Monday, 18 May 2015

TUNAWEZA KUZUIA AMA TUMWACHIE MUNGU?


Na.Moringe Jonasy.
Vuta picha upo ndani ya gari, pembeni yako yupo dada mrembo sana katingwa na simu yake kuna muda anacheka mara asonye mara amwoneshe mwenzake hiki na kile ilimradi tuu kupunguza urefu wa Safari Yake.
Mbele yako kuna kaka yeye tofauti na wenzake wanaofuatilia filamu inayoendelea kwenye video zilizomo garini amevaa 'earphone' huku akitikisa kichwa akionekana kusikiliza muziki unaomvutia sana mara chache akiongea na wenzake ambao bila shaka ni wanafunzi wenzake wanaomwambia kuwa anatakiwa kuwahi masomo chuoni.
Lakini nyuma yako wapo watu ambao nao bila kuuliza unahisi ni ndugu huku mmoyja wao akionekana ni mgonjwa ambaye ama anarudishwa nyumbani baada ya kuambiwa hospitalini kuwa wameshindwa la da ''wajaribu kuzunguka'' au wanaelekea hospitalini huku matumaini yao wamemwachia Muumba juu ya mgonjwa wao.Si hao tuu siti kadhaa mbele unamwona dada ambaye anaonekana kuchoshwa na maisha ya kijiji na kwenda kujaribu mjini kama kuna chochote cha kufanya kitabadili mtazamo wake juu ya maisha.Mkiwa mnaendelea na safari watu watatu wanapanda njiani ,ambapo ni kama porini vijiji vinaonekana mbali kilimani.Wanaonekana washamba kwanza hata kujitenga kwao na namna ya kuweka fedha ama tiketi na kundi kubwa la watu unaloliona likigeuza kuelekea kijijini wakionesha kuwa walikuwa wakiwasindikiza.Hao nao wamebeba matumaini makubwa ya wanakijiji ambao wameamua kujichanga ili wawape fedha vijana hao wakanunue mashine ya kusaga ya kijiji ili wasage mahindi kama wafanyavyo watanzania wengine duniani.
Dakika chache mbele gari linasimama ghafla , dada mmoja mchafumchafu kuanzia mwili hadi mavazi yake anapanda garini na kusababisha wale wabaojiona wasafi hadi utumbo wao kufungua madirisha na kusonyasonya, na kwa bahati ama mkosi huyo dada anakuomba akae jirani yako nawe kwa bahati unampa nafasi hiyo kwa kiswahili cha kubabaisha anakusalimu na kukuelekeza sababu ya yeye kuwa vile ama amekimbia kukeketwa ama amekimbia kuozeshwa lakini anaweza kukuambia ''naenda kutoa mimba niliyopewa na mwalimu wangu mwenye mke na watoto wakubwa'' lakini kabla hujamaliza kustaajabu mambo hayo unasikia kimya kutoka kwa mtu mmoja aliyejitambulisha kama mwalimu wa shule fulani ambaye alikuwa akijipambanua kwa kujua kila kitu na kukielezea, gari inayumba kabla ya kugonga mti na kubinuka mara mbili mkono unavunjika damu zinamwagika kisha kimyaaaaa,,,,.
Matumaini na malengo mangapi yanakuwa yamezimwa?
Mwanafunzi
Mwanakijiji
Mfanyabiashara
Mgonjwa
Mwizi
Muuaji na wengine wengi matarajio yao yanakuwa yamezimwa ghafla watu wanapata ulemavu wa kudumu na maumivu yasiyokoma.
Sikatai zipo ajali zinazotokana na ubovu wa barabara, vyombo vya usafiri na ajali nyingine kama nasibu tuu.
Lakini zipo zinazotokana na uzembe wa madereva ambazo nazo kama zitokanazo na ubovu wa barabara na vyombo vya usafiri ''TUNAWEZA KUZIZUIA''.
Juzi tumesikia mgomo wa madereva ambao wengi tuliushadadia pengine hata bila kujua madai ya madereva na serikali.Mgomo ule nilitegemea ungekuja kuwaweka serikali Kupitia SUMATRA, TANROADS na wadau wengine kwa pamoja na wamiliki wa vyombo vya usafiri na madereva wao kuungana na kujua namna sahii ya kuepukana na ajali hizo ambazo sinaathari nyingi kwa taifa letu.
Leo hii watu tunaogopa kusafiri kwa sababu ya ajali lakini tunasafiri kwa sababu inatupasa kufanya hivyo huku tukijipa moyo MUNGU YUPO SITOKUFA bila kujua hata wale wapatao ajali Mungu wao huyo huyo na wanakufa.
Nimekuwa nikiogopa kuingia kwenye mitandao ya kihamii hasa whatsapp kwa kuogopa kukutana na picha za kutisha za majeruhi na watu walokufa kwa sababu ya ajali hizo.
Je, hatuwezi kuzizuia ama tumwachie Mungu?
Mungu tunaomba uwaponye majeruhi wa ajali zote,pia zipokee roho za waja wako pia tunaomba tuondolee ajali hizi.
Amen.

0 comments:

Post a Comment