Na.Mwanakalamu
Imekuwa fasheni katika miaka ya karibuni watu kukosoana kwa asili zao, hali zao za maisha, rangi , maumbile yao na hata aina ya elimu waliyonayo ama waipatayo.
Si tatizo watu kukosoana , bali wakosoane kwa hoja na hoja haziji kwa hulka, mihemko ama mahaba na jambo jadiliwa bali hoja huja kwa ujuzi na maarifa ambavyo ni zao la elimu.
Elimu ni nini?
Ukitaka kujua maana ya neno elimu unaweza ukaja na majimbu mbalimbali kichwani mwako ama kwenye vichwa vya watakao kupa hiyo maana.
Kwa uelewa wangu elimu ni ujuzi ama stadi ambazo mtu ama kiumbe hujifunza (kwa hiari ama lazima) ama hufunzwa ili kukabiliana na mazingira.
Viumbe hukabiliana na mazingira ili kuweza kuishi na kutengeneza maisha bora ya vizazi tarajiwa.
Kwa binadamu elimu hutolewa /hupatikana kwa njia kuu mbili ile iliyorasmi na isiyo rasmi.Mifumo isiyorasmi ilianza tangu zama za ujima ambapo kupitia elimu moto ukapatikana, watu wakafuga, wakawinda na kufanya mengi ambayo yamekuja kusaidia vizazi vilivyofuata na mifumo rasmi kwa barani Afrika ililetwa kipindi bara hili lilipoanza kushirikiana na jamii za mabara mengine kama Asia na Ulaya huku mashirika ya dini ya kiisalam na kikristo.
Elimu hii ya mfumo rasmi ambako kuna mitaala iliyoandikwa ndiyo iliyoleta mbadiliko makubwa katika jamii nyingi za kiafrika.Hapo ndipo mgawanyo wa kazi na matabaka yakatengenezwa na kuimarishwa badala ya matabaka kuwa katika nyanja za uchumi na kisiasa pekee elimu hii iliongeza matabaka ya waliosoma na wasiosoma kisha hata uchumi na siasa ukaanza kuingiliwa na matabaka ya elimu.
Kwa Tanganyika, elimu ya mfumo rasmi iliyoletwa na watangulizi wa wakoloni ikatumika kipindi cha ukoloni hadi wakati wa azimio la Arusha.Elimu ile iliyolenga kutoa ujuzi kidogo na kuandaa watumishi wa kuwatumikiwa wakoloni na kuimarisha dola yao ,ilifanyiwa mageuzi kadhaa ambayo bado madoa yake ni ngumu kufutika.
Baada ya azimio la Arusha ikaonekana misingi bora ya kuifanya elimu kweli ni njia ya kuifanya jamii iweze kukabili mazingira(kuyafanya mazingira kuwa mahali pa kuishi na kupata mahitaji kiurahisi/maendeleo).
Ugunduzi ulizingatiwa ,uzalendo na utamaduni pia , lakini baada ya miaka kadhaa pale tulioingia kwenye ile mipango ya kimaendeleo ya kibepari (SAP na mingine kama hii) hapo tukapoteza lengo na kujikuta tukitumbukia kwenye ile elimu tuliyoikataa wakati tunaleta azimio la Arusha.
Mitaala ikaanza kubadilishwa na wanasiasa walivyojisikia, shule tena haikuwa mahali pa kupata uzalendo bali kuwagawanya watu katika matabaka ya waliosoma na wasiosoma.Kuwa na elimu ikawa ni kufika sekondari ama chuo kikuu na si shule ya msingi na VETA.
Baadaye ziakaanzishwa shule zilizokuwa na mlengo wa kijamaa (shule za kata) na zikaanza kufanya kazi ya kibepari.
Hapo ndipo ujanja wa kisasa ulipoanza, tuliobahatika kusoma shule hizo tukakosa ujanja, usichangie sehemu utaambiwa ulisoma shule za kata, hamna kitu ni kayumba nyie hamjui kiingereza sayansi hamuijui wazee wa zero na mengine mengi hapo ujanja ni kutosoma shule za kata wakijua umesoma huko una hatari.
Walioanzisha shule za kata na walioanza kutoa mawazo haya ni wale ambao ama walipata elimu ya kikoloni ama ya kijamaa sasa tumlaumu nani aliyesoma shule za kata ama aliyeanzisha shule za kata kwa kujua ama kutojua ili kuleta matabaka.Shule zilizoitwa za vipaji maalum hazikutosha kupokea wanafunzi wote walifahulu kukahitajika mbadala lakini hawa wasomi wa zamani wakatuletea mbadala usiokamilika na madaraja yakaongezeka.
Nitawaambia wanangu kuwa sikutoka kapa kusoma shule za kata japo tulionekana masikini na wasio na akili nilipata ujuzi ambao ulinifanya nikaishi maisha bora pengine kuwazidi wale waliojiona bora, shule za kata ndizo zilizokuwa daraja nikafika kidato cha tano na chuo kikuu ambako nikakutana na wajanja wa shule za matajiri wanaoongea kiingereza kama malkia lakini wana ujuzi sawa , zaidi ama kidogo kuliko ujuzi nilionao.
Hao ndio niliowahi kuwapa akili ya kupika wali na chai na kukifanya chakula cha jioni nilipowakuta wakilia hawana mboga huku wana mchele na sukari ndani kifupi walishindwa kupambana na mazingira licha ya ujanja wao.
Share ifike kwa kizazi kijacho
0 comments:
Post a Comment