Kawavalisha kaniki, ni walozi wabobevu,
Mkatuombea dhiki, kutupakaza maovu,
Na wala hamshituki, au kupata uchovu,
Nani alowadanganya, mkahisi mwatujua.
Mkaichapa misemo, na fitina mkajenga,
Kila baya siye tumo, kwa hila mlizotunga,
Tena mkatoa somo, eti mbele tutasonga,
Nani alowadanganya, kuwa mtatuvuruga.
Mkavibuni na visa, hadi tukaogopana,
Wanetu mkawatesa, pale tulipokwazana,
Mkamtia hamasa, eti lini twatengana,
Nani alowadanganya, mkajivika ujinga.
Kawafanya zumbukuku, mloikosa soni,
Mkawa kama kasuku, mkazipofua mboni,
Na hivyo vichwa vya kuku, yamewafika shingoni,
Nani alowadanganya, mnadhalilika ovyo.
Hamtujui wanazengo, wapi tulipotoka,
Sie ni kama mpingo, ngumu sana kukatika,
Mtahaha kama fungo, na huko kuneng'eneka,
Nani alowadanganya, kawaachia aibu.
Ashakumu si matusi, anijua namjua,
Mie chanya yeye hasi, na kwangu ameshatua,
Bado anajinafasi, anzeni jipya kuzua,
Nani alowadanganya, mtaweza kumtoa.
Vijembe vyenu naona, wala haviniyeyushi,
Kutengana bado sana, chuki kwetu hainyeshi,
Tunaweza kugombana, pendo hatuliangushi,
Nani alowadanganya, kuwa tutafika mwisho.
Kupenda ni fumbo gumu, ameweza litegua,
Kama mlileta sumu, zitaishia kuwaua,
Sie bado tunadumu, mtego tumetegua,
Nani alowadanganya, amewadhalilisha mno.
0 comments:
Post a Comment