Wednesday, 21 December 2016

SHAIRI;NAJUA NIPO SALAMAMama asante sana,pole kwa magumu yote,
Ninajua twafanana,kuliko viumbe vyote,
Siwazi tutagombana,ukinifanya vyovyote,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Najua umeteseka,kuumwa na kutapika,
Pia ulisonononeka,pia ulisikitika,
Moyoni ukaniweka,mama hukutikisika,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Marafiki ulikosa,wengi walipukutika,
Waliona kama kosa,wala hukusikitika,
Na hukufikiri posa,huruma ulijivika,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Bibi alinung'unika,kuona mama walia,
Uoga hukujivika,kweli ulivumilia,
Hujafa hujaumbika,moyo uliuambia,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Mwili ulipukutika,afya ikanyong'onyea,
Uoga ukafunika,huku ukiniombea,
Chakula hakikulika,mama ukanitetea,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Niliihisi faraja,ulipokuwa na baba,
Lilibomoka daraja,hukupunguza mahaba,
Nikawaza mama naja,wapi yupo wangu baba,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Ile sauti ya baba,ilinifanya niruke,
Nami nampenda baba,nilitamani nishuke,
Anayo hekima baba,daima umkumbuke,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Siku ile ninashuka,uliteseka mamangu,
Chakula hukukumbuka,hata ugali nachangu,
Neno lile nakumbuka,karibu sana mwanangu,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Usichoke usumbufu,na huku kulialia,
Kilio ni maarufu,pakiuma nitalia,
Utacheka maradufu,kiona nimetulia,
Nipo mikono salama,asante mama mpenzi.

Yapo mengi ya kusema,ila nakomea hapa,
Nimesharibu mama,mama usijenichapa,
Nibadili nguo mama,nzi wanifuata hapa,
Asante mama mpenzi,nipo mikono salama.

Nakupa ahadi mama,nitakuwa mama bora,
Sitokudharau mama,hata nipigwe bakora,
Daima nitasimama,nije kuwa mke bora,
Asante mama mpenzi,nitakupenda milele.

0 comments:

Post a Comment