Jioni tulivu baada ya mihangaiko ya siku nzima nimeamua kupitia mtandaoni na usoma vitu mbalimbali lakini kila nikisoma kitu naona hakipandi.
Sipo vizuri.
Kwa nini ? Sijui.
Akili imechoka na inatatizwa na jambo fulani ambalo awali sikulielewa mwanzoni.Naamua kuangalia nyimbo mbalimbali lakini nazo naona kama zinaniongezea mawazo tuu mapenzi yanasifiwa na kulalamikiwa ,shida zinaliza watu na lawama zinawapata wanaostahili na wasiostahili.
''Mhh huuu muziki''Naguna nikipasua chunusi iliyoiva kwenye mgongo wa pua yangu na kunisababisha nisikie raha na maumivu kwa wakati mmoja.
Naamua kuzima kompyuta yangu na kutaka kuingia mtaani ili nikasafishe macho na kuendeleea kushuhudia Raha na karaha za ulimwengu lakini nasita.
Kuna kilichonisitisha na kunivuta.
Wimbo wa nani kama mama, huu wimbo unanifanya niusikilize na kumtazama mwimbaji amabye yupo jukaani akiimba kwa hisia.Namkumbuka mama yangu ambaye miezi zaidi ya kumi imepita tangu nimwone si kama amekufa , bali yupo mbali nami.
''Wamama wote waishi miaka mingi''Bella anasisistiza maneno hayo yenye kiswahili chake cha kikongo kwa hisia sana na kunifanya nianze kutafakari.
Nakumbuka kuwa Bella yupo kwenye lile kundi la wengi ambao wamempoteza mtu huyo muhimu lakini anawaombea mama wa wengine ''nikiwemo' waishi miaka mingi.
Hapo najikuta nikiwaza kitu kingine 'Maumivu ya kumpoteza mama' kweli inauma na inauma haswaa naogopa...
Naogopa kumzika mama , kama wengine walivyofanya kwa uchungu mkubwa ambao kwangu nahisi kuwa siwezi kuuvumilia.
Wapo watu wengi wadogo zaidi yangu waliowazika wazazi wao wakati mwingine walizikiwa kwa kuwa walikuwa na umri mgumu hata kujua majina yao, mama waliopoteza maisha kutetea uhai wao, hao wanaumiaje?
Sijui na naogopa kufikiri hilo.
Naamua na kuomba kuwa basi mama anizike , hapo napo naogopa baada ya kufikiria kuhusu maumivu na machungu atakayoyapata mama yangu kunizika.
Ataumia sana...
Kwei ataumia zaidi ya ninavyofikiri .
Sasa kipi bora?
Sijui anajua yeye(Mungu) apangaye nani amzike nani, lakini mie siwezi kujua.
Mama aliyepoteza muda na akili yake kwa ajili ya raha yangu, yule anayemzungumzia Bellla kuwa hakuweza kulala kama yeye (Bella) alikuwa macho.Mama aliyeshika kinyesi na matapishi yangu bila kusita mama aliyejivunia mimi bila kujali ulemavu ama kasoro zangu, mama aliyeumwa nilipoumwa.
Mungu uumpe maisha marefu sana, naogopa kumzika naogopa kweli.
Machozi yananitoka na kunifanya nishindwe kufanya kingine zaidi ya kujiuliza kama kizazi niishicho kitatoa mama wa kuliliwa na kuombewa maisha marefu?
Niandikie #mwanakalamu kama u sehemu ya kutengeneza mama bora na yule mama mtarajiwa aniandikie kuwa #yeyenimamabora
Moringe Jonasy july 20, 2015
0 comments:
Post a Comment