ads

Saturday, 5 August 2017

SHAIRI:MWANANGU MZAZI NGAO

Mwanangu leta mkeka, utandike upenuni,
Najua unanicheka, kujanika juani,
Sijali naneemeka, na wewe ukae chini,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Mwanangu kuna magumu, ya kusemwa na kutendwa,
Nusu tuzilambe sumu, kukufanya ukalindwa,
Tukakubali hukumu, ili usije kupondwa,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Ile aibu ya mwaka, aliyoileta dadako,
Mioyo ikatuwaka, alipoumwa kakako,
Mamako anazeeka, kisa kero za babako,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Shule wafukuzwa ada, madeni huku na kule,
Twachekwa sie wa shida, kufanya mwanetu ule,
Huku na huko ni mada,tunanyoshewa vidole,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Siku nimekengeuka, namnyanyasa mamako,
Mamako hakugeuka, kaficha kulinda jiko,
Na nyumba haikubomoka, akailinda miiko,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Mishale ilituchoma, na miiba kututesa,
Na wala hatukukoma, na hatukomi sasa,
Twasema mwanangu soma, ‘siharakie usasa,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Hatuoneshi makovu, ama kuzinena shida,
Muhimu kwepa maovu, na uishike ibada,
Usijezitaka mbivu, kabla ya kufika muda,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Nilimsumbua mama, nilivyokuwa mtoto,
Nilimwona kasimama, mie damu ya moto,
Na leo inaniuma, sikuwa mwema mtoto,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Yauma sikuwa bora, kuigundua huzuni,
Sikuziona busara, nikaziweka kichwani,
Nikaivuna hasara, mama ninamtamani,
Mwanangu mzazi ngao, anayo makovu mengi.

Nakuona wasinzia, na kijua chanichosha,
Sijui yamekwingia, ama ndio nakuchosha,
Wanao ‘tasimulia, na wao utawachosha,
Mama kapika viazi, vipi wawaza mikate?

''Kauli za Makabwela 2017''

1 comments: