Na. Mwanakalamu
Asubuhi ya tarehe tisa April mwaka 2012 Tanzania na Afrika kwa ujumla iliamka na taarifa ya kifo cha aliyekuwa gwiji wa filamu nchini Marehemu Steven Kanumba.Ilikuwa ni taarifa iliyoshtusha na kuumiza watu wengi sana.Kwanza kutokana na sababu iliyopelekea mauti ya kijana huyo aliyekuwa mchapakazi wa kiwango cha juu ambayo ilimhusisha nyota mwingine wa filamu Binti wa Mzee Michael maarufu kama Lulu, pia mauti kumkuta kijana huyo akiwa kwenye kiwango cha juu kabisa cha mafanikio katika kazi zake.
Mengi yalizungumzwa baada ya kifo chake , huku kila mmoja akikiongelea kwa namna yake.Kuna walihusisha nguvu za shetani na ‘bla bla ‘nyingine nyingi za hapa na pale.Wapo waliodai kuwa Kanumba hakufariki na siku ingefika kuwa angeamka na kuwa hai tena, wapo waliodai kifo kilitokana na kile kilichoitwa, kutoa siri za Freemason kwenye filamu yake ya Devil Kingdom na kuwa alijua kifo kilikuwa karibu yake na namna kitakavyo kuwa kwa kuigiza kwenye filamu yake iliyokuwa ikifuatia kutoka ya ‘Power of Love’ kuwa mauti yake yangesababishwa na kuanguka baada ya kusukumwa bafuni.
Yote hayo ni kawaida kwa kila tumpendaye anapofariki ghafla inakuwa ngumu kukubali kama kweli ameenda na hatorudi.
Lakini kifo cha Steven Kanumba kilisababisha tukio moja la kushangaza Dada mmoja katika moja ya mikoa ya Kusini Mashariki mwa nchi kutaka kujiua aliposikia kuwa mwigizaji ambaye alikuwa akishabikia kazi zake alikuwa amefariki.Ilikuwa ni taarifa iliyoshangaza na kushtusha wengi huku wengi tukitafsiri tukio lile kama ushamba tuu na kulipotezea.
Kitendo kile kilikuwa na maana kubwa sana kwangu , kilionesha namna kazi za Steven Kanumba zilivyofanikiwa kiteka akili na mioyo ya wengi ambao walimlilia na kuumia kwa kifo chake lakini mmoja alijikuta akishindwa kuvumilia maumivu ya kuondokewa na mtu ambaye hakuwahi kumuona zaidi ya kwenye televisheni.Hakuwa ndugu yake , hakuwa jirani yake lakini alifikia kiwango kikubwa cha maumivu na kumfanya ashindwe kuvumilia taarifa ya kifo chake.
Binti alienda mbali kwa kusema kuwa alifiwa na kaka yake wa damu kabla lakini alihisi maumivu aliyoyapata kwa kifo chake hayakufikia yake aliyokuwa nayo baada ya kusikia taarifa ya kifo cha Steve.
Hii ilionesha mafanikio ya kazi ya Steve ambaye alijitahidi kwa hali na mali kukidhi haja ya walengwa wa kazi zake.Kupitia kazi zake nilipata kugundua kuwa Steve alikuwa ni mtu aliyependa kujibidiisha na kujifunza kwa kiwango cha juu kabisa.Alikuwa akiwekeza muda , pesa na akili yake kwenye kazi zake na hili nililiona kwenye filamu yake ya ‘’Crazy Love’’ filamu iliyobora kabisa kwangu kimaudhui.
Baada ya kifo cha Steve wengi walitabiri anguko la filamu nchini, na ndicho kilichotokea.Waigizaji wamekuwa maarufu kwa vitu vingine na si uigizaji tena, filamu na nchini zimekuwa zikipuuzwa na kushindwa kushindana sana na zile za utamaduni wa nje ya nchi sokoni.Dada wa kazi ambao ni miongoni mwa wafuatiliaji wakubwa wakifuatiwa na watoto (kwa takwimu zisizo rasmi) wamekuwa wateja na walevi wa filamu za Korea, China India na Marekani kwa akina kaka na si Bongo tena.
Sikushangazwa na kitendo cha wao kutumbukia kwenye kampeni za vyama kwenye uchaguzi mkuu uliopita wengine wakiyumba yumba huku na huku majukwaani wakionekana hawajui wanachokifanya majukwaani (kwani si waimbaji kusema wataimba ama wachekeshaji wakachekesha ) bali walijaribu kutumia umaarufu wao ambao waliuvuna kwenye uingizaji na kuukuza kwa ‘skendo’ na kazi nyingine zisizo za filamu.Nilijua ni njaa ya pesa itakayoendana na majina yao ambayo yalianza kufutika vinywani mwa wengi.
Filamu za nchini zinahangaika kufikia anga alilolifikia Steven Kanumba kwa nguvu nyingi (hata kwa maandamano) lakini bado shughuli ni pevu.
Ndiyo maana kisa cha Yule dada wa kazi nilikitafsiri na nitakitafsiri na kukipa maana kubwa sana.
Pumzika Steven Kanumba.
Leo wanamuziki wamewaacha mbali sana ndiyo maan hata Shilole kaamua kuwa mwanamuziki.
0 comments:
Post a Comment