Hawa watu wana nini, kila siku najuliza,
Mkiongea simuni, kweli watakuduwaza,
Ni mabingwa wa kughani, maneno watakujaza,
Juzi nilikuwa hapo, sema kazi za ofisi,
Atakweleza alipo, ukija kuna nafasi,
Karibu siye tupo, tena tutajinafasi,
Ile jichanganye wende, utajuta kuzaliwa.
Ataleta na matani, atakutoa ushamba,
Jiji utalitamani, kichwani utaliumba,
Jiji lisilo uduni, vile wanavyojigamba,
Ila jichanganye wende, utajuta kuzaliwa.
Mwezi ujao nakuja, utakuwa na nafasi,
Sema lini bwana waja, nipange mambo binafsi,
Tarehe utaitaja, bwana usiwe na wasi,
Ila jichanganye wende, utajuta kuzaliwa.
Kwa kuwa siyo ling'ombe, utapanga na bajeti,
Hutaki maji uombe, au undiwe kamati,
Wajipanga mkatambe, kipato chako cha kati,
Ila jichanganye wende, utajuta kuzaliwa.
Kakangu nipo mjini, nimefika tangu jana,
Ukisha toka kazini,ni vyema tukaonana,
Halafu tukae chini, sizijui nyingi kona,
Ila jichanganye wende, utajuta kuzaliwa.
E bwana huna habari, ninalo shamba Kimbiji,
Niko bize siyo siri, shamba naliweka mboji,
Vipi utanisubiri, au siyo mkaaji,
Ila jichanganye wende, utajuta kuzaliwa.
Pole sana usijali, ukija tutaonana,
Vipi Kimbiji ni mbali, cha mana jijini sina,
Tutete lile na hili, n'one mnavyopapana,
Ila jichanganye wende, utajuta kuzaliwa.
Wala usihangaike, nikupe namba ya Migi,
Popote akupeleke, kwangu kijana hazugi,
Ni kwa nini uteseke, kuja huku utabugi,
Ila jichanganye wende, utajuta kuzaliwa.
Wawaza Migi ni nani, humjui hakujui,
Heri urudi nyumbani, sije kutana na chui,
Wajipoteza hewani, kisha jijini hukai,
Dar na watu wake, usiende kichwa kichwa.
0 comments:
Post a Comment