Thursday, 31 December 2015

CHUNGU TAMU ,BONGO FLEVA MWAKA 2015

Na.Moringe Jonasy

Mwaka 2015 umebakiza masaa machache kabla ya kutokuwepo tena katika zama za dunia hii.Maana yake hakutakuja kutokea mwaka mwingine utakaoitwa 2015 ,umepita.Kwa walio wengi mwanzo wa mwaka mpya hujawa na matuamini na mipango kibao juu ya huo mwaka wakiamini kuna mengi watayafanya kuliko mwaka uliopita ingawa hadithi huwa ni ile ile kila ifikapo kwenye mwisho wa mwaka huo ambao unapoanza unahisiwa kuwa na baraka tuu bila kuwa na misukosuko.
Kwenye tasnia ya Muziki wa Bongo maarufu kama Bongo fleva(Hip hop,RnB ,zouk na Afro pop inayoimbwa na wanamuziki wa Tanzania) kumekuwa na mambo mengi matamu na machungu kwa wadau wote wa muziki na hata jamii kwa ujumla ambayo ndiyo huzalisha wanamuziki.Yafuatayo ni baadhi ya mambo yaliyougusa muziki wa Bongo kwa mwaka huu unaoisha leo;
1.KUIBUKA KWA WANAMUZIKI WAPYA
Huenda walikuwepo kwenye tasnia ya muziki tangu miaka kadhaa iliyopita lakini mwaka huu wameonekana na kutambulika kwenye jamii ndani na hata nje ya nchi.Miongoni mwao ni mwanamuziki wa kike Ruby ambaye licha ya kutoa nyimbo chache na kushirikishwa kwenye nyimbo mbili tuu ameonekana ni mmoja wa wanamuziki wa kike walioufaidi mwaka huu kwa mafanikio.Kwa upande wa wanaume Hamonize ameonekana kuwawakilisha kwa kufanya vizuri sana chini ya record label ya Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platnumz na kufanya nyimbo mbili na video moja ya kiwango cha juu.
2.WAKONGWE KUREJEA TENA KWA KISHINDO
Naam, wanamuziki wengi wamekuwa wakipata taabu kurejea kwenye masikio ya watu kwa kazi nzuri na kuuaminisha umma kuwa kweli wana vipaji na wanajua kushindana na wanamuziki wa zama hizi lakini wamejikuta wakiangukia pua na kuishia kulaumu media.Lakini kama ulivyokuwa mwaka jana ambapo Alikiba alirejea na kuwapiga vikumbo waliokuwepo na kuweza kufanya matamasha jijini, mikoani na hata nje ya Tanzania na Afrika mwaka huu umekuwa ni mwaka wa Q Chief na amefanikiwa kutoa nyimbo kadhaa huku wimbo wake wa For You ukiuthibitishia umma kuwa kuimba ni kipaji chake.Yumo pia Jay Moe ambaye mwisho wa mwaka huu ametoa wimbo uliodhihirisha ukali wake.Mb dog naye katangaza vita ya kimuziki kwa mwaka ujao kwani ameahidi kufanya mengi sana.


3.WAKONGWE KUSHINDWA KURUDI
Wako wapi Daz Nundaz, yupo wapi 20%, Ray C,GK,TNG,JI,Dataz,Chelea man,Ditto je,au hata Ferooz? Hawasikiki na ukiwasikia basi kwa mambo mengine kabisa yasiyohusu muziki ama ahadi za kurejea tena kwenye muziki huku wakiponda vipaji vilivyopo na kutuambia kuwa si halisi.Lakini wito wetu ule ule waje watuoneshe hivyo vipaji halisi basi kwa kufanya nyimbo kali.Hussein Machozi naye licha ya kufanya wimbo mmoja mkali wa 'Ulikuwa wapi' ameishia kulalamika kwenye vyombo vya habari mara anaacha muziki mara sijui anaenda kucheza soka na bilinga bayoyo nyingi zichoshazo.
4.BONGO STAR SEACH
Kama kumbukumbu zitakuwa sahihi huu ni msimu wa nane na shindano hili licha ya kuzalisha wanamuziki wengi bado limekuwa na 'gundu' la kutotoa washindi wanaong'aa baada ya shindano lakini kwa mwaka huu waandaaji na wadhamini wametengeneza mazingira ya kutuaminisha kuwa tutashuhudia washiriki wengi waking'aa.Malalamiko hayakukoma kwa mshindi kwa madai kuwa hakustahili lakini kwangu mwaka huu wameniridhisha zaidi kwani kuanzia kumi na mbili bora wote walistahili kuwa washindi kwani walionesha vipaji halisi kama wao walivyodai wadhamini wao.

5.VIDEO ZENYE UBORA
Naam, Tanzania tumepiga hatua leo hii katika video kumi zitokazo kwa wanamuziki wa Tanzania basi saba zina viwango vya kupigwa kwenye televisheni kubwa duniani.Waongozaji wa ndani wamejitahidi kuzalisha vilivyo bora kuendana na ushindani na kujaribu kuwabakiza wanamuziki waendao kutengeneza video za nyimbo zao nje na wakati mwingine walijikuta wakilazimika kutoka na wamuziki hata huko nje ya nchi.Uwekezaji kwenye video umeongezeka hata wale wanamuziki walionekana 'wabahili' wameamua kuvunja akaunti zao na kuwekeza kwenye muziki.

6.WALIKUWA BORA LAKINI WAKAPUUZWA
Hapa wapo wengi sana, yupo Richard Mavocal ambaye kwa muda mrefu amekuwa akifanya juhudi katika muziki wake amejikuta akipuuzwa sijui niseme na mashabiki wa muziki ama wadau wote wa muziki.Wimbo na video yake ya 'pacha wangu' ulianza na 'gundu' la kukosa video bora ya inayopendwa kwenye tunzo za watu lakini hata kwenye tuzo za muziki za kilimanjaro sidhani kama iliingia hata kwenye kipengele  kimoja.Yupo pia Lady Jay Dee ambaye licha ya kufanya nyimbo kali alionekana kuwa na mwaka mbaya sana.Pia kulikuwa na wanamuziki wengine kama Belle nine ambaye kwa bahati mwaka unamwishia vyema.

7.TUNZO ZA MUZIKI ZA KILIMANJARO
Naam kama ilivyo BSS na popote ambapo pana washindani lazima pawepo na maneno lakini mwaka huu ulionekana kuwa mzuri zaidi kwa Alikiba kwani alifanikiwa kutwaa tunzo sita kati ya vipengele sita alivyopendekezwa jambo lililovutia ni kuwa vipengele sita kati ya saba alivyowekwa vilikuwa vimetokana na wimbo mmoja wa 'Mwana'.Wengi walikandia ushindi wake lakini kwa nguvu ya mashabiki waliokuwa nayo alikuwa anaweza kubeba tunzo zote kama siyo kosa la mtengeneza poster wake kuweka code ya wimbo ulioshinda wa Nitampata wapi na poster kusambaa basi alikuwa anaweka rekodi yake ya kubeba tunzo kwenye kila kipengele.Licha ya makosa mengi yaliyoorodheshwa na wengi juu ya tunzo hizo ila utaratibu wa kura za mashabiki kuamua washindani na ushindi kwa asilimia mia moja uliharibu sana ubora wa tunzo hizo kwani ushabiki pekee ndio ulioamua ushindi na ni jambo ambalo likiendelea litaharibu na kushusha thamani ya tunzo hizo.

8.TUNZO ZA NJE
Ulikuwa ni mwaka mbaya kwa Wanaijeria waliokuwa wakituona kama washiriki wenye bahati kwani kila walipoliona jina la Diamond basi walijikuta wakiogopa , alikuwa mshindani mwenye uhakika wa kushinda.Diamond amefanya vyema sana na kumuweka si tu yeye bali hata nchi ya Tanzania katika nafasi za juu za muziki barani Afrika.Wanamuziki wengine kama Vanessa Mdee, Ommy Dimpoz, Alikiba walibahatika ama kushindania au kushinda kabisa tunzo hizo walizoshiriki.Licha ya Tunzo hizo kuwa kama alama ya mafanikio ya muziki wetu zilikuwa na dosari, kwa mfano moja ya tunzo hizo zilishindanisha nyimbo zilizotoka miaka ya nyuma wakihisi ni mpya pia kuwaweeka wanamuziki wenye nguvu na ushindani mkubwa nchini kwa lengo la kutaka 'kick' tuu nchini.Mashabiki wapuuzi pia walifanya upuuzi kwa kuwashabikia na kuwapa kura wanamuziki wa nje walioshindana na wanamuziki wa ndani mfano pale mashabiki wasiomtakia mema (wakiwemo baadhi ya mashabiki wa Alikiba na Wema Sepetu) walimpa sapoti Davido ili kumvunja moyo Diamond ,jambo hili halifai na likiachwa litakuja kuuvuruga umoja wa muziki na wanamuziki wetu.


9.KOLABO ZA NJE KUWA ISHARA YA MAFANIKIO
Naam , ilifika kipindi kila mwanamuziki alidai kuwa na 'kolabo' na wanamuziki wa nje baada ya kuhisi ndiyo alama ya mafanikio kimuziki.Sikatai huwa na matokeo chanya kama vile kuongeza mashabiki lakini ilifika mahali pabaya kwani ile 'Chemistry' haikuwepo tena walichojali ni kolabo.Diamond ndiye wa kubeba lawama kwani kitendo chake cha kufanya wimbo mkali na Davido basi kila mtu akaiga hadi naye akajisahau na kuona kolabo ni jambo kubwa kuliko muziki safi na akaja kufanya wimbo mbovu na Donard wa Afrika kusini.Lakini kwa Diamond kolabo zilikuwa na faida kuliko wanamuziki wengine kama Shetta licha ya Shikorobo kufanya vizuri akajikuta kama 'amestack' na kushindwa kutoa wimbo mwingine huenda kwa hofu ya kutoifunika Shikorobo'.

10.JIDE VS CLOUDS MEDIA
Kinachosemekana kama bifu kati ya Mwanamuziki Lady Jay Dee na wahusika wa sehemu aliyowahi kufanya kazi Clouds Media bado kimeonekana si tuu kuaathiri muziki wa Jide bali hata mashabiki wa muziki mzuri uliotoka kwa mwanamuziki huyu nguli ambaye aliwahi hata kuimba na nguli wa Afrika Oliver Mtukdzi wa Zimbwabwe.Kupotezwa kwa Jide kilazima kumeharibu kabisa ule ushindani wa wanamuziki wa kike kwani wengi walifanya muziki wakiangalia mafanikio yake.Hii pia imempunguza nguvu Vanessa kwa kukosa 'role model' na kuungia zaidi uzunguni kwani uwepo wa jide kwenye ramani huenda ungebadili mwelekeo wa Vanessa ambaye kama si unafiki wa wahusika basi video yake ya Never ever ingefungiwa.Clouds walienda mbali na kushindwa kulijumuisha jina la Jide wakati mwingine kuandika 'code za uongo' kwenye  matangazo ya tunzo za kili ambazo huenda yalikuwa yamelipiwa na kwa unafiki wa wenye matangazo waliamua kukaa kimya.Tunaomba hiki kinachoitwa bifu kiishie mwaka huu unaoisha baadaye.
11.KAMPENI ZA KISIASA
Mwaka huu ndio ulikuwa wa uchaguzi mkuu, wanamuziki wakajikuta wamegawana kwenye makundi ya pande mbili tofauti kubwa na wachache wakiwa kwenye upande mwingine.Kuna waliokuwa UKAWA na wale CCM na wachache wakawa ACT Wazalendo. Kulikuwa na matusi na lugha mbaya miongoni mwao ikifika hadi kwa mashabiki wao.Licha ya kuwa kilikuwa ni kipindi ambacho baadhi yetu tulikuwa tukiomba kiishe hayo mambo yaishe kwa wanamuziki walitamani hata kipindi hicho kiwe cha mwaka mzima kwani mifuko yao ilituna kwa matamasha na kampeni za mitandaoni.Tunachoshukuru kuwa kipindi hicho kimefifisha ile nguvu ya 'vitimu' vya wanamuziki ambavyo vilifikia pabaya sana kwani kulitokea hata kundi la watu walioshangilia matatizo ya wanamuziki wasiowakubali.


 12.KUFUNGIWA BAADHI YA WANAMUZIKI NA NYIMBO
Ulikuwa ni mwaka wa vituko kweli kweli, Silole alifungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa kutofanya shughuli za Muziki baada ya kukiuka maadili ya watanzania alipokuwa nje ya nchi licha ya kuwa wanamuziki wengine kama Rachel , wanaojiiita kanga Moko ndembendembe na wengine wakike wakifanya upuuzi zaidi ya huo.Lakini cha kushangaza zaidi tulimshuhudia Shilole kwenye majukwaa ya kampeni ya CCM , sijui alichokuwa akikifanya si muziki ni uigizaji? Hilo hatulijui lakini Shilole akajikuta kama kawehuka kwani alianza kutoa maneno ya ajabu mara ataanza kuiba waume za watu na uchafu mwingine kibao.kingine kilichoshangaza wengi ni kufungiwa wimbo wa Viva Roma wa ROMA lakini ukahiti na kuwa wimbo mkubwa nchini.
Pia kulikuwa na nyimbo zilizofungiwa Nigeria kwa kukiuka maadili lakini vyombo vyetu viliziona ni nyimbo za kwenye chati za juu. Kweli ulikuwa ni mwaka wa maajabu.

13.WANAMUZIKI KULIPWA KAZI ZAO ZIKIPIGWA REDIONI
Kilikuwa ni kilio cha wanamuziki kwa miaka mingi na mwaka huu serikali iliyopita kwa kushirikiana na wadau wa muziki wametengeneza mazingira rafiki kwa wanamuziki kunufaika na kazi zao zinazotumika kuwanufaisha watu wengine.Wadau na wamiliki wa vyombo vikubwa wamekubali ila kwa utafiti wangu mdogo vyombo vya mikoani ambavyo kuna wakati nimekuta vikipiga nyimbo zilizopakuliwa na matangazo zijui kwa kutokuwa rasmi ama kwa kukosa ushirikiano na wanamuziki wakubwa nimesikia eti eti za kupiga nyimbo za nje na nchi kukwepa kuwalipa wanamuziki.Hilo sina uhakika ila natamani kusiwe na hasara kwa upande mmoja pekee miongoni mwa wadau wa muziki.


14.COKE STUDIO
 Kwa miaka kadhaa imewafungulia njia wanamuziki wengi Joh makini ,Diamond na Vanessa wamenufaika zaidi kuliko Shaa na Lady Jay Dee kwa awamu zilizopita mwaka huu dalili mbaya imeanza kuonekana kwa Ben Paul  na Fid Q ambaye si uvivu wake bali vyombo vya habari na mashabiki walionekana kuwaangalia zaidi Alikiba na Vanessa Mdee.

15.HIP HOP KUONEKANA AFRIKA NA KWENDA LIVE JUKWAANI
Joh Makini ameufanya muziki wa kufoka foka kusikika nje ya Afrika Mashariki na pengina nje ya Afrika kupitia nyimbo zake za Nusu nusu na Don't Bother Joh amefanikiwa kujiingiza kwenye kundi la wanamuziki wa aina hiyo ya muziki wanaofanya vyema Afrika.Fid Q naye aliamua kuwafanya matamasha kwa live band na kuuupa uhai zaidi muziki wa aina yake.Pia katika hip hop Stamina alifanikiwa kuzindua albam yake kwenye uwanja wa Jamhuri  Morogoro na kuupa nguvu muziki wa Hip hop.

16.VIFO ,AJALI,KUIBIWA NA KUVAMIWA WANAMUZIKI
Kuna watayarishaji wa muziki , wanamuziki na wadau wengine wa muziki waliouoana huu mwaka mbaya kutokana na kuibiwa na kuvamiwa pia kuna wale waliotangulia mbele ya haki.Tunaamini matendo yao mema yatawaweka palipo pema na hata waliomkosea Muumba vyote tunawaombea wapunguziwe adhabu ya kaburi, wengi waliotangulia wametangulia na ujana wao kabisa mvi za uzee hawajazionja na mauti ikawamiliki.


0 comments:

Post a Comment