Monday, 18 May 2015

SHAIRI;MBELE YETU NYUMA YAKO


Kisikia jina lako,nachowaza kuimba,
Sisahau nyimbo zako,tangu kale twaziimba,
Za kusifu chama chako,na kifo uliziimba,
Mbele yetu yuma yako,Kapteni pumzika.

Poleni wana Songea,na Mbinga alikotoka,
Pole kwa watanzania,mwenzetu ametutoka,
Sasa tunakulilia,nyimbo tutazikumbuka,
Mbele yetu nyuma yako,Kapteni pumzika.

Poleni na wanachama,Mwenzenu katangulia,
Kaimba nyimbo za chama,nani atawatungia,
Msije waza kuhama,kisa nyimbo kusikia,
Mbele yetu nyuma yako,Kapteni pumzika.

Ulitunga za wenzako,nani atakutungia,
Leo hupo peke yako,wengi tunakulilia,
Nasi tunafwata huko,wewe umetangulia,
Mbele yetu nyuma yako,Kapteni pumzika.

Kikutana na mwalimu,mwambie twamtamani,
Mwambie yote muhimu,usimfiche jamani,
Mwambie wanashutumu,heri zama za zamani,
Mbele yetu nyuma yako,Kapteni pumzika.

Na ukimwona Balali ,mkae mpige soga,
Mwambie halisi hali,milioni ni ya mboga,
Watu tuna ngumu hali,sema tumezidi woga,
Mbele yetu nyuma yako,Kapteni pumzika.

Kaditama ninagota,machozi yananishinda,
Nahisi kama naota,ukweli unanishinda,
Mwalimu ukimkuta,mwambie yanatushinda,
Masope wanauawa,vituo vinavamiwa.

0 comments:

Post a Comment