ads

Tuesday 21 November 2023

KIBURI KINAVYOWAUA WAJERUMANI














Na. Kenny Anjelina

Waingereza wanamsemo wao, Curiosity killed a cat. Yaani udadisi mwingi ulimuua paka. Paka hudadisi hata vitu vinavyomzidi uwezo mwisho hupata madhara na hata kufa.

July 13, 2014, usiku ule Wajerumani walikuwa na furaha sana. Unajua kwanini? Walikuwa wanatwaa taji la Kombe la Dunia, tena njiani wakitoka kutoa semina elekezi kwa Brazil, palepale kwao waliwapa 1-7. Raha iliyoje?

Nafikiri usiku ule pale Rio de Janeiro ndo tulimaliza ubora wa Ujerumani. Tangu hapo hatujaona hata robo ya mafanikio ya ubora wa Ujerumani ile.

Mwaka 2018 waliishia hatua ya makundi pale kwa Vladimir. Walishindwa kufurukuta mbele ya Korea kusini na wahuni Mexico. Bingwa mtetezi, akatolewa hatua ya makundi.

Watu wa mpira walihisi ni bahati mbaya tu. Lakini kilichojirudia mwaka 2022, pale Qatar, kutolewa tena kwenye makundi tukajua tu Ujerumani imeanguka.

Dunia nzima inajua Ujerumani imeisha lakini wao tu pekee ndo hawaamini kama wameisha. Wana kiburi, ndo kinachowaua.

Baada ya Qatar, wakacheza mechi nyingi ambazo zinawapalia kila siku. Lakini hawataki kuanza upya, wanaamini wao bado wapo timamu.

Mpira umebadilika, umetoka kwenye matumizi ya nguvu na kucheza kwa nafasi hadi kwenye matumizi ya sayansi ya mchezo na kutimiza majukumu ya pamoja.

Uingereza, Ufaransa na Uholanzi wapo huko. Argentina ndo tusiseme, unaona jinsi Rodrigo De Paul anavyohaha uwanja mzima. Hakuna matozi tena.

Ila Ujerumani wao bado wanaamini katika nguvu na kupishana. Bahati mbaya wana Gundogan na Musiala ambao hawawezi kutumia mabavu.

Juzi walijaribu kuacha kiburi chao, wakaamua kuiga sayansi kwa kumchezesha Kai Havertz kama mlinzi wa kushoto lakini wakawa wamechelewa, wakafa 3-2 kwa Uturuki.

Ujerumani inabidi wakubali kwamba kizazi cha dhahabu kimeisha, inabidi waanze chini. Kama Uingereza na Uholanzi walivyofanya.

Wakiendelea na udadisi wao watakufa kama ambavyo Italia. Wamekosa michuano miwili ya kombe la Dunia mfulululizo na juzi ilibaki kidogo washindwe kufuzu Euro

0 comments:

Post a Comment