Huwa halioni wivu, wala kuchukia kitu,
Jua halina uchovu, halibadiliki katu,
Huwa linatunza nguvu, jua si kama msitu,
Jua shahidi wa vingi, wala haliji kusema,
Usiri kwake msingi, halijawahi kugoma,
Iwe mboga iwe bangi, moja hawezi kuchoma,
Heri ningekuwa jua, ningekuwa kitu bora.
Singetamani usiku, wote mkawa nuruni,
Na nikasirike siku, niwache wiki gizani,
Wacha munone kasuku, mkanitoa thamani,
Kama ningekuwa jua, ningekuwa kitu bora.
Mngeona tabasamu, hata nikiwa tabuni,
Mkininyima salamu, isinifike moyoni,
Hata nisiwaze simu, anayepiga ni nani,
Kama ningekuwa jua, ningekuwa kitu bora.
Nizipuuze ahadi, mliziweka gizani,
Nisipandishe midadi, mkikana hararani,
Ama kumwona hasidi, akitamba kanisani,
Kama ningekuwa jua, ningekuwa kitu bora.
Ugonjwa ningepuuza, na kuikwepa sonona,
Hili linalonunguza, nisingelijali sana,
Kimya ningejiuguza, nikafa hata kupona,
Kama ningekuwa jua, ningekuwa kitu bora.
Ningekuwa peke yangu, mwezi na wingu kwa mbali,
Nisingewaza uchungu, nyota siponikubali,
Zaidi ni wangu Mungu, langu pendo astahili,
Kama ningekuwa jua, ningekuwa kitu bora.
Singekuwa na wana, nife wakanililia,
Na mke tukagombana, ili aje nikimbia,
Wala kusema hapana, nishindwe kuvumilia,
Kama ningekuwa jua, ningekuwa kitu bora.
Nisingemuwaza mama, au baba kumjali,
Huko na huko kusoma, kisha nife kwa ajali,
Mama akashika tama, kuwazia yangu hali,
Kama ningekuwa jua, ningekuwa kitu bora.
Basi hivyo siyo jua, siyo mvua wala nyota,
Macho nitayakodoa, na kusota nitasota,
Nikiumwa naumia, na furaha pia napata,
Kama ningekuwa jua.....
0 comments:
Post a Comment