ads

Tuesday, 21 November 2023

BASI













Kaditama nimetua, sisongi sirudi tena,
Mambo nimeyatibua, hata nife hutoguna,
Kweli yote nimejua, ulianza mbali sana,
Basi.
Nilihisi tunaota, kumbe ninajidanganya,
Ilipita myaka sita, sina nililolifanya,
Mwenyewe ukajipata, mwenyewe sikujiponya,
Basi.
Nikaiweka busara, kumbe linaletwa shari,
Kaona kovu imara, kumbe njia ya hatari,
Ninazuia hasira, waniotea kaburi,
Basi.
Kaniundia ubaya, kwote wanone kituko,
Kutwa naijenga kaya, mwenzangu kucha mitoko,
Kila siku kwangu mbaya, kumbe kwako ni ujiko,
Basi.
Kihisi yule adui, kwake utajibagaza,
Nikajifanya sijui, sije wana waumiza,
Nilishajua wewe chui, heri kwangu kunyamaza,
Basi.
Niliposaka suluhu, wapasha vyako viporo,
Kavuka hadi Ruhuhu, Pwani hadi Morogoro,
Kumbe umeshakubuhu, mie kunipa kasoro,
Basi.
Umeutibua moyo, akili na wangu mwili,
Heri un'one na choyo, naipamba yangu hali,
Sasa ninatoka mbiyo, nikusanye zangu mali,
Basi.
Basi sasa imetosha, yote nimeyakubali,
Basi sasa yamekwisha, sasa ninakwenda mbali,
Basi sitokukumbusha, zile ahadi za kweli,

Basi. 

0 comments:

Post a Comment