Wakazi wa kijiji cha Gamboshi
Wengi tumekuwa tukisikia habari nyingi kuhusu kijiji cha Gamboshi kilichopo wilayani Bariadi.Kijiji hichi kimekuwa kikihusishwa na uchawi na ushirikina huku ikisemwa kuwa kina maajabu mengi sana.Kwa wale waliokuwa wakisikiliza kipindi cha sitosahau kupitia Redio Free Afrika kipindi kile watakuwa wamewahi kusikia habari kuhusu maajabu ya kijiji hicho, mwandishi nguli wa hadithi nchini Eric Shigongo aliwahi kuandika hadithi akitumia jina la kijiji hicho.
Kuna wale ambao walikuwa wakihisi kuwa jina hilo ni la kubuni na hakuna kijiji kama hicho.
Nimekuwekea makala iliyowahi kuwekwa kwenye gazeti la mwananchi miaka kadhaa iliyopita . isome hapa chini;
Kijiji hicho ambacho ni nadra sana kutembelewa, kimepata umaaurufu
mkubwa ndani na nje ya nchi kikielezwa kuwa ni kitovu cha uchawi na
wachawi wanaoweza kufanya miujuza, hali ambayo imekifanya kijiji hicho
kupitwa na mkondo wa kimaendeleo.
“Sisi ni wakulima wakarimu wa pamba, mahindi na mpunga. Yote
mnayoyasikia kwamba sisi ni magwiji wa uchawi ni uvumi uliotiwa chumvi
nyingi. Tunamwomba Rais wetu kwa kushirikiana na Mbunge wetu, Andrew
Chenge watusadie kulisafisha jina letu,”alisihi Zephania Maduhu, Ofisa
Mtendaji wa Kijiji cha Gamboshi.
Maduhu pamoja na wanakijiji wenzake walidai kuwa, hofu iliyoenezwa ndani
na nje ya nchi kuhusua uchawi uliovuka mipaka wa Kijiji cha Gamboshi
umesababisha madhara makubwa kwa kijiji chao kiasi chakutengwa na jamii
yote ya Watanzania.
“Hakuna aliyetembelea kijiji hiki kwa miaka mingi sana. Hata sisi
tunapotoka nje ya kijiji, wengi hawataki kutusogelea wakiamini
tutawadhuru, ” alisema Musa Deus (26), mmoja wa wakulima walionufaika
kilimo cha mkataba kijijini Gamboshi.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, tangu Uhuru mwaka 1961,
hakuna kiongozi yoyote wakitaifa aliyewahi kukanyaga kijijini hapo.
Anaongeza kuwa mtu wa pekee aliyewahi kuzuru kijijini hapo ni mbunge wa
Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, aliyefika kijijini hapo mwaka 2010,
wakati akifanya kampeni za ubunge.
“Tume ya Katiba ilitupita, mwenge wa Uhuru nao haujawahi kupita hapa.
Tuko kisiwani mbali na Watanzania wengine,” anasema Maduhu.
Kikiwa mafichoni kabisa, kiasi cha kilometa 44 kutoka mjini Bariadi,
Kijiji cha Gamboshi si rafiki wa watu wa Kanda ya Ziwa kama ambavyo
Mwananchi Jumapili ilibaini katika utafiti wake wa muda mrefu.
Mijini na vijijini, kumekwepo na ubishani mkali kuhusu ni mkoa gani
unaokimiliki kijiji hicho, ambacho baadhi ya wakazi wake wanadai kuwa
miongoni mwa vioja vyake ni mauzauza yanayoweza kuifanya Gamboshi
ionekane kama Jiji la New York, Marekani au London, Uingereza wakati wa
usiku.
Pamoja na umaarufu wake, bado uwepo wa Gamboshi umekuwa ni kitendawili
kikubwa kwa jamii ya Wasukuma kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga na
Simiyu.
Mbali na ubishani mkali kuhusu kuhusu mahali hasa kilipo kijiji hicho
cha miujiza, wengi wamekuwa wakidai wakazi wake siyo jamii ya Kisukuma.
Wakazi wa Shinyanga wanadai kuwa Gamboshi iko wilayani Magu, Mkoa wa
Mwanza, wakati wale Mwanza wakidai kuwa iko mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa Maduhu, Gamboshi iko katika Wilaya Bariadi, karibu na
mpaka unaotenganisha na Wilaya ya Magu iliyoko mkoani Mwanza.
“Tunaomba sana ndugu mwandishi, waambie Watanzania kuwa mengi
wanayoyasikia kuhusu Gamboshi siyo kweli kabisa. Tunawakaribisha wote
waje hapa kufanya biashara na sisi, waoleane na vijana wa Gamboshi kama
wafanyavyo katika vijiji vingine. Sisi ni binadamu wema,” anasema mkazi
wa kijiji hicho, Malimi Kidimi ambaye ni mkulima.
Ofisa Mkaguzi kutoka Bodi ya Pamba (TCB), Ramadhani Dissa, anaielezea
Gamboshi kuwa ni moja ya vijiji vilivyouza pamba nyingi msimu huu.
Anasema kuwa Wilaya ya Bariadi, kilipo kijiji hicho, imeweza kuuza robo
ya pamba yote iliyouzwa nchi nzima hadi kufikia katikati ya Oktoba mwaka
huu.
Kwa mujibu wa Dissa ni maofisa wa bodi ya pamba tu ndiyo wanaofika
kijijini hapo na kwamba siyo wananchi tu wanaogopa kufika hapo, bali
hata baadhi ya kampuni za ununuzi wa pamba.
“Kampuni ya Billlchard, moja ya mawakala wa kilimo cha mkatabaka
alishindwa kutuletea mbolea hapa, badala yake akaenda kuibwaga katika
Kituo cha Polisi Bariadi kwa kile ambacho wafanyakazi wake walidai ni
kuhofia usalama wao,”anasema Maduhu.
“Pigo tulilopata kutokana sifa mbaya tuliyobambikiziwa haisemeki na
madhara makubwa tunayapata kutokana na kutengwa na jamii. Wanakijiji wa
Gamboshi ni masikini kwa sababu mkondo wa maendeleo na mageuzi umepata
mbali sana nao,” anasisitiza Maduhu.
Chanzo cha hofu
Akifafanua kiini cha chuki na hofu hiyo, Maduhu alidai kuwa hapo zamani
ilitokea kijana mmoja kutoka kijiji jirani cha Ngasamwa kuwa na
mahusiano ya kimapenzi na msichana mzaliwa wa Gamboshi.
“Siku moja kijana huyo alikuja kijijini hapa akimsandikiza mpenzi wake,
kisha kushindwa kurudi kijijini mwake,” anasimulia Maduhu akiongeza,
“Juhudi za kumsaka kijina huyo hazikiweza kuzaa matunda, hadi
aliponekana kichakani baada ya siku saba, huku ngozi yake imebadilika na
kuwa nyeupe.”
Anaeleza kuwa alipouliza alifikaje kichakani hapo, kijana huyo alijibu
kuwa ameteremshwa na ndege kutoka Ulaya na baada ya hapo kijana huyo
alirukwa na akili na kushindwa kuuongea.
“Ilibidi achukuliwe na kupelekwa kutibiwa na waganga wa jadi na akapona
baada ya matibabu ya zaidi ya mwezi mmoja,” anasema Maduhu akieleza kuwa
kisa hicho kilitiwa chumvi nyingi licha ya kuwa na ukweli kiasi.
Anasema kuwa, tangu siku hiyo Gamboshi ikatangaziwa uadui na vijiji vingine kiasi cha kukifanya kuogopwa na kuchukiwa.
“Uvumi kama Gamboshi inaweza kuonekana kama Ulaya au Marekani ulianzia
hapo na umendelea kurudifiwa na kukikifanyakijiji hiki kiitwe jiji la
maajabu,” alidai Maduhu.
Sisi ni wasafi
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Malimi Kidima anasema kuwa wana Gamboshi
wangeweza kuitangazia dunia kuwa wao ni wasafi lakini, kwa miaka mingi
wamekosa jinsi ya kuifanya sauti yao isikike.
Hakuna redio wala Luninga
“Redio ndiyo njia ya pekee inayotufanya sisi tuwe karibu na dunia,
Hakuna mwenye luninga hapa kwa sababu hakuna umeme. Tunasoma magezeti
kupitia vichwa vya habari vinavyosomwa kila siku redioni,” anasema
Kidima.
Mkazi wa Lamadi, wilayani Magu, Anthony Mashimba alidai: “Gamboshi ni jiji la ‘masupastaa’ wa uchawi hawatakuachia ufike huko.”
Tofauti na wengine, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba ya Kanda ya Ziwa, Jones
Bwahama alitoa uhakika na kusema Gamboshi imekuwa ikifikiwa mara kwa
mara.
Mauza mauza ya kwanza
Kutoka Bariadi mjini ni lazima upitie kijiji cha Ngulyati kiasi cha
kilometa 30 Mashariki ya Bariadi katika barabara itokayo Bariadi kwenda
Magu.
Hakuna kibao kinachotambulisha Kijiji cha Gamboshi mwanzoni mwa barabara ya vumbi inayoelekea Gamboshi kuanzia Ngulyati.
Watu walikuwa wengi katika kilometa 5 za awali kuelekea Gamboshi, lakini
idadi ikazidi kupunguia kwa namna tulivyozidi kukikaribia kijiji hicho.
Barabara ilikuwa tupu hadi kilometa tano kukufikia Gamboshi hali ambayo ilianzisha hofu mpya hata kwa mwandishi wa makala haya.
Nyumba nzuri mfano wa shule za kisasa za ‘English Medium’ ilionekana
kuvutia macho kilometa chache kabla ya kukifikia Kijiji cha Gamboshi.
“Ile ni shule ya Serikali au ya mtu binafsi,” aliuliza mmoja wa watu
tuliokuwa nao katika safari hiyo baada ya macho yake kuishuhudia kwa
mbali.
Lakini kwa mshango dereva alisema: “Hakuna shule yoyote ule ni mlima tu wa mawe mengi.”
Ilioneka dhahiri kuwa ni nyumba, lakini hata tulipopiga picha kwa kamera
niliyokuwa nayo, picha ilionesha kuwa hakuna nyumba yeyote.
Baada ya mwendo, Kijiji cha Gamboshi kikaanza kuonekana kikipambwa na
miti ya Jakaranda yenye maua mekundu, kiliioenekana ni kijiji kizuri,
chenye nyumba chache na hali yake kunogeshwa na ubaridi uliotokana na
miti mirefu iliyopandwa kuzunguka nyumba chache zilizokuwepo.
Habari hii imenukuliwa kwenye tovuti ya Mwananchi kupitia gazeti lake la Mwananchi Jumapili, kama ilivyoandikwa na mwandishi Miguel Suleyman.