Waweza hisi waota,kuwa umepata mwana,
Kutwa mwili utatota,na mawazo kugongana,
Huku na huko kugota,kumbe walisaka jina,
Unapompata mwana,kabwela wahangaika.
Miezi ya kutazama,kama hukuiamini,
Yale machungu ya mama,kama hukuyaamini,
Mawio hadi kuzama,mama yupo taabani,
Unapompata mwana,kabwela wahangaika.
Ulishapanga na jina,ghafla linakupotea,
Lile waona hapana,na jinsi ulikosea,
Kumbe halina maana,ndivyo unajitetea,
Unapompata mwana,kabwela wahangaika.
Nawe waweza akiba,mwana aje kutumia,
Hujiwazii kushiba,yeye wamfikiria,
Wala huhofu shuruba,mwana wamtafutia,
Unapompata mwana,kabwela wahangaika.
Mkeo utamjali,nawe sasa unapika,
Waijali yake hali,wafua na kuanika,
Hutaki aende mbali,ili asije kuchoka,
Unapompata mwana,kabwela wahangaika.
Sasa wapokea simu,za wakwe na ndugu zako,
Maadili ni muhimu,umekua wimbo wako,
Ratiba zako si ngumu,wajiwekea miiko,
Unapompata mwana,kabwela wahangaika.
Waitwa baba fulani,jina lako lafifia,
Simu za akina Jeni,sasa unazichunia,
Wawahi na ibadani,swala unazingatia,
Unapompata mwana,kabwela wahangaika.
Atafanya kazi gani,kabwela unakisia,
Hata akiwa shambani,siyo jasho kutumia,
Wapenda awe rubani,ndotoyo isotimia,
Unapompata mwana,kabwela wahangaika.
Mwana kipata mafua,utahaha siku nzima,
Kucha utaliga dua,kumuombea uzima,
Tafikia kuagua,mwana imtoke homa,
Unapompata mwana,kabwela wahangaika.
Kipata hela ya nyama,husiti kuinunua,
Utaiandaa sima,hata kwa moto wa bua,
Utahimiza kusoma,mwanao atapokua,
Unapompata mwana,kabwela wahangaika.
Siku utazihesabu,lini mwana katembea,
Taweka kwenye vitabu,siku atayoongea,
Humwazii kuwa bubu,mwana utamuombea,
Unapompata mwana,kabwela wahangaika.
Utawaza kuwa baba,na mume aliye bora,
Utamwepusha shuruba,kumkwepesha bakora,
Tamganda kama ruba,na kumpa masikhara,
Unapompata mwana,kabwela wahangaika.
#kaulizamakabwela
0 comments:
Post a Comment