Saturday, 12 December 2015

KILIMANJARO USIKU ;SEHEMU YA KWANZA
SEHEMU YA KWANZA


Tanzania na dunia nzima inanijua si kama mtuhumiwa wa kesi ya ubakaji na uuaji wa binti wa miaka kumi na tano bali kama muuaji ambaye sheria inachelewa kunikata ili niwe funzo kwa wengine waliokuwa wanamipango wa kufuata mkondo wangu.

Sina wa kunitetea ,mashirika ya kutetea wanawake na haki za watoto yamenitwisha zigo ambalo sijui nani anaweza wa hata kuniwekea kata ili kichwa kisiumie zaidi,mama yangu na ndugu zangu nawaonea aibu hata sikutaka wajue juu ya jambo lililonisibu lakini dunia imshamfikishia taarifa yangu na zaidi imefikisha kwa namna ambayo haitawapa matumaini bali ni kama kuwalaumu kwa kosa la kunileta duniani na kunipa malezi ya ovyo bila kujua malezi yao kwangu hayakuwa na hata chembe ya dosari zaidi ya dunia hii tuipendayo kunitia dosari.
Mungu ndo nashindwa kujua lipi la kuanza kumwomba maana yapo mengi ya kumwomba kabla sijamwomba kuniepusha na hukumu kali ya dunia.Nitafanya nini mimi zaidi ya kujaribu kuuambia ulimwengu kuwa kuna ninayostahili na nisiyostahili. Labda niuambie tuu ulimwengu historia yangu na jinsi ninavyolijua hili tukio hadi mwisho nilipokuja kuhusishwa na hili tukio baya hata kuliota ndotoni.
Naitwa Joseph Komba ,mtoto wa kwanza kwa mama na baba yangu na nina wadogo zangu wawili mmoja wa kike mmoja wa kiume.Baba yetu alipoteza maisha miaka kumi na mbili iliyopita wakati huo mdogo wangu wa mwisho ambaye ndiye dada yetu wa pekee alikuwa na miezi miwili tuu.Sababu ya kifo chache tuliambiwa ni ajali japokuwa mwili wake sikuuona na jeraha lolote la ajali zaidi ya mashimo mawili yaliyozibwa na pamba yaliyokuwa kifuani mwake ambayo nayo niliyaona wakati nikijaribu kutafuta Rozali yake aliyokuwa akiivaa wakati wote , sikuiona zaidi ya hayo mashimo katika mwili wa marehemu baba yangu.Nayakumbuka yote kwa kuwa naweza kusema kipindi hicho nilikuwa na umri wa miaka kumi na tano.
Ilidaiwa kuwa sababu za kibiashara ndizo zilizomtoa ulimwenguni ,wengine waliai kuwa alikuwa akitaka kujiingiza kwenye siasa hivyo wapinzani wake walimmaliza kabla hajatimiza azma yake ya kuingia kwenye anga hilo na kuna waliodai kuwa aliuawa na mbaya wake ambaye alikuwa akihisi kuwa akimfanya mke wake kama mama yetu mdogo.
Hayo yote yalisemwa lakini hatukujua lipi lilikuwa la ukweli japokuwa la kwanza ndilo tuliloliamini zaidi kwani baba yetu alikuwa mfanya biashara haswa na kuna wakati niliwahi kutamani kuingia kwenye biashara hata kabla sijamaliza shule ya msingi lakini nilipata karipio lake kuwa sikutakiwa kuwa mfanya baishara bila kuwa na elimu.Kipindi hicho tulikuwa Iringa mjini lakini baada ya baba kufariki tuliondoka na mama kwenda kuishi na ndugu zetu wengine huko Nyasa ambako ndiko nyumbani kwa wazazi wetu wote.
Nilishika elimu hadi miaka miwili iliyopita nilipofika chuo kikuu ambako hadi sasa ndio utambulisho wangu kwa jamii.Jamii ambayo inataka nisiishushe hadhi ya chuo kwa kufanya matukio yasiyoendana na usomi wangu.
Nilikuwa mfano bora kwa vijana wenzangu kule kijijini na kwingineko walikonifahamu kwani nimekuwa nikijitahidi kutumia ujuzi na nguvu zangu kuiinua familia na ndugu zangu hata majirani zangu ili mradi tuu wanufaike na elimu yangu niliyokuwa nikiipata.Lilikuwa si jambo lakustaajabisha kuniona nikiwa nimezungukwa na wanafunzi wa shule za kata za kule kijijini wakipata somo kama si la darasani basi la duniani maana malalamiko ya kukosa vitabu na walimu yalinifanya nione haja ya kuwajibika kwa kufanya hivyo.
Kuhusu ndugu hakuna aliyelalamikia haki labda kwa wale waliozoea kulialia hata pasi na sababu kwani mradi wa kufuga kuku na bustani niliouanzisha ulihakikisha mahitaji madogo madogo pale nyumbani hayakosi jawabu.
Kwa kifupi familia yangu ilijivunia kuwa na mtoto kama mimi ndo maana hata nilipomtambulisha mpenzi wangu Jenifa maarufu kwa jina la Jeni hawakuwa na shaka na nilishapanga kufunga naye pingu za maisha miaka michache ijayo hawakuwa na mashaka na awalimpokea kwa mikono miwili kwani umri wangu ulionekana kufurahia kitendo hicho.
Jenifa mrembo wangu mwenye rangi ya asili ya kiafrika huku akisifika kwa kuwa na nywele zake ndefu nyeusi alikuwa chaguo langu la kwanza la ukubwani kuwa aje kuwa mama wa wana wetu huko mbele.Nilikutana naye kipindi nipo likizo mjini Njombe huku nikijihusisha na shughuli mbalimbali za kupambana na umasikini kwa kifupi nilijiona baba wa familia yangu hivyo likizo ilikuwa sehemu ya kuingiza kiasi cha fedha amabazo zingeisaidia familia yangu na matumizi ya kipindi cha shule.
Tulidumu kwa muda mrefu huku tukifanya mambo ambayo kwa mtu mwenye ufahamu na maisha lazima akubali kuwa tulikuwa tumedhamiria kuwa baba mama vijavyo.Halikuwa jambo la ajabu kusikia swali kutoka kwa mama kama nilikuwa nimekorofishana na Jeni kila aliponiona kwenye hali isiyo yakawaida, na mara nyingi nikiwa nimezama mawazoni juu ya Jeni wangu basi lazima nitakosa umakini na utulivu wangu wa akili.Lakini hayo yote yalikuwa yakipita na mara chache mama alikuwa akihusikia kutatua matatizo ya mahusiano yetu na kututaka kumwomba Mungu ili tuepushwe na majanga ya dunia.

Mwaka jana mwezi wa nane wakati najiandaa kurudi chuoni nilianza kuhisi hali ya tofauti kutoka kwa mpezi wangu Jeni ,kwani licha ya wote kuwa jijini Dar es saalam kwa shughuli tofauti wakati kwa upande wangu kazi ya kushughulikia uhamisho wa mdogo wangu wa shule mwenzangu alikuwa amepata kazi kwenye kampuni moja lililokuwa na ofisi nchi nzima akifanya kazi kama mhasibu wa tawi moja lililokuwa nje kidogo na jiji la Dar es saalam .


Shida ilianza pale nilipotaka kuoanan naye na kila mara alikuwa akidai hakuwa na muda na hata nilimpotaka kutaka kuonana naye nje ya ofisi yake wakati anatoka kazini basi, nalo hakutaka litokee kwa kudai hakupenda kunioana kwa dakika kadhaa na kama angepata muda basi angenitafuta na tungefurahia kama si mchana kutwa bali hata usiku kucha.

Ratiba ya kukaa jijini niliijua na haikuniruhusu kusubiri hiyo siku ya kuufurahia mchana mzima ama usiku mzima na Jeni wangu nilichokifanya na kuandaa safari yangu ya kueleka chuoni ambako ni mkoani Kilimanjaro nikimwacha mdogo wangu shuleni.
Lakini kipindi chote hicho nilijitahidi kuongea naye simuni lakini mwitio wake haukuwa wa kawaida kuna wakati nilikuwa nikimpigia simu na haikupokelewa ,ujumbe ukitumwa kwake kutoka kwake haukurudi na majibu yoyote na yakirudi majibu basi ni baada ya masaa kumi na mbili ama tatu na jibu likiwa ni Kuacha kumsumbua kwenye kazi za watu .Sikuwa na jinsi maana sikuwahi kufanya kazi rasmi hivyo nilijiridhisha hivyo hivyo huku kengele ya hatari ikigonga kichwani mwangu kuwa Jeni hakuwa wangu tena lakini niliipuuza kengelea hiyo kwa kuhisi kuwa wivu wangu uliopitiliza ndio uliokuwa ukinituma kufikiria jambo hilo.Nilijitahidi kuendana na tabia yake huku nikiwauliza watu wengine niliowafahamu waliokuwa wakifanya kazi kama yake maeneo mengine jijini na hata kuwapeleleza wale nisio wajua na kujua miendendo yao nikajikuta nikipata jibu kuwa Ubize wa Jeni wangu ulikuwa ni mara sitini ya mfanyakazi bora wa kampuni ile wa msimu uliopita na kuniongezea mashaka.

Kuna wakati alikuja kunitamkia kuwa atabadili namba ya simu kwa sababu ya jumbe zangu alizoziita  za kipumbavu eti 'Usiku mwema' ndo upuuzi ulioje?


 Elimu yangu haikuwa na maana yoyote kwenye namna yangu ya kuishi kwani bado aliniona mshamba kwenye suala la mahusiano na akaenda mbali zaidi kuwa nisithubutu kumwambia mama yangu suala hilo kwa madai kuwa nilikuwa mtu mzima hivyo kumtegemea ama kumshirikisha mama kwa kila nilililoliona tatizo ulikuwa ni Ulimbukeni uliopitiliza na hata mama yangu angenicheka kwa kuliona suala lile kama tatizo kubwa zaidi ya kubadili mazoea yangu tuu.Sikupinga wala kukubali zaidi ya kupima akili yangu kama ilikuwa imekosea kutoyachukulia mabadiliko yake kwa mtazamo chanya kwani akili ya kudai kuwa sikuwa na changu kwa mtoto yule ambaye jiji la Dar es saalam alilipokea kwa kustarabika ghafla kama alivyodai mwenyewe.

Niliendelea kushangaa huku ufanisi wangu kwenye masuala muhimu ukififia kutokana na kufikiria sana jambo hilo kwani nilifikia kupoteza tiketi yangu ya gari niliyokata kwa ajili ya kwenda chuoni na kuchelewa gari kulikonilazimu kukata tiketi nyingine.
Tukiwa safarini kuelekea Kilimanjaro gari letu lilipata hitilafu tukiwa nje kidogo tuu ya jiji na kutulazimu kusubiri kwa zaidi ya saa moja wakati gari hilo likifanyiwa matengenezo.
Muda huo wa kusubiri ndio uliotufanya abiria tutawanyike huku na huko tukiangalia mandhari na shughuli za watu waliokuwa maeneo yale.Zunguka zunguka hiyo ilinifikisha mbele ya tawi moja la benki ambako niliamua kuchukua kiasi kidogo cha fedha kwani kukata tiketi mbili kuliharibu mpangilio wangu wa fedha na kwa bahati mbaya kadi yangu ya benki ilikuwa imeisha muda wake.

Kwa kuwa watu hawakuwa wengi sana mle ndani nilisubiri wateja wawili walize shida zao nami nilijisogeza dirishani na sikuamini nilichokiona mbele yangu na nilijikuta nikishindwa hata kujieleza shida yangu kwa muda kama dakika mbili hivi hadi pale mtu aliyekuwa nyuma yangu aliponigusa bega langu na kuniuliza kama palikuwa na huduma.
Alikuwa 'Jeni wangu' mbele yangu tulibaki tukitazamana kwa muda wa zaidi ya sekunde mia moja huku bila kujua machozi yakinitoka lakini hadi leo sijui kama yalikuwa ni machozi ya furaha ama ya huzuni.
Aliniangalia kwa muda mrefu bila kusema kitu hadi pale nilipogeuza shingo yangu kumwangalia mtu aliyekuwa amenigusa bega langu na kuniuliza swali kama palikuwa na huduma , niliporudisha macho yangu kwake niliona kiti kitupu na hakukuwa na mtu mle ndani.Niliamua kuondoka na kutoka taratibu na hata nilipoulizwa tena maswali mengine na wateja waliokuwa wameongezeka pale ndani sikuwa na muda wa kuwajibu kwani nilihisi machozi yangu niliyoyafuta yaliacha alama na kuhisi kila mtu aliyaona, sikugeuka hadi nilipofika eneo ambalo abiria wengine walikuwa wakisubiri gari litengenezwe na baada ya muda safari ya kuelekea Kilimanjaro ilianza.
Nilimtumia meseji yenye maneni mawili tuu Nakupenda Jenifa na kuituma lakini haikujibiwa, nilibaki nikiangalia miti iliyokuwa ikikimbia kwa kasi huku nikiwa sijui hata kitu gani kilikuwa sahihi kukifikiria kwa wakati ule.Nilisubiri ujumbe kutoka kwake lakini haukuja na kila niliposikia mtetemeko wa simu yangu nilipatwa na wahka wa kutaka kujua mtumaji wa ujumbe ama mpigaji wa simu lakini nyakati zote walikuwa ni ndugu zangu na marafiki zangu waliokuwa wakinitakia safari njema na kutaka kujua kuwa tulikuwa tumefikia wapi nilijaribu kuwajibu lakini kila aliyekuwa amenipigia alihisi kuwa kulikuwa na kitu kilichonisumbua na waliponitumia ujumbe na kutaka kujua kilichonisibu niliamua kutowajibu kisha kuzima simu yangu hadi pale nilipofika Kilimanjaro saa mbili na nusu usiku niliposhuka na kupanda daladala kuelekea mahali nilipokuwa nikikaa.
Nakumbuka nilinunua chakula lakini sikukila kwani nilijikuta kikimuawaza sana 'Jeni wangu' huku wazo la kuwa nilikuwa nimempoteza na alikuwa ameangukia kwenye milki ya mwanaume mwingine likiwa na nguvu kubwa kichwani mwangu.
Kwani hata nilipowasha simu yangu na ili kuwataarifu ndugu kuwa nilikuwa nimefika salama sikufanikiwa kuupokea ujumbe wake na hata nilipomgia simu yake iliita mara moja kabla ya kukatwa na nilipopiga tena haikupatina na nilipopiga kwa mara ya tatu ilionesha kuwa ilikuwa ikitumika nilijikuta nikibamiza simu ukutani na kuamua kulala usingizi ambao haukujahadi nilipoamua kuokota simu yangu na kujaribu kumpigia tena lakini niliikuta ikitumika tena nikakata na kutaka kumtumia ujumbe wakati naadika ujumbe simu yangu iliita na mpigaji akiwa ni Jeni ambaye niliihifadhi namba yake kama  Mpenzi wangu na nilipoipokea kabla sijaongea chochote niliisikia sauti yake 'Nitakupigia subiri kidogo'  sikupata nafasi ya kuongea kitu nilisikia mlio wa simu kukatwa sikuridhika na kufikiri kuwa aliishiwa salio na kuamua kumpigia lakini nilikuta simu yake ikitumika, sikuwa na jambo lingine la kufanya zaidi ya kusubiri kama alivyotaka nifanye.
Dakika arobaini nyingine za kusubiri zilipita haraka kutokana na kusinzia na niliposhtuka kitu cha kwanza kukifanya kilikuwa ni kuchukua simu yangu na kumpigia Jeni wangu.Ajabu nilikuta bado ilikuwa ikitumika , nilijaribu kumpigia kwa zaidi ya mara tano hadi pale nilipokea ujumbe ulioniumiza zaidi uliosomeka''Acha ulimbukeni wa mapenzi wewe, kusoma huwezi hata picha huioni?''huku nikitetemeka na kupumua kwa kasi nilimpigia simu Jeni wangu na alipopokea hakuongea hadi pale nilipomuuliza maana ya ujumbe wake aliotuma kwangu huku akili yangu ikitaka aniambie kuwa alikuwa amekosea kuutuma kwangu lakini jibu lake lilizidi kuninyong’onyeza;

‘’Nimetumia Kiswahili sanifu tuu, kama hujaelewa rudi tena darasa la kwanza’’Ilisikika sauti ya 'Jeni wangu' na simu yangu ilikatwa.
Nilijaribu kujiuliza kama ilikuwa ni tarehe moja  mwezi april , lakini haikuwa tarehe hiyo wala mwezi huo, nikajaribu kukumbuka kama ilikuwa tarehe yake ya kuzaliwa ama siku yangu ya kuzaliwa wala haikuwa hivyo.Niliendelea kumpigia simu kama mara tatu huku nikipuumzika kwa dakika kama ishirini hivi lakini majibu yake yakawa yale yale ‘’ namba ya simu niliyokuwa nikipiga ilikuwa ikitumika’’ hadi baadaye niliposikia kuwa haikuwa ikipatikana.
Sikujua ilikuwaje nikachuliwa na usingizi kwani nilikuja kushtushwa na mtetemo wa simu yangu ulionesha kuwa kulikuwa na ujumbe uliopokelewa , kwa haraka nikaufungua na nilikutana na ujumbe ambao ulinifanya nibamize simu yangu ukutani kwa hasira .
‘’Acha ushamba wewe mapenzi si lazima mimi ‘’ Ulikuwa ni ujumbe uliotoka kwa Jeni wangu ambaye kabla ya matukio hayo niliamini mimi nilikuwa chaguo lake sahihi la kushiriki naye sakramenti ya ndoa.
Niligundua kuwa simu yangu ilikuwa imeharibika baada ya kujaribu kuiwasha tena lakini iliwaka na kuzima hapo nikaukumbuka ule wimbo wa Banana Zoro 'Hasira harasa ‘kwani hasira zangu zilipelekea kuharibu simu yangu na kukosa mambo mengi ya msingi ikiwa pamoja na mawasiliano na ndugu zangu hasa amma yangu amabaye daima alikuwa faraja kwangu hasa nilipokuwa kwenye kipindi kigumu kabisa.
Asubuhi ile nilijaribu kupita kwa mafundi kadhaa wa simu ili watengeneze simu yangu lakini hakuna fundi aliyeweza kuifanya simu yangu ikaendelea kuwa chombo cha mawasilaiano kwani walidai ni bora nikanunua simu nyingine lakini si kuhangaikia matengenezo ya ile simu ambayo walinihakikishia kabisa hata wangeipeleka kwa aliyeitengeneza angekataa kuwa kama ni moja ya simu aliyoiunda.
Sikuwa na namna nyingine zaidi ya kufikiria kununua simu nyingine , lakini kila nilipoangalia akiba iliyokuwa imebaki niliona haikuniruhusu kununua hata simu ya elfu kumi kwani chakula ,pango na hela ya usajili chuoni vilinifanya nisubiri tuu hela ya bodi ya mikopo ambayo ingetolewa kama baada ya wiki tano.
Nikabaki kuwa mtu wa kudandia simu za wanachuo wenzangu kuwasiliana na ndugu zangu na mara chache nilikuwa nikimpigia Jeni wangu lakini daima namba yake haikupatikana.Nilibaki mnyonge kwa kumkosa  Jenifa mwanamke ambaye akili yangu ilikuwa imeshajiaminisha kuwa alikuwa mwanammke aliyezaliwa kwa ajili yangu na si mtu mwingine duniani.
Nilikumbuka zile nyakati nzuri za kuitana mpenzi, mume na majina mengine ambayo tuliona yalitufaa nilikumbukaa pia harakati zetu za kutaka kulinda penzi letu nilikumbuka pia mtego wake amabo daima alipenda kuutumia ulikuwa ni wa kuwatumia rafiki zake kunishawishi kuwa nao kimapenzi lakini daima nilikuwa nikiiukwepa huo mtego jambo lililomfanya azidi kuniamini lakini kwa wakati huo yote hayo yalikuwa ni simulizi zilizokuwa zimepita na mambo yalikuwa hayana maana tena kwani kila kitu kilikuwa kimebadilika kama vile serikali mpya baada ya mapinduzi ya kijeshi.
Tabasamu langu la asili lilipotea zaidi ya kulitengeneza nikiwa chuoni kila mtu alikuwa anajua kuwa nilikuwa nimebadilika tangu nirejee kutoka likizo na kila aliyejaribu kuniuliza jibu langu lilikuwa fupi tuu ‘’matatizo ya kifamilia ila yameisha ‘’ sikutaka kueleza zaidi kwa namna gani hayo matatizo ya kifamilia yametokea na hata waliojiona ni marafiki wangu wa karibu walipotaka kujua sikutaka kuwaeleza kwani niliwaambia kuwa ;-
 Kwangu naweza kuliona kubwa nikawasimulia wakati kati yenu kuna wenye matatizo makubwa kuliko yangu hivyo ningejiaibisha na mngenidharau hivyo tuyaache yapite tuu halafu yalikuwa mwishoni Sikutaka kuwaeleza zaidi maneno hayo.
Mambo yaliendelea kwenda kombo hata pale niliponunua simu kwani licha ya kumtafuta simuni Jenifa namba yake haikupatikana na wazo la kumtafuta rafiki yake lilifuata baada ya siku kadhaa kwani awali alinitaka nifute namba zao kwa kuhisi siku tama na shetani atatushawishi kufanya kitu cha tofauti na makubaliano yetu.Japokuwa nilikuwa nimezifuta simuni alkini nilikuwa nimeziandika sehemu nyingine kwa matumizi kama hayo hasa ninapomkosa simuni 'Jeni wangu'.

Niliwapigia rafiki zake kama watatu wote walinipa jibu moja kuwa hawakumpata simuni kwa muda uliofanana na muda ambao nami nilimkosa. Kwa kuwa walijua jinsi nilivyompenda Jenifa  wanilipa namba za watu waliokuwa karibu sana naye na nilipompigia kwa bahati alikuwa naye karibu na nilifanikiwa kuongea naye na alinipa sababu za kutopatikana kwa muda mrefu kuwa alikuwa ameibiwa simu yake na alikuwa na namba mpya na aliahidi kunitafuta kwa namba yake mpya kwa madai kuwa hakuwa na namba yangu .
Japokuwa nilionekana kufurahia maelezo yake lakini akili yangu ilijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu sahihi kama vile;-
Namba yangu ya simu alikuwa ameikariri ilikuwaje akaisahau? 
Alikuwa ana marafiki aliokuwa akiishi nao na walikuwa na namba yangu hivyo ilikuwaje akashindwa kuwaomba?
Na nini sababu ya kunitumia jumbe zilizoniumiza kipindi natoka likizo?
Jioni ilipofika nilimuuliza maswali mengi kutaka kuhakikisha pendo lake kwangu.
‘’Pole mpenzi wangu najua umeumia sana kukosa mawasiliano yangu kwa muda mrefu lakini nami nimeumia zaidi kwani naweza nikawa sababu kubwa ya kuumia kwako’’ Aliongea Jenifa simuni baada ya kunisalimu.
‘’Asante lakini kwa nini hukuomba namba yangu kwa rafiki zako?’’ Nilihoji.
‘’Siyo kuomba tuu kwa rafiki zangu nilijaribu kukumbuka namba yako na nilipokupigia hukuwa ukupatikana hadi nikahisi kuwa ulikuwa umechukia utani wangu wa siku ile na umeamua kunichukia na umepata wanachuo wenzako’’Aliongea na ku nifanya nitake kujua utani ambao anajua kuwa ungenifanya nimuache.
’Utani gani Jeni?’’ ''Si wa siku ile nilipokuwa nikikutumia zile meseji'' .

‘’We Jeni ulikuwa utani ule?’’ Nilijikuta nikipatwa na hasira baada ya kukumbuka maumivu aliyonisababishia kipindi kile.
’Ndiyo mpenzi nwangu nilikuwa nina lengo la kukutania lakini kwa bahati mbaya niliibiwa simu yangu kwenye daladala na nilipokuja kununua simu nyingine na kukupigia ukawa hupatikani hali iliyopelekea kuhisi kuwa ulikuwa umechukia na kuniacha lakini niliapa kutokuacha hata kama ungenikana mbele ya mamia ya watu’’Aliongea kwa hisia jambo lililopunguza hasira nilizokuwa nazo.
‘’Kwa nini usirejeshe namba yako ya zamani ?’’ niliendelea kuhoji.
’Nilijaribu kuirejesha lakini sikusajilia kitambulisho changu alinisajilia ma mdogo na sahizi yupo Njombe nikaona nisajiri tuu kwa jina langu’’Aliendelea kunikamata na kunirudisha kwenye mstari.
’Sawa mpenzi ujue nakupenda sana?’’ niliamua kumaliza hivyo.
‘’Unanipenda wapi? wakati utani kidogo tuu basi ukawa hupatiakani najua una wanawake wengine huko chuoni kwenu lakini nakupenda sana ‘’Alilalama Jeni wangu.
‘’Nakupenda sana Mpenzi sema simu yangu ilikuwa imeharibika na nikawa sina simu hadi niliponunua nyingine wiki tatu zilizopita nikaanza kukutafuta sikukupata hadi mchana nilivyokupata kupitia ndugu yako’’Niliamua kuficha kisa cha simu yangu kuharibika kwani ninijua ningeonekana mjinga kwake kuharibu simu kwa kuwa alikuwa amenitania kama alivyosema.
‘’ Na namba ya ndugu yangu umeipataje wakati hakuwahi kukupigia kabla au uliiiba kipindi tupo wote’’Alianza kukasirika.
‘’Hapana Jeni mpenzi nilikuwa nimepigiwa simu na rafiki yako Lily akiulizia namba yako kutopatikana na nilipomwambia kuwa hata mie sikupati hapo ndipo alipohangaika kwa rafiki zake hadi alipoipata namba hiyo niliyokupigia mchana na kunipa’’Nilijieleza uongo.
‘’Sawa lakini nataka uifute namba yake na nampigia kumwambia kuwa asikutafute tena naijua tabia yake yule’’Aliagiza kwa ubabe kitu ambacho si tuu kilinikera bali nilijua kwa kuwa ataenda kwa kumfanya Lily mkosaji jambo ambalo Lily angelikataa na na kumweleeza jinsi nilivyompigia na kumwomba namba za ndugu zake na nitaaibika na kutupiwa lawama kwani alikuwa amenitahadharisha kumtaja kama mtoa namba.
‘’Sawa mpenzi achana naye tuu nishaifuta’’
‘’lakini lazima nimpigie ‘’Aling’anganiza jambo lililonikera.
’Lakini hujui kama tutakuwa tunajiaibisha kwa kuonekana hatuaminiani kwenye mapenzi yetu?’’Niliamua kumwambia huku nikijilazimisha kuficha hasira zangu.
’Kujiaibisha? Hakuna anayejiaibisha anapolinda penzi lakie’’Aliendelea kusimamia aliloliamini.
‘’Sema kama unaogopa watakuja kuniambia upumbavu unaoufanya’’Niliongea nikionekana kutokuwa na utani.
’Upumbavu, kwa hiyo mie ni mpumbavu asante kwa matusi yako nilijua tuu kuwa una mwanamke mwingine umeniona mie mpumbavu sawa’’Alilalamika na kukata simu.
Nilijaribu kumpigia lakini kila nilipompigia aliikata simu yangu, nilimtumia jumbe nyingi za kumwelewesha nilichokimaanisha lakini hakuna aliyoijibu, hadi siku ya pili nilipoamua kumwelewesha na kumwomba msamaha na hapo mapenzi yetu yakaendelea kama kawaida ambapo aliniomba namba ya simu ya mama yangu akimpigia na kuongea naye mara kwa mara.
Furaha na tabasamu langu lilirejea hadi kuwafanya rafiki zangu kuhoji kama nilikuwa nimeyarekebisha mambo yaliyokuwa yakinitatiza kabla na jibu langu lilikuwa ‘’Mungu mkubwa kayamaliza’’ maisha yakasonga kama kawaida na mapenzi yakawa si tatizo tena kwangu.

_____________


Tarehe ishirini na tano disemba kila mwaka ni tarehe ambayo wakristu wote duniani huungana na kuadhimisha kuzaliwa kwa kristu ambaye ndiye sababu na chanzo cha ukristu wao na nilikuwa miongoni mwa walioiadhimisha siku hiyo kwa mwaka uliopita.

Kwa kuwa nilikuwa na ndugu mmoja wa baba katika wilaya mojawapo wa mkoa wa Kilimanjaro niliona nisherekee siku hiyo kwa kuwa pamoja na familia yake jambo amabalo nilikuwa nikilifanya kwa miaka miwili iliyopita.
Si mbali kutoka chuoni kwangu ambako ndugu huyo anaishi ni mji mdogo wa Boma na niliamua kwenda siku hiyo hiyo asubuhi.Nikiwa garini nilimpigia simu Jenifa  ili kumtakia sikukuu njema lakini simu yangu haikupokelewa zaidi ya mara tatu na niliamua kumtumia ujumbe wa maandishi kumtakia sikukuuu njema na kumwambia kuwa nilikuwa nikimpenda.
Nikiwa kati kati ya maongezi na ndugu zangu hao huku tukipata mziki mzuri wa krismass simu yangu iliita na mpigaji alikuwa Jeni na haraka haraka nikatoka nje na kuipokea simu yake.
‘’Uko wapi’’ 
‘’nipo kwa baba mdogo Boma, vipi sikukuu inaendaje kwako?’’
‘’Kwa babako mdogo au bar mbona nasikia makelele ya muziki na walevi?’’
‘’Hahhahahaaa acha utani wewe kwa hiyo kwa baba yangu pamekuwa bar’’Nilijibu nikijua alikuwa akinitania.
‘’Kwa hiyo unanicheka mimi au na wewe umeshalewa?’’
‘’Subiri nitakupigia’’Niliongea baada ya kuona mama mdogo akija upande niliokuwa nimesimama na sikutaka anisubiri niongee simuni kwani alionekana kuwa na shida na mimi.
’Nenda na mdogo wako ukatuletee sprite pale dukani’’Aliniagiza mama mdogo akinipa noti ya shilingi elfu tano .
Niliipokea na kumwita Edger mdogo wangu ili twende huko dukani huku nikimpigia simu mpenzi wangu.
‘’Endelea na malaya wako , sitaki unipigie tena na sitokupigia tena asante sana nilijua tuu asante sana kwa kunipotezea muda’’Aliongea na kukata simu na nilipompigia tena hakupokea simu yangu niliishia kumtumia ujumbe kunweleza hali iliyonifanya nimkatie simu yake lakini jibu lake lilikuwa lile lile la kushukuru kwa kumwonesha jinsi gani sikumpenda ili asipoteze muda wake zaidi.
Nilijikuta hata nasahau chenji hadi muuzaji aliponikumbusha na kunipa na niliporudi nyumbani nikajikuta najilazimisha kuendana na sikukukuu lakini tabasamu langu lilikuwa bandia jambo ambalo baba mdogo aliligundua na kuniuliza kando lakini nimwongopea kuwa kuna mwanachuo mwenzangu alikuwa amenifuta kwenye kazi ya kikundi hivyo nilitakiwa niwahi kumwona mwalimu kesho yake asubuhi ili kuliweka jambo vyema hivyo nilimlaumu huyo rafiki kwa kuniharibia sikukuu.
‘’Au mkwe kaharibu?’’Alitania baba mdogo bila kujua alikuwa sahihi.
’Ahh, hapana baba ‘’Niliongea nikicheka.
Hapo ndipo naweza kusema palikuwa sababu ya mimi kuingia kwenye hii kesi kubwa ambayo sijui kama kuna muujiza unaoweza kuniweka huru, inadaiwa kuwa nimebaka kisha kuua tena matendo hayo nikimfanyia mwanafunzi wa sekondari na zaidi ni mtoto wa mchungaji nitapona kweli mbinguni na duniani?.

Je, ni kipi kiliniingiza kwenye janga hili?
ITAENDELEA JUMAMOSI IJAYO

0 comments:

Post a Comment