Saturday, 24 May 2014

KWA NINI HADI WEUPE?

Hili jambo tangu kale,na sasa nashuhudia,

Hata waloenda shule,bado wanalirudia

Kitu akifanya Yule,wengi tutashabikia, 
Kitu afanye mweupe,hapo wataona kweli.


Tuna mito na milima,hakuna anayejali,
Ila wao wakisema,nasi tutaona mali,
Na sasa nao walima,watu wadai vibali,
Kitu afanye mweupe,hapo wataona kweli.


Hata babu wa Samunge,alisema wakaona,
Walienda na wabunge,weupe walipowaona,
Tunajiweka wanyonge,badala ya kukazana,
Kitu afanye mweupe,hapo wataona kweli.


Mikumi na Serengeti,wendao watu wa nje,
Hulipi hakuna geti,wasoma kama wa nje,
Twawapigia magoti,kama vile tupo nje,
Kitu afanye mweupe,hapo wataona kweli.


Wameshalala na mbwa,kisa kasema mweupe,
Mweupe pesa aombwa,wambana kama kupe,
Kama maji watasombwa,nyie nunueni kope,
Kitu afanye mweupe,hapo wataona kweli.


Nini sisi twakiweza,ama kuimba ngololo,
Almasi twambeza,eti aimbe ndombolo,
Sitaki kuwagombeza,mnone ‘vuta ugolo,
Wao nao kama sisi,sema tunawatukuza..

0 comments:

Post a Comment