ads

Saturday, 20 August 2016

EATV AWARDS JAMBO JEMA LAKINI......!


Na.Mwanakalamu

Ni siku ya tatu leo kuna habari inasambaa kwenye vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii juu ya ujio wa tunzo mpya za burudani nchini.Tunzo hizo ambazo zitahusisha nyanja mbalimbali za burudani hasa muziki na filamu Afrika mashariki zinakuja wakati ambazo tuzo maarufu za muziki nchini zikiwa kama 'zimepotezewa' hivi si zile maarufu za Kilimanjaro ama hata zile zilizoanza kupata umaarufu "Tunzo za watu". Binafsi kama mpenda maendeleo ya muziki nichukue nafasi hii kuwapongeza waandaaji wa tunzo hizo IPP Media na wadhamini wakuu ambao ni Vodacom kwa kutuletea burudani hii ambayo si tuu huleta ushindani kwenye tasnia hiyo bali huiboresha na kuweka historia kwenyemausha yetu.Leo hii tunamkumbuka 20% kwenye muziki si tuu kwa nyimbo zake zenye ujumbe bali ile rekodi yake ya kuchua tunzo ingawa anaonekana kupotea kimuziki ama tuseme soko 'halimcommodate' lakini bado imeandikwa kwenye kumbukumbu zetu. Pia ni fursa mpya kwa wanamuziki kujitangaza hata nje ya mipaka yetu kwa kuwa tunzo hizi hujusisha taifa zaidi ya moja hii huweza hata kumfanya Galatone akawapelekee 'samaki' warembo wa Rwanda ama Uganda na wakampokea kwa kuwa wanamjua namna alivyomtoa jasho Eddy kenzi wao kwenye tunzo(huo mfano tuu). Licha ya pongezi hizo kuna mambo kadhaa ningependa kushauri juu ya tunzo hizo.Mambo hayo ni kama;-

 1.IDADI YA VIPENGELE WANIWA
Kuna vipengele kumi ambavyo bado havijanipa picha kamili ya mrengo wa tunzo hizi kwani haielekei ni katika kupaisha muziki wetu ama sekta ya filamu kwani kwenye muziki ni kama unaelea na filamu ndo kabisa.Kwenye muziki kuna vipengele vingekuwepo kuupaisha zaidi kama vile Kisingeli na aina nyingine za muziki wa asili ungepewa kipengele chake, taarabu na hip hop pia, hata watumbuizaji wangewekwa.Kwa upande wa filamu watu kama waongozaji na waandishi wangeongezwa.Ila kwa kuwa ni mwaka wa kwanza najua kuna mengi ya kujifunza kwanza hivyo tuwape nafasi muendelee kujifunza naamini mwakani kam tunzo zitakuwepo kutakuwa na vipengele zaidi.Walau muziki wa asili wa Rwanda upambanishwe na muziki wa Singeli.

2.UPATIKANAJI WA WASHIRIKI
Kwa mujibu wa taarifa ya waandaji imefaiwa kuwa washiriki watapatikana baada ta mameneja wao kujaza form itakayowanominate .Hapo naona pana ukakasi kidogo kwani inatengeneza ule mwanya wa kuujenga uhasama kati ya waandaji na wanasanaa pale meneja wa mwanamuziki ama mwigizaji anapopuuza taarifa na kutomnominate msanii wake kwa maksudi ama bahati mbaya na kuonekana mwanamuziki huyo amewadharau ikizingatiwa waandaji ni wamiliki wa vyombo vya habari vyenye nguvu sana kwenye ukanda huu.Tumeona mifano mingi ambayo imewafanya wanamuziki na wasanii wengine 'kupotezwa' kisa maelewano mabaya na vyombo vya habari licha ya vipaji vyao.Ningeshauri itumike namna nyingine ikiwa ni pamoja na kutumia majaji ambao wanakuwa na ujuzi na uzoefu wa tasnia hii kwafanye utafiti na kuwaweka wasanii wenye uzito sawa ama unaoshabihiana kwenye kipengele kimoja kisha wanamuziki hao wapewe taarifa ya kuwa wawaniwa kabla ya kutangazwa. 

3.UPATIKANAJI WA WASHINDI
Kwa mujibu wa waandaaji washindi watapatikana kwa kupigiwa kura na maamuzi ya majaji(hapa ndipo lilipo tatizo).Ni kweli tunzo nyingi zinazoheshika duniani huhusisha uamuzi wa majaji lakini kwa upande wangu naona tuachane na zama hizo.Kwa kuwa wawania wanakuwa na uzito sawa wa yeyote kuweza kuchukua tunzo kwa nguvu za wapiga kura ambao ndio walaji wa bidhaa zao nadhani ni wakati wa kuwaacha wawe majaji, majaji wenngine wahusike tuu kwenye kuhesabu kura na kufanya ule utafiti wa awali wa kuwapata "wenye uzito sawa" hii itasaidia kupunguza malalamiko yasiyo ya msingi juu ya kile kiitwao 'upendeleo' japo ni vigumu kumridhisha kila mmoja ila inawezekana kuwarudhisha wengi. Kwa kuwa wadhamini ni watu wanaohusika na mawasiliano wanaweza kutoa nafasi kubwa kwa watu wengi kupiga kura kurahisisha namna ya upigaji kura, kupunguza gharama ama hata kutoa motisha kwa wapiga kura kitu kitachoongeza thamani pia ya tunzo.Kwa mfano hata mama yangu kule Madaba aweza kutuma meseji kwa walau shilingi ishirini kumpigia kura TX moshi kama ni mmoja wa waliofanya mambo makubwa kwenye muziki wa bendi. Mwisho niwatakie maandalizi mema ya tunzo hizo ambazo naamini zinaweza kuleta mageuzi kwenye tasnia ya burudani kwenye jumuhiya ya Afrika mashariki na kuuleta ule umoja wa kiutamaduni.Pia niwakumbushe waandaaji kuwa wasanii na wapenda burudani wengi wanamatarajio makubwa saba na tunzo hizi zinazoonekana kama suluhisho ama mbadala wa 'ubabaishaji' kwenye tasnia ya burudani hivyo mkiwaangusha mtajishusha thamani kama wengine walivyojishusha thamani.Rai yangu kwa BASATA ni kwamba wasiwe ni watu wa 'kusaka ujiko' ulipo kwani kuna kiporo cha "Tunzo za ushairi za Ebrahim Hussein' ambazo mwaka wa pili unapita washindi wa mwaka jana hawajatangazwa na wakati zinaanzishwa palikuwa ahadi na mbwembwe za kufanyika tunzo hizo hata kwa miaka mitano mfululizo kwani pesa ilikuwepo na ilikuwa ikiendelea kuongezeka, hizo wameziacha kwa kuwa hazina ujiko tena wala kuwafanya waonekane kwenye TV. Naomba kuwasilisha.

0 comments:

Post a Comment