Uchungu wake mzazi,mlenzi ama
rafiki,
Moyo unakufa ganzi, ndugu
anapofariki,
Imekuwa wanafunzi, na kuleta taharuki,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa
hili gumu.
Zile ndoto zake mama,ama baba kwa
mwanaye,
Jana zimeshasimama,na kuisha
hatimaye,
Ni ajali siyo homa, leo hii hawanaye,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa
hili gumu.
Vimezimishwa vipawa,walivyobeba
watoto,
Bila ya kugusa dawa,imekuwa kama
ndoto,
Ni kama imezinduwa,ShauriTanga na
moto,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa
hili gumu.
Walimu waliopotea,na wale
waliowapenda,
Dereva katangulia,kaenda na
alowapenda,
Shule hakujatulia,myoyo yabaki
kudunda,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa
hili gumu.
Pole kwa wanafunzi, mloguswa na
hili,
Pole kwa mama wazazi,muweza
kustahimili,
Pole pia kwa walezi, leo mwaona
miili,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa
hili gumu.
Pole kwa watanzania,nchi
imetikisika,
Hili kulishuhudia,myoyo
inatetemeka,
Arusha yote walia,wanetu
kuwakumbuka,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa hili
gumu.
Naandika kama baba, kaka na
mwalimu wenu,
Kwenu darasa la saba,mlofiwa na
wenzenu,
Tuwaombee kwa baba,awapokee
wenzenu,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa
hili gumu.
Na wale wadogo zao,waliwaacha
shuleni,
Pole na ziende kwao, nguvu mtiwe yoyoni,
Msiwaze yale yasiyo, wamekufa
ajalini,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa
hili gumu.
Laweza mkuta yeyote, si fukara si
tajiri,
Hivyo tuyafute yote, kudhani
yasiyojiri,
Na tuwafariji wote, hima bila
kusubiri,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa
hili gumu.
Pia niwaase jambo, kwa watumao
zao picha,
Hayafai hayo mambo, ni watu siyo
mchicha,
Ama tuzishike fimbo, ndipo mtaja
zificha,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa
hili gumu.
Kaditama nasimama,poleni kwa mama
zao,
Ninaumia mtima,kuwazia baba zao,
Naingiwa na huruma,juu ya walimu
wao,
Mwisho nabaki kusema,wapo naMungu
wao.
0 comments:
Post a Comment