ads

Monday, 15 May 2017

NAANDIKA KUHUSU YULE MAMA


Na.Mwanakalamu
Haijalishi siku hii muhimu umeiadhimishaje, umemkumbuka mama yako na kumshukuru, kwa kuonana naye, kumpigia simu, kumtumia barua hata kubandika picha yake na kuambatanisha na maneno ya shukrani kwake kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.Lakini pia kuna wale wenzangu ambao kiumbe huyo muhimu hawakuwai kumuona, ama walimuona kwa muda fulani kisha kifo kikawatengeanisha.
Wapo pia waliowalilia mama zao na kuandika jumbe zilizogusa , kiasi kwamba siku hii imekuwa inatonesha vidonda vya kuwatamani mama kutokana na wale ambao wana mama zao walio hai huwakumbusha namna walivyoukosa upendo wa mama zao.Neno gani liwafaalo kuwapoza waliwapoteza viumbe hawa muhimu duniani, lakini binadamu tunaamini kila aliyezaliwa mauti ni haki yake ni suala la muda tuu.
Pia kuna waliotumia siku hii kutuasa na kutukumbusha juu ya wajibu wetu wa kutengeneza na kuandaa mama wa kesho na keshokutwa, mama mwenye ile thamani ya mama , thamani isiyolinganishwa na kiumbe yeyote ulimwenguni.Mama mwenye ile thamani zaidi ya kubeba kiumbe tumboni na kukileta ulimwenguni bali kuwa na thamani inayotufanya tushindwe kuielezea kwa hata kwa maneno milioni kwani inazidi maelezo yote.
Hao wanatuasa je, kwa kuupenda kwetu ujana na kutaka kushindana namabinti zetu kuwa mabinti tutakuwa na mama bora? Hawa wanahofu kubwa sana juu ya kizazi chetu kuweza kuipoteza ile thamani ya mama na kuufanya ule msemo wa ‘’Nani kama mama?’’ upate jibu ambalo kwa karne nyingi ulikuwa ni wenye kukosa jibu.
Lakini licha ya yote yaliyofanyika na kuandikwa kwa siku hii ambayo tumejikuta tukiitumia sana kwa ajili ya mama zetu hata ilivyo kinyume na mwanzilishi wa siku hii Mwanamama shujaa Anna ambaye alijikuta akiipinga kwa nguvu kubwa , leo nimeona niandike kuhusu yule mama.
Yule mama aliyepoteza mwanaye siku chache kabla hajamleta duniani,ambaye alimtabiria na kumpangia mipango mingi kiumbe aliyembeba tumboni mwake kwa muda unaokaribia mwaka.Mama aliyekubali kuhatarisha uhai wake kwa kubeba kiumbe huyu lakini licha ya kuhatarisha uhai wake matokeo yake kiumbe huyu alifariki kabla ya kuliona jua na kuiona dunia iliyojaa heri na shari.
Naandika leo kwa ajili yake , pole sana.
Mama ambaye alimpoteza mwanaye mara baada ya kumleta ulimwenguni, saa, siku, ama miezi michache baadaye.Najua tumbo lake linatetemeka na kuungua kwa uchungu kila amwonapo mjamzito na kukumbuka machungu ya kumpoteza mwanaye ambaye leo hii anaamini angekuwa mkubwa kama wana wa wenzie ambao walikuwa wote ‘leba’.
Naandika pole sana ingawa najua pole yangu haimponyi na kumpunguzia walau nukta ya maumivu , bali naamini Mungu kaisoma pole yangu na kampunguzia maumivu.
Naandika juu ya yule mama ambaye mwanaye amefariki akiwa ameshaanza kusoma, alikuwa ameanza kukuza matumaini aliyokuwa nayo lakini ghafla, ugonjwa ama ajali vikakatisha uhai wake.Najua ni maumivu yasiyomithilika lakini naandika katika siku hii pole sana.Mungu anajua mateso uyapatayo kila usikiapo mtu katupa mtoto ama umwonapo mtoto wa rika lile la mwanao na haiba ya mwanao.
Naandika tena pole sana mama.
Naandika kwa mama wote waliowazika wana wao katika umri wowote , wengine hamkupata hatwa muda wa kuwaaga ama kuwazika, maumivu yenu najua ni makubwa .Naandika kwenu poleni sana.Naandika pole nikitumai ni wengi tuwapao pole juu ya hayo mliyoyapitia naamini ,Mungu aliye juu atawapunguzia uchungu muupatao.

Naandika kuhusu nyote, mlioumizwa kwa kule tuu kuwa mama.
Poleni sana.

Alamsik.
Moringe Jonas.

0 comments:

Post a Comment