ads

Friday 14 October 2016

KWA HERI JK NYERERE HAYA NDIYO TUYAFANYAYO

Tunaoamini katika tukionacho tunaamini tukija Butiama na kufukua kaburi lako tutakutana na fuvu la kichwa na baadhi ya mifupa ya mwili wako na vipande vya mbao ambazo ninakaribia kuwa udongo. Lakini pia wale tunaoamini katika hisia na kitu kiitwacho roho tunaamini licha ya kuwa hakuna nyama iliyobaki kushikilia mifupa ya mwili wako lakini roho yako ipo mahali fulani. Wengine wameenda mbali na kutaka kukuweka kwenye kundi la wale waitwao watakatifu.
Nisikupotezee muda Mwalimu, kuna mengi tunayafanya tangu ulipotutoka siku ile.
     Mwalimu ilipotolewa taarifa ya kifo chako kuna ambao hawakuamini kama kweli umekufa wakaja na dhama mbalimbali ambazo zimebaki vichwani mwa wengi hadi leo.Mwalimu dhana hizo hudai kuwa uliuawa na binadamu wenzako ,wapo wanaowashutumu wazungu wengine huwahutumu waafrik waliokuwa na mtizamo tofauti na wako kuhusu uchumi na demokrasia.Hadi leo wapo wanaoamini hivyo mwalimu na hawataki kusikia lingine kuhusu hilo.
   Ulipofariki kulikuwa hakuna shule za sekondari za kata lakini leo hii zipo.Shule hizi licha ya kutegemewa kukomboa sie ambao tuliishia kuambiwa  tumefaulu ila tumekosa nafasi na hatukuwa na uwezo wa kifedha walau wa kwenda kusoma kwenye shule za Jumuhia za wazazi za chama ulichokiasisi cha kijani na njano ambazo sijui niseme nini kuzihusu maana zimekufa chali kifo cha mende zimebaki kuwa vituo vya wanafunzi walioshindwa kwenyw shule nyingine kitaaluma na kimaadili: lakini shule hizi za kata hazifanyi kazi iliyokusudiwa licha ya kuwa nami ni zao la shule hizo lakini kama si kujipendekeza kwangu kwa wanafunzi wenzangu watoto wa "vibosile" chuo kikuu ningeishia kukiona kwenye kampeni za chama chako cha kijani na njano kwenye runinga zao kubwa wakijinadi kuwa ni mafanikio ingawa.Mwalimu shule hizi ni mwiba kwetu na si faraja tena najua yule kapteni na Bwana Deo wa Ludewa watakuambia hili vizuri.
  Mwalimu kuna mtu aliitwa Zitto akawa shujaa wetu ghafla ushajaa ukapote na akavikwa sijui alijivisha usaliti na sahizi ana kiongoza chama kipya ambacho kinapata uungwaji kwa sera zako za kiazimio la Arusha, azimio lililoishia kuwa historia isiyopewa uzito wowote.Kabla ya Zitto kuna mtu mmoja aliyeitwa Dr. Slaa nahisi ulipata kumsikia kabla , huyu bwana alijikuta kwenye orodha ya mashujaa wengine tukiktabiria kama Nyerere mpya lakini kuna kilichofanyika  na ghafla leo amegeuka kuwa jamaa mmoja hivi mtalii ambaye siasa kwake ni kushauri tuu tena kwenye mambo mepesi  mepesi tuu.Kuna wengi mwalimu , Mtikila yule jamaa naye kakufuata mwalimu bahati mbaya kuna watu walikishangilia kifo chake kuliko walivyoshangilia kifo cha Iddy Amin, usishtuke mwalimu hili gonjwa ulilotulazimisha tulipokee kwa kudai kuwa ni tiba limekuja na majanga mengi hadi watu wanashangilia vifo za wenzao wakipanga tuu ratiba kuwa nani atafuata huku wengine wakiwaita wagonjwa ni maiti zinazotembea.
  Mwalimu uliwahi kutuambia kuwa kilimo ni uti wa mgongo na wengi tuliamini lakini nimejikuta napata shaka kwani bado tunalimia jembe la mkono huku wakulima ni wazee huku vijana tukiwa tayari kupiga debe kuwa madalali hadi wakati mwingine kuuza miili yetu kwa kufanya ngono ili tuu tusilime.Sitanii mwalimu hii ni kuanzia kwa mwenye elimu ya mtaani hadi mhitimu wa shahada ya udhamivu.Kuna Rais alileta sera ya kilimo kwanza lakini jamaa zake wakaiharibu haraka na imekufa chali kifo cha mende kiasi kwamba hadi leo kilimo ni adhabu wachache walioamua kulima wanalima kwa simu  wakiziacha pesa za kilimo huku waking'ang'ania kazi za kuwatajirish mabepari kwa kupewa visenti visivyowafanya wawe huru.
Mwalimi kuna Whatsap, facebook ,Insagram na mengine mengi ambayo yamekuwa kijiwe cha wafanyakazi kukutana na kupiga majungu na si kazi, usishangae hiyo siyo mikoa ni mtandao ya kijamii usije kudhani Songea, Butiama na Singid vimebadilishwa majina bado ipo vilevile na wameongeza mengine kama Geita na Simiyu huku lifti ya kwanza Mbeya ikizinduliwa na viongozi wenye ving'ora.
  Mwalimu mwenge unapigiwa kelele kiasi kwamba watu wanatamani wasikie sauti yako useme kuna nini cha ziada kwenye mwenge zaidi ya kuunganisha watu? Mwalimu huo mwenge haufanyi kazi hiyo tena watu wanatengana tuu kidini, kikabila kikanda na hata kiitikadi licha ya kuwa mwenge huzunguka kila mwaka. Nikuambie tuu ukweli watu wameaanza  kuuchukia kwa sababu ya ile michango yake na namna inavyokusanywa pia Mwenge unashushwa hadhi kwani umefikia hatua ya kuzindua nyumba za kulala wageni zilizokamilika na mapagale ya zahanati.Halafu nikuchekeshe kidogo( najua halitokuchekesha) mwaka huu walipanga kutumia siku yako kuhalalisha ulaji wa mamilioni mengine bila sababu ya msingi tena wameahirisha kwa namna ambayo siku hizi watoto wamjini wanasema kutafuta kick kwani watu walishapokea tonge halafu wameambiwa warudishe unga sahizi naona taratibu watu wanafanya yao zinarudi. Mwalimu huu mwenge leo umekuwa sababu ya wapinzani wa chama chako cha kijani na njano kupata pa kuikosoa serikali "tukukufu ipambanayo na mafisadi na ikusanyayo kodi bila kujali tajiri wala masikini haibagui ni haki sawa kwa wote".
  Mwalimu chama chako cha kijani na njano siku hizi kimepitia wakati mgumu watu wakiingia na kutoka kwa kashfa halisi na za kusingiziwa.Chama kimeleta wabunge mabingwa wa kupiga makofi na kukubali kila kitu huku ikimwona yeyote anayetofautiana nacho basi ni haitaki amani ya nchi.Mwalimu napata hata aibu kukueleza hili hali imekuwa mbaya sana yaani hadi lile bunge tukufu ulilokuwa ukiliota lilifikia sehemu ya majungu na vituko kiasi kwamba tulifikiria kuzuia wanetu wasiwe wanaangalia kwa ajili ya kulinda maadili kwani huyu anamsema yule huyu anamzomea yule mwalimu tulifika pabaya.
   Mwalimu najua yapo mengi lakini naomba leo niishie hapa kwa kukumbusha kuwa walimu wameaanza kuhisi kuwa hukuacha ualimu kwa kuwa ulitaka udai uhuru bali ujua kilichokuwa kikifuata kwenye ualimu. Leo mwalimu ni mtu asiye huru mbele ya wengine kuichumi na kifikra , mwalimu anaonekana ni mtu aliyeshindwa kwingine, mwalimu masikini na anayeweza kutumika popote watakapo watawala sensa na kusimamia uchaguzi ni mahali pekee ambapo walimu hupambana ili waongeze vipato vyao.Nyumba hawana lakini ualimu umeonekana fani halisi kiasi kwamba wanaingia hadi wasioweza ambao huishia kulala na wanafunzi wao.Wanafunzi ndo kabisaa wamekuwa ni washindani wa walimu kwenye mambo mabaya.
Mwalimu pumzika sasa nitakuambia mengine ila nikuambie tuu siku hizi vijana wamekuwa wagumu kuheshimu dola kiasi kwamba hukejeli hadi ikulu sijui nani chanzo lakini hali ni mbaya. Pumzika kwa amani Mwalimu wasalimu Kolimba, Sokoine na Iddy Amin najua umemsamehe.



0 comments:

Post a Comment