Wednesday, 20 May 2015

WE MWENZETU NGIRI?, (UMEKOJOLEA KABURI MBELE YA NDUGU.)

Na.Moringe jonasy
Zamani kidogo kabla ya kuibuka hizi smartphone zinazowafanya watu wawe bize na whatsap na instagram na facebook vijana na watoto tulikuwa tukipenda kukaa na wazee wetu tukisimuliwa hekaya na simulizi pamoja na visa mbalimbali vya kubuni.
Moja ya visa vilivyokuwa vikinivutia ni vile vya Sungura,fisi na ngiri.
Moja ya visa hivyo ni kisa cha ngiri kuchongewa na sungura kwa Simba kuwa alikiwa akimcheka na kumponza Ngiri mbele ya simba si tu kilinivutia na kumtaka babu yangu anisimulie kila mara kwa sababu moja kuu ya kumhurumia ngiri kwani aliadhibiwa kutokana na umbo lake ( kazi ya mwenyezi Mungu).
Tuachane na hekaya na visa vya babu, naomba niongelee jambo moja lililotokea usiku wa kuamkia juzi ( tarehe 2).Mwanamziki wa kizazi kipya Ally Salleh Kiba kuvamiwa nyumbani kwake na watu zaidi ya kumi na tano.Watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi walijihami kwa silaha mbalimbali likiwemo jiwe walilotumia kuvunja milango, vyuma,pistol na visu ambapo walitumia chuma kumtesa mtu waliyemkuta ndani wakimtaka awaoneshe alipokuwa Alikiba na baada ya kushindwa kumpata waliamua kuiba vitu kadhaa zikiwemo pesa za kama shilingi milioni mbili na nusu.
Asubuhi ya siku hiyo taarifa ilianzia Clouds fm Instagram kabla ya kusambaa huku na huko mitandaoni.Baadaye waandishi wa habari wa clouds walifanikiwa kufika eneo la tukio na kuangalia uharibifu uliotokana na tukio hilo na kupata taarifa sahihi kutoka kwa wahusika namna tukio hilo lilivyotokea.
Habari zilizungumzwa huku na kule huku wengine wakitaka ulinzi uimarishwe katika maisha ya Alikiba kwani walidai tukio la kuvamiwa halikuwa la kwanza.
Wapo ambao walianza kutokwa na maneno kuwa ni kutafuta kile kinachoitwa " kick'' jambo ambalo lilinishangaza sana kwani kwa ninavyomfahamu Ally kuna vitu vingi sana ambavyo angeamua kuvitumia kutafuta hizo ''kick'' na angefanikiwa lakini sii kwa tukio kama hilo tena kwa bahati mbaya kwa matukio yaliyokuwa yakifuata kama la shindano la ngumi haukuwa wakati sahii.
Na mengine mengi yalisemwa juu ya tukio hilo lakini jambo moja kubwa ambalo ndilo lililonileta hapa.
Jambo lenyewe ni hili; Baada ya mwandishi aliyeenda eneo la tukio la uvamizi huo kufika studio za clouds fm ambako kipindi kilikuwa kikiendelea aliwakuwa B12, na Adam Mchomvu na kuelezea lile tukio ambalo watangazaji hao sijui kwa kutojua maadili ya kazi yao ama kwa kuzidiwa na hangover za # whitepart walianza kuropoka ropoka mbele ya kipaza huku wakijua fika kulikuwa na maelfu ya watanzania waliokuwa wakisubiri kupata undani wa tukio la kuvamiwa nyumba ya Ally msanii ambaye kwa sasa ni miongoni mwa topics zinazozungumzwa sana mitandaoni na kwingineko.
Adam alianza kwa kuwashangaa wavamizi hao kuwa kwa nini hawakuvamia kwa Diamond kwa kudai Ally ana pesa gani ?( Akipuuza taarifa ya wavamizi kumtaka Ally na kuiba kuwa ni chaguo la pili). Hilo halihitaji shahada ya upelelezi kulifikiria hilo, lakini Adam aliendelea kuleta huu ninaouita ungiri pale alipoambiwa wavamizi hao waliiba raba za Abdu kwa kuuliza ni roli ngapi za raba atoe namba tumchangie.
Hakuishia hapo alipoambiwa kuwa waliiba na pesa milioni mbili basi hapo akasema basi hakuna video ya chekecha cheketua kwani hela wamekomba yote na akamilizia kuwa walibeba hadi boxer.
Sikatai Adam ni mtu wa utani na anaweza kujitetea ni utani( kama alivyoumbiwa ngiri na meno yake) lakini utani gani mbele ya kipaza masaa machache baada ya kufanyika tukio ambalo halikumuumiza tuu Ally na yule kijana(Innocent) bali liliwaumiza mashabiki wa muziki mzuri Tanzania na mama wa Ally, Inno na ndugu wengine wa wahusika.
Kutania wakati watu wanahitaji taarifa sahihi kwenu ni kutaka kuwaaminisha watu tukio lile lilikuwa la kawaida sana bila kujua nafasi ya Ally kwa familia yake na muziki wa Tanzania kwani ni moja ya viungo muhimu vya muziki wa Tanzania.
Adam jiulize maswali yafuatayo:
Kwa nini wavamizi walimtaka Ally na si mwingine?
Je, Ally angekamatwa na wavamizi wangemfanya nini?
Je,Ally angeuawa na wavamizi angefurahia kupata habari ya kuzungumzia ama angewalaumu kwa kutomvamia Diamond?
Kwa nini Ally asakamwe yeye pekee?
Na mwisho ajiulize mwenywe kuwa jambo lile lilikuwa la kulifanyia mzaha?
Mwisho nakuuliza Adam wewe mwenzetu ni ngiri? Yaani hujui la kusikitisha ama la kufurahisha?
Ujue umewakera maelfu ya watu na umepoteza maelfu ya mashabiki wako kwa kauli kama zile si mashabiki wako tuu pia kuna watu wameacha kusikiliza kipindi chako .kwa kawaida inaweza kuendelea kuchekea tukio hilo kama ilivyo kawaida yako ila ukweli unabaki kuwa UMEKOJOLEA KABURI MBELE YA NDUGU....... KWANI WENGI WA WALIOKUWA WAKISIKILIZA KWA UMAKINI NI MASHABIKI WA ALIKIBA .
Moringe Jonasy
04/05/2015


0 comments:

Post a Comment