Wednesday, 21 December 2016

NGOJA KAZI IWE KWANGU

Kazi ngumu ya kupewa,kijipa rahisi sana,
Katu huji kuchelewa,daima utakazana,
Huhitaji kuombewa,kazi yako itafana,
Ngoja kazi iwe kwangu,kuamua hili jambo.

Imeshapita miaka,nalia nabembeleza,
Sikuzihofu dhihaka,sikuchoka kuchombeza,
Leo ni wa tatu mwaka,pendo ninalikoleza,
Ngoja kazi iwe kwangu,kuamua hili jambo.

Maghani na mapambio,nilitoa kwa hisia,
Daima nakuja mbio,ninapohisi walia,
Hufurahii ujio,japo hujaniambia,
Ngoja kazi iwe kwangu,kuamua hili jambo.

Maneno yaniishia,nitasema jipya gani,
Moyo nauhurumia,umeshakupa thamani,
Kwako ulishahamia,ulihamia zamani,
Ngoja kazi iwe kwangu,kuamua hili jambo.

Jambo gumu kuamua,hilo ninalitambua,
Umeshindwa kuchagua, kati ya mvua na jua,
Moyo ulishaugua,nabaki napiga dua,
Ngoja kazi iwe kwangu,kuamua hili jambo.

''Kauli za Makabwela 2017''

0 comments:

Post a Comment