Monday, 2 May 2016

JUMA KASEJA ''TAJIRI ANAYEDAKIA MBEYA CITY'' 01

Na;Mwanakalamu
Katika kijiji kimoja kilicho kusini Magharibi mwa nchi ya Tanzania kikipakana na Nchi ya Malawi  kwa upande wake wa Magharibi na Msumbiji kwa upande wa Kusini , ni mwisho wa safari yangu ndefu iliyoanzia Dar es Salaam , Mbeya Mjini Kyela  hatimaye nikafika kwenye kijiji hiki.Ni safari ichoshayo kwani ni safari yangu ya kwanza ya ziwani ,tofauti na nilivyotoka jijini Dar es salaam hadi Kyela  kutoka Kyela hadi katika kijiji hiki imekuwa ni safari ya roho mkononi sala zote zimeisha njiani maana nimekuwa muoga sana kimeli kidogo ambacho kimekuwa kikizimika karibu kila baada ya Kilomita kumi kilikuwa kikitikiswa hata na kiwimbi kidogo kisicho na nguvu ya kubomoa tuta la viazi.
Jioni hii nimeshuka Melini na kumshukuru Mungu kwa kunifikisha salama nikijiapiza kutosafiri tena majini na kuelekea ziliko nyumba za wenyeji wangu ambaye alionekana kuchoka kunisubiri kwani ni siku ya tatu ananisubiri lakini Meli imechelewa kutokana na hitilafu 'zinazosemwa' kuwa ''zipo juu ya uwezo wao''.Nageuka nyuma mara mbili mbili kulitazama ziwa hili ambalo kwa siku kadhaa nilihisi kama lingekuwa kaburi langu lakini Mungu kaniepusha.Miale ya jua inapiga juu ya maji na kuleta madhari fulani ya tumaini, tumaini la maisha ambayo kuzama kwa jua ni maandalizi ya kuchomoza kwake baada ya saa kumi na mbili.
Naachana na ziwa na machweo yale na kufuata barabara inayoelekea yaliko makazi nikiwa katika kundi la wasafiri wengi ambao kwa safari ile walikuwa si tuu marafiki bali kama ndugu na mmoja wa wasafiri hao alikuwa ameamua kunipeleka hadi kwa mwenyeji wangu.
Nilijivunia Utanzania wangu, tuna sifa ya ukarimu.
Mita chache kutoka ziwani nakutana na uwanda  mkubwa ulio na nyasi  zilizolingana ni kama uwanja uliopandwa nyasi kwa ajili ya michezo.Kuna kundi la vijana ambao wanaendelea na michezo yao,kundi lingine ni la watoto wakiwa na mifugo mbali mbali ikila nyasi ,mbuzi na ng'ombe wanaonekana kuwa na haraka kwani wanakula majani huku watoto kadhaa nyuma yao na bakora wakielekezwa ziwani,nadhani kunywa maji kabla ya kupelekwa zizini.
Kundi lingine lilikuwa ni la watoto waliokuwa wakicheza mpira kwenye kiuwanja kidogo kilichokuwa pembeni tuu mwa ule uwanja wa wakubwa.
Hapo nikamwona mtoto mmoja akiacha kucheza mpira na kumkimbilia mwenyeji niliyekuwa nimetanguzana naye , kumbe ni baba yake.
Baada ya salamu na bashasha za baba na mwana ,mtoto yule ananigeukia na kunisalimu.Tunasalimiana na naanza kumuuliza maswali , mara shule mara ziwani na nikafika alipopapenda, kwenye mpira.
''Unacheza mpira kama nani?''Namuuliza swali ambalo ni kama alisubiri nimuulize.
''Kaseja, Tanzania One''Ananijibu akirukaruka akionekana kunizoea sana hana  habari tena na baba yake.
''Kwa hiyo wewe ni golikipa?''
''Ndiyo nadaka hadi penati kama kaseja'' Anaongea akinionesha kwa kidole nyuma ya fulana yake ya bluu , nakaza jicho sioni chochote.
''Namba moja''Naongea baada  ya kufanikiwa kuiona moja iliyoandika kwa wino wa kalamu yakili bila mpangilio inaonekana aliandika mwenyewe.
''Huioni Juma Kaseja hapo?'' Ananiuliza mtoto akiwa na furaha sana, hapo nayaona pia hayo maandishi.
''Umeshawahi kumwona Kaseja?'' Namuuliza swali ambalo ni kama linamfanya awe mpole akifikiria kitu.
''Ninayo picha yake, wakileta umeme tutakuwa tunamwona Kaseja kwenye TV''Ananieleza na kumhurumia yule mtoto kwani nahisi kama umeme huo utawafikia kabla ya kaseja hajaachana na soka.
''Utamwona tuu mdogo wangu''Namfariji.
''Nitamwona baba alisema Mbeya City wakicheza na Majimaji tutaenda nimwone kaseja''Namtazama baba yake ambaye anaonekana kuumizwa na ahadi ya mwanaye, namhurumia.
Tunafika nyumbani kwa mwenyeji wangu , namsalimu kisha  naagana na Kaseja Mdogo na baba yake''
Naendelea na taratibu nyingine hadi usiku  kisha nalala na mwenyeji wngu ambaye ni binamu yangu anayefundisha huko kwenye shule moja ya msingi.
Asubuhi, naamka kwa kuchelewa saa tano kamili tena naamshwa kwa ajili ya kifungua kinywa, natamani kuoga maana nilikuwa na uchovu sana naingia kwenye bafu ambalo hata buibui wameweka makazi kama halijawahi kutumika.
''Wenyewe tunaoga ziwani''Naambiwa na mwenyeji wangu akinieleza utaratibu wao, unaamka na kwenda ziwani kuswaki  na kuoga.
''Kifungua kinywa kipya kidogo, samaki aliyekwaushwa na chai, pia kuna ndizi zilizopikwa na samaki wabichi''
''Hizo ndizi amekuletea  yule mwenyeji wako wa jana alokuja na baba yake'' 
''Nani kasej....?''Sifanikiwi kumaliza swali langu nasalimiwa na yule mtoto mkononi ana kipande cha gazeti.
Baada ya salamu napewa kipande cha gazeti ambalo bila kuuliza inaonekana alilibandika ukutani na ugali wa mhogo, ni gazeti la malawi  lina picha ya kaseja.
''Huyo ndiye kaseja kaka'' Anaongea yule mtoto akiwa na furaha.
''Naam ni Kaseja...
KESHO JIONI TUNAENDELEA NA KISA HIKI CHA KASEJA

0 comments:

Post a Comment