Thursday, 1 June 2017

HADITHI: REHEMA WA NJIA PANDA SEHEMU YA PILI


MTUNZI: Moringe Mhagama
Jiunge na kundi langu la WhatsApp kwa 0717308038
KITABU CHA KWANZA
 SEHEMU YA PILI
Alishusha pumzi na kupeleka kidole chake shavuni alikopasua kichunusi kilichokuwa kimeiva na kumsababishia muwasho.
Alikunja uso kwa maumivu matamu ya kutumbua kichunusi kila kabla ya kuchukua kikaratasi alichojifuta nacho mahali alipotumbua na kupaka damu na majimaji yaliyokuwa yakionesha kuwa alikuwa amemaliza uhai wa kile kichunusi.
Alisimama ,akakaa alitamani kulalia meza lakini akaona si vyema bali aende tuu nyumbani kupumzika baada ya kufanya kazi kucha pale hospitalini lakini tena akajikuta akikumbuka tukio zima la usiku ule hadi mfanyakazi yule wa serikali wa mkoa alipogundulika kutoweka hospitalini katika mazingira ya ajabu.
Tukio hilo lilimfanya akose maamuzi kwani alijikuta akisimama na kukaa kitini pale ofisini kama vile palikuwa na mtu aliyekuwa akimwimbisha ule wimbo maarufu shule ya msingi wa simama kaa..
Hatimaye alipata wazo ambalo aliona lingempa mwanga kidogo juu ya jambo lile.Aliinuka na kutoka ofisini mwake ambako tangu wale askari polisi watoke aliamua kujifungia.
Kwa mwendo wa haraka aliliacha geti la hospitali na kuelekea nje huku akili yake ikimtuma kuonana na mtu mmoja ambaye alimpa umuhimu mkubwa kwa wakati ule kwani alijua kabisa angempa mwanga fulani juu ya jambo lile mtu huyo hakuwa mwingine bali Sikitu msichana wa kinyamwezi aliyeamua kumweka kama kimada cha muda mrefu.
Kuna kitu ambacho alitaka kukijua kutoka kwake na kitu hicho aliamini kingempa ujasiri wa kulifikiria na kuliongelea lile jambo kwa uhuru na namna nyingine kabisa.
Akiwa hana hili wala lile njiani huku mwendo wake ukipungua kadiri dakika zilivyosogea kutokana na fikra alishtuka baada ya kupigwa fimbo ya mgongo iliyomfanya ageuke baada ya kuachia tusi zito la nguoni ambalo lilikuwa miongoni mwa sifa zake mbaya kwani ilifikia hatua alikuwa akiwatusi hata wagonjwa waliokuwa wamemuudhi akiwa kazini tabia iliyomweka kwenye orodha ya madaktari waliokalishwa vikao vingi vya kupewa onyo na kusuluhishwa na wagonjwa.
''Hahahahah! Ulijifanya umeniweza kunifungia mle ndani leo utalala wewe hahahaha! '' sauti ya mzaha ilimtoka mtu aliyekuwa amechafuka kwa mavumbi na uchafu wa matapishi uliokuwa kwenye nguo alizokuwa amevaa kabla ya kumchapa fimbo nyingine ambayo ilimzindua yule daktari kutoka kwenye kumtafakari mtu ambaye alimwona alikuwa akimtia wazimu kumfikiria baada ya kutoroka hospitali kimaajabu .
Alitaka kuongea kitu lakini , yule kichaa aliyekuwa mbele yake alimwashiria kugeuka kwa kidole kuangalia kilichokuwa nyuma yake naye hulka ya udadisi ilimfanya ageuke kuangalia kulikoni akijipangia kugeuka kwa nusu sekunde na kumchunga yule kichaa aliyemwona kwani alihisi ni mbinu ya ama kukimbia au kumchapa fimbo nyingine ya mgongo.
''Baba sina tegemeo tena'' aliongea mwanamke aliyekuwa akija mbele yake akilia.
''Nini mama?" aliuliza yule daktari kwa wahka.
''Siki''
''Kafanya nini mama?"
Mama Sikitu badala ya kumjibu aliinua macho kuelekea upande alikokuwa yule kichaa ambaye siku moja iliyopita aliitwa Anord mfanyakazi wa serikali mkoani akiwa kama afisa manunuzi wa mkoa wa Tabora, jambo ambalo yule daktari alilifanya lakini alishuhudia Anord akichota vumbi chini na kuijimwagia kichwani kama vile mtu achotavyo maji yaliyomo kwenye beseni kwa viganja vyote vya mikono yake na kuoga ama kuosha kichwa.
Kila mmoja alijikuta akiahirisha kumtazama Anord na kumwangalia mwenzake na kujikuta wakigonganisha macho na wote kwa aibu walikwepesha macho yao kwani kabla ya kutembea na Sikitu yule daktari alikuwa akitembea na mama yake Sikitu jambo ambalo hapo nyuma lilileta matatizo makubwa kati ya mtu na bintiye.
''Siki amefariki''
''Nini?"
_________
"Siki kafariki usiku asubuhi nimemkuta amekufa"Aliongea yule mama akigeuza kurudi nyumbani kwake akiongozana na yule daktari mpenzi wake wa zamani ambaye aliamua kuachana naye baada ya kuwa na marehemu mwanaye ambaye daktari hakujua kama ni bintiye kwani walianzisha mahusiano wakiwa Arusha ambako Sikitu alikuwa akiishi na baba yake.
"Alikuwa akiumwa nini?"yule daktari alidadisi kwani alikumbuka kuwa alikesha usiku mzima na Sikitu wakitumia ofisi yake kama chumba cha kulia tunda wakisaidiwa na kitanda kidogo cha uchunguzi kukamilisha kazi yao na alfajiri Sikitu aliondoka na kurudi kwao na ile safari ilikuwa ni kwenda kuuliza kama alikuwa ameondoka na funguo za kile chumba na kumtorosha Anord ingawa alijua kuwa hakukuwa na uhusiano wowote kati yao lakini alihisi pesa  ingekuwa sababu ya jambo hilo kuwa na uwezekano wa kufanyika.
"Hakuna na tatizo lolote na jana kaingia mapema sana kulala"Mama Sikitu alijibu kwa sauti iliyojaa kilio.
"Kwa hiyo huku ukikuwa ukienda wapi?"
"Hata sijui nimejikuta tuu nipo pale njiani"
"Mhhh haya ngoja nipitie hapo nyumbani nipate kunawa uso maana ndo natoka kazini"
"Sawa"
Waliachana hapo na kumwacha kila mmoja akiwa na lake kichwani mwake ,wakati daktari akiwaza uwezekano wa mafua ambayo Sikitu alikuwa akidai alikuwa nayo usiku ule kuwa moja ya chanzo cha kifo chake kwa Mama Sikitu hakuamini kitu kingine kuwa chanzo cha kifo cha mwanaye zaidi ya nguu za giza kwani mwanaye hakuonekana kuumwa kabla ya kukata roho usiku akiwa usingizini.
Moyoni alijiapiza kuzunguka kwa waganga wa kienyeji kujua chanzo cha kifo chake baada ya mazishi huku akimshuku mke wa mumewe ambaye ambaye alikuwa akiishi naye huko Arusha.
Dakika kumi baadaye yule daktari aliungana na kundi kubwa la watu ambalo lilikuwa nyumbani kwa akina Sikitu na kuendelea na shughuli nyingine za msiba.Kama ilivyokawaida minong'ono juu ya chanzo cha kifo cha Sikitu ilisikika huku na kule kuna waliodai alikuwa amekufa kwa mipango ya Mungu , ila kuna wale walioamini mengine kama vile kurogwa habari za majini na hata kisasi na laana.
''We huyu binti nasikia huko Arusha ilikuwa kazi , kila mwanaume wake mradi akimwambia twende''Ilisikika sauti ya dada mmoja kwenye kikundi cha kina mama waliokuwa wakipanga samani sebuleni ili kupata nafasi ya watu kukaa.
''Hapana hukumbuki walichangia mwanaume na mama yake wa kumzaa?, Hii laana''Aliongeza mwingine.
Kila mtu akasema lake na kujaribu kuwaaminisha waliokuwa wakimsikiza kwa mifano na wingi wa maelezo.Ni kweli Sikitu alikuwa akielewa na mama yake mdogo ambaye alikuwa akiishi na baba yake huko Arusha pia alikuwa amechangia mwanaume na mama yake bila kujua lakini hata kutoyafanya hayo asingekikwepa kifo kwani kifo ilikuwa ni safari ya lazima kwa mwenye uhai japokuwa wengi huamini matendo na mienendo yetu huweza kuwahisha ama kuchelewesha vifo.
Lakini hakuna kitu kikosacho sababu ndiyo maana kundi la wazikaji ama niwaite waombolezaji walikuwa wakijariku kutafuta sababu ya kifo kile cha ghafla cha Sikitu binti mdogo na mrembo ambaye mtaani pale hakuna ambaye hakujua kuwa alikuwa ni mpenzi wa Daktari.
Walilokuwa hawalijui kuwa kulikuwa na sababu nyingine ambayo haikuwa rahisi kujulikana hata kwa mpenzi wake ambaye kichwa chake kiliamini kuwa alikuwa naye usiku wakila raha ya dunia.Daktari alianza kuhisi huenda baada ya kumalizana naye ofisini Sikitu alikuatana na mtu aliyemshawishi kutoa funguo za chumba alichokuwemo Anord kisha mtu huyo kumuua Sikitu kwa kupoteza ushahidi.
''Iliwezakanaje?''
''Iweje afie kitandani?''
''Ina maana muuaji likuja kumuulia nyumbani kwake?''
Maswali magumu yaliyokosa majibu yalipita haraka haraka kwenye akili ya daktari ambapo wazo la kutaka uchunguzi ufanyike kabla ya mazishi ya mpenzi wake lilikuja pia akilini lakini aliona ugumu wa kuuaminisha umma licha ya taaluma yake kwani kila mtu alijua ni kifo cha ghafla na hakukuwa na chembechembe za imani kuwa aliuawa zaidi ya walioamini katika ushirikina.
Siku iliyofuata shughuli ya kuuweka mwili wa Marehemu Sikitu kwenye nyumba yake ya milele na kutimiza ile hatua ya kurejea mavumbini kwa kila binadamu ilifanyika na kuacha simanzi kwa kila aliyehudhuria katika shughuli hiyo kwani vilio vya wazazi wake ambao kifo chake ni kama kiliwaunganisha katika maumivu viliongeza simanzi miongoni mwa waombolezaji.Historia yake fupi ya maisha yake ambayo waliamini ilikuwa imefupishwa sana na kifo chake.
Alitakiwa kuishi, tena kuishi sana.
Lakini mauti yalimuwahi. 
Baba alilia na kumuhisi mke wake mpya ambaye alidai kuwa hampendi mwanaye Sikitu kuwa  huenda alikuwa ameamua kumpoteza na kujikuta akiamua kuhangaika kwa waganga na waganguzi wa nyikani na mwambao kujua ukweli na ikifahamika kama ni kweli kilichomla kilikuwa nguoni basi angemwachia Mungu.
Kumuacha , hilo liligoma kuingia akilini liligoma kabisa na kujikuta akiamua kupoteza mawazo hayo na kuanza kumtuhumu mwanaye kwa utukutu na uhuni wake ambao kimoyo moyo alihisi aliurithi kwake ingawa angeulizwa na yeyeote angesema alirithi kwa mama yake.
Atasemaje karithi kwake wakati aliuaminisha umma kuwa mkewe alikuwa sababu ya yeye kuoa mwanamke mwingine , ndiyo hivyo wanaume tulivyo.
Mama naye alilia , alilia sana kwanza kuchangia mwanaume na mwanaye lilikuwa ni jambo lililomuumiza sana, aliumia kwani kitendo cha kukubaliana na mumewe mwanaye akakae huko kwa mama wa kambo akiwa na hasira za kutobaki na ukumbusho wa damu ya mwanaume huyo kilimuumiza sana ,alijiona mwenye hatia kwani angekaa na mwanaye wala wasingekuja ''kugongana''.
Kingine kilichomtoa machozi ni kifo kile cha ghafla ya binti yake mdogo ambaye aliamua tuu kuyawahi ya ukubwani ,alikuwa ni mwanaye wa pekee kwani tabia yake ya kuanza kutoa mimba kila baada ya kuinasa kilimfanya mgumba hivyo hakuwa na tegemeo la kuitwa mama tena na mwanaye wa kumzaa.Alijuta sana kitendo hicho lakini mwisho wa siku alimlaumu mwanaume wake , baba wa Sikitu kwani alimwacha bila kosa na kama kosa lilikuwa la mwanaume huyo aliyekwepa aibu ya kufumaniwa na kuamua kuwa mkali na kumwacha mkewe ambaye alimfumania chumbani kwao.Siku ile akiwa na Sikitu kichanga mgongoni anatoka kumzika mama yake simu hamna hakutoa taarifa si anakwenda kwake ,akafika nyumbani milango yote ipo wazi bila uoga akaingia moja kwa moja hadi chumbani aweke salfeti lake la nguo safi kuukaribia mlango wa chumbani akasikia miguno akahisi masikio yake yamechoka kusikia pepo za kasi alizokuwa akizisikia wakiwa kwenye Land lover ya serikali iliyowakuta njiani na kuwatoa senti kadhaa ili wafupishiwe safari.Hakuyaamini masikio yake akamua kuingia tuu kufika ndani alijikuta akitetemeka kwani alimkuta msichana akilalamika kwa raha ,amekunjwa haswa kama vile akipigwa.
Hakutaka kuiamini kama alikuwa akipata raha kwa mkunjo ule lakini aliona akishangilia kwa kufunga goli ,miguu ikalegea , mikono nayo ikachoka ,mapigo ya moyo yalienda kasi kabla ya kupunguza nguvu na kujikuta akikaa chini kama mzigo macho pima anatazama lakini haoni na mtoto wake anaanza kutoa kilio baada ya mama yake kuukandamiza mguu wake dhaifu.
Kelele za mtoto ambaye sasa alikuwa marehemu ziliwashtua makomando wale waliokuwa wakipigana kibabe bila mmoja kumwonea mwenzake licha ya tofauti yao kubwa kiumri.
Huo ukawa mwisho wa watu wale kuwa wanandoa , ndoa walioamini ilikuwa takatifu wakifungishwa na padre wa kizungu miezi kadhaa iliyopita na kuanzisha ndoa nyingine ambayo iliwahusu wale makomando waliofumaniwa wakikunjana na kufurahi pamoja , lakini uhalali wao waliamua kwenda kuutafutia Arusha walikobadili na dhehebu wakijiunga na dhehebu jipya lililokuwa likikusanya kila binadamu wakiamini kuwa walikuwa wakipokea kondoo waliopotea.
Mama Sikitu kuja kuzinduka akakumbuka kilichomzimisha , hakutaka kusubiri ruhusa ya daktari akatoka mbio hadi kwa mama mkwe wake na kumuachia kichanga , kichanga ambaye baada ya kukua kidogo walikipeleka kwa baba yake na mama yake wa kambo huko Arusha , kwa kuwa walikuwa wamekijiita ''walokole'' walimpokea Sikitu na kumlea huku mama wa kambo akiwa na chuki dhidi yake kwani hakuwa na uwezo wa kupata mtoto hivyo uwepo wa mtoto asiye wake ulimkera haswa.
Miezi ikasukumana na miaka ikasogea huku Sikitu akiingia kwenye umri wa kuitwa binti na ndoa ile ikihangaika kutafuta mdogo ake Sikitu bila mafanikio kanisani waliambiwa wawe na subira kama Ibrahim , hilo mwanzo liliwaingia lakini baadaye wakaanza kuhangaika huku na kule hadi walipotua kwenye kituo kimoja cha afya ya uzazi kilichotoa jibu liliwashtua kuwa mama hawakuwa na uwezo wa kuwa na mtoto, mke akakumbua ujauzito alioutoa kienyeji kama chanzo cha hali yake ila hakujua kwa mume wake pia ni tatizo , mume hakuamini kwani alijua Sikitu ni wake.
Ambacho hakukijua ni lile gonjwa alilolipata wakati akihangaika kutaka kumhakikishia mkewe kuwa alikuwa na baba kweli lilimaliza mishipa yake yote ya kumfanya awe baba.
Baadaye katika harakati za mama kutafuta heshima ya ndoa nje ya nyumba akajikuta akigongana na Sikitu ambaye ndo kwanza alikuwa kijifunza yale mambo, hakuamini kabisa kama mwanaume ambaye alikuwa akimpenda zaidi ya mumewe wa ndoa alikuwa ameonja tamu ya binti wa mumewe , hapo chuki , wivu na husda vikawa na nguvu na kumfanya mama wa kambo aanze kumjaza maneno mumewe kuwa Sikitu si mwanaye kumbe nyuma yake kuchukuliana mwanaume ndiyo sababu.
Usiku mmoja wakiwa katikati ya maraha baba anagugumia kwa raha akitaka kumwaga uji wake kiduchu ndani ya kikombe akakatishwa na kitendo cha mkewe kujitoa ulingoni.
''Baba Sikitu'' aliita mke.
''Naam...''Aliongea kwa kugugumia baba mtu macho yamemtoka pima haelewi kinachoendelea.
''Nataka Sikitu arudi kwa mama yake''
''Sawa mama asubuhi nampa nauli''
''Kweli ?'' mke aliongea akiwa amekaza macho gizani.
''Kweli mke wangu kipenzi''
''Haya njoo mume'' Mke aliongea akimpokea mumewe aliyekuwa katokwa na akili zake kwa raha alizokuwa amekatishwa na kujikuita akitetemeka.
Sehemu ya usiku iliyokuwa imebaki ilitawaliwa na vilio vya raha kutoka kwa mume ambaye hakuwahi kupata zile raha tangu alipoingia kwenye ulimwengu wa mahaba, hakujua kwa nini mkewe hakuwahi kumpa kabla yua siku ile.
Miguu yake ililegea kama viungo vingine vya mwili vilivyochoka hadi saa nne asubuhi alikuwa hajaamka na alipoamka saa sita kasoro alikutana na supu matata kutoka kwa mkewe ambayo aliifakamia kwa fujo baada ya kuogeshwa na kupewa mchezo mmoja tena kwa kinywa cha mkewe.
Raha ilioje, mara chakula cha nguvu kilifuata.
Mwanamke alijipanga ugali samaki na mnafu.
''Dah! hii kweli ndoa'' Baba mtu aliwaza.
''Baba Sikitu''
''Naam unakumbuka ahadi yako''
''Ipi?'' Aliuliza baba mtu akimwangalia mkewe.
''Kwa hiyo unajifanya kusahau?'' Aliuliza mke kwa sauti ya kulalamika.
''Tumeahidiana vitu vingi mke wangu naomba nikumbushe kipenzi''
''Yaani hukumbuki kabisaaa? kweli hapa nimejua kuwa sipendwi'' 
''Nakupenda sana mke wangu'' Mume aliongea kwa unyonge huku akijua fika mahaba ya siku ile kama yalikuwa yamerejesha mapenzi yake kwa mwanamke yule aliyekuwa akimchukia taratibu baada ya miaka kadhaa ya kuhangaika bila mtoto.
''Kuhusu Sikitu mume wangu'' Mke akadokeza kwa sauti legevu.
''Kwenda shule?''
''Yaani we nakuchukia hivi hivi kitu kidogo tuu umesahau ndo maana nasema siku zote hunipendi wala hunijali''Alilalama mke.
''Naomba nikumbushe basi mke wangu''Alibembeleza mume.
''Si uliniahidi kuwa leo hii ataondoka?''Mke aliongea na kumshtua mume kwani hakukumbuka kama aliwahi kutoa kauli hiyo.
''Kuondoka?'' 
''Ndiyo kuondoka si ulisema mwenyewe usiku ama umeshaanza kumtamani?'' Aliongea mke akiwa hana utani katika aliloliongea.
''Nimtamani mwanangu wa kumzaa inawezekanaje?''
''Yaani bado unaamini kuwa huyo ni mwanao , nakueleza siku zote mama yake alikuwa na ujauzito kabla ya kuja kwako hata huelewi''Aliongea mke bila masikhara.
''Hata kama unayoongea yakawa yakweli lakini bado nitamchukulia kama mwanangu wa kumzaa siwezi mtamani''Aliongea mume huku akiendelea kutafakari maneno ya mkewe kila siku akidai kuwa Sikitu hakuwa mwanaye halisi kutokana na ukweli kuwa aliamua kumuoa mama yake baada ya kumwambia kuwa alikuwa amebeba kiumbe chake tumboni.
''Huenda nilidanganywa kweli?'' Alijiuliza kimya kimya.
''Lakini umeniahidi kwa kinywa chako kuwa ataondoka leo''
''Sawa mama ngoja nimweleze ajiandae kwa safari''Aliongea mume baada ya kuhisi alikuwa ametoa ahadi hiyo wakati wa shughuli pevu juu ya uwanja wa usiku.
''Siyo ajiandae hata hela kama huna nitaongezea aende''
''Ataendaje leo na gari zitakuwa zimechelewa?''
''Akalale hata Moshi mjini , kesho aende Dar kesho kutwa aende huko Dodoma nikiweza nitamsindikiza''
''Sawa ''Alijibu mume na kutoka nje ya kile chumba kabla ya kumwita Sikitu na kumweleza kuwa kulikuwa na taarifa ya mama yake kuumwa akimtaka akusanye vitu tayari kwa safari.
Taarifa hiyo ya safari ilikuwa na pande mbili upande mmoja ukifurahi kwenda kuonana na mama yake ambaye hakumjua hata sura yake lakini upande mwingine wa taarifa ile ulimuumiza kwani aliona ule ulikuwa ni wakati wa kutengana na kipenzi chake ambaye alikuwa ni daktari ambaye alihisi mama yake wa kambo naye alikuwa akimvizia asichokuwa akikijua kuwa daktari yule licha ya kuwa na mama yake wa kambo kipindi alipokuwa Arusha alikuwa ameshatembea na mama yake mzazi wakati akiwa kwenye mafunzo kwa vitendo huko Dodoma.
Kwa bahati na mipango ya Mungu Sikitu alifika Dodoma na kuanza maisha mapya huku akimsahau mpenzi wake daktari aliyekuwa amemwacha Arusha hadi miaka miwili baadaye daktari yule alipohamia Dodoma na kuendeleza mapenzi yao kabla ya kuja kuhisi kuwa mama yake aliwahi kuwa na mahusiano naye ama alikuwa akimtamani lakini mama mtu alipojua kuwa mwanaye kulia kijiko chake akamwachia si kwa kususa bali kwa kuridhia huku akimwombea mwanaye asipaate laana na mikosi kwani Sikitu kama jina lake lilivyosadifu hakuwa na kitu cha kujivunia maishani mwake, hakulelewa na mama yake mzazi, alimshuhudia baba yake mzazi akimsaliti mama yake na pia alikuja kuchangia penzi na mama yake mzazi na yule wa kambo.
____________
Sikitu hakuwa kitu tena zaidi ya udongo ambao baada ya miongo kadhaa ungesahaulika, aliwaachia wazazi wake maumivu makali kumkosa lakini mbaya zaidi kila mmoja wao hakuamini kama kifo kile kilikuwa ni mipango ya Mungu.Mama mtu alijilaumu kuwa huenda ilikuwa ni adhabu ya Mungu wake kwa kuuua mimba nyingi alizozipata baada ya kumwachia mumewe mtoto na kuanzisha namna nyingine ya kuishi kiaharamu akiutumia mwili wake kupata ujira usiokatwa kodi ya serikali yoyote iwe ya mtaa, mji na hata taifa.
Baada ya kuzunguka kwa waganga njaa wengi waliojiita waaguzi ambao walimaliza pesa za kila mmoja kwa wakati wake yaani baba mtu na mama mtu ambao kila mmoja alifanya mambo yake kisiri zigo la tuhuma na lawama lilitua kwa mama wa kambo kila walipopita kuwa alimtumia jini lililompeleka udongoni.
Kwa nini wasimtaje huyo kama kila walipoonda walikuwa wakipishana mtu na mke bila kujuana na waganga njaa hao walikuwa wameweka mawakala wa kujua historia zao na kumjua mtu ambaye wakimtaja basi kila amtu atasema .
''Ila kweliii..''
Naam walizunguka haswaa hadi walipojikuta wakitua kwa mganga mmoja ambaye alikuwa akisifika kwa kuona ya ulimwengu wa giza na kujua kilichofanyika.Huyo hakuwa na porojo anakuwekea beseni la maji unaona kilia kitu kama televisheni, tena kwa kujiamini aliwaaweka pamoja mke na mume waangalie sinema hiyo iliyotisha.
Kwanza walimwona Sikitu akiwa kitandani akihangaika kama anawaza kitu, ghafla akapatwa na usingizi mzito yaani hageuki katulia tuli, mwanamke mmoja wa kizungu akaingia pale ndani akipitia dirishani tena dirisha likiwa limefungwa na kumwangalia binti yao kabla ya mwanamke huyo kugeuka sura na mwonekano kuwa kama wa Sikitu na kufanya Sikitu kuwa wa wawili.
Kama walivyokua ameiingia Sikitu mpya alitoka kupitia dirishani bila kulibughudhi ajabu alikuwa akitembea kama hapakuwa na ukuta.
Picha likahamia hospitialini ambako daktari alimpokea kwa bashasha akimsimulia juu ya habari za uwepo wa mgonjwa aliyeitwa Anord kabla ya kupeana penzi lilimpagawisha daktari na kusinzia akimwacha siku mpya akichukua funguo na kuelekea chumba cha Anord.
Hapo mganga huyo akakatisha kusema hayawahusu na hakutaka kuingia hatarini akakosana na majini ambao hushirikiana naye akiwa kazini.
''Kwa hiyo yule mwanamke wa kizungu ni jini aliyemuua mwanangu?''Baba mtu akauliza kwa hamaki.
''Ndiyo ila amemuua kwa sababu maalum kwani marehemu alikuwa akimvizia mpenzi wake yule jini'' Alijibu mganga akijiamini.
''Kwa hiyo huwezi kumuua huyo jini aliyetuulia mwanetu tutulize hasira zetu na huyo mwanaume wa huyo jini ni nani?''Aliuliza mama mtu akiwa na chuki kubwa juu ya jini muuaji wa mwanaye.
''Nani jini....?'' hakumalizia kauli yake walishuhudia kichwa cha mganga yule kikikatwa na jambia ambalo halikushikwq na yeyote na kuwafanya wapige kelele kwa hofu na kupoteza fahamu.
________
Kwa upande wa Anord baada ya kuithibitishwa kuwa hakukuwa na tiba yoyote ya kumaliza tatizo lake ambalo kila mtu alimwona ni kichaa ikashauriwa arejeshwe nyumbani ambako tofauti na ilivyotegemewa mchumba wake aliyemwahidi kumwoa hakutaka kujitenga naye zaidi alimhudumia kwa shida hivyo hivyo huku akishirikiana na wazazi wa Anaord wakihangaika kwa wanganga mbali mbali wa jadi ili kumrejesha katika hali ya kawaida jambo ambalo hata baada ya miezi zaidi ya ishirini kupita hakuna walichofanikiwa katika kumrejesha katika hali yake ya kawaida.
Mwili wake ulitisha, harufu kali ilitoka mwilini mwake, kinywa kilitisha kwa kuwa na meno yake ya njano yaliyotoa harufu mbaya ,vidole vyake vya mikononi na miguuni ilijawa na vunza waliokera hata kuwafikiria achana na kuwatazama mwili wake haukupenda usafi kwani licha ya juhudi kubwa ya mpenzi wake kumfanyia usafi lakini hakuna kilichofanikiwa kwani kama nguo safi itachafuliwa kwa maksudi na kuchanwa chanwa kisha tambala chafu la jaani basi litachukua nafasi ya nguo hiyo.
Mpenzi wake alitukanwa huku akimtaja Sikujua kama mke wake halali ambaye siku chache zilikaribia basi angefunga naye ndoa.
Hakuna alikuwa akimjua huyo Sikujua aliyemwita mchumba wake tajiri na mrembo kuliko wanawake wote duniani , ndoto zake tamu ziliendelea popote alipojisikia lakini safari hii ziliisha kwa kilio na maumivu kwani mwishoni Anord alikuwa akilalamika kuteswa kwa kung'atishwa nge wakali wenye sumu lakini baada ya muda mfupi alijipeleka jaani na kukusanya mabaki ya vyakula vilivyooza kuwa kama maji yake ya kuoga.
Anord hakutamanika, familia yake ilimchoka , hakukuwa na ndugu wala rafiki aliyekuwa tayari hata kujitambulisha kuwa alikuwa nduigu yake,baba alimchoka na kutamani hata achomwe sindano ya sumu ili afe apunguziwe mateso yale kwani sasa tuhuma zilienda kwa kila ndugu kwenye familia ile ambaye angefanikiwa kimaisha.
Wadogo zake walimchoka na kumwogopa kwa mambo aliyokuwa akiyafanya lakini licha ya wote kumwogopa na kumkimbia kulikuwa na mtu pekee ambaye hakujitenga naye huyo alikuwa Atuganile Mwakalile mpenzi wake ambaye alikuwa mtu pekee aliyemtia moyo mama yake Anord.
''Atu mwanangu'' Aliita mama Anord siku moja walipokuwa njiani kuelekea kwenye kijiji kimoja ambako waliambiwa kulikuwa na maji yaliyotoka kwenye chemchem ya moto iliyokuwa ikitoa maji ya moto waliyoamini ilikuwa ikitoa tiba kwa magonjwa yote ya ngozi , walitaka wayachote kisha wampeleke Anord ayanywe ili hata ngozi yake iwe nzima.
''Abee mama''
''Hujachoka?''
''Kutembea?''
''Hapana kuhangaika na Anord''
''Mama siwezi kuchoka Anord atapona siku moja haya ni mapito tuu ya dunia''Alijibu Atuganile akimwangalia aliyeamini ni mama mkwe wake mtarajiwa ambaye alikuwa amekata tamaa.
''Nikwambie ukweli mama yako nimechoka sahizi kuhangaika natamani hata Mungu amchukue apumzike''Aliongea yule mama wakati huo walikuwa wakishuka kilima cha mwisho kufika kijiji kilichokuwa na chemchem hiyo ya moto kwa mbali  waliona kundi kubwa la wa watu wakiwa wamezunguka bwawa dogo , watu jinsi la rangi karibu zote walikuwa hapo si wazungu si wachina na waafrika kibao walikuwa hapo.
''Mama usichoke atapona''
''Kweli mwanangu?''
''Kweli mama usichoke naamini atapona''
''Mhhh haya''walimaliza hivyo na kufikia kundi kubwa la watu ambao hawakuwahi kufikilika kuwa wameshuka na kupanda vilima kufika pale.
''Inatakiwa aje mgonjwa mwenyewe aingie kwenye hicho kibwawa kama unavyoona wengine''Aliongea mzee mmoja aliyekuwa akiratibu tukio lile ambalo halikuwa na malipo yoyote labda kwa mtu atakayejisikia angetoa chochote  kama shukrani baada ya kupona kwani ilikuwa ukitoka kwenye maji basi kila kitu kinakuwa safi.
Kuna waliokuwa wakiletwa wakiwa na degedege na kifafa lakini walitoka wakiwa safi kuna wakoma walitoka na ngozi nyororo hali hiyo ilimtia moyo Atu lakini mama Anord alikuwa ameshachoka hasa kilifikia namna ya kumleta Anord aliyekuwa mgumu kuongozwa bora hata ng'ombe kichaa.
Anord angeweza kweli kufika katikati ya vilima vile mchongoko masaa saba ya kutembea kwa miguu juani, mbaya Anord mwenyewe haambiliki na yeyote.
''Si tutarudi kesho mama?''Aliongea Atu wakati huo walikuwa wakipanda vilima kurudi kijiji kwao.
''Ndiyo '' aliongea mama kinyonge huku moyoni akijiwazia mengine.
''Nani atakuja na mbwa kichaa yule asiyemsikia yeyote huku vilimani ?'' Alijiwazia mama Anord kimya kimya.
''Sawa mama tutafika kama saa sita ama saa nne hivyo tukifika ukapumzike mie nitatafuta atakuwa amelala wapi leo.'' Aliongea Atu kwa dhati.
''Sawa''Alijibu mama Anord kifupi huku akiwa na yake kichwani.
''Nikifika naanzisha ungonjwa nisisumbuke tena huyu mwanamke gani kamng'ang'ania kichaa kama ruba vile wanaume kibao timamu na wenye hela wanamfuata ye yupo na kichaa Anord mwenyewe hamtaki anamtaka sijui kichaa mwenzake Sikujua''Alijiwazia mama Anord akimshangaa Atuganile ambaye aliamini Anord ndiye mwanamme pekee wa kumuoa.
Saa sita kasoro usiku Atu alimwacha mama Anord nyumbani kwake na kuelekea kwenye maeneo ambayo aliamini angemkuta mpenzi wake Anord.
Baada ya kuzunguka kwenye majalala kadhaa kuanzia shuleni, hospitalini na sokoni Atu hakufanikiwa kumwona mpenzi wake na kuamua kurejea nyumbani akipanga kumtafuta asubuhi.
Akiwa na uchovu wa safari na mawazo mengi juu ya maisha yake na ya kipenzi chake alirejea nyumbani kwake akipishana walevi wachache ambao walikuwa hoi hawana hali wakielekea makwao.Hatua chache kutoka nyumbani kwake alisikia sauti za watu waibishana kwa sauti kubwa nyumbani kwao.
''Nimesema nimekuja kumfuata mke wangu, mmempeleka wapi?''Sauti kali ilisikiaka Atu aliijua, ilikuwa ya kipenzi chake.
''Una mke wewe mwehu?,, hata mwanangu angekuwa kilema siwezi kukupatia umwoe''Sauti ya mama Atu ilisikika akiongea kwa hasira hapo Atu aliamua kujibanza nyuma ya jiko lao la udogo lililoezekwa nyasi ambalo usiku ule lilikuwa ni nyumba ya kuku waliokuwa wametotoa , kuku wanne kila mmoja kona yake.
''Atu mke wangu hata mfanyaje na mwenyewe anajua kuwa nampenda sana''
''Akupende Atu niliyemzaa au kuna 'liatu' lingine likichaa kama wewe?'' 
''Kati yangu na wewe nani kichaa ambaye hajua hata mwanaye yuko wapi muda huu?''Anord aliongea maneno yaliyomchoma mama mtu ambaye kwa kujibalaguza akajikakamua.
''Mwanangu yupo ukweni ameshaolewa na wasio mapunguani kama wewe'' 
''Mie nina akili zangu si kama wewe mwongo unayedai mwanao yupo ukweni kwa wenye akili na wasio mapunguani wakati nijuavyo Atu yupo na mama yangu kwetu na leo naenda kulala nyumbani maana mke kanifuata kwetu''Anord aliongea akiondoka akiwaacha wazazi wa Atu pale nje wakiwa hawana la kufanya kwani licha ya kuwa walikuwa wakibishana na Anord juu ya alikokuwa mwana wao hawakujua mahali halisi alipokuwa binti yao wakabaki wanamtazama Anord aliyekuwa akipotelea kwenye nyumba nyingine.
''Ila kama nilimwona Atu akiwa ametanguzana na mama yake huyu punguani?'' Aliongea baba Atu kwa sauti ya unyonge.
''Kweli huyu binti sijui anatutafutia balaa gani , yaani kwenye ukoo wa baba yake na mama yake hakuna punguwani wala aliyewahi kuwa punguwani sasa anataka kutuletea punguwani mkubwa, we Mungu tusaidie'' Mama Atu alinung'unika.
''Yaani kila siku watu wanakuja wanataka kumuoa lakini lenyewe limekazania hili punguani''
''Hata simwelewi sijui anatutafutia nini sijui wamemroga sijui wamemfanyaje si umesikia yule mtoto wa Kambona ambaye ni Mkurugenzi wa benki naye anatuma mshenga kesho lakini hili toto tulipe nini?''
Baba na mama walilalama pale nje kabla ya kuingia ndani bila kujua kuwa binti yao aliwasikia.Katika mambo ambayo Atu hakutaka kuyasikia ni kuolewa na mtu ambaye hakuwa Anord, aliyakumbuka maneno ya Anord kuwa alikuwa akimpenda na alikuwa akijua kuwa alikuwa anampenda akajikuta akiingiwa na furaha iliyoyeyushwa na maneno ya wazazi wake.Akakumbuka tena maneno ya kuwa Anord alienda kulala nyumbani kwa sababu yake akafarijika na kutamani kurudi akalale na Anord lakini akajikuta akiogopa wazazi wake wangemuuliza alipokuwa amelala na akiwajibu alikuwa amelala kwa waliyemwita punguani basi angewakera wazazi wake lakini hata wazazi wa Anord wasingeweza kumruhusu alale kwao.
Taratibu akasogelea mlango wa bati wa nyumba yao lakini akajikuta kisita kufungua baada ya kuwasikia wazazi wake waliokuwa wamesimama sebuleni wakimtupia lawama nyingi kwa uamuzi wake wa kushirikiana na mama yake Anord katika kutafuta tiba lakini mbaya zaidi kitendo cha kutaka kuolewa na Anord kiliwaudhi wazazi wake.
''Siwezi kulala humu ndani kama mwanangu wa pekee hayumo na sijui aliko, yule ni mke wa mtu mtarajiwa hatakiwi kulala mtaani huko atafundishwa tabia mbaya na mchumba wake yupo hapa hapa kijijini'' Mama Atu alisimama na kuingia chumbani na mumewe akamfuata nyumba.
Haraka haraka Atugaline akaamua kuondoka na kujificha nyumba ya banda la nguruwe ambao walianza kumpigia kelele ,hakujali akaendelea kuvumilia hadi pale alipowaona wazazi wake wakitembea kuelekea upande wa nyumba ya rafiki yake Agnes alichokifanya ni kuelekea jikoni kwao kwa lengo la kujificha lakini alipoingia humo kuku walianza kupiga kelele na kuhisi wazazi wake wangekuja kuchungulia kuona kulikuwa na nini.
Baada ya kubisha na nafsi yake kwa muda mrefu kidogo, aliamua kufungua mlango na kuingia chumbani kwake kujilaza kitandani huku kichwa chake kikiwa na maswali mengi ambaye hakumwona wa kumpa majibu zaidi ya mwenyezi Mungu ambaye aliona kuwa alikuwa jibu kwa kila swali la kila kiumbe huku akiamini juhudi zake ni njia pia.
Dakika kumi baadaye wazazi wake walisikika wakija nyumbani huku wakimlaumu sana kwa kujihusisha na Anord.
''Mbona mlango tuliufunga kuna mtu kaingia?''Aliuliza mama yake Atu baada ya kuufikia mlango.
''Labda kama ulijisahau mama''
''Hapana nilifunga na hii kamba ya kufungia nusura iniumize hapa kidoleni'' Alijibu mama Atu akifunga mlango baada ya kuingia.
Huko ndani lawama zilikuwa kwa Atu ambaye hawakujua kuwa alikuwa akiwasikia , mama yake alizunguka njia nzima akiwaomba 'mahoka' awalindie binti yao huku akimwombea msamaha kwao kwa kitendo cha kutaka kuolewa 'punguani' Anord.Wakati akiendelea 'kubwabwaja' pale ndani ghafla alisikia kikohozi ambacho aliyekitoa ni kama alikuwa akikizuia kisitoke.
''We Atu''
''Abeeh'' 
''Umeingia saa ngapi?'' 
''Muda si mrefu''
''Muda si mrefu , ulikuwa wapi?'' Aliongea mama yake akimwiga huku amebana pua.
''Mama Anord alise....''
''Ishia hapo hapo kila siku mama Anord sijui mama 'punguani' Anord , sitaki kusikia tena hilo jina hapa nyumbani''Mama Atu aliongea akiwa karibu kabisa na mkeka aliokuwa ameulalia Atu wakati huo baba yake alikuwa ameshaingia kulala.
''Lakini mama mb.....''
''Sitaki kusikia upuuzi wake , kwa taarifa tuu kesho kuna ugeni wako sitaki tena kumsikia Anord wako''
''Mama lakini simpendi mtu mwingine zaidi yake'' Alibembeleza Atu.
''Mwanangu ndoa si lazima umpende mtu kabla mtapendana huko huko, mbona mie niliolewa na baba yako nikiwa simjui kabisa na tukapendana, jitahidi mwanangu achana na lile 'chizi' si unaona hali yetu hapa nyumbani badili maisha yako sie jua limeshazama tunasubiri tuu giza liingie , hatutakuwa tayari kukuona unajiingiza kwenye majanga Anord hata wazee wake wameshamkatia tamaa, unasemwa mwanangu, wanakusema hata ndugu zake wangine wanakulaumu kuwa huenda umemroga sasa unajutia''Aliongea mama Atu kwa sauti ya upole.
''Hapana mama siwezi kuolewa na mtu mwingine zaidi ya Anord''
''Mwanangu, nisikilize mama yako, wasikilize wakubwa wako, Anord hana maisha mengine zaidi ya mateso yale angalia njia nyingine ya kufuata''
''Atapona mama niamini'' Atu alimwambia mama yake kwa upole.
''Mwanangu fikiria vizuri'' Aliongea mama Atu na kutoka chumbani kwa bintiye.
''Vipi amekubali?'' aliulizwa mama Atu na mumewe baada tu ya kufika chumbani kwao akijilaza kwenye godoro la sufi liliokuwa juu ya kitanda cha ngozi.
''Kesho hakikisha hatoki hapa , asije kutuaibisha bure''
''Sawa mume wangu nitamwambia''
Wakalala.
Asubuhi ya siku iliyofuata, ilikuwa siku muhimu na ngumu kwa wazazi wa Atu kwani licha ya kutegemea ugeni ambao waliamini ungeleta unafuu wa familia ile kimaisha , lakini hali ilikuwa ni ngumu kumshawishi Atuganile akubaliane na wazazi wake juu ya suala la ndoa.
Atu alikuwa hamfikirii mtu mwingine zaidi ya kipenzi chake Anord ambaye wazazi wake walidai ni chizi na asingepona.Kila alipofikiria ndoa wazo la kwanza kumjia lilikuwa ni kati yake na Anord na si vinginevyo , alitamani kuwasikiliza wazazi wake na kukubaliana nao lakini aliona kama alikuwa akimwonea Anord ambaye kuumwa tuu ndiko kunamfanya asifanye mipango ya kumuoa ,aliumia kumwona Anord akimpenda hata akiwa katika 'ukichaa' wake.
Alijua fika hali ngumu ya maisha yao, maisha ya familia isiyojua ladha ya chai na kama uliijua basi ni enzi za utoto wake ambapo alienda kwa akina Anord wakidowea chai baada ya ndugu wa Anord kuja na sukari watokapo Mjini.
Alitamani kuibadilisha familia yake lakini moyo ulimwambia wa kubadilisha ni ndoa yake na Anord na si mtu mwingine.
''Mama siwezi kuolewa na mtu mwingine isipokuwa Anord''Alisikika Atu akimwambia mama yake bila kujua kuwa aliyekuwa amesimama nyuma ya alipokaa si mama yake tena bali baba yake aliyekuwa akifikiria mengi sana juu yake.
''Umerogwa wewe utake usitake , utaolewa na leo sitaki uniaibishe labda kama mimi si baba yako, unikane kwanza mie ndipo umkane mchumba wako''Aliongea baba Atu kwa sauti ya chini lakini ya ukali.
''Lakini baba mbona mnanilazimisha'' Atu aliongea kwa sauti ya chini huku akitetemeka , hata mwenyewe hakujua alitetemeka kwa sababu ya hasira ama uoga.
''Ni kwa ajili ya maisha yako Atu, sisi siku yoyote tunakufa utaishi maisha gani huyo Anord leo mwezi wa ngapi yupo kwenye 'ukichaa' ?''
''Atapoana baba''
''Hujui mwanangu ukichaa hauponi , hutulia tuu na siku yoyote huibuka, atakuja akuue siku moja mwanangu'' Mama alichangia akiwa na bakuli lilijaa viazi vitamu ambavyo hakuna ambaye alikuwa na hamu navyo ila mazoea tuu yalimfanya awe amevipika.
'' Lakini.....''
''Lakini nini mwanangu fungua macho uone, ngoma zako za masikio zimekufa husikiii kabisa, unatemebea ila hujongei, umerogwa kirogo kibaya sana olewa mwanangu utakuja kutulilia kaburini kutuomba msamaha kwa kutotusikiliza lakini utakuwa umechelewa kama mie mama yako naomba usituaibishe leo tumepanga kila kitu''Mama Atu alimkatisha mwanaye na kumweleza maelezo ambayo licha ya kubeba hisia nyingi za upendo kwake lakini ujumbe huo uliingia sikio moja na kutokea la pili.
''Siwezi kama laana mniachieni nikaokote makopo na huyo mumuonaye kichaa siolewi na mtu mwingine zaidi ya Anord''Aliongea Atu kwa hasira na kuondoka.
''Atu....Atuuuuu ,,,,, Atu mwananguuu'' aliita mama lakini Atu aliwageukia kama kuwaaga na kuanza kukimbia.
''Anaenda wapi yule?''
''Achana naye atarudi tuu hana pa kwenda atarudi tuu hapa''Aliongea baba Atu na kuingia ndani huku akiwa na hasira sana.
Mama Atu aliangalia njia aliyopita mwanaye huku taswira ya tukio la Atu akiinuka na kuanza kuondoka nyumbani ikijirudia akilini mwake maneno ya mwanaye yalijirudia kichwani kama mwangwi ulijirudia na kukera akili yake.
Alimpenda mwanaye, na alitaka aolewe na mtu mwenye msimamo wa maisha kwa ajili ya maisha yake baadaye lakini mwanaye alikataa akimng'ang'ania mwanaume ambaye kila alimwona alimtazama kama 'chizi' ambaye maisha yake yalikuwa ni hadithi iliyokera na kutisha , akihisi mwanaye karogwa si bure.
''Anaenda kujiua?''
''Hapana, atajiuaje na mpenzi wake anayempenda hajafa?''
''Au laana tulizomtisha nazo?''
''Mbona hajawahi kuwa na tabia mbaya huyu mtoto?''
Mama Atu alijiuliza maswali yale peke yake na kuelekea ndani ya nyumba lakini kabla ya kuongia ndani alitupa macho kwenye njia aliyoondokea mwanaye.
''Ugeni''Alijikuta akiongea mwenyewe huku macho yamemtoka pima kwa mshangao.
________________
Ulikuwa ni ugeni walioutarajia lakini kutoka na hali waliyokuwa nayo wakati ule ni kama vile hawakuwa na taarifa nao.Kitendo cha binti yao kumng'ang'ania Anord kilitibua tumaini walilokuwa nalo wazazi hawa.
Zile ndoto za binti yao kunywa chai kila alipojisikia, kuangalia televisheni na hata kupanda gari la mumewe zilififishwa na msimamo wake juu ya penzi lake kwa 'kichaa' Anord.
''Karibuni ndani'' 
''Asante hapa hapa nje panatosha mama ,kaupepo ka mti kanahuisha ujana wetu''
''Hahahaaaaa! uzee haukwepeki mwanangu, ngoja niwaletee viti'' 
''Usihofu mama tutakaa hapa mkekani''
''Basi ngoja niukung'ute maana upepo umeshajaza vumbi'' Aliongea mama Atu na kukung'uta vumbi na maganda ya viazi vitamu yaliyokuwa yamegandiana mkekani.
''Karibu sana mwanangu''
''Asante shikamoo mama''
''Marhaba habari za utokako''
''Salama kabisa mama nimemwona Atu kwa mbali kule ng'ambo''
''Nilimtuma kwa shangazi yake kama akimkuta atafika sasa hivi'' Alidanganya mama Atu.
''Anhaaa , sawa sawa, kama nilivyosema siku ile leo nimekuja kukamilisha hatua za mwazo za mpango wetu'' Alianza kujieleza mshenga ambaye alikuwa ni mjomba  wa mchumbiaji ambaye hawakutofautiana sana umri.
''Hakuna tatizo kabisa mwanangu baba yako yupo ndani ngoja nimwite'' Aliinuka mama Atu na kuelekea ndani akimwacha mshenga na kijana mdogo ambaye ni kama alimsindikiza kupunguza ukali wa safari ya kufika pale.
Dakika mbili baadaye baba Atu alitoka akiusawazisha uso wake uliokosa tabathamu kutokana na msimamo wa bintiye.
''Karibu sana kijana''
''Asante sana , shikamoo''
''Marhaba''
''Shikamoo'' Aliamkia yule mdogo.
''Marhaba pole na safari''
''Asante sana''
Baaada ya maneno mawili matatu bahasha ndogo ilipokelewa na baba Atu na kuwakaribisha sebuleni ambako wageni walikaribishwa chakula, chakula ambacho kiutaratibu kilipaswa kupikwa na Mchumbiwaji ili kupimwa mapishi lakini kwa ubishi wa bintiye mama mtu akaamua kujitwika jukumu hilo kana kwamba ndiye aliyekuwa akiolewa.
Ugali wa muhogo na kuku aliyekaangwa vyema, kilikuwa ni chakula kitamu haswa tena kuku mzima si mbavu mbili , shingo na kipaja kimoja.
Shukrani na pongezi kwa mpishi zilitolewa baada ya mlo ule safi na wageni wakaaga na kuahidi kuja safari ya mwisho kwa kumalizia kabisa safari hiyo wangekuja na mchumbiaji kabisa. Wageni wakasindikizwa mita kadhaa kisha wazazi wakabaki na tafakari juu ya binti yao ambaye ndiye sababu ya ugeni ule.
''Kwa hiyo chakula umekipika wewe?''
''Hapana kapika mwenyewe''
''Nilijua umepika wewe , ningeshangaa kwani siye uolewaye''
''Kapika lakini sikumwambia kwa sababu gani kwani ningemweleza asingepika yule binti na kiburi chake cha usichana''
''Hivi kama asingepika basi shughuli ingeharibika kabisa''
''Tena ingeharibika sana na tungeaibika''Alijibu mama wakati huo walikuwa wamekaa mkekani chini ya mti huku hewa safi ya oksijeni kutoka kwenye majani ya mti ule ikiburudisha nafsi zao na kupooza miili yao iliyokuwa imechoka kutokana na shughuli za miongo kadhaa.
Walijikuta wakikaa kimya kwa muda huku kila mmoja akiwaza lake, wakati mama Atu akifikiria namna ya kumpanga Atu ili isijulikane kama alikuwa amepika chakula badala yake.Kwa upande wa baba Atu Mzee Mwakalile alikuwa akiwaza yake, tathmini ya maisha yake na ya familia yake kwa miongo kadhaa huku akijaribu kubashiri maisha ya mwanaye kama akiamua kukubaliana nao ama akiamua kuifuata njia yake.Hofu kuu ilimeingia alipojaribu kubashiri maisha ya mwanaye akiwa ameamua kufuata njia yake, kuishi bila mume na kutangatanga huku na huko baada ya mauti kumkwaaa Anord ambaye hataki hata kulisikia jina lake kutokana na upunguani wake lakini pia picha ya mwanaye akiwa punguani kama alivyo Anord kwani ukienda na kichaa waweza kuwa kichaa zaidi ya kichaa halisi.
Hapo akajikuta akishusha pumzi na kuingia sebuleni ambapo alikiendea chungu cha maji kilichokuwa konani kilichohifadhi maji yaliokuwa na  ubaridi ulioburudisha koo na nafsi na kurejea mkekani ambako alikutana na ugeni mwingine ambao haukuhitaji maelezo ya kinywa kumtia mashaka.
''Kulikoni mbona hivyo?'' Aliuliza mama Atu aliyeshtushwa na mwonekano wa Agnes rafiki wa Atu.
''Atu anakimbizwa na Anord akiwa na panga ni....''
''Wapi huko mwanangu?'' Alikatishwa na sauti nza wazazi wale waliojawa na uoga.
''Kule kilimani nimesikia kwa watu waliokuwa wakitoka kijiji jirani ni muda umepita sasa''
''Mungu wangu mwananguuu...!''Mama Alianza kutoa chozi na kelele ambazo ziliwashtua na kuwavuta majirani.
___________
Atuganile Mwakalile, wengi walipenda kumwita Atu wakati mwingine alijikuta akijisahau kabisa pale alipoitwa jina lote Atuganile , alipotoka kukwazana na mama yake juu ya suala la Anord aliamua kuelekea kwa mama mkwe wake mtarajiwa kama alivyojiaminisha Mama Anord ili wapange namna ya kumfikisha Anord kulikokuwa na maji yenye kuponya ngozi walau kuboresha mwonekano wa ngozi yake.Lakini tofauti na alivyotegemea alikutana na wanafamilia wengine ambao walipomwona tuu walianza kumcheka.
''Anord katusumbua kucha hapa anakuulizia ulimdanganya utakuja kulala hapa?''
''Mbona bila hata ya salamu jamani, habari zenu jamani''
''Salama'' Walijibu wanafamilia wale wakiwa ni pamoja na binamu zake Anord wakiendelea kucheka.
''Sasa kiwachekeshacho ni kipi?''Aliuliza kwa hasira.
''Tunacheka hiyo nguo uliyovaa akikuona lazima akutimue mbio maana rangi nyekundu kwake ni sumu tunashangaa mke wake hujui hilo''Aliongea mmoja wa wanafamilia ile.
Hapo Atu kuna kitu kilimjia akilini na kutabathamu, alitamani sana kuitwa mke wa Anord si katika utani tuu hata katika uhalisia lakini upande mwingine wa moyo wake ulimuuma sana kwani haukuwa utani bali ni kejeli kilichomuumiza zaidi ni zile kejeli kutoka kwa ndugu wa Anord na si watu baki.
''Kwa hiyo alilala hapa?'' 
''Alale wapi unataka aje kutuletea ukoma kwenye mashuka yetu?, mama alimtimua mapema kabisa tena alitaka amwone mwamba wa kumfungulia wenyewe tunamwogopa''Alijibu mwingine na kuwafanya wote waliomsikia watabathamu na kucheka vicheko vya chini chini isipokuwa Atu ambaye moyo ulimuuma sana kusikika mama mzazi akiwa wa kwanza kumchukia na kumwogopa mwanaye.
''Na mama yuko wapi?''
''Kaondoka na katuambia akija yeyote tusimwambie''Aliongea mama mmoja ambaye kwa haraka hara alikuwa ni mdogo wake mama Anord kutokana na kufanana kuanzia sura hata sauti zao.
''Sawa , baadaye'' aliaga Atu huku akiwa na donge la uchungu moyoni mwake kwani alijua yule mama aliamua kumpiga chenga kwani alionekana kukata tamaa.
Hakukumbuka kama waliitikia kuaga kwake zaidi ya vicheko vilivyosikika huku na kule , alitembea haraka haraka hadi maeneo ambayo aliamini angemkuta Anord na kujaribu kumfikisha kule kuulikokuwa na maji ya tiba kwa mbinu iliyomjia akilini mwake aliamini mtembea bure si sawa na mkaa bure.
Alienda sokoni hola, shuleni hakuna , hospitalini nako akamkosa akaamua kwenda sehemu ambayo hakuwaza kama angemkuta lakini tofauti na alivyotegemea alimkuta Anord kipenzi chake akiingiza kama mchungaji afungishaye ndoa kabla ya kuanza kujifanya bwana harusi akikata keki kichekesho kilikuwa ni alichokifanya kuwa keki , tofali kubwa lililochomwa na cha kukatia ni upanga ambao ulikuwa mpya kabisa.
''We Anord ndo nini unafanya?'' Aliongea Atu akimrushia jiwe dogo alijua kabisa katika vitu vilivyomkera Anord ni kurushiwa mawe kwani alikuwa akimkimbiza yeyote atakayemrushia jiwe hadi amkamate sasa alikuwa ameongezewa kitu kingine nguo nyekundu alijua lazima Anord angemkimbiza kitu alichoamini kingemfanya amfikishe kijiji kilichokuwa na yale maji yaliyoponya.
Anord alivyogeuka alimwangalia aliyerusha jiwe kama akitafakari kitu na kumpumbaza Atu ambaye ni kama alizubaa na kujikuta akiwa mikononi mwa Anord huku panga likiwa kwenye mkono mwingine hapo Atu akababaika huku akili yake ikifanya kazi haraka haraka.
''Umemwona Mwalimu Chiwatho yule?'' Aliuliza Atu akimtaja mwalimu ambaye Anord alikuwa hapatani naye wakati wakisoma shule ya msingi na mara kwa mara hata katika ukichaa wake alikuwa akimtaja mwalimu yule akiahidi kumchapa kama alivyokuuwa akimchapa.
Kugeuka na kulegeza mkono uliokuwa umemshika Atu lilikuwa kosa kwani alishtukia kuona Atu akiwa kama mita mia mbili kutoka alipokuwapo na akimrushia mawe madogo madogo kitu kilichochochea hasira za Anord sasa vichocheo vya hasira zake viliongezeka kuanzia kurushiwa mawe, kuiona rangi nyekundu na kudaganywa kwa kukumbushwa mbaya wake ambaye alikuwa na miaka kama mitano kaburini.
''Nitakukamata nikugeuze supu ya kwenye harusi yangu na Atuganile Mwakalile''Aliongea Anord na kuanza kumkimbiza Atu ambaye naye alikimbia akiacha mita kama mia na hamsini kati yao njia ikiwa ni kuelekea kwenye kijiji kilichokuwa na maji ya uponyaji magonjwa ya ngozi.
Mwanzoni watu hawakugundua kama watu wale walikuwa wakikimbizana kutokana na umbali kati yao na namna Atu alivyokimbia kwa na kusimama simama na kuwachanganya waliokuwa wakimwona kuhisi kuwa alikuwa ameamua kukimbia na kuwahi sehemu.Hadi walipokuwa nje ya kijiji kile walipoonwa na watu waligundua kuwa Anord alikuwa akimkimbiza mtu tena kwa sababu ya nguo yake nyekundu kumchanganya waliamua kutoa nguo nyekundu nje ya nyuma zao lakini hakuchepuka zaidi ya kunyoosha njia akimfuata Atu ambaye licha ya kuwa hakuwa na kasi sana lakini ile ari ya kutaka kumsaidia Anord ilimfanya azidi kukimbia huku akijitahidi kumwokoa Anord.
Wakiwa wamebakiza kilima kimoja kukifikia kile kijiji walikutana na kundi kubwa la watu ambao walikuwa wakitoka kijijini huko, hapo alipata hofu kuhisi Anord angezuiwa na wale watu na njia yake ya kutaka kumponya ingeshindwa.Kabla ya hapo umbali baina yao uliwaokoa na hata watu walichelewa kugundua tena waligundua baadaye sana baada ya kutafakari hivyo wangeshindwa kuwafikia kwa kuwa wakikuwa wakikimbia pia kitendo cha Anord kuushika ule upanga kwa namna ambayo hakuna aliyejua kuwa alikuwa na shari kana kwamba alikuwa ametoka kununua na alikuwa akimkimbilia mtu aliyekuwa naye safari moja.
 

0 comments:

Post a Comment