kujiandaa.
‘’Ngoja nitangulie kanisani ‘’Aliongea na kuinuka kuelekea.
‘’Sawa baba namimi nakuja sasa hivi’’Alimjibu na kuingia ndani kubadili nguo alizovaa awali ambazo zilikuwa ni sare wanakwaya.
_________________
Jioni ilinikuta mle ndani huku nikipata ubaridi mkali ambao nyakati za usiku uliongezeka kutokana na na kukaa sakafuni.Nilimwomba Mungu aniepushie mateso zadi kwani niliamini sikustahili mateso yale, niliwakumbuka wazazi na mdogo wangu ambao niliamini kuwa siku moja ningekuja kuonana nao tukafurahi na kuongea pamoja.Lakini nilikuwa ni kama kujipa matumaini ya kutokufa wakati kifo ni haki ya kila kiumbe aliyepo duniani.
Nilitamani kuuza sehemu ya mashamba niliyoachiwa lakini nilijikuta napingana na wazo hilo kwani nilijua baadaye ningenyang’anywa mashamba yote na wale watu ambao wangekuwa na uwezo wangeniua mapema ili waitwae ardhi ile ambayo wazazi wangu walinisisitizia kuitunza na kuitumia mimi na familia yangu kama ningebahatika kuiunda huko mbele.
Usiku ule wa mateso uliisha nikiwa sina hata lepe la usingizi huku baridi na mawazo vikiwa vikwazo vya mimi kulala.Nilisikia sauti za watu ambao wengi wakinilalamikia mimi kwa kitendo cha kuchoma mashamba yao ambayo wengi waliyategemea .Njaa ambayo usiku mzima ilionekana kuzidiwa nguvu na fikra nyingi ilionekana kuchukua nafasi asubuhi ile lakini sauti zilizosikika nje zilionekana kunikatisha kabisa tamaa.
‘’Jamani kitoto hiki chenye laana mkilete tukimalize kwa mawe hapa nje’’Ilisikika sauti ya kijana mmoja ambaye ni kama alinitahadharisha juu ya hatari iliyokuwa kule nje.
‘’Yaani kitoto hata shule hakijamaliza kinavuta bangi?’’Aliongea mama mmoja ambaye sauti yake sikuitambua, jambo ambalo lilinifanya nishtuke kwani katika maisha yangu sikuwahi hata kuiona hiyo bangi sembuse kuivuta.
‘’We mtendaji kama una hela sio sisi hapa tuleteeni hako katoto kama hakana hela kakauze mashamba tupewe fidia yetu’’Ilisikika sauti nyingine ambayo niliigundua alikuwa ya binamu yangu ambaye hata sikujua kama alikuwa na shamba maeneo yale.
‘’Mie nilisema hiki kitoto kikiendelea kubaki hapa ni laana tuu tukifukuze ama hata kukiua tuu’’Ilisikika sauti ya baba yangu mdogo ambaye naye hakuwahi hata kupokea salamu yangu licha ya kumsalimia kila nilipomwona.
‘’Eee, Mungu inusuru roho ya,’’Kabla hata sijamaliza sentensi ile nilikiona kitasa cha mlango ule kikizungushwa hali iliyonifanya nitetemeke kwa uoga.
Mke wa mtendaji wa kijiji aliingia mle ndani na kuninongóneza kitu, ambacho sikukisikia vizuri kabla ya kutokea mlango wa nyuma wa ile ofisi. Sikusikia chochote zaidi ya ishara yake ya mwisho wakati anatoka ambayo ni kama alinikataza kitu Fulani.
Dakika chache baada ya yule mama kutoka nilisikia sauti za kuzungushwa kitasa cha mlango wa chumba nilichokuwemo jambo lililoongeza uoga.Harufu ya kilevi ilitangulia kabla ya Mtendaji wa kijiji ambaye licha ya kuwa ilikuwa asubuhi alionekana kuzidiwa na pombe aliingia na mgambo wawili akiwemo baba yangu mdogo waliingia na kunisimamisha kwa nguvu.
Nilipelekwa ofisini lakini kosa kubwa nililofanya ni kutaka kukaa kitini hali iliyomfanya ,mtendaji anipige kofi lililonipeleka sakafuni na kunisababishia jeraha ambalo hadi leo hii nina kovu lake kwenye paji langu la uso.Nilisimama huku nikiugulia maumivu ya uso wangu huku nikiona nyota kwa dakika kadhaa kabla ya kupata mwangaza sahihi na kuona watu si taswira tena zilizotokana na kipigo.
Niliwaangalia watu waliokuwepo pale ofisini lakini sikumwona mtu yeyote ambaye angekuwa msaada kwangu kuanzia Diwani hadi Mwenyekiti wa kitongoji ambao waliokuwa wakiyataka mashamba niliyoachiwa na wazazi wangu ambao hawapo tena Duniani.
‘’We mtoto unatakiwa kuwalipa wananchi wote hapo nje’’Aliongea Diwani akininyooshea kidole bila kujua alinizidishia hasira kwani katika vitu ambavyo sikupenda kufanyiwa licha ya umri wangu mdogo ni kunyoshewa kidole huku ukiongelewa vibaya.
‘’Tunaongea na kisiki mbona hutujibu?’’Aliongea mzee mwingine ambaye naye nilimweka kwenye kundi la wale wengine licha ya kutowahi kumwona.
Nilibaki nawaangalia kwa zamu wazungumzaji bila kuwajibu kitu chochote jambo ambalo niligundua kuwa niliwaudhi kutokana na jinsi walivyoniangalia kwa macho makali.Wakati naendelea kuwaangalia kwa zamu mwenyekiti wa kijiji alisimama na kuniletea karatasi niandike jina langu sehemu ya chini kabisa ya ile karatasi.
Nilitapotaka kupokea ile karatasi na kuisoma nilizuiwa huku nikisisitiziwa kuandika jina langu jambo lililonifanya niongezewe kipigo kutoka kwa mtendaji kata ambaye alionekana kuchukizwa na ujeuri wangu.
Licha ya kipigo kutoka kwa Mtendaji kata sikuandika jina langu zaidi ya kutaka kuisoma ile karatasi na kuwafanya washauriane kwa muda kabla ya kuniingiza tena ,mle ndani ambako nilikuwa sina nafasi ya kwenda haja zaidi ya kujitengea upande wa kukaa na kujisaidia.
Kwa msaada wa chakula kutoka kwenye familia ya Mchungaji nilimaliza wiki mbili mle ndani huku nikishindwa kabisa kujua hatima yangu hadi pale Yule rafiki yangu ambaye niliamini ndiye ndugu yangu wa pekee hapa duniani alipokuja kutoka kwenye semina na kunitoa kwa dhamana na kuwalipa fidia wale walioathirika na janaga nililokuwa nimesababisha.
Badala ya kufurahia malipo yao wengi walionekana kukerwa na kitendo cha kulipwa pesa zao ambazo walidai ndiyo sababu ya kuniweka ndani kwa muda wa wiki mbili .Kilio cha wengi kilikuwa ni kunifukuza pale kijijini wakiamini nilikuwa ni laana huku viongozi na wafanya biashara wakiyataka mashamba niliyokuwa nikiyamiliki hasa baada ya kujua kuwa yalikuwa katika eneo zuri kwa Mradi mkubwa wa maendeleo hivyo ningekuwa mnufaikaji mkubwa wa Mradi huo.
Shuleni nako licha ya sababu ya kutohudhuria shuleni kujulikana nilikutana na adhabu ambazo ziliniweka nje ya darasa kwa zaidi ya wiki mbili na nusu.Nilifanya adhabu hizo huku nikimwomba Mungu anijalie uvumilivu kama wazazi wangu walivyonitaka kufanya hivyo kila nikutanapo na matatizo enzi za uhai wao.
Nilipata pigo mara baada ya kusikia yule Bwana Mifugo ambaye niliamini ndiye rafiki na ndugu yangu wa pekee ambaye alikuwa amebaki duniani kupata uhamisho ambao nao ulionekana ni kama kupangwa na kusababishwa na wale viongozi ambao walimwona kama sababu ya jeuri yangu.Nakumbuka siku niliyopata taarifa hiyo nilishindwa hata kwenda kanisani nikijifungia chumbani kwangu nikilia kwa uchungu hadi pale mtu huyo aliponihakikishia kuwa angenihamisha nikaishi naye.
Tofauti na mipango yangu tumaini langu lilizimika baada ya mtu yule kuugua ghafla na kupoteza maisha siku chache kabla ya kuhama jambo lililowavuta wengine kwenye kundi la walionichukia nikionekana kweli nilikuwa ni laana na hatari kwa yeyote ambaye angeweka ukaribu nami.
Hata familia ya Mchungaji niliona ikiwa mbali tofauti na awali jambo lililonifanya nitamani kufa kwani niliona dunia haikufaa tena kuwa makazi yangu.Nilijiona ni kama Swala aliyekuwa katikati ya kundi la simba wenye njaa nikisubiri tuu kufanywa kitoweo.
Nilibaki peke yangu tena, sikuwa na marafiki wala ndugu waliokuwa wapo upande wangu zaidi ya wazazi wangu ambao niliokuwa nikiwaota karibu kila siku wakinisisitizia kutokata tamaa.Niliwakubalia usingizini lakini kila kulipokucha nilitamani mawio yafike ili nikaburudishwe na ndoto za matumaini nilizokuwa nikiziota.
________________
Nilikuja kushtuka usiku wa manane na kujiuliza nilipokuwa , huku kumbukumbu za nyuma zikinifanya nitamani kupambana na si kurudi nyuma .Niliona hakukuwa na mateso niliiyoyapata maishani kama yale yaliyopita na si kukurupushwa na wale wanaume ambao sikuwa na uhakika kama kweli walikuwa wanachuo ,nilihisi ni vibaka tuu.
Sikupata usingizi hadi asubuhi nilipojikuta nililala kwenye nyumba ambayo ilikuwa kwenye ujenzi baada ya kusikia kukurukakara za mafundi waliokuwa wamejihimu sana kazini.Kwa kujificha niliondoka eneo lile huku nikijiuliza kwa kuelekea kwani sikuwa na begi langu ambalo lilikuwa na nguo nakiasi kidogo cha pesa ambazo sikuwa na uhakika kama zingenifikisha Kilolo.
Taratibu niliinua na kuanza kutembea nikitoka nje ya lile jengo ambalo lilinihifadhi usiku kucha bila kuonwa na yeyote kati ya wale mafundi waliokuwa upande wa pili wa lile jingo ambalo mwenye nalo ni kama alikuwa amelikumbuka baada ya kulitelekeza kwa muda mrefu.Akili yangu ikawaza matukio ya usiku uliopita huku kumbukumbu ya maisha yangu ya nyuma zikijirudia kichwani na kuniumiza nikiumia zaidi baada ya kujiona mtu mwenye mkosi zaidi duniani lakini nikaamua kumwachia Mungu ambaye niliamini katika yeye hakuna kinachoshindikana.
Sikujua wapi kwa kuelekea wakati ule, nilijua kuwa sikuwa na begi la nguo tena zaidi ya hela ya nauli ambayo nayo sikuwa na uhakika kama ingenifikisha nilikokuwa naenda.Wazo la kwenda tena kwa Eliza mwenyeji wangu ambaye aliniachia majanga usiku uliopita lilinijia lakini hofu ya kupigwa tena ilinijia na kuniogofya.Baada ya kujishauri sana niliamua kwenda kwa Eliza kujari kbahati yangu ya kuchukua nguo zangu kasha kuwahi gari la kwenda Dabaga ingawa sikuwa na uhakika wa njia sahihi ya kunifikisha kwa Eliza niliamua tuu kufuata njia iliyopanda kwani kumbukumbu zangu zilinieleza kuwa usiku uliopita nilikuwa nikishuka.


Baada ya kuzunguka kwa zaidi ya nusu saa nilifanikiwa kuiona nyumba ambayo jana yake nilianzia kulala hapo kabla ya kwenda kwenye jumba lililokuwa likijengwa na kwa mbali nilimwona Eliza akiwa na wenzake wawili wakifua nje ya nyuma ile.Taratibu na kwa makini niliangalia kama palikuwa na mtu mwingine ambaye angehatarisha usalama wangu kama ilivyokuwa usiku uliopita lakini hadi nawafikia Eliza na mwenzake hakukuwa na mtu mwingine zaidi yao ambao baada ya salamu walinipa pole kwa tukio lililokuwa limetokea usiku uliopita na kuniomba msamaha kwa walichokuwa wamekifanya wale wavamizi ambao walikuwa wamekosea chumba walichokuwa wameelekezwa kuwa mtu waliyekuwa wakimtafuta.

Kumbe walikuwa ni ndugu wa binti ambaye usiku uliopita alikuja pale nyumbani na yule mwanachuo ambaye nilikuwa nimepewa habari zake za kuendekeza zinaa hasa na wanafunzi na ule usiku aliingia na msichana ambaye alikuwa mwanafunzi ndugu wa wale jamaa ambao nilikwepa kipigo chao usiku ule.Purukushani zetu pale nje ndizo zilizomshtua na kuchoropoka na dada wa watu hadi wakati ule hakujulika alikokuwa.

Baada ya habari mbili tatu ambazo kwangu hazikunitoa woga na kunisaulisha kiichokuwa kimetokea jana yake niliwaomba niondoke ili nisije kuchelewa gari kama jana yake.Eliza na rafiki yake ambaye alitambulishwa kwa jina la Janeth walinichukulia begi langu na kunisindikia stendi ya mabasi huku wakionekana kunihurumia sana licha ya kutowaeleza mengi sana yaliyonihusu kwani sikutaka kila mtu ajue mapito nipiayo ambayo niliyaona makubwa sana halafu wenzangu wakawa na magumu kuliko yangu.

Tulisibubi gali kwa muda wa zaidi ya saa tatu tukizungumza hili na lile ilimradi tuu muda upite lakini nikiwa najianda kuingia garini tayari kwa safari Eliza alinipa mfuko mdogo mweuzi ambao sikujua kilichokuwemo ndani na akinitaka nifungue nikiwa garini, nilimshukuru na kuingia garini na nilipofika garini sikuwa na haraka ya kuuufungua mfuko ule zaidi ya kuwapungia mkono nikiwatazama akini Eliza hadi pale gari lilipoondoka na wao kupotea kwenye upeo wa macho yangu.
Gari lilipofika stendi ndogo ya Ipogoro na kusimama ambapo kundi kubwa la watu liliingia garini na kutufanya hata tuliokuwa tumekaa tushindwe hata kuona nje ya gari na kunifanya niweke ule mfuko mweusi kwenye begi bila hata kuufungua na kulikumbatia begi langu nikiwa nimebanwa kila upande na abiria wenzangu na kunifanya nione hatari ya safari ile kwa mara ya kwanza kwani gari lilionekana kuelemewa na mzigo huku abiria wakizidi kupanda garini.
Gari liliondoka kwa shida sana hadi dereva akaomba watu wapunguze mizigo, lakini hakukuwa na abiria aliyekuwa tayari kuuacha mzigo wake na baada ya mabishano ya muda mrefu dereva aliamua kuondoa gari na kuanza safari iliyotupeleka Dabaga kwa tuliokuwa tukielekea Uluti na vijiji vingine vilivyokuwa njia iendaye Madege na gari likiendelea na safari ya kuelekea Bomalang’ombe.Gari lilienda kwa kuyumbayumba hku mara kadhaa baadhi ya mizigo iliyofungwa juu ya gari ikiangua na kuwapa kazi ya kukusanya na kuifunga tena mizigo utingo walikokuwa wamekaa juu ya gari.
Baada ya saa zaidi ya nne za safari ile iliyojaa mashaka tulifanikiwa kufika Dabaga mji mdogo uliochangamshwa na shughuli mbalimbali zikiwemo kilimo cha matunda na viazi mviringo pamoja na biashara ndogondogo.Abiria wengi tuliokuwa tukiishia pale ama kuendelea na njia nyingine mbali na ile ya Bomalang’ombe tulishuka na kufanya utaratibu wa malazi huku nikifikiria mahali ambapo ningepumzisha ubavu wangu kutokana na kutokuwa na pesa ya kutosha.
Nilichukua begi langu na kwenda kukaa mbali kidogo na pale palipokuwa na mkusanyiko wa watu.Hapo wazo la kufungua mfuko mweusi niliokuwa nimepewa na Eliza lilinijia na nikaamua kufungua ambapo nilikutana na suruali mpya ya kitambambaa na simu ndogo ya mkononi ambayo ilikuwa na redio , tochi na kadi ya kuhifadhia muziki.Niliiwasha ile simu na baada ya muda nilipokea ujumbe ulionitaarifu kuwa ilikuwa ni zawadi yangu kutoka kwa Eliza ambaye alidai kuwa alikuwa akinihurumia sana kwani aliamini nilikuwa kwenye matatizo makubwa nilijaribu kutuma ujumbe kama kulikuwa na salio la muda wa maongezi ujumbe ukatumwa na kumfikia mlengwa ambaye wakati huo huo alinipigia na tukaongea machache akinitakia safari njema nami sikuwa na mengi zaidi ya kumpa shukrani kwa wema aliokuwa amenitendea.
Nilirudisha suruali ile kwenye begi na kuweka simu mfukoni huku nikiwa na wazo la kwenda kununua chakula kwani tumbo langu lilionekana kuwa tupu likitoa milio mingi ya kulalamika kukosa chakula.Nilipofika kwa wauza chakula nilifanikiwa kupata wali maharage ambao baada ya kula vijiko vitatu nilijikuta nikisita kuendelea kuula kwani nilikutana na mifupa ya samaki, harufu ya mchuzi wa nyama huku nikitonesha jino langu lililokuwa limetoboka kwa mchanga uliokuwa kwenye chakula hiyo ambacho si kwamba nilikuwa nimepewa bure bali nilikuwa nimenunua kwa pesa ambayo niliamua kuitumia na kesho yake nitembee badala ya kupanda pikipiki hadi mahali fulani ili nipunguze umbali wa kwenda huko Uluti.
Nilijikuta nikijilaumu kwa kununua chakula na badala yake ningeenda kuchukua chumba cha kulala kwenye nyumba ya kulala wageni.Nikajikuta nikiamini ule msemo wa Majuto ni mjukuu na kuondoka pale nikiwa na maumivu makali ya jino nililokuwa nimelitonesha baada ya kutafuna mchanga kwenye wali ule ambao bila shaka yoyote ulikuwa ni mabaki ya vyakula vya wateja wengine.Sikuwa na uelekeo maalum zaidi ya kwenda mahali ambapo hapakuwa na watu ili nikae peke yangu nikitafakari mahali pa kwenda kulaza mbavu zangu kwani usiku ulikuwa ukiingia.
Giza lilinikuta nikiwa chini ya mti mmoja ulikuwa mbali na nyumba za watu huku akili yangu ikinituma na kuwa ningekaa pale hadi panakucha lakini baada ya giza kuingia kabisa kuna jambo lilinitisha na kunifanya nisogee kulikokuwa na watu ambako ni kwenye migahawa na vilabu vya pombe ambako kulikuwa na watu wengi walikuwa wakinywa na kula.Jambo hilo lilikuwa ni mizunguko ya mbwa waliokuwa eneo lile wakipiga kelele wakikimbizana kuelekea upande niliokuwa nimekaa nikisikiliza muziki mzuri uliokuwa ukitoka kwenye ile simu mpya niliokuwa nimepewa zawadi.
Kilabuni nilikutana na watu wengi niliokuwa nimesafiri nao kutoka Iringa mjini lakini pia nilikutana na sura mpya ambazo nilijua kuwa walikuwa ni wenyeji mahali pale kwani wengi walionekana kuzungumza Kihehe huku wakifarijiwa na ulevi ambao uliwahamishia kwenye ulimwengu wa tofauti kabisa huku ugomvi wa hapa na pale ukilifanya eneo hilo kuwa na kelele wakati wote niliokuwepo pale.Kwa kuwa sikuwa mteja wala mtumiaji wa kilevi chochote niliamua kutoka ndani ya kilabu na kuzunguka zunguka huku na huko ili mradi nipoteze muda asubuhi ifike niendelee na safari yangu ya kwenda Uluti.
Mizunguko isiyokuwa na uelekeo maalum ilinirejesha kilabuni ambako nilikutawatu wengi niliokuwa nimewaacha awali wakiwa wameshaondoka.Nilijilaza kwenye benchi lililokuwa nje ya kilabu kile ambalo halikuwa na mtu huku nikikumbatia begi langu la nguo hadi pale niliposhtuka na kukuta kuna ukimya wa hali ya juu katika eneo lile.Nilipochukungulia ndani ya kilabu kile kilichokuwa cha mabanzi ya mbao nilikutana na mwanga hafifu wa kibatari na sauti za miguno ya watu ambao kwa haraka haraka nilijua kuwa walikuwa wakivunja amri ya sita.
Nikaamua kuzunguka zunguka tena lakini mji ule mdogo ulikuwa kimya sana hadi nilipofika kwenye kilabu kingine ambacho kilionekana kuwa na watu wengi kidogo lakini wakiwa kama kwenye ugomvi kwani matusi na tambo za hapa na pale zilisikika na kunitisha kidogo.Nikaamua kuifuata njia nyingine ambayo nayo ilinifikisha kwenye majengo ambayo nilikuja kugundua kuwa yalikuwa ni ya shule nikaingia kwenye darasa moja na kujilaza juuu ya dawati huku usingizi ukigoma kabisa kuja nikabaki nimetumbua macho huku nikipigwa na baridi kali.
Mara maumivu ya jino yalianza tena safari hii yaliongezeka mara dufu na kunifanya nitokwe na chozi , nililala , nikakaa nikainuka na kutembe atembea lakini maumivu yalizidi kuongezeka na kuendelea kuniliza bila kutoa sauti.Nikaamua kwenda kwenye kilabu cha mwisho ambapo nilisikia watu wakitukana kwenda kumwonba mtu yeyote kama alikuwa na dawa ya kutuliza maumivu.Nilipofika niliwakuta watu wachache ambao baada ya kuwasalimu na kuwaeleza shida yangu kila mmoja alidai kuwa hakuwa na dawa yoyote ambayo ingenisaidia na baadaye mmoja walinipa wazo ambalo lilikuja kukubaliwa na wenzake.
Alishauri ninywe pombe ambayo aliamini ingeniondolea yale maumivu lakini nilipodai kuwa sikuwa hata na shilingi mia moja wakanipa kikombe kizima cha pombe ya kienyeji ambapo kwenye maisha yangu sikuwahi hata kuonja pombe lakini kutokana na maumivu niliyokuwa nayo niliafikiana nao na kuanza kuibwia ile pombe ambayo si tuu ilinikera kwa harufu yake , bali ladha na ubaridi wake vilishtua tumbo langu na minyoo yake ikaanza kuhaha huku na huko kuusakama utumbo wangu.Nikiwa katika hali ya kutaka kutapika baada ya kubwia kikombe kimoja cha pombe nilipewa kingine na kitakiwa kuinywa kasha nikaambiwa nipumzike kwa dakika kama kumi hivi kasha ningeona nafuu lakini baada ya dakika kama kumi nilianza kuhisi kichwa kikizunguka huku midomo imekufa ganzi.Sikusikia tena maumivu bali midomo ilikuwa mizito na macho pia hayakuwa yakifanya kazi vizuri kwani nilikuwa nikiwaona watu wakiwa wawili wawili na hata begi langu sikuliona moja bali niliyaona mawili na kunifanya nipapase na kulichukua.
Ulevi.
Kweli nilikuwa nimelewa kwani hata nilipotoa simu ili niangalie muda lakini sikuweza kusoma muda badala yake niliirudisha ile simu mfukoni nikikwepa mwanga wake.
‘’Kumbe una simu, uza hiyo simu ukapate pa kulala’’Aliongea mama mmoja aliyekuwa ameshikwa kiuno na mmoja wa walevi waliokuwa pale kilabuni ambaye baadaye nilimkumbuka kama nilikuwa nimesafiri naye kutoka Iringa Mjini.
‘’Ndiyo uza kijana halafu kesho utapata hata bodabada ya kukufikisha uendako yaani unateseka hivyo halafu una simu nzuri kabisa?’’ Aliongeza mwenzake na kunifanya niitoe tena ile simu bila kuiwasha niliiangalia na kuirudisha tena mfukoni.
‘’Kijana uza mie nikupe hela hapa ukalale kesho usipate shida ya kusafiri’’Yule kijana ambaye nilikuwa nimesafiri naye kutoka mjini aliongea kilevi akihamisha mikono yake hapa na pale kwenye mwili wa mwanamke aliyekuwa amemshika.
Nilijikuta nikijilaumu kuwaelez kuwa nikiuwa ninataka kusafiri kesho yake kwa miguu baada ya kukosa nauli ingawa niliwadanganya kuwa nilikuwa nimeibiwa garini lakini nilijikuta naogopa kwani kwa kutowauzia wangeweza nivizia na kuninyanganya ile simu hasa katika ile hali ya ulevi ambayo nilikuwa nayo kwa wakati ule.
‘’Kuna mwenye elfu hamsini nimuuzie?’’ Niliuliza kwa sauti ya taratibu ambayo kila aliyeisikia alijua kuwa ilikuwa inatoka kwa mtu anayeshindana na ulevi.
‘’Hamsini hapana labda elfu thelathini’’Aliongea mwingine ambaye naye alionekana kuelemewa na ulevi.
‘’’Thelathini na tano nakupa’’Yule kijana aniliyesafiri naye aliongea akinishika mkono kuniinua na tukatoka nje huku akiwa na yule mwanamke aliyekuwa amemshika tangu ndani.
‘’Poa kaka lakini unipe keshi’’Niliongea wakati huo tulikuwa tukitembea kuelekea barabarani kabla ya kuivuka na kufika kwenye nyumba ya wageni iliyokuwa ng’abo tuu ya barabara ambapo kwa wakati ule ndipo nilipogundua kuwa palikuwa na umeme baada ya kukerwa na mwanga wa taa zilizokuwa zikiwaka nje ya jingo lile na kunifanya nizibe uso wangu kwa viganja.
‘’Twende kule nakulipia chumba upumzike nakupa na pesa yako’’Alinijibu wakati huo tulikuwa tukiiingia ndani ya nyumba ile baada ya kufunguliwa na mama mmoja aliyekuwa ametoka usingizini.
‘’Sawa nilimjibu kisha nilisalimiana na yule mama aliyetufungulia niliyekuja kugundua kuwa alikuwa mhudumu kwenye nyumba ile ya wageni.
Lakini baada ya yule kijana kulipia shilingi elfu mbili kwa ajili ya kulala usiku mmoja nilimtaka tuandikishane na yule mama nikimwomba awe shahidi wetu ili kuepuka kukiukwa kwa makubaliano yetu kuhusu malipo ya ile simu niliyoamua kuiuza.Yule mama alitoa katarati ambapo niliandika maelezo juu ya kuuzwa kwa ile simu na namna malipo yatakavyofanyika nikatia saini na yule mama na kijana aliyekuwa akinunua simu wakafanya hivyo kasha nikaandika kwenye karatasi nyingine mbili namna hiyo hiyo kisha tukaweka saini na kila mmoja akawa na nakala ya makubaliano yale yaani muuzaji mnunuzi na shahidi.
Kwa mwendo wa kilevi nikaongozana na yule mama hadi chumba nilichokuwa nimelipiwa kasha nikaangia kulala nikiwacha yule kijana na yule msichana aliyekuja naye wakiingia kwenye chumba kingine.Usiku niliamshwa na maumivu ya jino ambalo lilikuwa limeongeza kuuma nadhani baada ya ile ganzi la pombe kuisha.Machozi yalinishuka huku nikiwa nimeshika tama kwa viganja vya mikono kana kwamba nilikuwa nikizuia shavu lisianguke.Mateso ya maumivu hayo yalinifanya nikose usingizi hadi alfajiri ambapo yalipungua ambapo nilitoka kujisaidia kwenye choo kilichokuwa cha nje.
Baada ya kujisadia nikaingia bafuni kuoga licha ya baridi kali niliyokuwa nayo lakini harufu ya pombe niliyokunywa nilihisi ikitoka kwenye kila sehemu ya mwili wangu na kunifanua ninuke pombe kama pipa la kuhifadhia pombe hali ambayo sikuipenda kwani kabla ya hapo sikuwahi kunywa pombe na zaidi nilikuwa nikikerwa sana na harufu yake.
Nilipomaliza kuoga nikarudi chumbani lakini wakati naingia chumbani nilipishana na mtu ambaye kama niliwahi kumwona mahali lakini sikukumbuka ni wapi niligundua kuwa naye alikuwa akinikumbuka kwani aligeuka kutaka kuthibitisha alichokuwa amekiona alivyogeuka name nilikuwa nageuka haraka haraka akaacha nami na kuendelea na mambo yake.Niliporudi kitandani nikawa namfikiria sana yula mtu niliyekuwa nimepishana naye nikijaraibu kukumbuka wapi nilipokutana naye kabla lakini sikupata majibu hadi nilipopitiwa na usingizi.
Nilikuja kushtuka saa nne asubuhi baada ya kusikia mlango ukigongwa kwa nguvu, nilipotoka kwenda kumwangalia mgongaji alikuwa ni yule mama ambaye alinitaka nitoke chumbani kupisha usafi ufanyike pia muda wa kukaa mle ndali ulikuwa umeisha hivyo kma nilitaka kuendelea kukitumia chumba basi nilitakiwa kuongeza pesa.Kwa kuwa sikuwa na pesa nikaamua kutoka na begi langu kabisa nikimsubiri amalize kufanya usafi halafu nimuulize kuhusu yule kijana na hela yangu ya simu ambayo nilikuwa namdai.
Baada ya yule mama kumaliza kufanya usafi nilimuuliza kuhusu hilo jambao akanieleza kuwa yule kijana alikuwa ameelekea kazini lakini angerudi saa sita hivyo alikuwa ameahidi kuniletea hela iliyokuwa imebaki kunilipa.Kwa kuwa nilikuwa na uhakika kuwa gari la kwenda karibu na nilikokuwa naedna lingefika saa tisa ama saa kumi nikaona hakukuwa na hatari yoyote ya kukosa gari nikatoka nje ya ile nyumba ya wageni na kwenda kukaa kwenye kibanda kimoja kilichokuwa na fundi cherehani nikisikiliza hili na lile utoka kwa wenyeji wangu amabao walikuwa waongeaji wakubwa nami nikiwa msikilizaji ambaye sikuwa na mengi ya kuchangia hasa abaaada ya wazungumzaji hao kutumia sana lugha ya Kihehe ambacho sikukielewa zaidi ya kudaka neno moja moja lililofanana ama na neno la Kiswahili au la lugha yangu ya Kimanda.
Niliwasikiliza na moja ya jambo lililonivutia pengine kunistaajabisha ni kuhusu utaratibu uliowekwa pale kijijini hasakatika kuepukana na tabia za uzinzi kwa wanafunzi , ilikuwa ni arufuku kwa kijana yeyeote wa kiume asiye mwanafunzi kusimama na mwanafunzi wa kike iwe has njiani maeneo mengine yasiyo ya kanisani , shuleni na kwingineko na ukikamatwa ni ndani bila mjadala.Jambo hilo niliiezwa baada ya kumwita binti mmoja aliyekuwa amevaa sare za shule aliyepita njiani mbele ya kibanda nilimokuwa nimekaa nikiwa na lengo la kumuuliza kama kulikuwa na uhitaji wa walimu wa masomo niliyokuwa nasomea ili nikaombe nafasi ya kwenda kufundisha huko alikokuwa akisoma nikiwa na lengo la kupata pesa ya kwenda kulipa shuleni baada ya kufungua.
Maneno yao yakanifanya niahirishe jambo hilo na kuanza kuwaulizia walipokuwa wakifanya kazi wale vijana ambao mmoja wao nilikuwa nimemuuzia simu. Nikaambiwa kuwa walikuwa wakipakia mapeasi kwenye magari kasha kupeleka Iringa Mjini na nilipouliza kama wangewahi kurudi nikaambiwa kuwa ingetemea na walipokuwa wameenda kukusanya mapeasi kwani kuna wakati hurudi usiku sana kutokana na umbali na ubovu wa njia za kwenda huko shambani hasa kwa kipindi kile cha mvua.
Hofu ya kudhurumiwa iliniingia lakini nikapiga moyo konde na kuamini kuwa siku ile wangewahi kwani yule kijana aliniahidi kuwa asingenidhurumu.Lakin kutomfahamu yule mtu nako kulinifanya nione dalili za kutopewa hela iliyokuwa imebaki licha ya kuwa na makubaliano ya maandishi kuhusu kupewa ile hela.Niliamua kutoka na kwenda kwenye mashamba ya mapeasi ambako niliambiwa walikuwa wakifanya kazi huko lakini sikumkuta mtu zaidi ya lundo la mifuko iliyojazwa mapeasi na nilipozunguka huku na kule kuwauliza watu kuhusu walikokuwa vibarua wale niliambiwa kuwa walikuwa wameshaondoka na mzigo kuelekea mjini na wangerudi siku iliyofuata.
Nikajikuta nikijilaumu kwa upumbavu wangu wa kumwamini mtu niliyekuwa simfahamu tena ugenini, nikarudi hadi pale kwenye nyumba ya kulala wageni lakini wakati naenda nilipishana na mtu niliyemwona alfajiri wakati natoka kuoga.Alikuwa juu ya pikipiki ambapo alinitazama akipunguza mwendo kasha kuondoa pikipiki kwa mwendo mkali ambao kila aliyemwona alijikuta ama akishika kichwa kwa mikono yake miwili au akiziba mdomo kwa mashangao.
Nilipofika kweye ile nyumba ya wageni nilimkuta mvulana mmoja ambaye alikuwa zamu muda ule nilipomuulizia kuhusu mama aliyekuwa hapo awali akaniambia kuwa aliondoka kwenda nyumbani kwake hivyo angerudi jioni.Nilipouliza alikokuwa akikaaa akanieleza kuwa alikuwa akikaa kijiji cha pili kutoka hapo na kunifanya nipoe nikiwa sina cha kufanya.
‘’Kwani uliacha chenji kwake?’’ Aliniuliza yule kijana akiniangalia usoni.
‘’Hapana ila alikuwa shahidi kwenye jambo hili’’Niliongea nikimpa ile karatasi iliyokuwa kama makubaliano kati yangu na yule kijana niliyekuwa nimemuuzia simu.
‘’Nisomee mie nimeshika maji’’Aliongea yule kijana akinirudishia ile karatasi ingawa nilimwona alikuwa na mikono mikavu nikaamua kumsimuliza sehemu ya kisa kile.
‘’Anhaa! Pole sana ile kama mtu mwenyewe ameshandoka unadhani atakusaidiaje?’’
‘’Kwa kuwa huyo mtu alichukua chumba hapa na vitu vyake vipo ndani najua atarudi hivyo niliaka nijadiliane na huyo mama hata uwezekeano wa kulala hapa kwa makubaliano kwamba yule kijana akija kunilipa atavyokuja hiyo kesho basi nilipe’’
‘’Da! Unadhani itawezekana, kwani simu yenyewe iko wapi nikupe hela halafu we uendelee na safari yako?’’
‘’Simu anayo huyo kijana na ameondoka’’Nilimjibu kinyonge.
‘’Ulikosea ilitakiwa usimpe hadi atapokumalizia hela yako’’Alitoa ushauri ambao nilingeuona wa maana kama ningepewa kabla ya yote kutokea.
‘’Sikujua kama angeondoka bila kunilipa’’Niliongea nikitoka na kuelekea kibandani nilipokuwa nimeacha begi langu kwani nilijikuta nikiingiwa na hali ya kutomwamini yeyote.
Nilipofika nilipokuwa nimeweka begi nililichukua na kumfuata Yule kijana ambaye alikuwa kwenye ile nyumba ya wageni na na kumwomba anielekeze kwa Yule mama ili niende kwake nijue kama naye angeweza kunisaidia.Lakini kwa maneno ya Yule kijana kuhusu Yule mama niliona kma ningejisumbua tuu hivyo nikaamua kuachana na jambo la simu na kujaribu kufikiria njia nyingine ya kwenda nilikokuwa naenda na kuhesabu kuwa nilikuwa nimeshadhulumiwa.
Baada ya kufikiria kwa muda mrefu nikajikuta sina cha kufanya na wakati huo gari la kwenda karibu na nilikokuwa naelekea lilikuwa limefika na mizigo mbalimbali ilikuwa ikishushwa.Nilitamani nipande gari lakini sikuwa na pesa hivyo nikajikuta sina cha kufanya hadi nilipoamua kuondoka karibu na lile gari na kwenda kukaa mbali kidogo nikitazama jiografia ya kijiji kile ambacho kilionekana kama mji kwa wenyeji wa mzingira yale.Kijiji kilichotawaliwa na ukijani uliotokana na misitu ya asili na ile ya kupandwa pia mashamba makubwa ya mapeasi na Chai yalizidi kuifanya mitelemko na miinuko iliyozunguka kile kijiji kuzidi kuvutia.
Kwa mbali nilisikia gari likiondoka na kunirudisha tena kwenye mawazo ya safari yangu ambayo nilikuwa nimeisahau baada ya kuzama kwenye mawazo juu ya mwonekano wa kijiji kile. Fikra za safari zikanifikisha kwenye wazo moja mabalo nilihisi kuwa lilikuwa limechelewa kuja kichwani lakini licha ya kuchelewa kwake niliona lingenisaidia kidogo.
Lilikuwa ni wazo la kuuza baadhi ya nguo ili nipate chakula na kulipia sehemu ya kulala, taratibu nilijisogeza kwenye kibanda cha fundi na kutoa suruali mpya niliyokuwa nimepewa na Eliza mjini Iringa na kumwambia fundi na watu wachache waliokuwa kwenye kibanda cha fundi cherehani kuwa nilikuwa nikiiuza.Kila mtu aliyeiona ile nguo alionekana kuvutiwa na ile nguo lakini nilipowatajia bei yake kila mtu alionekana kutokubaliana nayo.
Kila mtu alidai bei yake ilikuwa kubwa sana tofauti na thamani yan]ke ingawa nilijua nilikuwa nimetaja bei ambayo ni chini ya nusu ya bei ya suruali , shilingi elfu tatu mia tano kwa suruali mpya ya kitambaa ilikuwa ni bei kubwa sana kwa watu wale ambao licha ya kujua kuwa walikuwa ni wakijijini na kuwa huenda hawakujua thamani halisi ya nguo ile kutokana na ama kununua mitumba mnadani ama nguo za kitambaa cha thamani ya chini zaidi ya kitambaa cha suruali ile niliyopewa na Eliza kwani kilikuwa kitambaa cha gharama sana.Nadhani pia kusambaa kwa taarifa kuwa nilikuwa kwenye shida sana kutokana na kukosa pesa ya kula, kunisafirisha ama kulala kuliwafanya washushe bei ya nguo ile wakiamini kwa shida zangu lazima ningewauzia kwa bei waliyokuwa wakiitaka.
Pia tabia ya watanzania ya kupenda kupunguziwa bei wakiamini wauzaji hupandisha bei kwa lengo la kuombwa kupunguziwa nahisi ilichangia kuwafanya wale watu kukataa kununua suruali ile kwa bei niliyokuwa nimewatajia wakiamini niliweka na hela ya kupunguzwa.Hawakujua mwenzao nilikuwa nimeweka elfu mbili ya kulipia mahali pa kulala mia tano ya kula na elfu moja ibaki kulinda mfuko nikiwa nimefikia uamuzi wa kutembea siku iliyofuata bila kuhangaika usafiri wa gari ambao nao ungeniachia saa mbili hadi tatu za kutembea kwani ulikuwa haufiki hadi kijijini nilikokuwa naenda ambako gari ziendazo kule ni gari za kupeleka mitihani ya kitaifa kutokana na ubovu wa barabara haa kipindi kile cha masika.
Wote walipoonekana kutojishughulisha na kununua ile suruali ambayo niliamua kuiuza kutokana na ubora wake kwani zilizokuwa zimebaki kwenye begi zilikuwa chakavu sana na za hali duni sana na zilizokuwa na unafuu ni suruali mbili za shule ambazo zikutaka kuzihusisha kwenye ile biashara kwani nilijua ningeenda kusumbuka sana shuleni baada ya kufungua kwani kwa hali ya hewa ya shule ilipokuwa ilikuwa si ajabu nguo kumaliza wiki moja bila kukauka.Baadaye nilitoa shati la moja la shule ambalo nilikumbuka kuwa liliuwa la tatu kwani nilikuwa nimepewa na rafiki yangu mmoja aliyekuwa amehitimu kidato cha sita na kuliunganisha na ile suruali kwenye ile biashara nikiwatajia bei ile ile niliyotaja kwenye suruali.
Hapo kila aliyekuwepo pale alionekna kuvutiwa na nyongeza hiyo lakini kulikuwepo na wale waliotaka nipunguze shilingi mia tano lakini Yule fundi alizinunua na bei niliwatajia na kunifanya niondoke eneo hilo na kwenda kutafuta chakula kwani machweo yalikuwa yamekaribia na njaa ilikuwa ikiniuma sana.
Nilijisogeza kwenye kibanda kimoja palipokuwa pakiuzwa chakula na kuagiza chakula ambapo nilishtuka baada ya kumwona aliyeniletea chakula , alikuwa ni mtu aliyenikumbusha kitu fulani nilimkumbuka lakini sikuwa na uhakika na mahali nilipowahi kumwona.Naye alionekana kunikumbuka na alishtuka aliponiona, kisha akaleta chakula na kutaka kuondoka kwa haraka lakini nilimwita kabla ya hajaondoka.
‘’Samahani dada tulionana wapi?’’ Nilimuuza baada ya kuitika wito wangu.
‘’’Kwa hiyo hujui tulipoonana basi hatukuonana?’’Aliongea kwa sauti ya utani na kunikera hali ambayo nahisi aliigundua.
‘’Kwa hiyo ningeuliza kama nakumbuka?’’Nikamjibu kwa swali kama yey alivyonijibu awali.
‘’Jana wakati umekuja kulalamika maumivu ya jino’’
‘’Anhaa, ulikuwa na jamaa wa simu?’’ Nilimuuliza baada ya kumkumbuka.
‘’Ya simu mnajuana wenyewe kama mlidhurumiana mie sihusiki’’Alinijibu na kuondoka nilimfuatilia kwa macho hadi pale alipotelea kwenye kundi la watu waliokuwa pale nje ambapo palikuwa na kilabu cha pombe.
Nikala haraka haraka na kutoka kwenda kufuatilia nyendo za Yule dada ambaye naye sikumwona kwani muda niliokuwa nimeutumia kula chakula ulimtosha kwenda ambako nisingemwona.Niilijaribu kumtafuta huku na huko nikiamini kuwa alikuwa na taarifa chache zilizomhusu Yule kijana ambaye alikuwa amenidhurumu kwa kutonilipa hela iliyokuwa imebaki baada ya kununua simu.Nilijikuta nikiumia tena baada ya kukumbuka kuwa nilikuwa nimeuza simu kwa shilingi elfu mbili tuu na mbaya zaidi nilikuwa sijabakiza zawadi yoyote ya Eliza zaidi ya wema wake wa kunipokea ambao ulibaki kuwa akilini mwangu na umebaki hadi hii leo.
Katika harakati za kumtafuta Yule dada nilijikuta nikiparamiana na kijana mmoja aliyekuwa amebeba maziwa kwenye ndoo na kumwaga maziwa aliyokuwa ameyabeba.Kundi kubwa la watu lilisogea mahali tulipokuwa tumesimama na kumshawishi Yule kijana kijana anipige huku wengine wakinitaka nimlipe nakajikuta nimebaki tuu chini nikitetemeka mikono na begi langu mgongoni.
Wote wawili tulikuwa chini huku tukiwa tumezungukwa na kundi hilo la watu waliokuwa wakipiga kelele wengi wakiwa walevi waliokuwa wakinywa kwenye kilabu kilichokuwa jirani.Nilijikuta nikiogopa hata kumtazama kijana niliyekuwa nimeparamiana naye kwa uoga huku nikitegemea kipigo kitakatifu kutoka kwake hadi pale niliposhtuka baada ya kuhisi begi langu limeguswa, naikajua ni Yule kijana ameshainuka na aliamua kunishushia kipigo.
‘’Naomba nisamehe kaka ni bahati mbaya’’Nilitoa sauti ya uoga na kuwafanya watu wacheke na hapo nikaamua kumwngalia aliyegusa begi langu.
Alikuwa ni Yule kijana niliyekuwa nimeparamiana naye kumbe alikuwa ameshainuka na alikuwa akiniinua na kunifuta tope lililokuwa limeharibu kabisa mwonekano wangu kwani hata nilipokuwa kuwa naongea kuomba msamaha nilikuwa nikiwachekesha watu kwani hata uso wangu ulikuwa umezibwa na tope hivyo nilivyokuwa naongea nilikuwa nawachekesha.
‘’Usijali ndugu njoo’’Aliongea Yule kijana kwa upole.
Upole ambao haukunifanya nihisi kuwa alikuwa na jema kwangu zaidi ya kuhisi kuwa alikuwa akinitoa kiaina na kuntafuta eneo la kutaka kuongea kuhusu kumlipa maziwa yaliyokuwa yamemwagika na kwa haraka haraka hela niliyokuwa nayo isingefika nusu ya thamani ya maziwa yale yaliyokuwa yamejaa ndoo kubwa ya lita ishirini ambayo niliiona ikiwa tupu na alama za maziwa ikionekana.
‘’Njoo kaka, usiogope’’Alizidi kuniita kwa sauti ya upole.
Nikaamua kumfuata Yule kaka na kuwaacha watu wakicheka mwonekano wangu uliobadilishwa na tope.Tulitoka eneo lile na kuifuata njia moja iliyoelekea kanisani ambako nilitambulishwa na mnara uliokuwa juu ya jingo hilo.
‘’Pole kaka’’Alivunja ukimya uliokuwa umetawala.
‘’Asante samahani sana kaka sikukuona nilikuwa na mawazo sana’’Niliongea kinyonge.
‘’Usijali kaka yangu kuna mambo nilikuwa nafikiria nilikuwa sijakuona ndo tukaparamiana pale njiani’’
‘’Asante pole kaka kuna matatizo nimekutana nayo yameniweka kwenye mawazo hadi najikuta sina umakini’’Niliamua kumweleza baada ya kuhisi alikuwa mtu mwema kwangu wakati huo tulikuwa tumeshafika kwenye nyumba zilizokuwa mbele ya kidogo ya lile kanisa.Zilikuwa nyumba nyingi za nyasi zilizojengwa kwa mzunguko na kuacha uwazi mkubwa ambao ukiwa na vibanda ambavyo bila kuambiwa nilihisi kuwa vilikuwa ni jiko na vibanda vya kuku ambao niliwaona wakiingia vibandani huku kila jiko likitambulishwa na moshi uliokuwa ukitoka milangoni madirishani na kwenye paa la nyasi liliokuwa limewekwa kwa mzunguko uliofanya mazingira yale yawe katika mwenekano ulifanana na kuvutia.
Pia palikuwa na maghala ya nafaka yaliyotambulishwa na mwonekano wake kwani yalikuwa kama kichancha kilichoezekwa juu yake kwa mtundo ule ule wa jiko na vibanda vya kuku lakini vilitofautina ukuwa na vibanda vingine kwani vyenyewe vilikuwa vikubwa zaidi.
‘’Karibu ndani kaka’’Aliongea yule kijana baada ya kuniona nimesimama nje nikiyaangalia mazingira ya lile boma ambayo nilikuwa nikiyasoma tuu na kusimuliwa kabla ya hapo.
‘’Asante kaka’’Niliongea nikiingia ndani na kupokelewa begi langu na watoto waliokuwa pale uwanjani wakiwa na nyuso za furaha lakini nusura waangue kicheko baada ya kunitazama usoni lakini katazo la ishara usoni kwa kaka yao liliwafanya warudishe vicheko vyao wakiweka akiba na kwenda kucheka jikoni walikoingia huku wakiwa wameziba vinywa kwa viganja vyao.Walistahili kucheka kwani nilichekesha basi tuu ndo staha zetu waafrika walijikuta wakinyimwa uhuru wao kwa kulinda heshima mbele ya mgeni wasiyemfahamu.
Baadaye niliwekewa maji bafu na kuelekezwa kwenda kuoga kwenye moja ya vibanda vilivyozunguka ule uwazi ambacho awali nilihisi kilikuwa ni moja ya zile nyumba kwani kilikuwa kimeezekwa kama nyumba na huko kulikuwa na vyumba tofauti vya bafu na vyoo.Baada ya kuoga na kubadili nguo nilimsimulia kwa kifupi kilichonitokea tangu na toka Iringa na nilipofika kwenye maelezo kuhusu simu nikatishwa na yule kijana.
‘’Kwa hiyo wewe ndiye uliyedhurumiwa simu?’’ Aliniuliza akionekana haamini alichokisikia.
‘’Ndiyo’’ Nilijibu kwa kifupi na kumsikiliza.
‘’Mungu mkubwa!’’ Aliongea akikutanisha viganja vyake akiangalia juu kama ishara ya kumshukuru na Mungu na kuniachia maswali mengi kichwani yaliyokuwa yamekosa majibu.
''Kwani kuna nini?''Nilijiuliza kichwani nikisubiri maelezo juu ya mshtuko wake baada ya kujua kuwa ndiye niliyekuwa nimedhurumiwa simu yangu.
TUTAENDELEA KESHO


0 comments:

Post a Comment