ads

Sunday, 8 May 2016

Hadithi: Kisasi cha ajabu


HADITHI; KISASI CHA AJABU
MTUNZI; MORINGE JONASY
MWANZO
Akiwa katika siku yake ya pili kwenye mafunzo kazini Muuguzi Melina Joseph anakutana na jambo la ajabu ambalo linamfanya ajute kusomea uuguzi.Japokuwa aliwahi kuwaona watu wakipoteza maisha lakini si kwa idadi na namna ile aliyoiona.Wajawazito watano kati ya kumi walipoteza maisha ndani ya dakika kumi na tano wakipishana kwa dakika chache sana lakini jambo la ajabu ni kwamba wote walitokwa na povu mdomoni kabla ya kukata roho.
Melina aliingia ofisini kwa wauguzi na kutoka bila sababu yoyote huku akijaribu kumpigia muuguzi mwenzake ambaye hadi muda huo alikuwa hajafika .Kila alipompigia simu haikupatikana hadi pale alipofika dakika ishirini baadaye ambapo naye alishtushwa na idadi ya wauguzi na madaktari ambao walikuwa wakihangailka kuihamishia miili ile Mochwari. Alimuita Melina pembeni na kuanza kuteta naye juu ya sababu ya hali ile lakini jibu alilopata na kuamua kuungana na wauguzi wengine kuwashughuliia wajawazito wengine ambao walikuwa wakiingizwa kwenye chumba cha wagonjwa waliohitaji uangalizi maalum ( ICU).
Idadi ya wagonjwa waliopoteza maisha ilizidi kuongezeka ikiwashangaza madaktari wa hospitali ile ya serikali iliyopewa hadhi ya kuwa hospitali ya Rufaa.Daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama aliwaita wauguzi waliokuwa zamu muda ule na kuwauliza juu ya tatizo lile katika harakati zake za kutaka kujua sababu iliyopelekea vifo vile ambavyo hadi kwa wakati ule ni mjamzito mmoja tuu ndiye alikuwa ambebaki tena akiwa chini ya uangalizi maalum wa jopo la madaktari waliokuwa wakijitahidi kwa hali na mali kuokoa maisha yake.
Hata hivyo hawakuwa maelezo yoyote ambayo yaliyosadia kujua sababu ya vifo vile huku Melina akionekana kuwa na uoga kujibu maswali yale jambo lililogunduliwa na yule daktari ambaye aliamua kumruhusu yule mwenzake na kumtaka Melina abaki hali iliyompa uoga yule mwenzake kutokana na kuchelewa kwake kufika zamu jambo ambalo alilikuwa kawaida kwake japo alikuwa amepewa onyo zaidi ya mara tatu.
Tabia ya utoro na uchelewaji kazini ilisababisha vifo vya wagonjwa wengi lakini muuguzi yule hakupewa adhabu nyingine zaidi ya kuonywa ,huku ikisemekana uhusiano wake wa kimapenzi na mganga mkuu ukiwa sababu ya kutofukuzwa kazi. Wakati hayo yakiendelea Daktari mmoja kijana ambaye alikuwa na miaka miwili tuu pale kazini alifikiria kitu kilichomfanya aende kwa baadhi ya wauguzi na kuwauliza juu ya mwanamke mmoja ambaye alikuwa na kawaida ya kufika pale hospitalini na kupitiliza hadi wodi ya kinamama wajawazito. 
Bwana Stivin Ngonyani kijana mwenye umri usiozidi miaka thelathini alikuwa akitafakari juu ya makazi halisi ya Mwanamke yule ambaye baada ya kuuliza aliambiwa kuwa alikuwa akiitwa mama Rose japo hakuwepo hata mmoja aliyefanikiwa kujua alikokuwa akiishi licha ya kuwa na urafiki na wauguzi wengi ambao walizoea kumwona akiwaletea chakula wajawazito waliokuwa hawana ndugu wa kuwasaidia.
Mama Rose alikuwa mtu mwema , na hata Stivin alijikuta anajiuliza kitu kilichomfanya apate mashaka juu ya yule mama.Hakujua kitu kilichomfanya amhusishe yule mama na vile vifo lakini alijikuta akizidi kupata shauku ya kutaka kumfuatilia na kujua makazi yake na sababu iliyomfanya apende kuwapelekea chakula wagonjwa hasa wajawazito. Ilipotimu saa moja na nusu jioni bwana Ngonyani aliinuka na kuingia ofisini kwake akijiandaa kuondoka na kuanza uchunguzi usio rasmi juu ya yule mama ambaye nafsi yake ilimhusisha na vifo vile. 
Akiwa kwenye harakati ya kukusanya vitu alivyoona vya muhimu kutoka navyo ghafla mlango wa ofisi ile ulifungwa na mfungaji alionekana kuondoka na ufunguo licha ya kujua kuwa palikuwa na mtu mle ndani. Kitu cha ajabu katika ofisi ile hakukuwa na daktari mwingine ambaye alikuwa akiitumia zaidi yake na mwenzke ambaye alikuwa Masomoni , hivyo kitendo kile kilimfanya akose jibu huku maswali yakizidi kuongezeka kichwani mwake juu ya sababu ya vifo vya akina mama wale wajawazito.
Kelele zake za kuomba msaada hazikumfanya yeyote aliyezisikia kwenda kumsaidia jambo ambalo halikuwa la kawaida pale ofisini.Aliamua kurudi kitini akitaka kuchukua simu yake ili awapigie watu waliokuwa nje ya ofisi ile ili wamsaidie ajabu kila aliyepigiwa simu hakuipokea. Mara taa za mle ndani zilizima na hazikuwaka tena japokuwa palikuwa na jenereta lililowaka mara tuu umeme ulipokata.Nje kulionekana kuna mwanga lakini ndani ya ofisi ile hapakuwa na mwanga wowote jambo lililomfanya Ngonyani asogelee swichi ya ukutani na kuhakikisha kama taa ziliwashwa, jambo lililomfanya apigwe na shoti ya umema kurushwa hadi palipokuwa na makabati kabla ya kutua sakafuni na kupoteza fahamu. 
Kishindo kilichotokana na kuanguka kwa Daktari Stivin Ngonyani kilimshtua Muuguzi Melina aliyekuwa akipita karibu na ofisi ile na kumfanya asimame na kusikiliza ilikotoka ile sauti. Ukimya uliofuatia kishindo kile ulimtisha Melina huku kumbukumbu za maiti za wale wajawazito zikijiridia kichwani na kuamua kuondoka eneo lile. Lakini kabla ya kuweka chini mguu wa kwanza kuunyanyua sauti ya kike inaita jana lake na kumfanya ageuke kumwangalia muitaji.
"Ha! Mama Rose, shikamoo...."aliongea baada ya kugeuka. 
"Marhaba mwanangu, poleni na matatizo"alijibiwa na Mama Rose ambaye alikuwa ameshamkaribia. 
"Asante sana mama yaani hapa hadi naogopa"Melina aliongea akigeuka geuka kwa uoga. "Mipango ya Mungu mwanangu, hivi Ngonyani yupo?"mama Rose aliuliza akiangalia mlango wa ofisi iliyokuwa jirani. 
"Mbona pamefungwa, atakuwa ameshaondoka",alijibu. 
"Ina maana funguo kazisahau hapa?"mama Rose alitikisa funguo alizokuwa amezichukua kwenye dirisha la ofisi ile.
"Mhh labda amezisahau ",Melina aliongea akipokea zile funguo na kuzichunguza kwa muda huku akiangalia ofisi ile. Alitamani kuifungua lakini ugeni ma uoga ulimfanya aamue kuzipeleka kwa daktari mwingine . 
"Haya mwanangu ngoja niende tutaonana kesho",mama Rose aliondoka na kumwacha Melina akiingia ofisini kwa daktari ambapo hakumkuta licha ya mlango kuwa wazi. Kwa uoga alitembea kwa haraka hadi palipokuwa na kundi la watu ambao baada ya kuwasalimia waliendelea na mazungumzo yao. Alifanya hivyo kwa vikundi kama vitatu lakini hali ilikuwa vile vile.Alianza kupata mashaka juu ya wale watu kwani uitikiaji wao wa salam ni kama ulifanana hivi. Akaamua kukisogelea kikundi kimoja na kuwaangalia wahusika bila kuwasemesha. Uchunguzi juu ya mwonekano wao uliishia kwenye miguu ambayo ilimfanya aishiwe nguvu na kuanguka kama mzigo na funguo zake mkononi
Mwonekano ya miguu ya watu wa kundi lile ulimfanya Melina akose nguvu kabla ya kupoteza fahamu.
Hakuwahi kuona zaidi ya kusimuliwa kwenye hekaya kuwa kulikuwa na viumbe-watu waliokuwa na miguu iliyofanana na ng'ombe.
"Mtu awe na miguu kama kwato za ng'ombe?, unatudanganya Melina"aliongea mmoja ya madaktari baada ya Melina kurejewa na fahamu na kueleza kisa cha tatizo lake.
"Kweli walikuwa kwenye vikundi kama vitatu Dokta" Melina alijaribu kumshawishi yule daktari huku kumbukumbu za kuwaona wale watu waliokuwa na kwato zikimfanya afumbe macho yake.
"Enhee na kisa cha kumfungia Dokta Ngonyani na kuzunguka na funguo ni kipi?"yule daktari aliuliza swali lililomstua Melina na kung'aka.
"Kunfungia?, haya mauza uza kabisa yaani mbele ya macho yangu mama Rose ameokota funguo na nilikuwa namtafuta Dokta nimpe funguo zake.
"Tangu lini dokta ofisi zake zikawa mochwari, kweli ulikokuwa ukienda ndiko kuna ofisi yake?"yule daktari alihoji wakati huo bwana Stivin Ngonyani alikuwa ameshaingia mle ndani na kubaki kimya bila kuongea chochote.
"Nilifika mochwari!, Mungu wangu mbona nilikuwa hapo nje ya ofisi yake tuu" Melina aliongea kwa mshangao.
"Mhh haya mambo sasa magumu"aliongea yule daktari na kushusha pumzi kwa nguvu mara baada ya kumwona Ngonyani nyuma yake.
"Pole sana dada Melina" aliongea Ngonyani akikisogelea kitanda.
"Asante pole na wewe kwa kufungiwa ofisini"Melina aliongea na kumgeukia Ngonyani lakini alishtuka baada ya kuona weusi uliokuwa upande mmoja wa uso wake.
"Jamani dokta nini tena hicho?" Melina aliuliza kwa uoga.
"Ni ajali ndogo tuu hapa nimepaka dawa ya kukausha"Ngonyani alijibu akimwangalia Melina kwa macho ya upole zaidi na kusababisha Melina kuyakwepesha macho yake.
"Dawa gani nyeusi hivyo?" Aliuliza Melina kwa upole.
"Ni ya kienyeji nimepewa na mama Rose" Ngonyani alijibu.
"Mama Rose!" Alishangaa Melina lakini baadaye alibaki kimya.
"Ehee kwani ana tatizo gani?" Alihoji yule daktari mwingine aliyeonekana kuwa kimya kwa muda kidogo.
"Hamna kitu nimejikuta tuu nimeropoka"alijibu Melina na kunyong'onyea.
"Lakini nina mashaka na yule mama" Ngonyani aliongea akiangalia mlangoni kuhakikisha usalama wa alichokizungumza.
"Ehee hata mimi hivi anakaa wapi?" Melina alidakia lakini swali lile ni kama lilimkera yule daktari.
"Na wewe ushaanza habari za kwato zako, ngoja nikupe dawa upumzike"yule daktari mwingine aliongea kwa hasira na kufungua kipakti cha dawa kilichokuwa pale mezani.
"Samahani dokta hizo dawa si nzuri kwa tatizo la huyu binti ''Ngonyani aliongea na kujaribu kupokonya zile dawa lakini yule daktari alimgeukia na kumwangalia kwa macho makali yaliyomfanya Ngonyani na Melina wapoteze fahamu.
Asubuhi ya siku ya pili Melina aliamka kutoka kitandani na kujipapasa kama alikuwa na majeraha yoyote mwilini mwake lakini hakuona kitu chochote wala kusikia maumivu mwilini mwake.Alipomwangalia muuguzi mwenzake ambaye alikuwa zamu kuanzia saa mbili asubuhi ,dakika arobaini zilizofuata alimwona akiwa kwenye usingizi mzito lakini badala ya kumwamsha Melina alianza kuzunguka mle chumbani akishika hiki na kile kama akihakikisha kitu fulani.
Hakutaka kuamini kama kweli alikuwa amelala kitandani pake,alifikaje nyumbani hakuelewa,ina maana aliyokuwa akiyaona yalikuwa ndoto? Alibaki anajiangalia huku wazo la kumwamsha mwenzake likimjia akilini.
Lakini kabla hajamwamsha yule mwenzake aliamka na kumwangalia kwa macho makali kabla ya kuangalia chini.
"Vipi mbona unaniangalia hivyo?"Melina aliuliza.
"Yaani hata siamini kama ni wewe"yule mwenzake alimjibu safari hii akimtazama usoni.
"Kwa nini", aliuliza.
"Mara utake kukimbia ,mara watu wanakwato, mara Mama Rose yaani hadi tulimwita huyo dokta jirani atusaudie maana ulitushinda mi na dada Sarah"alieleza yule mwenzake kwa kirefu.
"Inamana nilikuwa naota,enhee nilifikaje nyumbani''?Melina alihoji huku taarifa ya uwepo wa daktari jirani yao mle ndani ikimkera kwani tangu anafika pale alikuwa akimtaka kimapenzi licha ya kuwa na mke.
"Si ulikuja na Mama Rose ukidai kichwa chakuuma ulilala saa moja yaani bila Mama Rose sijui ungelala njiani, ukipona ukamshukuru sana"alieleza yule mwenzake.
"Mbona sikumbuki kabisa" aliongea Melina akijaribu kuvuta kumbukumbu.
"Tuachane na hayo wajisikiaje?"
"Mi mzima sikumbuki kama niliumwa"
"Sawa ila jana umeumwa kweli,kama mzima wacha tupumzike kwani napumzika nikikuuguza " aliongea yule mwenzake akijiinua pale kitandani.
"Wacha wee kwa hiyo leo mapumziko?" Aliropoka Melina.
"Mhhh nawe siku mbili tuu umechoka unataka kupumzika" yule mwenzake alimsuta.
"We yale yaliyotokea jana kazini yanavumilika kweli? Ingekuwa si umasikini ningekuwa nimeacha kazi"alilalama Melina
"Ila tangu nianze kazi sijawahi kushuhudia hali kama ile"alieleza yule mwenzake.
"Yaani hata sijui tumwombe tuu Mungu".
Hodi ....hodi wenyewe mpo? Sauti kutoka nje iliwashtua.
"Karibu ,karibu hadi ndani, tupo"alijibu yule mwenzake akielekea sebuleni.
"Ha dokta Ngonyani karibu sana"alikaribisha Melina.
"Umemwona Ngonyani tuu mi hujaniona?"yule daktari aliyekuwa akimtaka Melina aliuliza kabla ya kukaa.
"Jamani we si mwenyeji, basi Karibu"Melina alijibu na kukaa.
" Haya lakini unaendeleaje?" Aliuliza yule Daktari.
"He dokta Ngonyani mbona hivyo?" Aliuliza Melina baada ya kuona weusi kwenye upande wa kushoto wa shavu lake.
"Ajali ndogo tuu dada" alijibu Ngonyani akipapasa shavuni.
"Pole sana kaka" waliongea Melina na yule mwenzake kwa pamoja.
"Asante",Alijibu.
"Ilikuwaje kaka?"yule mwenzake aliuliza.
"Jana nikiwa ofisini nilipata hitilafu kidogo nikapigwa shoti, yaani ashukuriwe Mama Rose asingekuwa yeye ningeweza kufia mle ndani"alieleza Ngonyani.
"Yaani huyu Mama Rose Mungu ampe maisha marefu ,amemwokoa Melina akaenda kumwokoa na Dokta"aliongea yule mwenzake na Melina.
"Kweli yule mama sijui mwanaye alipata malezi gani yaani ule wema umepitiliza"Ngonyani alichangia.
"Mwanaye tuu mumewe je?"aliongeza yule daktari mwingine akicheka.
"Hata ana mume kweli?"alihoji yule muuguzi mwingine.
"Afu kweli maana sijawahi kumwona" alieleza yule yule daktari.
"Huenda akawa mjane,halafu huyo Rose amewahi kuonekana,hata anapoishi mnapafahamu?"Ngonyani aliuliza.
"Mie mwanaye hata akaapo sipajui atakuwa anaishi huko chini anakoelekea"yule daktari alieleza akionesha kwa mkono upande aelekeako yule mama.
Alikumbuka kuwa miongoni mwa wanawake aliowataka kimapenzi ni yule mwanamke ambaye jibu lake moja lilikuwa ni lilelile kuwa 'nimeolewa'.
"Sasa mgonjwa ngoja tuwahi kazini, ugua pole ehee"aliaga Ngonyani akiinuka.
"Asante kazi njema na pole kaka Ngonyani"Melina aliaga akimwangalia Ngonyani kwa macho ya kichokozi.
"Haya mgonjwa ugua pole utapona eee"yule daktari mwingine aliongea akimkonyezea macho Melina aliyegeukia pembeni kwa dharau.
"Huyu mbaba anaonekana mhuni"Melina alimwambia mwenzake baada ya kujipa uhakika kuwa walikuwa wawili tuu pale ndani kwa kuchungulia mlangoni.
"Mhhh ehhe.. mi amenitaka kweli ananidanganya kuwa ana hospitali yake atanipeleka baada ya kunisomesha"alijieleza yule mwenzake akijua fika alidanganya kwani alikuwa kwenye penzi zito na yule daktari na kutaka kusababisha kuvunjika kwa ndoa yake.
"Eboo! Huko shule si angempeleka mkewe anayeshinda kuuza maandazi au binti yake aliyemaliza sekondari mwaka juzi mbona yupo tuu nyumbani akibadilisha tuu wanaume kama siti ya daladala, wazee wengine nao sijui wana laana?" Melina alimaliza na swali na maneno yale yakamwingia yule mwenzake huku akijiona mjinga kwa kuwa kwenye mahusiano na mzee wa umri wa baba yake.
"Hajiheshimu tuu wala si laana" yule mwenzake alijibu kwa kifupi huku moyoni akijilaumu kudokeza lile jambo kwa Melina.
Baada ya tukio la vile vifo hali ikajerea kama kawaida huku kila mtu akichukulia lile jambo kwa ukawaida tofauti na awali.Watu walizidi kusahau huku kumbukumbu juu ya Mama Rose zikipotea baada ya kutoonekana hadi miaka saba baadaye siku ya kuagwa kwa yule dokta mpenda dogodogo baada ya kustaafu na bwana Stivin Ngonyani alipokuwa akipewa udaktari mkuu wa ile hospitali huku Melina akiwa mkewe.
Uwepo wa Mama Rose ulimfurahisha kila aliyekuwepo kwenye ile sherehe na hata zawadi alizowapa wahusika zilipewa umuhimu sana na wahusika.
___________
Jioni ya ile siku kama ilivyokuwa kwa Ngonyani yule daktari mwingine aliifungua boksi lililokuwa na kuanza kuanza kutoa vilivyokuwemo.
Kadi nzuri ya pongezi yenye maneno yaliyomfurahisha kila aliyeisoma ilikuwa juu huku harufu nzuri ya marashi ghali ilifunika eneo lile hali iliyowavuta hata wake zao kusogea karibu ili kujua kilichokuwemo.
Zawadi iliyokuwa chini yake haikumfurahisha kila mmoja kwani palikuwa na biblia mpya.
Walifungua zile biblia na kukuta karatasi zilizokuwa na maelezo ya vifungu vya kusoma.
Walifungua vifungu vilivyoelekezwa na kuanza kuvisoma huku wake zao wakiwa wanahangaika na zawadi nyingine.
Saa nane na nusu usiku kama vile waliambizana yule daktari na Ngonyani waliamua kulala baada ya kuona wamezidiwa na usingizi licha ya mioyo yao kuwasukuma kuendelea kusoma.
Asubuhi iliyofuata, siku ambayo bwana Stivin Ngonyani ilikuwa ni siku yake ya kwanza kama Mganga mkuu wa hospitali ile alifika mapema sana tofauti na siku nyingine huku kichwani akiwa na malengo makubwa katika kuongeza sifa hospitali aliyokuwa akiiongoza.
Alienda moja kwa moja hadi kwenye ofisi aliyokuwa amekabidhiwa jana yake na kuanza kupitia pitia taarifa fulani.
"Dokta Ngonyani kumbe upo humu tunakuomba wodini" sauti ya kike ilisikika kutoka nje ya ofisi yake dakika ishirini tangu alipoingia .
Ngonyani alikurupuka kutoka alipokaa na kutoka nje alipokutana na kundi la wauguzi walioonekana kuchanganyikiwa.
"Kuna nini?"aliuliza baada ya kutoka nje.
"Twende wodini"aliongea muuguzi mmoja aliyeonekana mtu mzima kidogo.
Alipofika wodini alishangaa kukutana mapazia ya kijani yaliyozunguka karibu robo tatu ya ile wodi.
"Mungu wangu !"alijikuta akiropoka Ngonyani baada ya kuona maiti za wajawazito zaidi ya ishirini na tano huku zikiwa na povu mdomoni.
Idadi ya wajawazito walipoteza maisha iliongezeka kila dakika hadi kufikia saa tatu na nusu jumla ya wajawazito waliopoteza maisha ilifikia arobaini na tatu hulu wengine wakiwa katika hali mbaya.
"We huyu Mngoni si mchezo anataka kujisimika"aliongea mmoja wa wafanyakazi aliyeungwa mkono na wenzake waliokuwa wamekaa kwenye benchi.
"We huyu kijana anaogopa kupinduliwa"aliongea mzee mmoja aliyesimama jirani na alipokuwa akipita Ngonyani.
"Huyu mwoneni hivi hivi alivyo" alikazia yule mzee ambaye alionesha chuki zake wazi wazi bila kujali kama alichokiongea kilisikika hata kwa Ngonyani ambaye alionekana mwenye mawazo lukuki.
Kila alipopita vidole vilinyoshwa kwake kuashiria kuwa tuhuma za sababu ya vile vifo kuwa ni yeye.Hakuwa na raha hata kidogo,alikaa ofisini kwake huku akiwa na wazo moja tuu ,'kuomba kuacha kazi' kwani tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwake zilikuwa zimemwelemea.
Maiti ziliongezeka mochwari kila baada ya dakika, magari nayo yaliingia pale hospitalini na kulifanya eneo la wazi lililokuwa pale hospitalini lionekane dogo.
Waziri wa afya aliyekuwa ziarani kwenye mikoa ya jirani alikatisha ziara yake na kufika hospitalini pale kuangalia hali iliyokuwepo pale.
Kikao cha dharula kilifanyika pale ofisini ukiwahusisha madaktari na wauguzi kadhaa pamoja na waziri wa afya aliyeonekana kushtushwa na mwenendo wa ile hospitali.
Wakiwa katikati ya kikao mama mmoja aliomba kuingia mle ndani baada ya kubembeleza sana na kutambuliwa kuwa alikuwa ni Mama Rose aliruhusiwa kuingia.Alipoingia mle ndani aliuliza kama palikuwa na yule Mganga mkuu aliyetoka kustaafu jana yake na alipooneshwa aliomba wasaa wa kuzungumza akidai kujua chanzo cha vile vifo.
"Mama kama unajua inabidi ukaeleze polisi" aliongea waziri wa afya aliyeonekana kukerwa na madai ya yule mama aliyeonekana kama alikuwa na upungufu wa akili mbele yake.
"Nikaeleze polisi kwani kuna mtu ameua?" Aliongea yule mama kwa ukali jambo lililowafanya wauguzi wenyeji kutaka kumtoa yule mama kwa nguvu lakini kabla hata ya kumfikia waliashiriwa na waziri kuwa wamwache.
"Samahani mheshimiwa Waziri naamini wengi hapa wananifahamu kwa jina la Mama Rose lakini jina langu nililopewa na wazazi wangu ni Rose Daniel" aliongea yule mama huku akitoa kitambaa kilichokuwa hakibanduki kichwani kwake , na kuonesha sura yake yote ambayo ilionesha jinsi umri wake uliokuwa ukielekea machweo.
" Waliofanya kazi hapa mwishoni mwa miaka ya themanini watakuwa wanaikumbuka hii sura hasa hili kovu" aliinama kuwaonesha kovu kubwa lililokuwa kichwani kwake.
" Mnakumbuka eee au mmenisahau"aliongea yule mama akimsogelea Ngonyani akimshika mabegani.
" Umesahau mimi wa mtoto aliyekufa" aliongea kwa hasira huku machozi yakimtoka na kurudisha kidogo kumbukumbu yuma lakini yule mama alisimulia kisa chote.
_____________
SEPTEMBA 1988
Kundi la wanafunzi saba kutoka vyuo mbalimbali vya uuguzi nchini walifika kwenye hospitali kukiwa na wavulana watatu na wasichana wanne.Ujio wa wauguzi wale waliokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo ulipokelewa kwa hisia tofauti na wauguzi wenyeji na wagonjwa.
Wakati wagonjwa wakiamini ni muda wao wa kupata huduma bora kutokana na wingi wa watoa huduma ,upande wa wahudumu wenyeji waliona ni wakati wa kutegea kazi na kuwaachia wale wanafunzi.
Tofauti na mawazo ya makundi yale daktari mmoja alifikiria jambo tofauti juu ya ujio wa wale watu.Kilichokuwa akilini mwake ni juu ya uwezekano.wa kuwapata wale wasichana kuwafanya wapenzi wake huku akiamini mbinu yake ya kuwadanganya kuwa alikuwa na hospitali yake binafsi ingekuwa chambo.
Alitumia mbinu ile kwa wale wauguzi watatu na kufanikiwa kufanya nao mapenzi kwa nyakati tofauti ila ofisi yake ikiwa sehemu pekee ya matukio.
Alipofika kwa Rose Daniel haikuwa rahisi kumpata kama ilivyokuwa kwa wengine,mbinu zake zote hazikuwa na matokeo chanya kwake.
Rose alijiheshimu kama msichana wa kiafrika anavyofunzwa kubaki na usichana wake hadi atakapoolewa,marehemu wazazi wake kabla ya kufariki walikuwa hawaishi kumwonya juu ya hilo hata shangazi.yake aliyekuwa akiishi naye alimtaka ajitunze na kuzingatia masomo ili akawasaidie wadogo zake ambao nao walipoteza maisha kabla hata ya kumaliza masomo.
Siku moja akiwa kazini kama ilivyokuwa kawaida yule daktari alimwita Rose na kumtaarifu kuwa alikuwa zamu muuguzi mmoja mzoefu usiku wa siku ile jambo ambalo alikubaliana nalo bila kuhisi chochote.
Usiku akiwa kazini yule muuguzi mwenyeji alimtuma Rose maabara akimweleza kwenda kuchukua daftari alilokuwa amelisahau mchana.
Baada ya kuingia mle maabara mara mlango ulifungwa na taa ilizimwa na kusababisha giza totoro.Rozali aliyokuwa ameivaa Rose ilimwonesha alipokuwepo kutokana na kung'aa gizani jambo lililorahisisha kazi ya adui yule kumkamata.Mikono iliyokomaa ya yule daktari ilimshika Rose kwa nguvu kabla ya kurarua nguo zake.Kitendo hicho kilichukua dakika chache sana huku sauti dhaifu ya Rose ikishindwa kufika popote.
Baada ya kumfanyia unyama ule alimwinua kwa nguvu na kwenda kuwasha taa.
"Mungu wangu! Dokta "alilalamika Rose baada ya kumwona aliyemfanyia kitendo kileAliinua chuma kilichokuwa kilichokuwa mezani na kumwangalia yule daktari kwa hasira.
Tofauti na mawazo ya yule daktari.kuwa huenda angemdhuru, alichukua kile chuma na kutaka kujichoma kichwani kabla ya kuzuiwa na yule daktari lakini damu zilikuwa zimeshaanza kumtoka.Baadaye alipoteza fahamu na yule daktari alimpa huduma ya kwanza kabla ya kwenda kumwita yule muuguzi mwenzake ambaye walipanga ule mchezo.
"He! Ulitaka kuua?" Aliuliza yule muuguzi baada ya kuliona lile jeraha.
" Alitaka kujiua mwenyewe" alijibu yule daktari alitetemeka.
"Sasa tutafanyaje?"alihoji yule muuguzi.
"Akipata fahamu unibembelezee akaseme aliangukia sehemu yenye chupa" alishauri yule daktari.
Kama walivyopanga baada ya Rose kurejewa na fahamu alipewa somo na kiasi kikubwa cha pesa ambazo alizikataa lakini alikubaliana nao juu ya kutunza ile siri.
Siku moja akiwa njiani kuelekea nyumbani alikutana na kiumbe wa ajabu ambaye alimshangaa kwa kumsamehe yule daktari kwa kumtunzia siri, Rose alishtuka kusikia maneno yale kutoka kwa kiumbe yule wa ajabu ambaye baadaye alijitambulisha kuwa ni shetani.
Hakuamini kabisa kama shetani kiumbe anayefahamika kama chanzo cha dhambi duniani kulaani kitendo alichofanyiwa na yule daktari.
"Ni uongo tuu ulioenezwa na malaika wengine ili nionekane mbaya kwa wanadamu" aliongea yule kiumbe baada ya kusoma mawazo ya Rose.
"Nasamehe" alisema na kuondoka huku moyoni akiwa na hofu kuu.
Sura ya yule kiumbe ilimtokea kila mara hasa akiwa ndotoni hadi pale alipoamua kukubaliana naye kulipa kisasi.
Ile sura haikujitokeza tena hadi siku aliyomaliza mafunzo kwa vitendo na kurudi chuoni aliposisitizwa kulipa kisasi.
Wiki mbili baada ya kurudi chuoni Rose alikuwa miongoni mwa wasichana watano waliokutwa ni wajawazito baada ya kupimwa kama ilivyokuwa kawaida ya kile chuo.
Japokuwa walikuwa katika mwaka wa mwisho walifukuzwa chuoni kwa upande wa Rose alifukuzwa pia nyumbani jambo lililomfanya amrudie yule daktari aliyekuwa mwanaume pekee aliyefanikisha kuujua usichana wake.Mwazo alionekana kukataa lakini baadaye alikubali kumsaidia akidai angempeleka shule baada ya kujifungua.
Alimtafutia nyumba ya kukaa huku akimhudumia kwa mahitaji muhimu lakini kila usiku alitoa huduma ya penzi kwa yule daktari.Hali ile iliendelea hadi siku ya kujifungua ambapo alikutana na daktari Stivin Ngonyani aliyekuja pale hospitalini kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.
Kabla ya kumpa huduma Rose, Ngonyani aliitwa na yule daktari aliyemwelekeza kumuua mtoto atakayezaliwa na kumwonesha maiti ya kichanga kilichoandaliwa .Ngonyani alikubaliana naye na kuendelea na kazi ambapo kama alivyoelekezwa alionesha ile maiti lakini yule mtoto alimkabidhi mwanamke mwingine aliyejifungua maiti.
Alikuwa kichanga mzuri wa kike ambaye alipokelewa vyema duniani.na watu alioamini kuwa ni ndugu zake.
" Mwanamke gani unanizalia maiti tokaaa!" Ilikuwa sauti kali ya yule daktari ambaye alikuwa akimfukuza Rose usiku wa siku aliyojifungua.
" Ni mipango ya Mungu mpenzi" alibembeleza Rose.
"Mungu huleta maiti? Tokaaaa!" Alimsukumia nje yule mama ambaye alitakiwa awe chini ya uangalizi maalum baada ya kujifungua masaa machache yaliyopita.
Baadaye yule mama kwa kutambaa alijisogeza mita kadhaa kutoka nyumba ile kwani alihofia kipigo kutoka kwa yule daktari ambacho kilikuwa njiani.
Akiwa pale chini ile sura ya kutisha ilimjia tena na kumtaka alipe kisasi lakini alikataa kata kata na kumtia hasira yule kiumbe aliyejiita shetani aliyeamua kumtoa roho yake na kujiingiza kwenye ule mwili

"Hapo ndipo KISASI CHA AJABU KILIPOANZA ya uongo haya?" Aliuliza Mama Rose aliyeonekana kubadilika mwonekano wake na kuwa wa kutisha.
" Nilitaka kusahau yule mtoto uliyemwokoa ndiye mkeo bwana Ngonyani" aliongea alimnyoshea mkono Ngonyani kabla ya kumgeukia yule daktari aliyeanza kutapatapa kabla ya kutoa povu na kupoteza maisha.
Yule muuguzi aliyesaidia kubakwa kwa Rose naye alikufa kwa namna ileile kabla ya kiumbe yule wa ajabu kutoweka.
Ngonyani aliwekwa chini ya ulinzi na kupelekwa kituo cha polisi kabla ya kupelekwa mahakamani alikohukumiwa kifungo cha miaka mitano huku akipoteza kazi yake.

MWISHO.


2 comments: