ads

Wednesday 28 May 2014

SHAIRI MAALUMU LA ALBERT MANGWEA KUMBUKUMBU YA KUTIMIZA MWAKA MMOJA TANGU KIFO CHAKE

Natoka zangu shuleni,moyoni nina amani,
Mara simu mfukoni,yapigwa sijui nani,
Hata salamu jamani,ameshakufa jamani,
Ninahisi kama ndoto,ipo siku atarudi.

Mangwea hatupo naye,nakumbuka alisema,
Ondoa matani weye,maneno gani wasema,
Sikiza redio weye,hata mimi niligoma,
Ninahisi kama ndoto,ipo siku atarudi.

Baadaye nahakikisha,Millard anatangaza,
Amepoteza maisha, mwenzake tumemlaza,
Ubishi uliniisha,ni kweli aliniliza,
Ninahisi kama ndoto,ipo siku atarudi.

Walisema mengi sana,madawa mara visasi,
Wengine tuligombana,kubishana nini sosi,
Si wazee si vijana,waajiri na mabosi,
Ninahisi kama ndoto,ipo siku atarudi.


Walisema ni dhuluma,akajikuta mhanga,
Majani akalalama,hata siku ya matanga,
Omari naye kusema,si zogo wakalitunga,
Ninahisi kama ndoto ,ipo siku atarudi.

Siku mwili wawasili,nilitega redioni,
Nilistaajabu kweli,idadi ya uwanjani,
Kama kawa waswahili,mara kazaa na nani,
Ninahisi kama ndoto,ipo siku atarudi.

Kama siku ya taifa,Jamuhuri palijaa,
Kumbe kaka amekufa,si mtu kumshangaa,
Kweli sisi  si malofa,sema tuu kuzubaa,
Ninahisi kama ndoto,ipo siku atarudi.

Siku naenda Kihonda,machozi yalinitoka,
Kaka kweli ameenda,ni kweli ametutoka,
Ni kweli tulimpenda,ila mungu kakutaka,
Si ndoto katangulia,tunakuja nyuma yake.

Umeenda kaka yetu,nyimbo zako tumaini,
Sasa wewe funzo kwetu,kuwa wote kaburini,
Hii dunia si yetu,kumbe tumo safarini,
Si ndoto katangulia,tunakuja nyuma yake.

STAREHE KWA AMANI ALBERT MANGWEA

0 comments:

Post a Comment