Saturday, 26 July 2014

ZAIDI YA KUTOKULA

ZAIDI YA KUTOKULA
Habarini marafiki,mlofunga hongereni,
Nitakuwa mnafiki,nikijifanya sioni,
Siyo ishara ya dhiki,bali mwongozo wa dini,
Zaidi ya kutokula,funga ina mengi mambo.

Wagonjwa na wengineo,mlioshindwa kufunga,
Myafanye megineyo,itakavyo yenu funga,
Sio kucheka wenzio,eti yule hakufunga,
Zaidi ya kutokula,funga ina mengi mambo.

Wewe usiye husika,naomba acha makwazo,
Sije mtu kwazika,wewe ukawa ni chanzo,
Mtu dini kaishika,kwako liwe kubwa funzo,
Zaidi ya kutokula,funga ina mengi mambo.

Na humu mitandaoni,si sehemu ya dhihaka,
Eti nani simuoni,siyo lazima kwandika,
Si mtafute simuni,siyo humu kuanika,
Zaidi ya kutokula,funga ina mengi mambo.

Pia ule unafiki,kujifanya umefunga,
Waenda kwa marafiki,kuharibu yako funga,
Mola hilo haafiki,ni bora usingefunga,
Zaidi ya kutokula,funga ina mengi mambo.

Liombeeni taifa,msisahau dunia,
Tuyaepuka maafa,mola atawasikia,
Pia wale walokufa,huko naijeria,
Zaidi ya kutokula,funga ina mengi mambo

0 comments:

Post a Comment