Jioni imekaaje,rafiki zangu jamani,
Hili jambo likoje,lanichanganya jamani,
Ama hadi Mark aje,atueleze jamani,
Nawaona matapeli,na hizi barua pepe.
Mwanzo walinichanganya,nikahisi lile zali,
Wajanja wakanionya,kunambia siyo kweli,
Ila leo nawasonya,hawa kweli matapeli,
Nawaona matapeli,na hizi barua pepe.
Ujinga walionao,wote watwona vidume,
Na umbali tulonao,penzi letu lisimame,
Wala sisumbuke nao,ukajiona kidume,
Nawaona matapeli,na hizi barua pepe.
Hata sehemu nyingine,wajifanya wakimbizi,
Leo huyu na mwingine,wafanana sio wizi,
Wakamshike mwingine,mie hapa hawawezi,
Nawaona matapeli,na hizi barua pepe.
Pia wapo waswahili,wanatuona mambwiga,
Sitowaona wakweli,hata kipi wangeiga,
Muda wako wewe ghali,usipende igaiga,
Nawaona matapeli,na hizi bara pepe.
Najua mmeelewa,hakuna chakuongeza,
Najua sijachelewa,ndugu nawaelekeza,
Usije ukaibiwa,tamaa kiendekeza,
Mara Lisa mara jane,nasema ni matapeli."
0 comments:
Post a Comment