ads

Wednesday 31 August 2016

KUSHUKA KWA BEI ZA MAZAO NA KISA CHA MTEGO WA PANYA


Na.Moringe Jonasy 

Tarehe nane mwezi huu unaoisha leo ilikuwa ni ile siku maarufu ya maadhimisho ya wakulima 'nane nane' ambapo imekuwa kama mazoea wakati mwingine hata tunasahau kabisa inahusu nini.Sikutaka kuandika kwa nilichokiona kwenye kilimo katika miaka kadhaa ya kushiriki kwenye kilimo kama mnufaikaji ( kwa kuwa ni mtoto wa mkulima) , mtazamaji ( nikiwatazama wengine) na baadaye mkulima nikiwa nimehamasika na sera ya kilimo kwanza ambayo nadharia yake iliniingia vyema akilini na kuamua kwenda kuwa mkulima. 
Sitaki kuzungumzia namna nilivyoshawishiwa na sera hiyo iliyoishia hewani na kinadhari na kuwa mwiba kwa tulioingia 'mkenge' na kuwaamini wanasiasa kwenye nadharia ile iliyovutia kwenye ' karatasi' bali kuna kisa cha mtego wa panya kinavyohusiana na kilimo chetu.

 Kisa cha mtego wa panya ni pale mfugaji mmoja alikuwa akifuga kuku mbuzi, na ng'ombe lakini alikuwa akisumbuliwa na panya kila siku hivyo akaamua kuweka mtego wa panya uvunguni mwa kitanda.Panya alipoona hivyo akaamua kwenda kwa kuku kumweleza juu ya mtego huo lakini kuku akamshangaa panya na kumwambia "hayamuhusu" ye hawezi ingia chumbani kwa mfugaji. Panya akaenda kwa mbuzi huyu tena kwa kicheko akamwambia "hayamuhusu" huo uvungu wa kumwingiza yeye una majani ama kisima cha maji?. Panya akaamua kupeleka habari hiyo kwa ng'ombe akicheka hadi akajamba akimshangaa panya kwa 'upuuzi' wake na kumwambia "hayamuhusu" panya akaondoka kajiinamia kwa unyonge akisubiri matokeo.
 Usiku ule nyoka aliingia kwenye uvungu wa kitanda cha mfugaji na akanasa mkiani na kuanza kujinasua, mkulima aliposikia kelele akajua tayari panya amenaswa kizembe kizembe akapeleka kichwa uvunguni amwone huyo panya anavyohangaika na amuulie mbali. Hakujua alikuwa akimchungulia nyoka mwenye hasira ya kunaswa mtegoni, yule nyoka akamgonga kichwani na kumwachia sumu ambayo ilimpa maumivu makali.Baada ya kupiga kelele zilizoita watu waliokuja kumuua yule nyoka. Asubuhi ya siku iliyofuata mke wa yule mfugaji akaamua kumwandalia supu ya kuku mumewe hivyo yule kuku akachinjwa siku iliyofuata jamaa wa mfugaji wakaja kumjulia hali , mboga ikawa tatizo mke wa mfugaji akaamua kumchinja mbuzi na kufanya mboga kwa ajili ya  ugeni uliokuja kumjulia mumewe hali.
Siku ya iliyofuta yule mfugaji akafariki na ng'ombe akachinjwa msibani , hivyo mtego wa panya ukawasomba na wasiokuwemo. 
Kisa hicho nakilinganisha na hali ya kilimo ilivyo nchini, bei za mazao imeshuka sana kiasi kwamba wakulima walioingia kwenye kilimo " kujaribu" wajute na kujiapiza kutolima tena.
Nawatazama kwa jicho la huruma kwani walikuwa wameshapanga hata aina za magari ya kununua wakiuza mazao yao. Mijadala kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari umepamba koto kiasi cha kutishia hata utawala wa mada za siasa nadhani si kwa sababu ya waandishi kujua umuhimu na mchango wa kilimo bali nadhani kwa kuaa kuna baadhi yao wamewekeza kwenye kilimo kwa kuwa waliambiwa "kilimo ni mbomba" na ' kinatoa'. Ingawa kuwa waliojaribu kutoa maoni juu ya namna ya kupandisha thamani ya mazao yanayoharibika(kuoza) kama nyanya lakini kuna wale waliokuja na kile ambacho naweza kukiita "kebehi" ama dhihaka kudai kuwa bei ya bidhaa hizo ni halali wakiwa na maana kuwa kabla ya hapo wakulima na wafanyakazi wa bidhaa za kilimo walikuwa wakiwaibia wateja kwa kuwauzia kwa bei isiyo halisi. Huenda kwa sababu ya kutojua kwake ama kwa sababu ya pengine tambo za jamaa ama jirani yake ambaye alimtambia kuwa amelima na atakuwa tajiri kwani ameonekana kufurahia janga hili ambalo leo linawalisa wakulima. Kwa akili na mawazo yake hajui kilio cha wakulima ambao wameweka nyumba zao rehani ili wapate mikopo kisha wakalima pia kuna wale ambao licha ya kutumia mitaji yao ya kuunga unga waliweza kutoa ajira kwa wenzao wakiwa na matarajio ya kubadili hali zao za kiuchumi na mbaya zaidi hajui nini kinaenda kutokea huko mbele kwani ile ari ya wakulima kulima itapungua na kupandisha bei ya mazao hayo zaidi hata na ilivyokuwa huko nyuma na kupelekea naye kuingia kwenye " mtego wa panya" alioamini kuwa haumuhusu.
Hiyo ni tabia ya wanadamu wengi kufurahia majanga ya wengine kisa wanaamini hayawahusu bila kujua kuna athari kubwa yaja upande wake. Wengi hawaangalii gharama zinazotumika kwenye kilimo na kuamini wakulima wanapata faida kubwa wasiyostahili kwa kusoma tuu nadharia za kusimuliwa ama kuzisoma Jamii Forum kutoka kwa wataalam waoga kutekeleza nadharia yao kwa vitendo. Niwaombe wakulima wenzangu tusimate tamaa kwani kipindi cha kuja kutengeneza 'super profit' kinakuja kutokana na waliokuja kujaribu kilimo kukata tamaa na kutuangalia kama kuku alivyosubiri kusikia taarifa ya kifo cha panya. Naomba kuwasilisha karibuni shambani...

0 comments:

Post a Comment