ads

Thursday, 21 April 2016

ANAITWA ALLY SALEH KIBA





Na.Mwanakalamu

Alikiba ama King kiba alianza harakati za muziki kitambo kidogo tofauti na wanamuziki wengi wanaotamba kwa muda huu.Mwanamuziki huyu anayetamba na nyimbo kadhaa mjini akiwa chini ya usimamizi wa Rockstar 4000 hajaanza leo kutoa hit baada ya hit na tangu 2006 alionekana kuteka masikio na akili za watu wengi na mwaka uliofuata alikuja na albam iliyokuja kuvunja na kujiwekea rekodi ya mauzo.Ingawa mitandao ya kijamii haikuwa na nguvu sana katika kutangaza nyimbo na kazi za wanamuziki mwanamuziki huyu alifanikiwa kuwateka wengi kuwa na albam  yake iliyokuwa na nyimbo kali ambazo hazikuhitaji watu kusubiri zaidi kumkubali mwanamuziki huyu.

Nilikuwa miongoni mwa maelfu walionunua albam hiyo na sikuwahi kujuta kuitoa poket money yangu ya shule kuinunua ingawa nilikuja kupitia kipindi kigumu cha kupuliza(kupiga uji bila kitafunwa) kwa karibu wiki moja na nusu.Kwa kifupi muziki wake ulikuwa ni zaidi ya maandazi ama viazi vitamu vilivyokuwa vikiuzwa shuleni.

Katika albam yake ya kwanza aliyoipa jina la Cinderella   ambapo kazi kubwa ya kuiandaa ilfanywa na producer KGT kulikuwa na nyimbo zifuatazo ambazo nyingi ziligusa hisia za vijana wengi ambao kipindi hicho ndo mahusiano na mapenzi yalikuwa yakisumbua na kufurahisha nafsi zetu.

1.CINDERELLA

Huu ni wimbo uliokuwa ukihusu stori ya binti mmoja ambaye alimsumbua sana kimapenzi kipindi wapo kwa bibi yake kigoma abla ya Kiba kwenda Dar es Salaam ,ambako alimpata Cinderella wake.Msichana huyo alipofika kwa Kiba  akaanza kumwomba msamaha na kuomba kurudiana naye lakini alikuwa amechelewa sana kwani nafasi yake ilikuwa imechukuliwa na Cinderella.

Katika wimbo huo aliimba pia Sesseme.

2.NAKSHI NAKSHI MREMBO.

Huu ulikuwa wimbo ambao Alikiba alitamani uwe wa kwanza kumtambulisha kwa mujibu wa muono wake lakini wasimamisi wa kazi zake waliona Cinderella ianze kwanza.Naam Cinderella ikapata nguvu ambayo hakuitegemea lakini Nakshi Nakshi ikaja kuuteka uwanja wa muziki Tanzania na kuwafanya wengi tuamini kuwa hakubahatisha kwenye Cinderella.

Nakshi nakshi ulikuwa wimbo ambao alimwimbia mrembo akimwambia ni namna gani alikwa akimpenda akimsisistiza kumpenda yeye zaidi na si umaarufu ama uanamuziki wake.

Kuna stori ya kuchekesha kwenye wimbo huu kwani kwenye video yake anaonekana Kiba akiwa amevaa suti moja nyeupe ambayo ilikuwa ni kubwa sana, kumbe ile suti aliingizwa mjini na rafiki yake ambaye alikuwa amemshawishi kuinunua dukani kwake akimwambia ni kali na fashemi mpya na aivae kwenye video.Akiangalia video ya wimbo huu huwa anacheka sana na wakati mwingine kumpigia simu rafiki yake kuwa alizingua.

Kwenye wimbo huu aliimba na Hakeem 5.



3.YATIMA

Huu ni kati m nyimbo ambazo ukiimbwa na unaweza kulia kwani umebeba hisia sana akiimba kisa cha bingti mmoja yatima ambaye aliupata uyatima baada ya kufiwa na wanzazi wake ambao walikuwa matajiri sana, hivyo kabla ya kuwakosa wazazi hakuzipata shida na ubaya wake.

Baada ya wazazi wake kufariki alianza kupata mateso kutoka kwa ndugu wa wazazi wake ambao walifikia kumwachisha masomo na kumfanyisha kazi nyingi za nyumbani jambo ambalo lilimfanya pate wazo la kutoroka  na kuingia mtaani.

Mtaani nako hakukumpokea vyema kwani alijikuta akitumbukia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya na baadaye alikuwa akilewa wenzake walikuwa wakimbak.

Mwisho Kiba anasisitiza kwenye chorus kuwa tusiwatenge yatima ,uliyebahatika kuwa na baba na mama yako hongera.

Ni wimbo mkali sana na wa hisia.

4.NAMZIMIA

Huu ni moja kati ya nyimbo zilizogusa hisia za vijana wengi wa kipindi kile, alizungumzia namna anavyompenda/mzimikia binti mmoja ambaye hakuwa na mapenzi kwake.Inafikia kipindi anapojitosa na akutembelea kwao binti anaonekana kutokuwa na hamu naye kabisa na akimwona ananuna na kumsonya.

Ukiwa hujaumizwa na mapenzi unaweza kumwambia sasa kwani yupo peke yake mbona analazimisha gari kusafiri baharini lakini kama umeumizwa unaweza kumhurumia kijana kwenye hu wimbo.

Ulikuwa ni kati ya nyimbo ambazo nilikuwa nikizirudia sana, usiniulize sababu.

5.MAC MUGA

Ulikuwa ni wimbo mwingine ambao ulikuwa mbali na mahusiano ya kimapenzi ,huu  ulimuhusu kijana mmoja aliyeitwa Mac Muga aliyeamua kwenda Afrika kusini kusaka maisha mazuri na bahati ikawa kwake akafanikiwa lakini aliamua kushiriki starehe za kila aina kisha akaishiwa pesa hadi kufikiria kujiua.

Katika wimbo huu wengi walijaribu kubashiri mlegwa wa wimbo kuna waliodai alimwimba Mwisho Mwampamba aliyefanikiwa baada ya kushiriki shindano la Big Brother Africa, wengine walidhani kamwimbia Mr.Nice lakini wimboo huu alimwimbia rafiki yake mmoja ambaye mengi yaliyoimbwa kwenye wimbo yalimuhusu, alikuwa akicheza naye mpira pamoja kabla na baada ya kurejea kutoka Afrika kusini.



6.SABRINA

Huu ulikuwa ukihusu mapenzi, akimwimbia mpenzi wake ambaye watu wengi ambao walikuwa hawapendi kuwaona pamoja hasa wakipita baadhi ya maeneo lakini Kiba alikuwa akimsisitiza namna maneno na matendo ya watu wengine yasivyoweza kuvunja penzi lao.

Alimwonesha kuwa alikuwa akimwamini na hakuwa na shaka yoyote kuwa penzi lao lingevunjika.

Kuna mahali Kiba anaimba

‘’hakuna anayekupita we ndo unaniweza,nafsi yangu imekita pale ulipooza’’

7.KUFOSI  MAPENZI

Hapa anaamua kuwaimbia wale wanaolazimisha mpenzi hata pale  wasipopendwa,anaimba mengi sana pia anaamua kumshangaa yule aliyejisifia kuwa alikuwa amependwa hasa kisha analalamika kuwa ametendwa hiyo yote baada ya kufosi wakati mwingine mtu anaamua kumwacha hata anayempenda na kumfuata anayemtamani.



8.RAGGA TONE

Ni wimbo fulani hivi wa kuchezeka , ameuimba ka ustadi wa hali ya juu akimwimbia msichana fulani juu ya kutoka na kwenda viwanja kasakata rhumba.Kuna mahali ameipanga mistari kwa kuzitaja namba moja hadi tisa(kwa kiingereza).

Kwa kifupi ni wimbo ambao hauchoshi kuucheza na kuusikiliza ukiwa umetulia pia.

Aliimba na Kalama P.

9.NICHUM

Kuchum/kubusu  ni moja kati ya mambo ambayo kwa kizungu huwa ni ishgara ya upendo ingawa kuna mabusu ya usaliti kama ya kina Yuda lakini kwenye wimbo huu Kiba anamwambia mpenzi wake amchum naye amchumu yote tuu mkumwonesha mapenzi mpenzi.

Ila kwenye wimbo huu alinichanganya kidogo alipoimba.

‘’Kaa ukijua sitokuoa nitakuchezea, umaskini utatufanya mi nawe kutoendelea’’

Sasa mpenzi wake ajue kuwa namchezea? Huenda ni masikio yangu ila nimeusikiliza wimbo huu zaidi ya mara mia moja lakini sijafanikiwa kusikia kitu tofauti zaidi ya nilichokiandika hapo juu.

Ukiachana na mstari huo wimbo unakuwa romantic kweli kweli.



10.SIKUONI

Ni wimboo mmoja hivi kama una fujo fulani hivi lakini Kiba anamlilia mpenzi wake ambaye anamtafuta pasi mafanikio akimpigia simu imezimwa.Ni wimbo mtamu sana kuusikiliza.

Kuna mahali anasema.

‘’ukizungumzia mapenzi allright wamzungumzia shetani wa mahaba asiyependa kumwona Alikiba akiwa nawe milele hata kufa’’

Pia katika wimbo hu ameimba na wanamuziki wenzake wengi ambao walikuwa pale kwa KGT.

11.NJIWA

Hapa njiwa anatumwa kupeleka salamu za mpenzi  wake ambaye daima alikuwa akihangaika ikli ampate kwani kabala ya njiwa Dakota alitumwa na jibu lilikuwa hapana lakini kwa njiwa alitegemea majibu mazuri baada ya kumtuma njiwa.

Ni wimbo uliobeba fikra tamu za mapenzi ambapo njiwa ndege alitumika kufikisha ujumbe wa mapenzi kwa mpenzi wake si unajua njiwa ni kiumbe mtiifu na anayevutia? Naam inavutia sana.



12.ZAIDI YANGU

Hapa aliamua kutunga kisa ambacho kwa sasa imekuwa kama fasheni ndugu ama marafiki kuchukuliana wapenzi.Kiba anamlalamikia mdogo wake kuwa kwa nini hakuwa akimheshimu shemeji yake na kuamua kuwa naye kwenye mahusiano.

Ni wimbo ambao kwa kipindi kile wengi waliporwa wapenzi wao na marafiki zao uliwagusa sana ilikuwa si ajabu kuwaona wakiuimba kwa hisia sana.

13.MSELA

Kiba alimua kuuvaa ukuwadi na kumsaidia msela wake ambaye alikuwa akiteswa na msichana chaguo la moyo wake.Alimua kukaa naye na kumwambia namna anavyomshuhudia akiteseka kwa sababu yake.

Kuna mahali anaimba;

‘’Usimwone anakonda sababu wewe unamringia kwa pozi unazomletea mi nimeona nije kukuwambia, usinione mi kipemba sababu Ally K nahurumia….’’

Najiuliza kwa masela wa siku hizi wanaweza kufanya hivi ama wanaishia kuomba ‘mzigo’ na wasichana wa kizazi hiki wanaweza kukupatia jibu la kukarahisha na huruma zikakuisha , anaweza tuu kukuambia….

‘’Kama una huruma mpe wewe’’ Utabaki kweli?

14.KUTESEKA NIMECHOKA

Hapa mwanakalamu mwenzangu Mtu makini Steven Mwakyusa anaweza kuwa na maneno mengi kwani wimboo huu ulikuwa ukimgusa haswaa… Dully Sykes alifanya yake kwenye wimbo huu akimpa nguvu mwankariakoo mwenzake.

Hapa waliamua kumtolea uvivu msichana aliyekuwa akiishia kuchuna tuu huku akiwa hana penzi lolote.

Kuna mahali anaimba.

‘’Nasema mimi , sikuhitaji tena ulinifanya bwege , kipofu ulinitenda ulivyowezaaa….’’

15.NAMSHUKURU MUNGU

Naam wengi tunaamini Mungu ndiye mgawa vyote, Alikiba alimua kumshukuru Mungu, wazazi wake walimu wake, na wote waliofanikisha yeye kuwa Ally anayewaburudisha maelefu ya watu.

Ni wimbo uliojaa mengi sana ambayo ukiyasikia unaweza tiskisa kichwa kukubaliana naye kuwa hayakuwa ya uongo na kila mmoja anapaa kushukuru hata kwa kile anachokiona amepewa.

Nami nawashukuru kwa kusoma maneno haya ambayo nahisi yatakuwa #TBT ya ukweli kwa wale waliokuwa kipindi hicho.

Share ifike mbali na kama kunamahali nimekosea na kuchanganya naomba mnisamehe si mwajua kumbukumbu huweza kupungua hasa na vyakula vyetu hivi tulavyo.






0 comments:

Post a Comment