Friday, 8 April 2016

RIWAYA;NI YEYE KWELI SEHEMU YA PILI

‘’Mungu mkubwa!’’ Aliongea akikutanisha viganja vyake akiangalia juu kama ishara ya kumshukuru na Mungu na kuniachia maswali mengi kichwani yaliyokuwa yamekosa majibu.
''Kwani kuna nini?''Nilijiuliza kichwani nikisubiri maelezo juu ya mshtuko wake baada ya kujua kuwa ndiye niliyekuwa nimedhurumiwa simu yangu.
''Mungu ndiye aliyepanga tukutane ndugu yangu , si umesema yule mwalimu wa Uluti ni ndugu yako?''
''Ndiyo''
''Yule mwalimu mkarimu sana alinisaidia nikasoma sekondari nikiishi kwa ndugu yake pale Iringa na kunipa huduma zote kama ndugu yake wa damu, na siku zote nilikuwa nikiwaza jinsi ya kulipa fadhila zake kwangu, Mwalimu Julias ni mtu mwema sana''Aliongea yule mtu huku tumaini la kupata msaada likiongezeka kichwani.
''Kwa hiyo unafahamiana na Baba yangu mdogo?''Nilijikuta nikiuliza bila hata ya kufikiri sana.
''Ndiyo sasa ni ndugu yangu nawe u ndugu yangu nitakusaidia kufuatilia  simu yako ikishindikana nitakupa simu yangu''
''Asante sana ndugu yangu, ila kama nitakosa hiyo simu usihangaike nitapata nyingine''
''Usijali wewe upo safarini mie nipo nyumbani simu haina matumizi sana hata ukienda nayo haina shida''Aliongea.
''Asante kaka usijali tutaipata kwa kuwa nimepata mwenyeji maana ugeni nao ulinifanya nikose uamuzi sahihi''Niliongea wakati huo nilianza kuhisi maumivu ya jino kwa mbali.
Mazungumzo yaliyokuwa na matumaini makubwa kwangu yalikatishwa na maumivu makali ya jino yaliyopelekea wenyeji wangu kunichemshia mizizi na majani ya mti uliokuwa nje na nyumba. Baada ya kuyanywa hali yangu ilirejea katika ukawaida wake kabla ya kuelekezwa pa kulala ambapo nililala na yu;le kijana aliyenileta pale akinieleza wema aliofanyiwa na babaa yangu mdogo ambaye nilikuwa nikielekea kwake.Maneno yake yanilijaza tumaini kubwa sana la kusaidia na ndugu huyo wa baba yangu na kunifanya nijaribu kutabiri picha ya maisha nitakayokuwa nikiishi huko hadi pale nitakaporejea shuleni hadi nilipopitiwa na usingizi huku mikikimikiki ya kutwa ikionekana kusahaulika.
Saa kumi alfajiri kwa mujibu wa saa ya iliyokuwa kwenye simu ya mwenyeji wangu ambaye alidai angeniachia simu hiyo kama ningekosa kupata simu yangu.Haikuwa simu ya thamni sana kama ilivyokuwa simu yangu kwani simu ya mwenyeji wangu ilikuwa ikijulikana kama six button  simu iliyokuwa ya kiwango cha chini sana.Nilijilazimisha kupata usingizi tena lakin i kumbukumbu za maumivu na mateso ya siku iliyopita yanilifanya nikose kabisa lepe la usingizi na kunifanya nisikie kila ukelele na harakati zilizofanyika alfajiri ile.Panya walihangaika huku na huko wakikimbizana kuerejea kwenye maficho yao wakikwepa mwanga ambao ungewaumbua kwa binadamu binadamu nao walisikia kutoka kwenye vyumba vingine wakimshukuru Muumba mbingu na nchi kuwaamsha salama shkrani hizi zilisikika kutoka vyumba vya jirani kwani havikuwa na dari.
Nikajikuta nami nikimshukuru Mungu kimya kimya kwani licha ya kuwa nilikuwa nikienda kanisani sikuwa na mazoea ya kusali asubuhi au jioni kama familia ile ilivyofanya kwani kabla ya kulala nakumbuka familia ile ilijumuika kumshukuru na kumwomba Mungu, nilikumbuka utaratibu niliokuwa nimezoeleshwa na wazazi wangu ambao sikujua hata ni kipindi gani niliupoteza kwani ni mara chache sana nilikumbuka kushukuru na kuomba kabla na baada ya kulala tena nilipokuwa kwenye magumu sana.
Baada ya sala za kipekee kwa kila mtu nilisikia sauti za watu waliokuwa wakisalimiana sebuleni kwa mbali nilimsikia kijana tuliyekuwa tumelala pamoja akimshukuru Mungu kwa sara ndefu sana ambayo kwa kukadiria nilihisi ilichukua nusu saa na kunifanya nijione kuwa nilikuwa sijui kusali si kwa kuomba, kusifu wala kushukuru kama alivyokuwa mwenzagu nikajiapiza kimoyo moyo kuwa nitaanza utaratibu wa kusali kila ilipobidi nikiamini kuwa huenda kutokusali kwangu kulinifanya niingie kwenye mengi magumu.Baada ya ile sara ndefu ya yule kijana mwenyeji wangu tulisalimiana na kujuliana hali zetu kabla ya kuelekea sebuleni tulipokutana na wanafamilia wengine.
Saa mbili na nusu ilinikuta nikiwa nimeongozana na yule kijana mwenyeji wangu na  tulikuwa pale kwenye nyumba ya kulala wageni tukijaribu kufuatilia simu yangu na kwa bahati tulimkuta yule mama ambaye alikuwa kwenye makubaliano ya simu na yule kijana.
''We kijana bado hujaondoka''Aliongea yule mama akionekana kushtuka kumaanisha hakuutegemea uwepo wangu pale wakati ule akipuuza hata salamu tulizokuwa tumempa.
''Shikamoo mama''Tulirudia kumsalimia kana kwamba hatukusikia alichokuwa amekiongea.
''Marhaba hamjambo vijana''
''Hatujambo mama''
''Halafu yule kijana amerudisha simu nimemlipa hela aliyokupa kwa hiyo unipe hela yangu''Alijieleza yule mama.
''Hii hapa nipe chenji''Aliongea yule mwenyeji wangu akimpa noti ya shilingi elfu kumi.
''Sawa lakini subiri mtendaji aje maana aliakuwa ameipokea''
''Alipokea kama nani?''Niliuliza nikionekana kukereka kwani nilihisi kulikuwa na kuzungushwa tena.
''Kama mtendaji wa kijiji hiki''Aliongea kwa hasira kama akiniumbua vile.
''Kama mtendaji ama kaka yako?'' Aliuliza yule mwenyeji wangu.
''Vyote vyote kwani we unaonaje ?'' Sauti ya kiume ilisikika ikisikika kutoka nje ikiiingia pale tulipokuwa.
''Shikamoo''Tulisalimia kwa pamoja.
''Marhaba , kijana mwenyewe ni huyu?''Aliongea yule mtu akininyooshea mkono kana kwamba alikuwa na hasira nami.
''Ndiyo''Alijibiwa na yule mama ambaye nilijua kuwa alikuwa ndugu yake kwani walifanana sana.
''Kwa hiyo kijana unafanya mambo kienyeji tuu, ungetapeliwa ungemlaumu nani?''Sikumjibu zaidi ya kumtazama tuu , na kumfanya aendelee kuongea.
''Kwanza unaweza ukawa jambazi wewe utakujaje kijiji kwangu bila kuripoti kwangu?''
''Nilikuwa nasafiri''Nilimjibu.
''Kama unasafiri si upo kijijini kwangu kwa nini hujaripoti kwangu''Aliongea kwa ukali.
''Huyu ni mgeni wangu kwa hiyo naomba usimsumbue anasafari muda huu mpe simu yake aendelee na safari''Aliingilia yule mwenyeji wangu.
''Na wewe usijifanye mjuaji mie nipo kazini kama utakuwa umemhifadhi mhalifu utajibia wewe''
''Nitajibia naomba umpe simu aondoke''
''We kijana usiniingilie kazini kesi itakugeuka huoni hata rangi na nywele zake zinaonesha kuwa si Mtanzania huyu''Aliongea mtendaji akionekana kuwa na hasira.
''Huo sasa ubaguzi kwani kuwa na nywele na rangi kama za huyu mwenzangu ndio kutokuwa mtanzania?''Aliuliza yule mwenzangu ambaye nilimwona kama ameshtuka baada ya kugundua kuwa licha ya kuwa aliniona nikiwa mweupe lakini hakujua kama nilikuwa na nywele shombeshombe.
''Mwenyewe umeshtuka huenda ni msomali huyo, huoni hata simu aliyokuwa akimiliki ni ghari sana halafu hata kiswahili chake hakifanani na cha kwetu, usije kujiingiza kwenye matatizo kwa tamaa ya kupata hii simu''Aliongea akiitoa ile simu yangu niliyokuwa nimepewa na Eliza mjini Iringa na nilikuwa nimeiuza siku chache zilizopita.
Nilitoa vitambulisho vyangu kuanzia cha shule , kuzaliwa cha mpiga kura na hata cha kipaimara kuonesha kuwa nilikuwa mtanzania na baada ya kuvichunguza na kunitazama yule mtendaji akatokwa na neno.
''Kijana uliyekuwa umemuuzia simu alikuwa ameshapanga kukudhulumu asingekuwa huyu mama kunishirikisha basi usingepata simu yako''
''Asante sana'' niliongea nikiweka vyeti vile kwenye begi langu.
''Nimetumia muda mwingi sana kushughulikia jambo lako , kwa hiyo inatakiwa ukubaliane na mashati yangu''Alingea akinikazia macho yake ambayo wakati huo ndipo nilipogundua kuwa alikuwa chongo.
''Masharti ya nini ,wakati umefanya kazi yako mtendaji?''Yule mwenyeji wangu akaingilia.
''Siongei na wewe kijana , tafadhari usiingilie yasiyokuhusu''Alimkanya yule mwenyeji wangu.
''Huyu ni ndugu yangu , hakuna cha mashareti hapa''
''Angekuwa ndugu yako ungemwacha hadi auze simu yake na nguo zake ili apate kula na kulala, ama hadi anywe pombe kupooza jino lake?'' Aliropoka yule mtendaji hapo nikijikuta nikiamini kuwa viji havina siri kwani katika mambo ambayo sikutaka mwenyeji wangu ayajue ni kitendo changu cha kunywa pombe ili nipooze maumivu ya jino na hata kwenye maelezo yangu usiku wa jana yake sikulieleza hilo.
Nikajikuta naona aibu , lakini nikajikaza kisabuni.
''Hayo hayakuhusu ndugu Mtendaji tunachikuomba mpe simu yake aendelee na safari''Alijibu yule mwenyeji wangu baada ya kuniona nimepoozwa kwa maneno ya Mtendaji.
''Ndiyo maana nasema wewe tamaa yako itakuingiza matatizoni hakuna unachokitaka zaidi ya simu ya huyu kijana na ulokole wako sijui uko wapi huo ni utapeli''
''Kati yangu nawe nani anaitaka simu nimesema mpe aende sitaki simu ya mtu''
''Sasa usiniingilie kazini kwangu''
''Kazi gani unayoifanya? usimsumbue ndugu yangu hapa''
''Sasa kija nitakupa hela aliyokuwa yule jamaa uliyemuuzia simu na nitakuongezea elfu tano kisha uniachie hii simu''Aliongea Mtendaji akiwa amenigeukia.
Niliwatazama wote watatu kuanzia yule mama ,Mtendaji nikimalizia na kwa mwenyeji wangu ambaye alinionesha kwa ishara kuwa nisikubaliane naye.
''Nakupa hela uliyompa yule jamaa unipe simu yangu yaishe''Niliongea nikiwa na uchungu mkubwa kwani niliona dalili za kuonewa nikiona nikiwa nimepoteza zawadi zote nilizokuwa nimepewa na rafiki yangu Eliza.
''Bila kukuhangaiikia ungeipata hii simu''Aliongea yule Mtendaji kwa hasira lakini nami nilimwangalia tuu kwa hasira kama alivyoongea.
''Nakuuliza , ungeipata simu hii bila kufuatilia?''
''Ningeipata Mungu angependa''
'' Basi Mungu hajapenda ,hesabu umedhulumiwa hupati simu wala hela''
''Nani kanidhulumu kati yako wewe unayejifanya mwema na yule aliyenisaidia nikalala?''Nilimuuliza nikiwa na hasira sana kiasi kwamba mikono yangu ilikuwa ikitetemeka.
''Utajijua mwenyewe, hapa simu hupati na hela sikupi''yule mtendaji aliongea kwa ghadhabu.
''Hapo tutafikishana mbali, naomba umpe simu yake akupe hela aondoke''Aliingilia yule mwenyeji wangu.
Ubishi uliendelea kwa takribani dakika arobaini na tano hadi pale nilipokubali kwa shingo upande kupewa shilingi elfu kumi kisha nikamwachia simu yule mtendaji.Nilisikitika sana kwani licha ya kuikosa ile simu na kupewa hela niliskitika kwani licha ya yule mwenyeji wangu kunisaidia sana alionekana kutoridhishwa na uamuzi wa mtendaji yaliyokuwa ya kibabe sana.Kwangu nilitamani kumewachia ile simu yule mwenyeji wangu kama shukrani  badala yake nilitoa shilingi elfu tano katika ile elfu kumi ya simu nkumshukuru mwenyeji wangu ambaye aliikataa sana licha ya kunipa simu yake.
Saa tatu na nusu anga likiwa limetawaliwa na mawingu na ukungu huku matone ya mvua yasiyokuwa na nguvu hata ya kulighasi jani yalidondoka, nilikuwa kwenye barabara iendayo huko Madege nikiwa nimeshaamua kufika Uluti kwa miguu na kama lingetokea gari njiani basi lingenisaidia kunifikisha niendako au karibu na nilikokuwa naenda.
Nafsi yangu ilitawaliwa na mawazo ya yaliyokuwa yametokea  ambayo yalinikera nikajikuta nikifikiria nitakayokutana nayo huko nilikokuwa naelekea lakini yote niliyaona hayakuwa na nuru  hivyo nikahamisha mawazo kwenye ndoto zangu za kuwa na maisha mema tena nikiwa na maarufu.Niliamini kuwa siku itafika nitakuwa mtu maarufu na mwenye maisha mazuri na juhudi katika kila jema nililokuwa ndiyo silaha yangu.
Mvua na jua vilikichoma kichwa changu na huku nikihesabu bila kuizihifadhi idadi ya kona za barabara ile iliyokuwa katikati ya msitu na vilima vingi vilivyochekana kwa miundo na sura zake zilizotisha hadi pale nilipofika mwisho wa safari yangu kijijini Uluti saa mbili usiku nikiwa taabani kwa maumivu makali ya mwili na jino ambalo halikukubali vidonge vya kutuliza maumivu nilivyokuwa nikivitafuna njia nzima.
Mwenyeji wangu ambaye alikuwa ni baba yangu mdogo alinipokea kwa furaha akinipa pole kwa safari yangu ambayo bila hata kumweleza aligundua kuwa ilikuwa ya mashaka na maumivu makubwa kutoikana na mwonekano wangu.Nilioga na kupata chakula ambacho licha ya njaa niliyokuwa nayo nilichindwa kukila kutokana na maumivu makali ya jino.
Siku iliyofuata niliendelea kujipooza kwa uchovu na maumivu ya jino nikiulizia maeneo ambayo ningepata kibarua cha kupanda miti ambapo sikupata kwani wengi walidai msimu wake ulikuwa haujafika hivyo nilitakiwa kusubiri kwa muda kama wa mwezi mmoja.Kwa kuwa likizo yangu ilikuwa ya mwezi mmoja na nusu nilijiona nilikuwa na nafasi ya kusubiri.Katika harakati za kutafuta shughuli za kufanya kwa ujira nilijikuta nikipata kazinyingine ambayo sikupanga kabisa kuifanya kabla, ilikuwa ni kazi ya kuchimba mabwawa ya kufugia samaki ,licha ya kuwa sikuwahi kufanya hiyo kazi nilijivika ujuzi.
Ndani ya wiki moja nilikuwa nimeshachimba mabwawa mawili madogo na moja kubwa ambayo yalikuwa ni mradi wa shule ya msingi Uluti ambako baba yangu mdogo alikuwa mmoja wa walimu wa ile shule.Baada ya kumalizana na mradi wa ile shule niakaanza kuchimba mabwawa mengine kama matano madogo madogo ya watu binafsi  kabla ya kuanza kufanya kazi ya kupanda miti ya mbao kwenye mashamba mapya ambayo yalikuwa mapori yaliyozeeka.Mradi wa kupanda miti ya mbao na ufugaji  samaki iliibuliwa na shirika moja la kutunza mazingira na kupambana  na umasikini na ilipokelewa vizuri sana na wananchi wa kijiji kile ingawa kuna ambao hawakuangalia suala lile kiuchumi zaidi kwani kuna waliokuwa wakipanda miti kwenye vilima vya mbali sana na barabara na ngumu kufikika hata kwa miguu lakini basi walishaambiwa miti ni dili basi wakajua ni dili popote.
Sekunde,dakika, saa , siku, wiki vilisukumana kwa kasi ya ajabu hatimaye mwezi  wiki mbili ziliisha na kutakiwa kurudi shule.Lakini tofauti na nilivyotegemea hakukuwa na mtu hata mmoja aliyekuwa amenilipa kwa kwazi nilizokuwa nimezifanya hiyo ilikuwa ni kwa mujibu wa maelezo ya baba yangu mdogo ambaye alikuwa mwenyeji na msimamizi wa kila kazi niliyokuwa nikiifanya kutokana na ugeni wangu na kuogopa dhuluma.
''Shule hadi kamati ikae, kisha wakachue hela upewe hela yako''
''Kwa hiyo nitasafirije?''
''Kwani huna hata nauli?''
''Ndiyo''
''Utatembeaje kihasara hivyo unapoenda sehemu uwe na nauli ya kurudia siyo unakuja kihasara hasara tuu''
''Sikuwa na hela ndiyo maana nikaja kufanya kazi za vibarua huku''
''Si ulisema unakuja kutafuta ada , ulisema waja kuitafuta nauli huku, si ungeenda tuu nyumbani?''
''Nilijua,......''
''Acha upumbavu wako unadhani upo na baba yako huku yatima hadeki pambana , tumia akili dogo usipoangalia hata kidato cha sita humalizi maana kila sehemu ni pesa''
Yalikuwa ni maongezi yangu na baba yangu mdogo ambayo si tuu yaliniumiza bali yalinikera sana, nilijikuta nikijuta kwenda mahali pale kwani licha ya tumaini nilipata mateso.Nilimwangalia baba mdogo kwa macho yaliyokosa tumaini huku chozi likikosa subira na kutoka.
''Unalia mtoto wa kiume?''Aliuliza baba mdogo kwa sauti ya kebehi.
''Haya shika nauli hii na ikitoka hela yako nitakata''Aliongea baba mdogo akinikabidhi shilingi elfu ishirini na mbili na mia nne, hiyo ilikuwa ni nauli kamili kutoka gari ilipoanzia safari hadi shuleni hivyo kama ningepoteza hata shilingi tano basi nisingefika.
''Asante''Niliitikia nikipokea ile hele huku moyo wangu ukiwa na simanzi lakini kabla sijazipokea zile hela alizichukwapua tena.
''We mpumbavu sana yaani unapokea pesa bila kuandikiana nitakuamini vipi ukinidhulumu?''Aliongea baba mdogo akileta karatasi na kunitaka niandikia kuwa nilikuwa nimekopeshwa kiasi kile cha pesa kisha nikatia saini.
Baada ya maonyo mengi sana juu ya kuzingatia elimu ambayo niliyaona ni upuuzi mtupu kutokana na matendo yake mengi kwangu niliingia chumbani kulala lakini usingizi uligoma kabisa kuja kwani matendo niliyokuwa nikifanyiwa na ndugu na wasiokuwa ndugu yalinifanya nikose kabisa wa kumtegemea zaidi ya Mungu.Nilikumbuka mateso ya jino ambayo licha ya jino kuniuma kwa muda wote niliokuwa pale baba yangu mdogo hakuwahi kunisaidia hata hela ya kidonge cha kutulia maumivu zaidi ya kunishauri kuwa nikang'oe jino lililokuwa likiniuma kwenye zahanati iliyokuwa kijiji kingine mwendo wa kama masaa matatu mbaya zaidi hakuku na ganzi hivyo jino linatolewa kavu kavu maumivu yalioje hayo niliahirisha kwenda huko kitu ambacho hakukipenda.Kitendo changu cha kumwomba anisaidie niende wilalani kilolo nikang'oe jino kilimuudhi sana na kunitolea maneno yaliyoniumiza sana.
Asubuhi nilikurupushwa na na sauti ya baba mdogo aliyekuwa akinilalamikia kulala hadi muda ule.Niliamka na kujiandaa haraka haraka kwani nilivyojua kuwa gari lilikuwa likondoka saa mbili usiku kwenye kijiji cha nne kutoka pale Uluti hivyo hata ningeondoka  saa tisa jioni basi ningefika kabla gari halijaondoka.
''Chukua miche ipo kwenye beseni huko uani utaniwekea pale shambani kwangu''Ilisikika sauti ya baba mdogo na kunishtua kwani sikuwahi kuliona shamba lake kabla.
''Sahamba gani?'' niliuliza nikiwa na beseni lililokuwa na miche kichwani mwangu huku nikiwa na kibegi changu mgongoni.
''Lile shamba ulilokuwa umeanza kupanda wiki hii''Aliongea na kunifanya nihisi kuwa kuna mashamba ambayo nilikuwa nikifanya kazi nikihisi ya watu wengine kumbe ni mashamba yake hapo wazo la kuwa hata mabwawa aliyodai kuwa yalikuwa ya shule yalikuwa yake.
''Sawa baba''Niliongea nikiweka lile beseni chini kwani nilikumbuka kuwa nilikuwa nimesahau kopo la asali niliyokuwa nimenunua mwanzoni kabisa mwa likizo ile kwa hela ile iliyobaki katika mauzo ya simu na ununuzi wa vidonge vya kutuliza maumivu ya jino nikiamini kuwa ningeitumia katika kuongeza utamu kwenye uji wa shule ambao haukuwa na radha ya sukari kabisa.
''Umesahau nini ama umeniibia vitu, hembu shusha begi lako nikague''Aliongea baba mdogo kwa sauti iliyosikika hadi shuleni ambako wanafunzi walikuwa wakihesabu namba ya asubuhi.
Kwa aibu nilishusha begi langu na kulifungua nikimwacha akague.
''Hii simu umeipata wapi?''
''Niliinunua''
''Dogo haya maisha siyo ya kupenda starehe hela ya kununua simu unayo ila ya kulipa ada na nauli huna''Aliongea baba mdogo akiiweka ile simu mfukoni mwake.
''Na hii asali umeiba wapi?''
''Niliinunua"
''Kwa hiyo wewe una hela enhee?''
''Hapana''
''Endelea dogo hii dunia utakuja kukosa pa kushika leo unatuona unafanya ujinga tutakufa kama alivyokufa baba yako sawa, hembu funga begi lako si unaiona mvua''Aliongea baba mdogo maneno niliyoyaona kuwa yaliniaibisha kwani wanafunzi wote waliokuwa pale shuleni jirani kabisa na nyumbani tulipokuwa walikuwa wamegeukia upande wetu wakitazama na kusikiliza kilichokuwa kikiendelea.
''Samahani baba''Niliongea nikipokea kopo la asali na kujitwisha beseni la miche ya miti.
''Samahani baba''Niliongea nikipokea kopo la asali na kujitwisha beseni la miche ya miti.
''Haya utayaona dogo''Aliongea nami nikaanza safari yangu huku nikiwaza namna ya kupanda na kushuka milima miwili kabla ya kulifikia shamba la baba mdogo na miche ile iliyokuwa mizito sana.Taratibu niliziacha nyumba na kushuka kilima cha kwanza na kupandisha kilima kilichofuata na kushuka kabla ya kupandisha kingine na baada ya saa moja nilifika shambani niliweka ile micha mbani na kufuata barabara ya kuelekea nilikokuwa naenda wakati huo mvua iliongezeka.Viatu vyangu vya wazi viliingia maji na kuonekana mzigo uliokera.
Nilipita njia kadhaa za mkato nilizokuwa nikielekezwa na wanakijiji niliowakuta njiani baada ya kukerwa na safari yangu ya kwanza iliyonitaka nitumie barabara tuu.
Njia iliyokuwa katikati ya msitu iligeuka kijito kidogo kilichokusanya maji yote ya mvua iliyokuwa ikinyesha na kunifanya nivue viatu na kuvibeba mkononi na kutembea kwa shida sana hadi mvua ilipokata saa tisa na nusu na jua likaanza kuwaka kwa mbali.Katikati ya msitu wa asili uliokuwa umetenganisha vijiji vile vilivyojichomeka ndani kabisa ya hifadhi ya milima ya Udzungwa nisijihisi ni binadamu peke yangu huku viumbe wengine nikihisi ni wanyama wa porini ndege na wadudu wengine wadogo wadogo ambao kuna walisherekea mvua ile iliyokuwa imeisha na wale walioshukuru Mungu kwa mvua ile kuisha kama ilivyokuwa kwangu ambapo taratibu niliiona nuru ya tumaiani la kuponywa na radi iliyokuwa ikipiga wakati mvua ikinyesha.Nilichoshukuru ni njia ile kufuata vilima na kukwepa mapitio ambayo yangekuwa na mito na kuanzisha tatizo lingine la kushindwa kuivuka.
Saa kumi na nusu nilikuwa nimefika kwenye kijiji cha idete ambacho kilikuwa ni makao makuu ya kata ya Madege iliyokijumuisha pia kijiji nilichokuwa nimetoka cha Uluti.Hapo nilikutana na vija kadhaa ambao kwa kutumia ulimi wangu nilijikuta nimepelekwa kwa daktari wa zahanati ya pale na kunmweleza shida yangu ya kung'oa jino bila na kwa kuwa nilijitambulisha kuwa nilikuwa ndugu wa mwalimu Julius ambaye alikuwa ni baba yangu mdogo haikuwa kazi ngumu kunielewa na kutaka kunisaidia lakini hali yake ya kupepesuka kutokana na ulevi nikajikuta nikibadili mawazo kwa kuhisi asingenipa tiba stahiki na kuniletea madhara zaidi kwa kuomba dawa za kutuliza maumivu.
Baada ya kupewa hizo dawa nilijiunga na wasafiri wengine waliokuwa wakipanda kilima kuelekea Madege ambapo ndipo gari ilishia kutoka Iringa na kugeuza kuelekea Dabaga ambapo hulala hapo kabla ya kuanza safari ya kuelekea Iringa Mjini.Kulikuwa na vijana ambao nilikuwa nimewaeleza shida yangu ya kuomba msaada wa kumpata Daktari wakiniuliza kama nilikuwa nimefanikiwa nikawadanganya kuwa niamua kuahirika kwa hofu ya kushindwa kusafiri vyema.Kuna waliogundua kuwa nilikuwa nimeogopa ulevi wa Daktari nilipinga hilo na wakaniunga mkono kwa kutoa sifa kemkem kwa yule daktari kuwa akiwa amelewa basi hufanya kazi vizuri jambo ambalo niliona kama hekaya tuu walizoaminishwa lakini nikaa kimya hadi tulipofika Madege na kukaa tukisubiri gari ambalo tulitegemea saa kumi na mbili na nusu lingefika.
Kama tulivyotegemea saa kumi na mbili na nusu basi jeupe lilikuwa na maandishi mbele , nyuma na ubavuni MWAFRIKA liliingia kwa madaha huku honi zake zikivuka vilima na kutengeneza mwangwi uliofika mbali.Wakushuka walishuka wakiwa na vifurushi na mizigo mingi sana huku wa kuingia wakihangaika kuwahi siti walizozipenda wakibishana na makondakta waliowataka wawe na subira lakini wapi watu kwa ubishi walisukumana kwa fujo lakini wengine ambao nguvu zilikuwa tatizo tulijikuta tukionekana watiifu na kuwafurahisha makondakta.
''Hata muwahi siti basi lishajaa wameshakata tiketi Dabaga''Alisikika mmoja wa makondakta.
''Wawe na tiketi mie nina siti na sitotoka nalala kwenye siti tuone nani mjanja''Alisikika mmoja wa abiria aliyekuwa amepata siti ya nyuma ya basi.
''Lero hatutoruhusu watu kulala kwenye basi''Alisikika kondakta mwingine ambaye kama aliwashtua wengi walisikia ile sauti.
''Haa! kwa nini?'' sauti kutoka kwa abiria waliokuwa nje ilisika kwa pamoja.
''Nawatania jamani, samahani''Alisikika yule kondakta kwa sautio ya utulivu na kuwafanya watu washushe pumzi za tumaini.
Moyoni mwangu nilikumbuka kuwa kama wasingeturuhusu kulala kwenye basi ningekuwa kwenye taabu ingekuwa ni vigumu kwangu kwenda kuwaamsha wale wenyeji wangu wa kipindi kile kwani muda ambao gari lile lingefika ingekuwa usiku sana hivyo nikajikuta nikimlaumu kimya kimya yule kondakta kwa utani wake mbaya.
Baada ya kukuru kakara za kupanda na kushuka hatimaye saa mbili kasoro kila mtu aliyepanga kusafiri na basi lile alikuwa ndani ya huku basi likiwa limejaa na kutufanya tuliokuwa wa mwisho kuingia tusimame baada ya siti zote kukaliwa.
''Ona gari limejaa na wadai wakifika Dabaga watachukua abiria wengine''Ilisikika sauti miongoni mwa abiria tuliokuwa tumesimama.
''Gari haijai wewe imekuwa ndoo hii?''Alijibu mmoja wa makondakta kwa namna ya kutaka kumwaibisha aliyetoa ile kauli.
''Kujaa kwa ndoo ni kufika pomoni na gari siti zote zikikaliwa basi limejaa tungekuwa tunawekwa kama magunia ya mapeasi basi tungesema halijajaa''Alijitetea yule msemaji wa kwanza.
''Subiri gari liondoke ndipo utajua kuwa halijajaa'' Aliongea yule kondakta na kumpa ishara dereva kuondoa gari.
Basi liliondoka kwa kuyumbayumba na kutufanya abiria tuliokuwa tumesimaa tusukumane kabla ya gari kutulia kwenye njia na safari kuanza ilikuwa kama saa mbili na robo.Tukiwa nusu ya safari tulikutana na kitu ambacho kilimsikisha kila mmoja.Lilikuwa gari la mizigo lililokuwa na mbao nyingi likiwa nimeanguka kwenye kilina na kufanya mao zimwagikie barabarani huku dereva wake akiwa katika hali mbaya sana kwani alikuwa amevunjia mguu akiwa hana msaada.Abiria wengi tulishuka na kutoa zile mbao na kuziweka pembeni na tulipofikia mbao za chini kabisa tulikiona kitu ambacho hatukukitegemea kabisa.
Je, ni kipi hicho?

0 comments:

Post a Comment