Na. Kenny Anjelina
April 30, 2022 juu ya kitanda kimoja kwenye hospitali ya San Raffaele nchini Italia, Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 54, alikuwa anavuta pumzi ya mwisho.
Huyu alikuwa ni Mino Raiola, mzee wa fix, mzee wa kuchezesha miamala. Dalali na huni la kimataifa.
Mino alikuwa na nguvu haswa na kazi yake aliifanya kisomi kwelikweli.
Jana, Mbappe amefikisha magoli 300. Nawaza kama Raiola angekuwa hai halafu awe wakala wa Mbappe. Nafikiri vilabu vingi Ulaya vingekaa kwa adabu. Sio PSG siyo Real Madrid, wala Barcelona.
Kwanza angeenda Sky Sports na kusema, "PSG ni timu kubwa, lakini tupo tayari kwa changamoto mpya. Kuna ofa nyingi mezani na tunazifanyia kazi. Lakini kwasasa ni mchezaji wa PSG na anafuraha ".
Hapo PSG wangehaha, kusikia hivyo wangepanga noti nyingi kumshawishi Mbappe aongeze mkataba.
Jumatano, angeenda kwenye gazeti la THE MIRROR na kusema, "Real Madrid ni klabu kubwa na ni ndoto ya kila mchezaji mkubwa. Tunawasikiliza Madrid wanasemaje " Hapo Perez angekunjua noti na kukaa mkao wa kula.
Jumamosi, angeenda THE SUN na kusema, "Jumatatu tutakutana na wawalilishi wa Manchester United kuhusu uhamisho wa Kylian. Ni kijana mdogo ambaye juzi amefikisha magoli 300. Lazima thamani yake iwe kubwa "
Kwahiyo kwa wiki moja tu tayari angewachonganisha PSG, Real Madrid na Manchester United. Ila sasa kumepoa sana.
Haland alitakiwa na Real Madrid wakati akiwa Salzburg. Lakini yeye akampitisha kwenye vituo vingi vya Dortmund na Manchester City ili apige pesa ya udalali mwote humo kabla ya kwenda Madrid au Barcelona. Mino ni Msela haswa.
Kwa vurugu zake na umaarufu wake, angepiga Pauni Milioni 25 pekee yake kwenye dili la Mbappe kwenda Madrid au kwingineko.
Kisha angechukua boti na kwenda kupumzika kwenye fukwe za Venezia akiwa tumbo wazi na mvinyo na warembo pembeni.
RIP RAIOLA
0 comments:
Post a Comment